Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 11 Machi 2013 13:49

Nabii wa Rehma (9) + Sauti

Nabii wa Rehma (9) + Sauti

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Ni matumaini yangu kuwa hamjambo popote pale mlipo. Nakukaribisheni kwa furaha na moyo mkunjufu kujiunga nami katika sehemu hii ya tisa ya kipindi hiki  kinachodondoa yale yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Nakutafadhalisheni muendelee kuwa nami hadi mwisho wa kipindi chetu kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Kuchomoza kwa nuru ing'arayo ya Uislamu na kudhihiri kwa Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu ilikuwa nukta yenye umuhimu wa kipekee katika historia ya wanadamu ambayo athari na matunda yake yasiyo na idadi yanaweza kushuhudiwa katika maendeleo ya ustaarabu wa zama zetu hizi. Moja ya matunda ya mti huu mtoharifu wa mbinguni ni ukuaji na ustawi wa elimu ya sayansi. Elimu ambayo ilichanua kutoka kwenye kitovu cha ustaarabu wa Kiislamu au kukulia na kustawi kwenye mbeleko za ustaarabu huo kisha ikahamia Uhispania, Ufaransa, Italia, Ujerumani, Uingereza na mataifa mengine ya Ulaya na hadi mwishowe ikaenea ulimwengu mzima. Watafiti na wanahistoria wengi wanaamini kuwa bila ya kubaathiwa na kutumwa Mtume Mtukufu Muhammad SAW na dini ya mbinguni ya Uislamu aliyokuja nayo, staarabu za kale kama za Rumi, Misri na Iran ya kale zisingeweza kuungana na staarabu za zama hizi. Kwa kujenga hoja zao kulingana na ushahidi wa kihistoria, watafiti na wanahistoria hao wanasema Mtume wa Uislamu sio tu ni mmoja wa shakhasia wa daraja ya kwanza wa ustaarabu wa mwanadamu bali hata kuenea Uislamu ulimwengu mzima kumetokana na sifa nyingi za kipekee ilizonazo dini hiyo.

Katika kipindi chetu kilichopita tulitupia jicho mitazamo ya John Davenport, mwanafikra wa Kiingereza kuhusu shakhsia ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Katika kitabu chake kiitwacho "Kumwomba Radhi Muhammad na Qur'ani" mbali na kumsifu na kumwelezea Bwana Mtume kuwa ni msanifu na mjenzi mkuu wa historia, Davenport amenukuu pia mitazamo ya kitafiti ya wanafikra wengine wa Magharibi kutilia nguvu mtazamo alionao kuhusu nabii huyo wa rehma. Katika sehemu moja ya kitabu chake, John Davenport anasema:"Maoni ya Thomas Carlyle, mwanahistoria na mwanafikra wa Uingereza kuhusu Mtume huyu shujaa ni sahihi kabisa na ya msingi na hayawezi kuachwa bila ya kuzungumziwa. Carlyle ameandika haya yafuatayo katika kitabu chake kiitwacho" Utafiti":" Mwana huyu wa jangwani alikuwa na moyo mpana, na hakuathiriwa na fikra zozote za kupenda jaha na ukubwa. Yeye alikuwa mmoja wa watu walioumbwa na maumbile aliye na upendo na ikhlasi. Wakati watu wengine walikuwa wakitoa maneno ya upotoshaji na madai ya kuhadaa watu, mtu huyu hakujiingiza katu katika medani hizo". Carlyle anaendelea kuandika kuwa "maneno ya mtu kama huyu ni sauti iliyonyooka kutoka kwenye moyo wa ulimwengu. Watu wanapaswa kuyasikiliza, na kama hawatosikiliza maneno kama haya basi haifai wao kushughulishwa na sauti nyengine yoyote".

Wapenzi wasikilizaji, kabla ya Thomas Carlyle, watu wenye kalamu za sumu walikuwa wakiandika mengi dhidi ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Lakini baada ya makala aliyoandika Carlyle kuhusu Bwana Mtume katika kitabu chake kiitwacho "On Heroes, Hero-Worship" yaani "Kuhusu Mashujaa, Heshima Kubwa kwa Shujaa", ukweli mwingi ulidhihirika na wimbi la hujuma zisizo na insafu alizokuwa akielekezewa Bwana Mtume katika zama hizo lilipungua. Carlyle anasema:" Enyi ndugu zanguni, hivi nyinyi mmepata kuona mtu mwongo kuwa na nguvu kama hizi za kuweza kuanzisha dini na kuieneza duniani? Naapa kwa Mungu kwamba mtu mwongo na asiye na elimu hawezi kuwa na uwezo wa kujenga nyumba. Haiwezekani yeye kuweza kujenga nyumba ambayo mamilioni ya Waislamu wanaishi ndani yake kwa kipindi cha karne 14. Kama nyumba hii ingekuwa imejengwa na mtu mwongo, hivi sasa ingekuwa imeshabomoka na kutoweka." Carlyle anataasafu kwa kusema: "Inasikitisha! Udhanifu wa aina hii unatia aibu kubwa! Watu wenye fikra hizi ni masikini na dhaifu kiasi gani...wakati mimi ninapoiangalia historia ninaona kwamba ukweli na usafi vilikuwa ndio msingi wa maisha ya Mtume pamoja na matendo na mwenendo wake wenye kupendeza".

Katika kumtetea Mtume Mtukufu wa Uislamu, Thomas Carlyle anasema, mtukufu huyo ana ilhamu za wahyi na amepambika na sifa aali za kiutu. Katika maelezo yake ya kumtetea Bwana Mtume, Carlyle ameandika hivi:" Nyinyi mnasema yeye ameitwa Mtume. Ndiyo! Mtu huyu ni Mtume aliyetuletea sisi ujumbe kutoka kwenye chemchemi isiyokauka ya ulimwengu wa uumbaji. Hebu nyinyi yaangalieni maneno yake. Mwenyezi Mungu amemfunza shakhsia huyu adhimu elimu na hekima, na kabla ya kitu chochote inatupasa sisi kuyataamali maneno yake. Tokea siku za mwanzoni yeye alikuwa kijana safi na mwelewa, na marafiki zake walikuwa wakimwita Mkweli na Mwaminifu. Watu wote walikuwa wanamjua hali yake; alikuwa akifua nguo zake yeye mwenyewe na kujitengenezea viatu vyake. Alikuwa akishauriana na watu, pamoja na kwamba alikuwa mtawala na kiongozi wao. Nyinyi mpeni jina lolote lile mtakalo lakini mjue kwamba hakuna mfalme mkubwa na mtawala yeyote katika historia mwenye kila aina ya mataji na mapambo aliyetiiwa kama mtu huyu aliyekuwa akifua nguo zake yeye mwenyewe. Shakhsia huyu adhimu ambaye alivumilia machungu na mashaka yote yale kwa muda wa miaka 23 alionyesha uthabiti katika majaribu na mitihani mikubwa na migumu kiasi kwamba mimi ninaamua kumwita yeye "shujaa" na ninahisi anastahiki cheo hiki".

Kwa mtazamo wa Carlyle wapenzi wasikilizaji, sifa za kipekee za Bwana Mtume Muhammad SAW zinatokana na ukweli kwamba tangu utotoni mwake mtukufu huyo alikuwa muda wote katika hali ya fikra na tafakuri. Carlyle ameandika hivi: "Tangu zamani, fikra aali na za upeo mpana zilikuwemo akilini mwa mtu huyu; alikuwa akijiambia nafsi yake: Mimi ni nani? Huu ulimwengu adhimu ambao ninaishi ndani yake ni kitu gani? Maisha ni nini? Majabali makubwa ya mlima wa Hira na mafungu ya mchanga wenye kuunguza wa ardhi ya Hijaz havikuwa na jibu la kumpa. Mbingu za samawati, licha adhama yake yote, pamoja na nyota zing'arazo ambazo zilitandaza mwanga wake juu ya kichwa chake, havikuweza pia kumpa jibu. Jibu halikuweza kuja kutokea upande wowote ule. Ni roho yake tu mtu huyu pamoja na ilhamu za Mwenyezi Mungu zilizokuwa zikimfikia ndivyo vilivyoweza kumpatia jibu, na si kitu kingine chochote kile!"

Baada ya kuzifuta tuhuma dhidi ya Bwana Mtume, mwanafikra huyu wa Kiingereza anabainisha mahaba na mapenzi yake kwa Nabii adhimu wa Uislamu kwa kusema:" Mimi ninampenda Muhammad kwa sababu hulka yake ilikuwa ya ikhlasi na hakuwa na ria, kujionyesha wala hadaa na udanganyifu katika matendo yake. Hakuwa na kiburi, lakini pia hakuwa dhalili. Alikuwa mtu adhimu kifitra na kimaumbile. Qur'ani ilikuwa ikitiririka kutokea kinywani mwa Muhammad na kuacha taathira ndani ya nyoyo za wengine. Pamoja na yeye kuwa hakusoma, hakwenda skuli na wala hakuwahi kuwa na mwalimu, hakuwa akivihitajia hivyo. Alikuwa mithili ya wembe ambao haukuwa na haja ya kunolewa".

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kukomea hapa kwa leo na kukuageni hadi juma lijalo inshallah tutakapokutana tena katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …