Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 14 Januari 2013 14:12

Nabii wa Rehma 4 + Sauti

Nabii wa Rehma 4 + Sauti

Amani ya Mwenyezi Mungu, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wasikilizaji wapenzi. Kwa furaha na moyo mkunjufu nakukaribisheni tena kuwa nami katika kipindi hiki kinachodondoa machache kati ya mengi yaliyosemwa kwa insafu na wasomi, waandishi na wanafikra wasio Waislamu kuhusu Nabii wa rehma, mbora wa viumbe na mwalimu wa wanadamu wote, Muhammad SAW. Ni matumaini yangu mtaendelea kuwa nami hadi mwisho wa sehemu hii ya 4 ya kipindi hiki kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

&&&&

Kwa miaka kadhaa sasa ujahilia mpya katika zama zetu hizi umekuwa ukizilenga kwa hujuma heshima na hadhi za walimu, walezi na viongozi wakubwa wa wanadamu hususan Mtume Mtukufu wa Uislamu Nabii Muhammad SAW. Kukaririwa vitendo hivyo huko Ulaya na Marekani kumewatia wasiwasi na jakamoyo wanafikra wenye adili na insafu na kuwafanya wajiulize, ulimwengu wa Magharibi unaelekea wapi? Ni kwa nini serikali na vyombo vya habari vya Magharibi vinashupalia na kung'ang'ania kuendeleza hujuma chafu za namna hii dhidi ya akhlaqi na thamani za kimaanawi?

Profesa Annemarie Schimmel, mwanamama wa Kijerumani na mtaalamu wa masuala ya Ulimwengu wa Mashariki ni mmoja wa wasomi na wanafikra wa Magharibi wenye adili na insafu. Yeye anaamini kuwa maudhi ambayo Wakristo wanawafanyia Waislamu hayatokani na busara wala kuwa na nadhari. Na sababu yake anasema kama ninavyomnukuu:" Muhammad SAW ni Mtume aliyeleta harakati ya kidini iliyofanikiwa zaidi katika sayari ya ardhi. Yeye ni ruwaza bora kabisa na kigezo cha kuigwa na kila mtu anayetaka kufikia njia ya saada. Katika kipindi cha zama zote hizi kuna watu wengi mno waliompa heshima na kutawasali kupitia kwake yeye. Yeye alipambika kwa lakabu bora na tukufu zaidi. Mtume huyu ataendelea hadi milele kuwa mfano mwema kwa ajili ya maisha."

Wapenzi wasikilizaji, shakhsia wakubwa katika watu, kwa kawaida hujulikana kupitia njia mbili. Ya kwanza ni kwa kuzitafakari athari na turathi wanazoacha, kama ambavyo Qur'ani Tukufu ni muujiza mkubwa zaidi wa Nabii Muhammad SAW na dhihirisho la ukweli wa utume wake na shakhsia yake ya kiroho na kimaanawi. Amma njia ya pili ni kwa kuzitalii athari za watu mashuhuri, wanafalsafa na wanafikra zinazowazungumzia shakhsia hao. Nabii Muhammad SAW alikuwa shakhsia wa kipekee kabisa mwenye sifa maalumu za kimaanawi na ambaye ameuathiri mno ulimwengu kutokana na fikra na mitazamo yake. Na huo ni ukweli na hakika isiyoweza kupuuzwa na wanafikra wenye busara, hekima na insafu. Bi Schimmel, anamuelezea Bwana Mtume kuwa ni "jua lenye kutoa nuru" na katika kitabu chake kiitwacho" Na Muhammad ni Mtume Wake" kwa kimombo 'And Muhammad Is His Messenger' ameandika hivi:" Mwenyezi Mungu ameifanya nuru yake isiyo na mpaka wa mahala wala zama iuangazie ulimwengu kupitia kwa Mtume. Yeye ni taa itoayo mwanga ambayo imetoka kwenye ulimwengu wa ghaibu na kudhihiri katika ulimwengu wa maumbile. Nuru hiyo ilianza kudhihiri kupitia kwa Adam na kufuatiwa na Mitume wengine na hatimaye ikakamilika kupitia kwa Muhammad na kuuangazia ulimwengu mzima wa maumbile". Kisha baada ya kueleza hayo Profesa Annemarie Schimmel anazivuta hisia na akili za wasomaji wake kwenye tafakuri kwa kusema:" Japokuwa Mtume alifikia daraja ya juu ya utukufu wa kimaanawi lakini aliendelea kubakia kuwa mja wa Mola wa haki."

Katika kitabu chake hicho kiitwacho "Na Muhammad ni Mtume Wake", Profesa Schimmel anabainisha majonzi na masikitiko yake kuhusu chuki na uadui wa Magharibi kwa mjumbe huyo wa Mwenyezi Mungu. Katika kitabu chake hicho amejaribu kutoa picha na taswira sahihi ya kiutu na kimaanawi ya Bwana Mtume ili kusahihisha dhana na uoni usio sahihi wa Wamagharibi juu ya mbora huyo wa viumbe, na kumuelezea Nabii Muhammad SAW kuwa ni Mtume wa rehma na upendo. Katika faslu moja ya kitabu chake, Bi Schimmel ameandika hivi:" Mtu ambaye ametumwa na Mwenyezi Mungu kuwaelekeza watu kwenye uongofu anapaswa yeye mwenyewe awe mja mteule na mwenye sifa aali na tukufu. Muhammad, tangu utotoni mwake alijitenga na mila na desturi chafu za kuabudu masanamu zilizokuweko Makka na hakuwa akichanganyika na watoto wa rika lake katika michezo yao ya kitoto. Kwa hakika kumfuata Muhammad SAW kunatokana na umuhimu huu, kwamba yeye hakuwahi kuteleza na kufanya makosa na wala hakuruhusu vumbi la madhambi litande kwenye roho na moyo wake safi. Muhammad alikuwa alikuwa mtu aliyekamilika, aliyeweza kujidhibiti na ghariza, shahawa na matamanio ya nafsi. Katika wakati wote wa maisha yake alitekeleza mafundisho ya Mwenyezi Mungu kwa fikra na amali sahihi na kumfanya shetani asalimu amri mbele ya irada yake isiyoshindika. Sifa za Muhammad zilikuwa za kipekee kiasi cha kuwafanya wataalamu na wanazuoni wasisitize kwamba katika kuienzi na kuitukuza daraja aali ya mtukufu huyo haifai kumlinganisha yeye na wanasiasa, watawala na watu wenye vyeo vya kidunia".

Katika kipindi chote cha uhai wake wote Profesa Annemarie Schimmel, ambaye alizaliwa mwaka 1922 na kuaga dunia mwaka 2003 alikuwa na mapenzi makubwa ya ustaarabu na utamaduni wa Kiislamu katika sura na madhihirisho yake yote. Aliandika vitabu na makala zaidi ya 100 kuhusu utamaduni na irfani ya Kiislamu na pia kuhusu shakhsia mashuhuri wa Ulimwengu wa Kiislamu. Mnamo mwaka 1961, Profesa Schimmel alianza kufundisha Taaluma za Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Bonn nchini Ujerumani. Na kuanzia mwaka 1967 hadi mwaka 1992 alipostaafu alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani akiongoza kitengo cha Utamaduni wa India na Uislamu. Akiwa katika chuo hicho Bi Schimmel alikuwa akifundisha irfani na fasihi ya Kiislamu. Baada ya utafiti na uhakiki wa kina kuhusu utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu, msomi huyo mashuhuri wa Kijerumani aliuelezea Uislamu kuwa ni tunu adhimu iliyoletwa na Bwana Mtume. Kuhusu sumu na propaganda chafu za vyombo vya habari vya Magharibi dhidi ya Uislamu, Profesa Schimmel anasema:"Inanisikitisha sana kuona duru za Magharibi zinaitazama dini ya Kiislamu kwa jicho baya. Uislamu una hadhi ya juu na inapasa usomwe na kuhakikiwa kwa umakini zaidi. Dini ya Muhammad imezivutia nyoyo za mamilioni ya watu, na ni dini ya amani, utulivu na uadilifu. Dini hii inalaani ugaidi na kuua watu", mwisho wa kumnukuu. Msomi na mwanafikra huyo mwenye insafu alibainisha hadhi na heshima kubwa aliyokuwa akimpa Nabii wa rehma na huruma Muhammad SAW kwa kutumia lugha ya maneno mufti na murua pale aliposema hivi katika utangulizi wa kitabu chake:" Haya ni matunda ya miaka 40 ya mapenzi yangu kwa shakhsia ya Mtume wa Uislamu. Hamu yangu juu ya suala la kumuenzi na kumpa heshima Mtume na daraja yake aali na kuyaakisi hayo katika fasihi na hasa mashairi ilinifanya niandike makala kadhaa. Mchapishaji wa Kijerumani wa vitabu vyangu alinishajiisha kuzikusanya makala hizo katika sura ya kitabu na kuzungumzia kwa ufafanuzi kumuenzi kwangu Mtume na kubainisha sifa na mazuri yake."

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu umemalizika, nami sina la ziada ghairi ya kukuageni hadi tutakapokutana tena katika kipindi kingine katika siku na saa kama ya leo inshallah

 

 

 

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …