Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 22 Januari 2013 14:37

Nabii wa Rehma 5 + Sauti

Nabii wa Rehma 5 + Sauti

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Ni furaha iliyoje kupata fursa na wasaa wa kuwa nanyi tena katika kipindi hiki kinachodondoa machache kati ya mengi yaliyosemwa kwa insafu na wasomi, waandishi na wanafikra wasio Waislamu kuhusu Nabii wa rehma, mbora wa viumbe na mwalimu wa wanadamu wote, Muhammad SAW. Ni matumaini yangu mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa sehemu hii ya tano kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Profesa Carl Ernst ni mtaalamu na mhadhiri wa Taaluma za Kiislamu katika Chuo Kikuu cha North Carolina nchini Marekani. Mtaalamu huyo anasema:" Mitume wa Mwenyezi Mungu wanahesabiwa kuwa watu wakamilifu zaidi, ambao Mwenyezi Mungu amewalinda na upotofu na machafu; na kwa sababu ghairi ya hivyo hawawezi kuwa walimu wa kiakhlaqi na kidini wa wanadamu. Ni kwa kupitia wahyi wa Mwenyezi Mungu tu ukweli hasa na mafundisho safi kuhusiana na ulimwengu na matukio yaliyopita na yajayo yanaweza kufikishwa kwa wanadamu. Kwa kutegemea hoja hii kudhihiri kwa kiongozi adhimu wa kidini mithili ya Muhammad SAW katika giza totoro la Bara Arabu ni ishara dhahiri ya rehma na uraufu wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu." Profesa Ernst amefanya utafiti mwingi kuhusu Uislamu na hivi sasa anaendelea na utafiti wa kihistoria juu ya dini hiyo. Yeye anauangalia zaidi Uislamu kwa mtazamo wa Irfani, yaani elimu ya kumfikia Mwenyezi Mungu kwa tafkira. Profesa Carl Ernst anaitakidi kwamba hakuna dini ambayo haikutendewa insafu zaidi kama Uislamu na kutazamwa kwa jicho baya na Magharibi. Ili kubadilisha mitazamo hiyo hasi ya Wamagharibi juu ya Uislamu na Mtume wa Uislamu, mwaka 2003 Profesa Ernst aliandika kitabu kiitwacho:" Following Muhammad: Rethinking Islam in the Contemporary World" yaani "Kumfuata Muhammad: Kuufikiri Upya Uislamu Katika Ulimwengu wa Zama Hizi". Katika kitabu hicho ameandika hivi:"Katika ulimwengu wa leo Uislamu unashambuliwa kutokea pande mbili na unakabiliwa na makali ya pande mbili za mkasi. Upande mmoja kuna maorientalisti walioko Ulaya na Marekani wenye ujinga na mtazamo mbaya juu ya Uislamu na ambao wanajaribu kutoa sura mbaya kuhusu Uislamu. Na upande mwengine katika nchi za Kiislamu kuna watu wenye misimamo ya kufurutu mpaka kama makundi ya al Qaeda, Taliban na Mawahabi ambao wanavipatia fursa vyombo vya habari vya Magharibi ya kueneza propaganda dhidi ya Uislamu. Wanaoumia katikati ya pande hizo mbili ni mamia ya mamilioni ya Waislamu wanaoishi katika ulimwengu wa leo. Wao hawana nafasi katika faharasa ya kambi ya ustaarabu wa Magharibi wala hawana mchango wowote katika fikra mgando na za utumiaji nguvu za mtu kama Bin Laden".

Kitabu kiitwacho "Kumfuata Muhammad" wapenzi wasikilizaji kimealifiwa katika faslu sita. Faslu ya tatu ya kitabu hicho yenye anuani ya "Maandiko Matakatifu ya Kiislamu"inahusu Qur'ani, Mtume na Uislamu. Katika faslu hiyo ujumbe anaotoa Profesa Ernst kwa Magharibi ni kwamba nyinyi mnaiangalia shakhsia ya Mtume wa Uislamu kutokea nyuma ya pazia la ujinga hali ya kuwa Mayahudi na Wakristo wa mwanzoni mwa Uislamu hawakuwa asilani wakimuelezea Mtume kwa sura kama hiyo". Mtaalamu huyo wa Magharibi ameendelea kuandika hivi:"Kuhusu shakhsia iliyokamilika na ya pande kadhaa ya Muhammad si insafu kumzungumza yeye kwa maelezo mafupi tu na tena yanayohusiana na baadhi ya matukio tu. Profesa Carl Ernst anasema:" Watu wote wanakubaliana kwa kauli moja kwamba Muhammad alikuwa mtu mwenye mvuto mkubwa na mashuhuri kwa ukweli na uaminifu, na kwa sababu hiyo akapewa lakabu ya Muhammad Muaminifu. Tangu alipokuwa katika rika la ujana alikubaliwa na watu wote kuwa ni 'hakam' yaani mwamuzi asiyependelea upande wowote.

Kwa mtazamo wa mwanafalsafa huyu wa Magharibi hakuna mgongano au mkinzano wowote kwa Bwana Mtume Muhammad SAW kuwa kiongozi madhubuti, imara na mwenye tadbiri na wakati huohuo kuwa dhihirisho la rehma na huruma. Anaendelea kusema kuwa muamala wa Muhammad ulikuwa wa namna moja kwa watu wote, wawe wenye mamlaka au watu wa kawaida, na mwenendo wake huo ukatoa mfano wa kuigwa wa haki na uadilifu".  Profesa Carl Ernst anasema yeye binafsi anaitakidi kwamba kati ya sifa kadha wa kadha zilizotajwa kumzungumzia mtu huyu mkubwa inapasa kuongeza pia sifa hii, kwamba yeye alikuwa dhihirisho na nembo ya juu kabisa ya uadilifu na uhuru wa kijamii. Anasema:" Imani na umaanawi wa Muhammad haumfanyi tu kuwa mwalimu wa akhlaqi bali unamdhihirisha pia kama nuru ya milele inayouangazia ulimwengu daima dawamu".

Suala la ndoa za Mtume wa Uislamu ni maudhui nyengine iliyozungumziwa katika kitabu kiitwacho: "Kumfuata Muhammad". Malalamiko dhidi ya ndoa za Bwana Mtume ni kitu kilichomshangaza Profesa Carl Ernst na kumfanya aandike hivi:"Wakristo, na hasa katika kulinganisha maisha ya ukapera ya Isa AS na ndoa za Muhammad wanalitumia suala hilo kipropaganda dhidi yake. Huenda sisitizo la mwanzoni la Wakristo kuhusu kuwa bikira bibi Maryam na mwenendo wa utakasifu wa maisha ya bibi huyo, umewafanya wazipinge ndoa za Nabii Muhammad. Hali ya kuwa kuishi maisha ya utawa kunaendelea kupungua Marekani na katika Ulaya ya kisasa. Katika jamii ya leo ya Magharibi ambapo vipindi vya matangazo ya biashara na utoaji burudani kwa umma vimejaa taswira za kusisimua matamanio ya kijinsia, mshangao wao juu ya ndoa za Mtume wa Uislamu unazusha masuali". Carl anasema:"Ukweli ni kwamba yeye alikuwa kiongozi mwenye taathira na vilevile mume na baba mwenye ghera na huruma. Akiwa Mtume na kiongozi wa kisiasa, wakati huohuo Muhammad SAW alikuwa akitekeleza majukumu kama baba na mume. Alikuwa na mafungamano makubwa na familia na watoto wake. Baada ya kufariki Khadija, Mtume Muhammad SAW alioa wake wengine kadhaa. Baadhi ya ndoa hizo zilitokana na sababu za kisiasa na zilikuwa na lengo la kuimarisha umoja na mshikamano wa kikabila. Licha ya kuwepo matatizo chungu nzima, kushughulikia masuala ya familia ilikuwa sehemu kubwa ya maisha ya Mtume."

Katika uhitimishaji wa faslu hiyo ya kitabu chake, Profesa Carl Ernst anasema:" Katika kipindi cha mwishoni mwa maisha yake, Muhammad alikuwa na mamlaka ya uongozi wa jamii kubwa. Yeye, ambaye alikuwa rehma kwa walimwengu aliungana na makabila yote ya Hijaz huko Bara Arabu. Muhimu zaidi ya yote ni kwamba mafundisho yake yaliyotokana na wahyi yalijenga mazingira ya utekelezaji amali za ibada zenye msisimko mkubwa, malengo adhimu ya kiakhlaqi na misingi muhimu ya kijamii, mafundisho ambayo yamekuwa na uthabiti mkubwa wa kubakia katika historia".

Hayo mliyoyasikia wapenzi wasikilizaji ndiyo niliyokuandalieni katika sehemu hii ya tano ya kipindi hiki. Nakuageni hadi juma lijalo panapo majaaliwa ya Mola katika siku na saa kama ya leo

 

 

 

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …