Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 03 Machi 2013 17:09

Nabii wa Rehma (7) + Sauti

Nabii wa Rehma (7) + Sauti

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Kwa furaha na moyo mkunjufu nakukaribisheni kujiunga nami tena katika sehemu hii ya saba ya kipindi hiki kinachodondoa machache kati ya mengi  yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu lakini wenye insafu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Wanadamu wote wapenzi wasikilizaji wanapenda wawe watu wenye kupata saada na fanaka katika maisha yao yote, lakini wakati huohuo wengi wao hawana uelewa unaohitajika kwa ajili ya kuifikia saada hiyo. Kwa karne kadha wa kadha, kutokana na kuwa na taswira isiyo sahihi kuhusu Mtume wa Uislamu, Ulimwengu wa Magharibi umejaribu kuitia doa sura halisi ya shakhsia huyo adhimu na asiye na mfano katika ulimwengu wa wanadamu, ili kwa njia hiyo kuwafungia watu njia ya uokovu. Lakini ni nani awezaye kuifanya dhahabu ionekane shaba?

Kwa mtazamo wa wataalamu wa Magharibi hivi sasa ufahamu na uelewa wa wakaazi wa upande huo wa sayari ya dunia kuhusu Uislamu na Mtume Mtukufu wa dini hiyo umeongezeka kwa kiwango fulani, na kila mwaka kuna mamia ya vitabu na makala zinazochapishwa katika nchi za Magharibi kuhusu Uislamu. Tab'an lengo la mazungumzo yetu haya si kutaka kuwatumia wanafikra wa Magharibi au Maorientalisti, yaani wataalamu wa masuala ya Ulimwengu wa Mashariki watusaidie kuthibitisha hadhi, utukufu na daraja aali aliyonayo Nabii wa rehma Muhammad SAW; hasha wa kalla. Lakini pamoja na hayo ni jambo lenye kutoa mguso kwa watu wengi kuelewa jinsi baadhi ya wanafikra mashuhuri wa Magharibi na hata wa Mashariki walivyokiri kuhusu hakika ya shakhsia ya Bwana Mtume SAW. Mwenyezi Mungu Mtukufu amemsifu Mtume wake kwa sifa bora kabisa, na kwa sababu ya akhlaqi zake adhimu akamfanya kuwa ruwaza ya kufuatwa na kigezo cha kuigwa na walimwengu wote.

Leo Nikolayevich Tolstoy, aliyezaliwa mwaka 1828 na kuaga dunia katika mwaka 1910 ni mwandishi mashuhuri wa Kirusi aliyeandika kitabu kiitwacho"Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu". Katika kitabu hicho Tolstoy ameyapinga madai ya watu waliomtuhumu Bwana Mtume kwamba alikuwa mtu mwenye kupenda kutawala, na badala yake amemtukuza kwa kumpa heshima na taadhima nabii huyo wa rehma. Katika sehemu moja ya kitabu hicho mwandishi huyo amezungumzia baadhi ya hadithi za Bwana Mtume, na katika sehemu nyengine ya kitabu hicho zimechapishwa baadhi ya barua alizokuwa akiandikiana Leo Tolstoy na baadhi ya watu, barua ambazo zinadhihirisha wazi mtazamo aliokuwa nao mwandishi huyo wa Kirusi kuhusu shakhsia tukufu ya Nabii Muhammad SAW na dini aliyokuja nayo ya Uislamu.

Moja ya barua hiyo ni ile iliyoandikwa na Bi Yalna Vakilava ya kutaka ushauri kwa Tolstoy. Barua hiyo inasema:" Mimi ni mama mwenye mapenzi makubwa na yasiyo na kifani kwa wanawe; na hivi ninavyokuandikia barua hii macho yangu yanabubujikwa na machozi. Hivi sasa akili zinaanza kuniruka na hakuna jengine nililoweza kufikiria ghairi ya kukuandikia wewe barua. Watoto wangu wawili wa kiume, mmoja anasoma chuo kikuu na mwengine ni afisa wa jeshi. Wao ni Wakristo lakini wamekuwa na imani kwamba inapasa waiache dini yao na kuingia kwenye Uislamu na kuwasaidia Waislamu...ni kitu gani ninachoweza kufanya mimi? Ni wewe tu ambaye kutokana na elimu yako na uhodari wako unaweza kunipatia njia ya kulitatua tatizo hili. Naomba unitulize kwa maneno ya kuliwaza."

Barua ya majibu aliyoandika Leo Tolstoy kwa mama huyo aliyejawa na wasiwasi inasema hivi: "Mwanadamu akiwa ndiye kiumbe bora ulimwenguni na mwenye vipawa vya batini na vya kustaajabisha anastahiki heshima na haki ya kuchagua njia na mwenendo wa maisha yake. Kwa sababu hiyo dini za mbinguni zinapaza sauti moja ya kumtetea mwanadamu na heshima yake, zinasimama dhidi ya njia potofu na kubainisha njia mwafaka ya kufuatwa. Kutokana na kuwa na misingi ya pamoja ya kimaanawi na kimaadili, dini hizo zina hazina kubwa ya uongofu, miongozo ya kiakhlaqi na thamani za kiutu. Lakini pamoja na hayo ni dini gani kati ya zote iliyokamilika zaidi na kusalimika na upotoshwaji na kwenda pogo? Baada ya maelezo yake hayo na kuuliza suali hilo, Tolstoy anaisifu dini ya Uislamu na kusema, anavyoitakidi yeye dini hiyo inamfikisha mtu kwenye kilele cha izza na kumwonyesha njia sahihi ya maisha.

Akiendelea kutoa maelezo katika barua yake ya majibu kwa Bi Yalna Vakilava, Leo Tolstoy anasema:"Ikiwa wanaochafanya watoto wako ni kwa ajili ya njia hii ya fikra ya dini za mbinguni basi mimi ninawapa hongera; na katika fikra hii niko pamoja na wao kwa udhati wa moyoni. Mimi ninayekuandikia maneno haya ni Mkristo. Japokuwa nimeyazoea mafundisho ya Ukristo kwa muda wa miaka mingi, inanibidi niseme kwamba dini ya Uislamu na mafundisho ya Muhammad pamoja na sifa yalizonazo, na kutokana na jinsi yanavyojionyesha wazi kabisa ni dini iliyokamilika zaidi na yenye thamani zaidi kuliko Ukristo. Mambo iliyonayo dini ya Uislamu hayawezi kulinganishwa na Ukristo. Kama tutachukulia mfano kwamba kuna uwezekano kwa kila mtu wa kuchagua moja kati ya dini mbili za Uislamu na Ukristo, na kumwabudu Mungu kulingana na dini hiyo inabidi kabla ya jambo lolote mtu atafakari na kuelewa kwamba kuwaabudu waungu kadhaa ni jambo lisiloyumkinika, na ufanyaji ibada wa namna hiyo unapingana na mafundisho ya msingi ya dini za mbinguni. Hali ya kuwa kinyume na hivyo kuna dini ya Uislamu ambayo ndani yake anaabudiwa Mungu mmoja tu peke yake na si mwenginewe. Hoja hii pekee inaufanya Uislamu kuwa bora kuliko Ukristo. Katika kufanya uchaguzi huo, bila ya shaka mtu yeyote mwenye akili timamu na ufahamu wa kutosha atauchagua Uislamu tu na si dini nyengine yoyote. Katika shakhsia wa dini ya Uislamu, wa kwanza kabisa ni Mtume Muhammad SAW ambaye katika mafundisho yake inashuhudiwa misingi ya mafundisho ya dini zote takatifu, na mafundisho hayo yanalingana na kukaribiana na mengi ya ukweli wa dini ya Ukristo.

Wapenzi wasikilizaji mwandishi huyu mkubwa wa Kirusi alikuwa akizungumza kila mara na marafiki zake pamoja na jamaa zake wa karibu kuhusu dini ya Uislamu na shakhsia ya kipekee na isiyo na kifani ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Tabibu wa Tolstoy aitwaye Mokovitski ameandika yafuatayo katika kitabu cha kumbukumbu zake:"Katika mazungumzo yangu niliyofanya na Tolstoy tarehe 13 Machi mwaka 1903 aliniambia hivi:"Muhammad SAW akiwa ni Mtume, kila mara na kila mahala yuko katika nafasi ya juu zaidi kuliko Mitume wengine wa Mwenyezi Mungu. Muhammad hakumfanya mwanadamu aonekane duni, wala hakumkweza kwa kumfikisha kwenye daraja ya Mungu; yeye mwenyewe pia hajifanyi kuwa na sifa za kumkaribia Mwenyezi Mungu wala kukaa mahali pa Mungu. Waislamu hawamwabudu mwengine yeyote ghairi ya Allah, na Muhammad ni Mtume wao." Mwisho wa kumnukuu Mokovitski.

Baada ya miaka mingi ya utafiti na uhakiki Leo Tolstoy alitamka bayana haya yafuatayo:" Kwangu mimi, kuwa mtu wa Muhammad kuna thamani zaidi kuliko kutukuza msalaba, na katika ulinganishaji huu mimi ninaichagua dini ya Muhammad. Bila ya shaka yoyote kutokana na dini ya Muhammad kukubaliana na akili na hekima, katika zama zijazo itakuja kuenea ulimwengu mzima. Mtume wa Uislamu halinganii kitu kingine ghairi ya Mungu Mmoja na upendo".

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kukomea hapa na kukuageni hadi juma lijalo inshallah tutakapokutana tena katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki...

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …