Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 19 Februari 2013 15:52

Nabii wa Rehma (6) + Sauti

Nabii wa Rehma (6) + Sauti

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Kwa furaha na moyo mkunjufu nakukaribisheni kujiunga nami tena katika sehemu hii ya sita ya kipindi hiki kinachodondoa machache kati ya mengi  yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu lakini wenye insafu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Ni matumaini yangu kuwa mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa kipindi kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Katika kurasa za historia, kwenye laha, sahifa na mawe yaliyonakishiwa kuna maandishi na athari zilizosalia tokea enzi za kale za maisha ya wanadamu za majina na habari za watawala wakubwa wakubwa na wafalme wasio na idadi ambao walipata ushindi mkubwa na wa kutajika katika enzi za falme na tawala zao. Hao ni watu waliokuwa wakijali nafsi zao tu walioghariki kwenye starehe, raha na anasa za maisha waliyoyaponda kwenye makasri yao ya makuu na fahari kubwa. Mabaki ya majengo ya aushi na yenye adhama yaliyoko Misri, Iran, Ugiriki na Rumi ni kumbukumbu zilizoachwa na wafalme na watawala hao waliokuwa na uchu wa dunia. Pamoja na hayo licha ya jitihada zisizo na kifani walizofanya watawala na wafalme hao waliotajika ili kutaka wabakie daima katika historia, lakini kadiri zama zilivyopita ndivyo athari na majina yao yalivyozidi kusahauliwa. Yale makasri ya fahari waliyoyajenga na yaliyosimama kwa nguvu za maelfu kwa maelfu ya vibarua waliovumilia sulubu na mateso hayakuweza kuyafanya majina ya wafalme hao yaendelee kutajwa vinywani mwa watu. Kumbukumbu za watu hao waliovuma na kutajika kwa nguvu na madaraka zilifutika katika dunia hii sambamba na kuondoka kwao. Na kama kuna mahala ambako athari na majina yao yanatajwa, basi si kwa fahari wala kujivunia.

Jina na athari inayobakia milele katika historia wapenzi wasikilizaji ni ya yule mtu ambaye ameuachia ulimwengu athari za kudumu daima dawamu zinazomtengenezea mwanadamu njia ya kheri na saada. Mitume na manabii wa Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa watu hao. Waja hao wateule walishikamana na njia ya haki kwa uthabiti na ujasiri, na kwa amri ya Mola wa ulimwengu walifanya juhudi na idili isiyo na kifani ili kuwagomboa na kuwatoa wanadamu kwenye minyororo ya ujinga na dhulma. Kati ya viongozi wakuu hao wa wanadamu ni Nabii Muhammd SAW mtume mtukufu wa Uislamu ambaye nuru ya nyota yake imetanda ulimwenguni kote. Kwa sababu alikuja na risala na ujumbe uliokamilika wa kudhamini kheri na saada ya mwanadamu kiasi kwamba kudhihiri kwake kuliipambanua njia ya haki na ile ya batili.

Kama tulivyowahi kuashiria katika sehemu ya kwanza hadi ya tano ya kipindi hiki cha "Yaliyosemwa na Wenye Hekima Kuhusu Nabii wa Rehma" kuna mengi yaliyosemwa kuhusu shakhsia ya Bwana Mtume SAW na mchango wa kuibadilisha historia ya mwanadamu uliotolewa na mbora huyo wa viumbe. Tumejionea wenyewe kwamba hata miongoni mwa wasiokuwa Waislamu kuna watu, na si wachache walioamua kuweka kando ukereketwa na utashi wa kibinafsi na kufanya utafiti kwa insafu ili kujua ukweli kuhusu nabii huyo wa rehma na dini aliyokuja nayo. Miongoni mwa watu hao ni Constantin Virgil Gheorghiu mwandishi na mtafiti raia wa Romania aliyezaliwa Septemba mwaka 1916 na kuaga dunia mwezi Juni mwaka 1992. Yeye anaitakidi kwamba Muhammad ni Mtume anayehitaji utafiti mpya kuweza kumtambua. Yeye anasema: "Muhammad Ibn Abdillah SAW ni mtu aliyepata tabu na mateso na aliyekuwa akiwaonea watu uchungu na huruma kwa maana yake halisi. Kati ya watu mashuhuri waliopata tabu na machungu wakati wa utotoni na mwanzoni mwa kipindi cha ujana wao huwezi kumpata yoyote aliyepata machungu, ghamu na majonzi kwa ajili ya wanadamu mithili ya Muhammad...Qur'ani nayo imeusia kuwajali mayatima na masikini na kuwapa msaada, na kuwataka wafuasi wa mtukufu huyo wapendane na kuoneana huruma".

Baada ya kufanya utafiti wa kina Virgil Gheorghiu alibainikiwa na nukta hii, kwamba Mtume wa Uislamu, akiwa ni mja na mjumbe wa Mwenyezi Mungu ana shakhsia ya kustaajabiwa, na kuna ulazima kwa watu wa Ulaya, Wakristo na watu wote kuielewa vyema historia ya maisha yake, kujitolea kwake na jitihada alizofanya. Kutokana na mtazamo huo aliamua kuandika kitabu kwa lugha ya Kifaransa, alichokipa jina la:" Muhammad, Mtume ambaye inapasa kumjua upya". Katika kitabu hicho Virgil Gheorghiu ameandika hivi:"Mimi sikubaliani na wale watu wa Ulaya wanaomtazama Muhammad kama mtangazaji wa sheria za dini tu. Katika ujumbe wa utume wa Muhammad vinashuhudiwa vitu vya kuvutia mno kwa mtazamaji mwenye insafu. Ujumbe wa Muhammd si ujumbe wa kidini tu bali ni ujumbe adhimu wa kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi. Kuanzisha harakati kama hii katika ardhi mithili ya Bara Arabu iliyokuwa imezama kwenye mila na desturi za kijahilia, tena basi katika kipindi cha karne 14 zilizopita ni tukio la ajabu na lisilokuwa la kawaida, na hili ni jambo ambalo aliweza kulifanya Muhammad katika ujumbe wake adhimu. Muhammad alikuwa mletaji wa dini mpya na vile vile kiongozi wa harakati kubwa katika jamii ya wanadamu, na ni kwa sababu hiyo alikuwa akiteremshiwa sheria za Mwenyezi Mungu hatua kwa hatua".

Mtafiti huyu wa Kiromania anaongeza kuwa:"harakati adhimu ambayo iliongzowa na Muhammad SAW ilileta vuguvugu na mwamko kwa Waarabu kwa kadiri kwamba katika kipindi cha chini ya nusu karne tangu hijra ya Mtume Waarabu walizifanya tawala kubwa za dunia ya kale ukiwemo utawala mkubwa wa ufalme wa Iran kuwa sehemu ya ardhi ya Uislamu. Huwezi kupata dini yoyote ile duniani iliyoenea kwa kasi kubwa kama hii. Na sababu yake ni msingi huu, kwamba Muhammad SAW alikuwa na fikra ya umoja kwa jamii ya wanadamu wote. Mtume alikuwa akizungumza kwa lugha ya Qur'ani, kwamba jamii ya wanadamu ni umma mmoja na hitilafu zilizopo baina ya mataifa zinatokana na dhulma, ufisadi na uonevu".

Constantin Virgil Gheorghiu, anaielezea dini ya Muhammad SAW kuwa ni muongozo mkuu wa elimu, maarifa na uelewa. Anasema:" Mimi ninawapa hongera Waislamu kutokana na wahyi wa kwanza alioteremshiwa Muhammad ambapo suala la kutafuta elimu na maarifa limepewa umuhimu kiasi hiki. Huko nyuma, na kwa kutegemea aya za mwanzo za Suratul Alaq alizoteremshiwa Mtume, baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu walitangaza kwamba kama ambavyo ni wajibu kwa Muislamu kusali na kufunga, kujifunza elimu ni jambo la wajibu kwake pia".

Wapenzi wasikilizaji maneno haya yenye ujumbe unaohitajia tafakuri ya kina uliotolewa na msomo huyu asiye Muislamu lakini mwenye insafu kutoka Romania ndiyo yanayotukamilishia sehemu hii ya sita ya kipindi hiki cha "Yaliyosemwa na Wenye Hekima Kuhusu Nabii wa Rehma". Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa ya Mola nakuageni kutoka hapa studio huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu

 

 

 

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …