Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 12 Januari 2013 10:51

Nabii wa Rehma 3 + Sauti

Nabii wa Rehma 3 + Sauti

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Ni matumaini yangu kuwa hamjambo popote pale mlipo. Nakukaribisheni kwa furaha na moyo mkunjufu kujiunga nami katika sehemu hii ya tatu ya kipindi hiki  kinachodondoa yale yaliyosemwa na wasomi na shakhsia mbalimbali wasio Waislamu kuhusu Mtume wa Mwisho wa Allah, mbora wa viumbe na Nabii wa rehma Muhammad SAW. Nakutafadhalisheni muendelee kuwa nami hadi mwisho wa kipindi chetu kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.

Baada ya kupita takribani karne sita tangu zama za Nabii Isa Masih AS, alibaathiwa na kupewa Utume nabii ambaye aliwaletea walimwengu ujumbe wa Tauhidi na wito wa upendo, uadilifu na heshima ya mtu kulingana na mafundisho ya wahyi. Mjumbe huyo wa Mwenyezi Mungu ni yule mja aliyebarikiwa mno ambaye kuja kwake kulibashiriwa na Isa AS. Jina la mtume huyo ni Muhammad SAW na ndiye aliyehitimisha silsili ya manabii wa Mwenyezi Mungu. Yeye aliwaenzi na kuwataja kwa wema Mitume wa kabla yake na akasadikisha risala za utume wao. Nabii Muhammad SAW alimpwekesha na kumtukuza Mola Muumba wa ulimwengu na kuzivunja hoja na itikadi za watu juu ya waola na miungu bandia. Historia imeshuhudia baadhi ya viongozi wenye taasubu wa Kanisa ambao walidai kwamba mafundisho ya Mtume huyo wa mwisho yanapingana na yale yaliyofunzwa na Nabii Isa AS na kwa hivyo wakaamua kuyapiga vita mafundisho ya dini tukufu ya Uislamu. Lakini kuanzia kipindi cha mwishoni mwa karne ya 18 miladia hadi sasa wamejitokeza baadhi ya watafiti na shakhsia mashuhuri wa Ulaya ambao wamekuja na mitazamo na uoni tofauti kuhusu Nabii wa rehma Muhammad SAW mitazamo ambayo inapasa kuzingatiwa. Johann Wolfgang von Goethe, malenga mashuhuri wa Kijerumani aliyeishi katika kipindi cha kati ya karne ya 18 na 19 amemzungumzia Bwana Mtume SAW katika athari na maandishi yake ya kwanza kwamba mtukufu huyo ni shakhsia adhimu aliyekuwa na mvuto usio wa kawaida wa kifikra na kimaanawi. Mnamo katikati ya karne ya 19 Thomas Carlyle, mwanafalsafa na mwanahistoria wa Scotland alitoa hotuba mashuhuri mjini London chini ya anuani ya semayo "Kuhusu Mashujaa" kwa kimombo "On Heroes". Katika hotuba zake hizo Carlyle alimsifu Mtume wa Uislamu akimuelezea kuwa ni mtu sharifu, mtukufu na adhimu katika historia na akaikosoa mitazamo ya chuki na ya kiadui ya Wamagharibi kuhusu Bwana Mtume Muhammad SAW na dini aliyokuja nayo.

Katika zama hizohizo wataalamu wa masuala ya Mashariki kutoka barani Ulaya wanaojulikana kitaalamu kama Orientalists au Mustashriqin waliingia katika ardhi za Ulimwengu wa Kiislamu na kuuelewa kwa karibu ustaarabu, utamaduni na itikadi za Waislamu. Lakini wengi miongoni mwao, badala ya kuandika ya kweli na kwa insafu waliathiriwa na uoni na mtazamo hasi waliokuwa nao tokea kabla na kuandika mambo yasiyowiyana na ukweli juu ya utamaduni na mafundisho ya Kiislamu. Kwa hakika kilichofanywa na watu hao ilikuwa ni kuendeleza kazi ileile iliyoanzishwa na Makasisi ya kukabiliana na Uislamu.

Pamoja na hayo hamu ya utambuzi wa irfani ya Kiislamu na mila na desturi za Ulimwengu wa Mashariki ilianza kushuhudiwa kidogo kidogo barani Ulaya. Kutokana na hamu hiyo Uislamu ukaanza kuelezewa kama dini ya fitra na maumbile, yenye fikra safi na angavu zinazoambatana na thamani za kimaanawi. Nchini Ujerumani, malenga na mshairi mashuhuri wa mashairi ya Kijerumani Rainer Maria Rilke, alikuwa mmoja wa watu walioguswa na kuathiriwa mno na mafundisho ya Nabii Muhammad SAW. Yeye aliuelezea na kuusifu Uislamu kuwa ni dini ambayo wafuasi wake wana mahusiano ya moja kwa moja na Mwenyezi Mungu, na wala hawahitajii wasita au mwokozi kwa ajili ya kumfikia Yeye. Katika miaka ya baada ya muongo wa 1950 wataalamu wa Elimu za Kiislamu barani Ulaya pamoja na wale wa masuala ya Ulimwengu wa Mashariki waliacha kushupalia mitazamo ya chuki na taasubu ya Magharibi juu ya Uislamu na kuanza kutalii vyanzo na marejeo ya asili ya dini hiyo. Baada ya wataalamu na waandishi hao kuitarjumu Qur'ani Tukufu kwa lugha zao za asili walifikia natija kwamba kinyume na imani na mitazamo iliyopo, Muhammad SAW, alikuwa shakhsia adhimu, sharifu na asiye na kifani.

Kutokana na utambuzi mpya waliopata kuhusu Uislamu na ili kuwa na uelewa bora zaidi wa thamani za dini hiyo wasomi waliokuwa na insafu na hekima waliamua kuzihakiki na kuzifanyia utafiti mpya baadhi ya fikra za kidini na kijamii za Uislamu. Ni kwa sababu hiyo maandiko ya baadhi ya wanazuoni wa Ulaya na wa masuala ya Ulimwengu wa Mashariki walioalifu vitabu na makala mbalimbali kuhusu Bwana Mtume katika miaka ya karibuni yameakisi zaidi ukweli halisi kulinganisha na athari za wasomi na waandishi wa kabla yao. Kitabu kiitwacho "Muhammad, Mtume na Mtawala Mweledi" kwa kimombo "Muhammad, Prophet and Statesman" cha William Montgomery Watt ni moja ya athari maarufu zaidi ya utafiti huo.

Watt, alikuwa profesa katika Chuo Kikuu cha Edinburgh nchini Uingereza wa Taaluma za Kiislamu na lugha ya Kiarabu na pia mtaalamu wa Masuala ya Ulimwengu wa Mashariki. Uga wa asili wa utafiti aliofanya msomi huyo ulikuwa ni kuhusu Sira ya Mtume, Tafsiri ya Qur'ani, Falsafa, Irfani na Historia ya Ulimwengu wa Kiislamu. Lilikuwa tukio lililomtokezea kwa bahati katika mwaka 1937 ndilo lililomtia hamu na shauku Watt ya kuuhakiki Uislamu ambalo ni kuwa na mpangaji nyumbani kwake aliyekuwa mwanachuo Muislamu kutoka Pakistan. Kujuana na kijana huyo ulikuwa mwanzo wa yeye kuitambua dini ambayo hakuwa na uelewa nayo wowote. Baada ya kupata uelewa wa mafundisho aali ya Uislamu William Montgomery Watt, alianza kufanya utafiti kuhusu maisha ya Mtume. Mnamo mwaka 1953 alialifu kitabu kiitwacho "Muhammad akiwa Makka" na mwaka 1956 akaandika kitabu kingine alichokiita "Muhammad akiwa Madina" na kisha baadaye akatayarisha muhtasari wa vitabu hivyo viwili kwa kitabu chenye anuani ya "Muhammad, Mtume na Mtawala Mweledi". Watt anasema:"Tangu miaka 40 iliyopita hadi sasa, katika maandishi yangu yote kuhusu Muhammad nimekuwa nikisisitiza juu ya nukta hii, kwamba Muhammad amesema kweli katika maneno yake kuwa Qur'ani si usanifu wake yeye bali imefunuliwa kwake kwa njia ya wahyi kutokea ulimwengu wa juu.... Tangu mwaka 1953, wakati nilipoandika kitabu cha 'Muhammad akiwa Makka' nimekuwa muda wote nikiitakidi kwamba Qur'ani ni maneno ya Mwenyezi Mungu".

Athari na maandishi ya Watt yamepongezwa na Waislamu na hata wamezitarjumu athari zake kadhaa. Japokuwa watafiti wa Kiislamu kutoka Iran na nchi za Kiarabu wamezifanyia ukosoaji athari na maandishi ya Watt lakini wote wanakubaliana kwa kauli moja kuwa mtaalamu huyo alikuwa na insafu na amekiri kuhusu makosa waliyofanya Maorientalisti waliomtangulia na pia kuhusu sifa aali za shakhsia adhimu na tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Watt anawausia watafiti wa masuala ya Ulimwengu wa Mashariki kwa kusema:" Ili tuweze kuwa na mawasiliano mazuri na Waislamu inatubidi tukiri kwamba tuna deni kwa utamaduni wa Kiislamu...Ni makosa kulificha suala hili na hii ni ishara ya ghururi na majivuno yasiyo na msingi". Kwa mtazamo wa Watt Waislamu wanawakilisha ustaarabu wenye mafanikio makubwa na kwamba katika kipindi hiki cha historia kuna ulazima kwa watu wa Ulaya kukiri kuwa wana deni kubwa mno kwa Ulimwengu wa Kiislamu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu umemalizika, nami sina la ziada ghairi ya kukuageni hadi tutakapokutana tena katika kipindi kingine inshallah katika siku na saa kama ya leo.

 

 

 

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …