Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 23 Machi 2013 09:27

Nabii wa Rehma (11)

Nabii wa Rehma (11)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Kwa furaha na moyo mkunjufu nakukaribisheni kujiunga nami katika sehemu hii ya 11 ya kipindi hiki kinachodondoa machache kati ya mengi yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu lakini wenye insafu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Katika kuzungumzia shakhsia ya Nabii wa rehma Muhammad SAW ambaye ni mlezi na mwalimu bora wa wanadamu kuna athari nyingi za maandishi zilizoalifiwa na watafiti na wahakiki mbalimbali ambazo kila moja kwa upande wake inastahili sifa na pongezi. Lakini kabla ya kuziangalia athari hizo kwa leo hebu na tusikilize yale yaliyosemwa na Kitabu Kitukufu cha Qur'ani kuhusu mbora huyo wa viumbe. Aya ya 110 ya Suratul Kahf inasema: "Sema: Mimi ni mwanaadamu kama nyinyi tu nimeletewa Wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja."

Gostave Le Bon ni mmoja wa Maorientalisti mashuhuri wa Kifaransa, yaani wataalamu wa masuala ya Ulimwengu wa Mashariki ambaye amefanya utafiti mkubwa kuhusu Uislamu na ustaarabu wa Waislamu. Katika athari za maandishi ya mtaalamu huyo wa masuala ya jamii aliyezaliwa mwaka 1841 na kuaga dunia mwaka 1931 ni nadra kushuhudia fikra za taasubi, upendeleo na mitazamo hasi juu ya Uislamu na Waislamu, na hii ni moja ya sifa za kipekee aliyokuwa nayo Le Bon.

Baada ya safari za kielimu na za utafiti alizofanya katika nchi mbalimbali, Gostave Le Bon aliandika vitabu vyenye thamani kuhusu historia na ustaarabu wa baadhi ya mataifa. Miongoni mwa vitabu hivyo ni kile kiitwacho "Uislamu na Ustaarabu wa Waarabu". Moja ya sifa za aina yake za kitabu hicho ni maelezo yenye murua na ya kuvutia ya msomi huyo kuhusu Bwana Mtume Muhammad SAW na uchanganuzi aliofanya kuhusu sababu za kuenea Uislamu na mchango wa dini hiyo kwa ustawi wa ustaarabu.

Katika kitabu chake cha "Uislamu na Ustaarabu wa Waarabu" Le Bon anasema, vipindi tofauti vya kiongozi mkuu wa Uislamu Nabii Muhammad (SAW) kuanzia utotoni mwake hadi siku alipobaathiwa na kupewa Utume na mpaka wakati alipoelekea ulimwengu wa milele, vimejaa matukio ya kusisimua. Matukio haya, Le Bon anasema, yanabainisha ukweli huu, kwamba Mtume wa Uislamu ni shakhsia mteule na mtakatifu ambaye maisha yake yaliambatana na miujiza na ishara zisizo na shaka za kuthibitisha utukufu aliokuwa nao. Kwa mtazamo wa Gustave Le Bon, Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa na irada thabiti na lengo aali na tukufu. Na ndiyo maana vitisho na stihzai za watu wa Makka, hazikumteteresha hata chembe katika kutekeleza kazi aliyokusudia, bali aliwaeleza watu wake kwamba: Kama jua litawekwa kwenye mkono wangu wa kulia na mwezi kwenye mkono wangu wa kushoto, sitoacha katu kuifanya kazi hii.

Le Bon anasema, Nabii Muhammad (SAW) alisimama imara kukabiliana na maudhi, mateso na manyanyaso ya maadui kwa subira na uvumilivu na kwa mlahaka wa kiungwana; na kwa baraka za balagha na ufasaha aliokuwa nao katika uzungumzaji, kila siku aliendelea kupata wafuasi wapya waliomwamini na kuingia katika dini yake.

Moja ya sifa maarufu alizokuwa nazo Mtume wa Mwenyezi Mungu ni akhlaqi njema zisizo na kifani. Ni hii ni sifa ambayo Mwenyezi Mungu Mwenyewe ameieleza katika kubainisha sifa za Mtume wake huyo kwa kusema: "Na hakika wewe una tabia tukufu". Yeye mwenywe Nabii Muhammad SAW alikuwa akiwaambia watu kwamba:" Sikutumwa kwa jambo jengine ila kuhuisha na kukamilisha mafunzo ya akhlaqi njema". Akiizungumzia nukta hii katika kitabu chake chini ya anuani isemayo:"Maisha ya Mtume wa Uislamu na sifa zake za Kiakhlaqi", Gostave Le Bon ameandika hivi:" Mtukufu huyo aliwazidi watu wote kwa akili na busara, na fikra zake zilikuwa pana na makini kuwashinda wote. Hakuwa akizungumza ovyo, bali kila wakati alikuwa ameshughulika kumdhukuru Mwenyezi Mungu. Daima alikuwa akilahikiana na watu kwa uso wa bashasha, na mara nyingi akikaa katika hali ya ukimya na utulivu. Hulka yake ilikuwa ya upole na tabia yake ilikuwa safi na njema. Hakuwahi hata mara moja kuwatizama watu wanyonge kwa jicho la dharau kwa sababu ya umasikini na ufakiri waliokuwa nao; na hakumwekea heshima katu ya unyenyekevu jabari yoyote yule kwa sababu ya nguvu na ubabe wake. Le Bon anaendelea kuandika: Kwa mujibu wa wanahistoria wa Kiarabu, Nabii Muhammad (SAW) alikuwa mtu mkinaifu na mwenye kutafakari, asiyependa kusema sana, mwenye uono wa mbali, moyo mwema na safi; na katika milahaka na miamala alikuwa akichunga mno staha na adabu. Hata alipofikia kwenye hali ya utajiri na nguvu za mamlaka hakuwaruhusu katu watu wengine wamfanyie kazi zake. Muhammad alikuwa na hima kubwa, mpole mno na mwenye huruma sana katika kuamiliana na watu. Mmoja wa mahadimu wake anasimulia kwa kusema, nilikuwa pamoja naye kwa muda wa miaka kumi na nane, lakini katika muda wote huo sikuwahi hata mara moja kumwona akizungumza kwa ukali au kuonyesha mlahaka wa kuudhi hata katika kuadibisha.

Nguvu na adhama ya taifa lolote lile wapenzi wasikilizaji inafungamana na umoja na mshikamano wa watu wake. Tangu pale shakhsia adhimu wa shani wa Uislamu, yaani Nabii Muhammad SAW alipodhihiri kama kitovu na mhimili mkuu wa umma wa Kiislamu, mvumo wa neno lenye kusisimua nyoyo la umoja ulisikika na kutanda ulimwenguni. Kwa mtazamo wa Gustave Le Bon, umoja wa umma wa Kiislamu ni moja ya miujiza muhimu iliyofanywa na Bwana Mtume. Analielezea suala hilo kwa kusema:"Muujiza mkubwa wa Mtume ni kwamba kabla ya kufariki kwake aliweza kuyaunganisha pamoja matapo yaliyotawanyika ya Waarabu na kuasisi kutokana na matapo hayo yaliyokuwa katika hali ya kuemewa na kutangatanga umma mmoja, ambao wafuasi wake wote walionyesha unyenyekevu na utiifu wao kwa dini moja na mbele ya kiongozi mmoja. Ni jengo hili adhimu lililosimamishwa na Mtume linalodhihirisha vizuri na kwa uwazi adhama na ukubwa wa shakhsia yake.

Kwa kumalizia Gostave Le Bon anasema:" Ikiwa tutazipima thamani za watu kwa matendo na athari zao hakuna shaka yoyote kuwa Muhammad (SAW) ndiye shakshia mkubwa zaidi wa historia. Inajulikana bayana kuwa Mtume alikuwa Ummiy, yaani asiyejua kusoma wala kuandika, na hili ni jambo linalokubaliana na hoja. Lakini pamoja na hayo alikuwa na kiwango cha juu kabisa cha akili, kipawa na hekima hata kama taasubi za kidini na za kifikra zimeyatia upofu macho ya baadhi ya wanahistoria na kuwafanya wawe wakaidi wa kukiri juu ya fadhila na adhama ya Muhammad".

Wapenzi wasikilizaji maneno haya ya Gostave Le Bon ndiyo yanayotukamilishia sehemu hii ya 11 ya kipindi hiki cha "Yaliyosemwa na Wenye Hekima Kuhusu Nabii wa Rehma". Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa ya Mola nakuageni kutoka hapa studio huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …