Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 05 Machi 2013 15:16

Nabii wa Rehma (8)

Nabii wa Rehma (8)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Kwa furaha na moyo mkunjufu nakukaribisheni kujiunga nami tena katika sehemu hii ya nane ya kipindi hiki kinachodondoa machache kati ya mengi  yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu lakini wenye insafu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Kati ya shakhsia wakubwa wa historia hakuna yeyote miongoni mwao aliye mfano wa Mtume wa Uislamu ambaye aliasisi ustaarabu aali na wenye adhama kutokana na jamii ya kijahiliya na ya watu waliobaki nyuma kimaendeleo. Na huu ni ukweli wanaoukiri hata waandishi wa historia wa Mashariki na Magharibi. Historia imeshuhudia kwamba katika zama ambapo ulimwengu ulikuwa umeghairiki kwenye dimbwi la ujinga, ujahili na upotofu wa kifikra alidhihiri shakhsia adhimu ambaye aliwaletea wanadamu dini mpya. Mafundisho aliyoleta Nabii Muhammad SAW yalisimama juu ya msingi wa akili na hekima na kukabiliana na ujinga na ibada za khurafa.

Michael H. Hart, msomi wa Kimarekani na mwandishi wa kitabu maarufu kiitwacho:  The 100: A Ranking of the Most Influential Persons in History yenye maana ya "Orodha ya safu ya watu mia moja wenye taathira zaidi katika historia", Hart ameliweka jina la Bwana Mtume Muhammad SAW kwenye nafasi ya kwanza kati ya shakhsia hao mia moja waliotoa mchango mkubwa na wenye faida zadi kwa jamii ya wanadamu. Katika kitabu chake hicho Michael Hart ameandika hivi:" Chaguo langu la kumweka Muhammad (SAW) katika nafasi ya kwanza ya watu wenye taathira zaidi katika historia ya ulimwengu huenda litawastaajabisha baadhi ya wasomaji au litakosolewa na baadhi yao, lakini yeye ndiye mtu pekee katika historia aliyepata mafanikio makubwa zaidi katika uwanja wa kidini na wa kidunia".

Wapenzi wasikilizaji, katika kipindi chetu cha leo tutatupia jicho yale yaliyoelezwa na John Davenport, mwandishi wa Kikristo na raia wa Uingereza aliyezaliwa mwaka 1597 na kuaga dunia mwaka 1670, kuhusu nabii wa rehma Muhammad SAW. Yeye anasema, kwa mtazamo wake sifa muhimu zaidi ya Bwana Mtume ni kujulikana kwa uwazi kabisa maisha yake tangu kuzaliwa hadi kufariki kwake. Katika kitabu chake kiitwacho:"An Apology for Mohammed and the Koran" yaani "Kumwomba Radhi Muhammad na Qur'ani" Davenport ameandika, hii ni nukta iliyowazi na isiyo na shaka kwamba kati ya waasisi wa sheria na wakomboaji wa ardhi mashuhuri duniani hakuna wasifu na historia ya maisha ya yeyote miongoni mwao iliyoandikwa kwa ufafanuzi zaidi na kwa namna yenye itibari zaidi kama historia ya maisha ya Muhammad (SAW). Hata kaumu ya Waarabu wa ardhi ya Hijazi wamepewa umuhimu na mataifa mbalimbali kwa baraka ya shakhsia ya Muhammad (SAW). Katika sehemu nyengine ya kitabu chake hicho John Davenport ameandika:" Watu wanaozusha tashiwishi kuhusu Muhammad – Mtume wa Uislamu – wajue kwamba nukta muhimu katika msimamo wake wa kuhakikisha anafikia lengo lake kuu ni kwamba alilifanya suala hilo kuwa ndio ghaya katika maisha yake na akasimama imara na kwa uthabiti katika utekelezaji wake. Na ni nukta hii inayowafanya watu wote wamsifu na kumuenzi. Aidha wamekosea kabisa wale watu ambao wangali wanadhani kuwa Mtume wa Uislamu alieneza dini yake kwa upanga. Kwa sababu wasomi na wanafikra wenye uelewa wa masuala ya historia wanaeleza bayana kuwa Muhammad alikomesha umwagaji damu na ugomvi kati ya koo na makabila, na akaiweka Sala na Zaka kwenye nafasi ya wahanga na makafara ya watu, na badala ya dini yake kushupalia vita na mizozo isiyokwisha ilipulizia ndani ya nyoyo za watu roho ya upendo, kutakiana mema na kheri na fadhila za maadili na akhaqi njema.

Katika faslu moja ya kitabu hicho chenye anuani ya "Kumwomba Radhi Muhammad na Qur'ani" John Davenport anazijibu tuhuma moja baada ya nyengine zilizotolewa dhidi ya Bwana Mtume. Katika sehemu moja ya faslu hiyo ameandika:"Nchi kama Hijazi ilikuwa imeghariki kwenye dimbwi la ibada ya masanamu. Muhammad alifanya mageuzi makubwa na endelevu katika ardhi hiyo; alitangaza kwamba kuwaua watoto wadogo na kuwazika watoto wa kike wakiwa hai ni kitendo kiovu, na akaupiga vita mpaka akautokomeza mwenendo huo usio wa kiutu. Alipiga marufuku vinywaji vyenye vileo pamoja na uchezaji kamari. Aliuwekea mpaka maalumu uoaji wa wake wengi na akaushurutisha na utekelezaji uadilifu kati ya wake hao. Sisi tunauliza, inawezekana kweli ujumbe wa mtu kama huyu uwe umetokana na ubunifu wake mwenyewe? Muhammad hakuwa katu na uchu wa madaraka na wa fahari na hadhi za kidunia. Alikuwa akiwausia watu kuamiliana kwa uadilifu na kuwa na murua na uungwana. Hapana shaka kuwa yeye ni mtakasifu zaidi kati ya shakhsia wote adimu kuwahi kushuhudiwa ulimwenguni hadi sasa. Inatupasa tukubali kwamba yeye ni shakhsia mkubwa zaidi na wa kipekee ambaye kuwepo kwake kunaufanya ulimwengu wa uumbaji ujivunie na kujifaharisha naye.

Kwa mtazamo wa John Davenport, sababu muhimu zaidi iliyopelekea kubakia milele jina la Mtume wa Allah, Muhammad SAW ni shakhsia yake isiyo na mfano na dini aali na tukufu aliyokuja nayo. Davenport anasema, Qur'ani na mafundisho yake vilipenya ndani ya roho na nafsi ya Muhammad (SAW) na kumfanya kuwa mfano hai wa mtu aliyekamilika na aliyetukuka. Katika kuitolea ufafanuzi zaidi nukta hii Davenport ananukuu maneno ya mwanafikra mwenzake wa Magharibi aitwaye Edward Gibbon kuonyesha jinsi alivyotekwa na kuvutiwa na maelezo aliyotoa Gibbon kumuelezea Bwana Mtume. Gibbon, ambaye alikuwa mwanahistoria aliyeishi katika karne ya 18 anazielezea sifa za Mtume kwa kusema:"Muhammad alikuwa na sifa za aina yake kwa mtazamo wa jamali na tabia njema. Kabla ya kuanza kuzungumza na kuhutubia aliweza kuwavuta na kuwateka hadhirina, awe ni mtu mmoja au hadhara kubwa ya watu. Sura yake ya kuvutia na yenye haiba ya taadhima, macho yake yenye mvuto, tabasamu lake la kupendeza, ndevu zake zilizojaa na hatimaye umahiri aliokuwa nao katika uzungumzaji, vyote hivyo vilikuwa vikiwafanya watu wote wamsifu na kumpongeza. Katika masuala ya kijamii na mambo yanayohusiana na maisha alikuwa mtu mwenye kuheshimu ahadi na makubaliano. Ufasaha na uwadhiha aliokuwa nao katika maneno yake ulibainisha wazi yale aliyokusudia. Uwezo wake wa kuhifadhi ulikuwa mkubwa na mpana na alikuwa na uelewa usio wa kawaida. Muhammad alikuwa na nguvu ya fikra na hekima na vilevile uwezo mkubwa wa amali na utendaji." Mwisho wa kumnukuu Gibbon.

Katika kitabu chake kiitwacho "Kumwomba Radhi Muhammad na Qur'ani" John Davenport anazibanisha kwa ufupi sifa za fadhila na utukufu wa nabii wa rehma Muhammad SAW kwa maneno yafuatayo akisema:" Muhammad alishuhudia hakika za mambo kutokea nyuma ya pazia la mambo ya kidhahiri ya ulimwengu huu. Alikuwa amekamilika kwa akili, uoni na uelewa na alikuja na ratiba na mfumo aali kabisa kwa ajili ya uokovu wa wanadamu. Ukweli ni kwamba kutokana na taathira ya utengamano uliopo kati ya dini ya Muhammad na akili na hekima walimwengu wamefaidika na kunufaika na baraka za kimaanawi na za kimaada za dini hii."

Wapenzi wasikilizaji maneno haya John Davenport ndiyo yanayotukamilishia sehemu hii ya nane ya kipindi hiki cha "Yaliyosemwa na Wenye Hekima Kuhusu Nabii wa Rehma". Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa ya Mola nakuageni kutoka hapa studio huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu...

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …