Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 01 Januari 2013 10:40

Nabii wa Rehma (2) + Sauti

Nabii wa Rehma (2) + Sauti

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji. Ni furaha iliyoje kupata fursa na wasaa wa kuwa nanyi tena katika kipindi hiki kinachodondoa machache kati ya mengi yaliyosemwa kwa insafu na wasomi, waandishi na wanafikra wasio Waislamu kuhusu Nabii wa rehma, mbora wa viumbe na mwalimu wa wanadamu wote, Muhammad SAW. Natumai mtaendelea kuwa nami hadi tamati ya kipindi hiki kusikiliza niliyokuandalieni kwa juma hili.

*********

Wasomi na wanazuoni waelewa wanasema, kama ambavyo jua linaiangazia sayari ya dunia, na kutokana na athari ya mwangaza wake hupatikana siku mpya, katika uga wa kijamii pia hudhihiri mtume na nabii ambaye nuru ya kudhihiri kwake huangazia na kubainisha haki na hakika ya mambo. Kudhihiri na kuchomoza kwa siku kuna maana ya kuanza hali ya vuguvugu na msisimko mpya wa maisha. Kwa mtazamo wa watu weledi na waelewa, mitume pia ni watu wenye nafasi hiyohiyo katika hali mpya ya mabadiliko yanayopatikana katika shakhsia za wanadamu na jamii zao kwa ujumla. Kama ambavyo jua ndio nukta kuu ya mfumo mzima wa sayari kwa kimombo Solar System na ndio chanzo cha harakati na mabadiliko katika mfumo na majimui hiyo, mtume pia ndiye kitovu cha mvuto na uunganishi wa wanadamu na ndiyo chemchemi ya mageuzi, ukamilifu na utukukaji wa viumbe hao. Ni kwa sababu hiyo kuteremshwa kwa aya za wahyi kwa nabii na mjumbe wa mwisho wa Mwenyezi Mungu Muhammad SAW ulikuwa mwanzo wa harakati adhimu katika jamii ya wanadamu na chachu ya ustawi na ufanisi wa viumbe hao. Kutokana na nuru ya mafunzo ya Mtume huyo wa Allah watu waliokuwa hawajastaarabika wa zama za ujahilia walibadilika kikamilifu. Nabii Muhammad SAW aliwafanya watu wa Bara Arabu, ambao kutokana na mazingira yao ya kijiografia na ya hulka za kibedui walikuwa watu makatili na wasio na huruma, wabadilike kuwa watu wenye upendo, huruma na moyo wa ajabu wa kujitolea. Tarikh inasimulia kwamba katika moja ya vita vya Jihadi Waislamu kadhaa waliokuwa wamejeruhiwa walikuwa wameanguka huku na kule. Mmoja wa wapiganaji wa jeshi la Waislamu aliwapelekea maji ya kunywa majeruhi hao. Lakini kila mmoja alisamehe kuyanywa na kumwachia mwenzake ili apunguze kiu aliyonayo mpaka mwishowe wote hao wakakata roho na kufa shahidi huku midomo na koo zao zikiwa zimekauka kwa kiu. Kutokana na taathira ya mafundisho ya Bwana Mtume, vuguvugu na harakati ya kujifunza kusoma na kuandika kwa wote ikaanza ndani ya jamii, mpaka Waislamu wakaweza kufikia kilele cha elimu na taaluma muhimu za zama hizo. Kidogo kidogo skuli na vituo kadha wa kadha vya elimu vikaanzishwa. Kupitia fat-h na ukomboaji wa ardhi mbalimbali wimbi la elimu lilisambaa na kuenea mpaka maeneo ya mashariki na kusini mwa Ulaya. Na baadaye kutokana na athari za Vita vya Msalaba yaani Crusade War na uelewa waliopata Wazungu wa Ulaya juu ya fikra, maandiko na elimu iliyonawiri katika Ustaarabu wa Kiislamu, nuru ya elimu ikazagaa katika pembe mbalimbali za bara hilo. Hakuna shaka yoyote kuwa chanzo cha kuchanua na kustawi elimu hizo za wanadamu kilikuwa ni mafundisho ya Qur'ani Tukufu na miongozo adhimu ya Mtume wa Uislamu.

*******

Wasikilizaji wapenzi, wakati tunapozipitia kurasa za historia, katika baadhi ya vipindi tunakutana na maandiko na harakati zilizoonyeshwa na watu wasio na chembe ya busara na insafu juu ya Mtume wa Uislamu. Watu hao walioko mbali kabisa na misingi ya akhlaqi na mantiki wameamua kuiandama shakhsia adhimu na isiyo na kifani ya Mtume wa Allah kwa matusi na kejeli kwa dhana na tamaa kwamba wataweza kuzuia kuenea nuru ya dini aliyokuja nayo. Lakini kinyume na kundi la watu hao kuna watu ambao ni wanafikra na wasomi wenye insafu. Hao wanaiangalia shakhsia ya Bwana Mtume Muhammad SAW kwa jicho la staha na heshima na kuienzi nafasi na mchango wa mwalimu huyo mwenye huruma na mlezi wa jamii ya mwanadamu. R.F. Boodli, ni mwandishi wa Kikristo wa Magharibi ambaye ameguswa na kusikitishwa mno na tuhuma zilizotolewa na wenzake dhidi ya Qur'ani na Bwana Mtume. Katika kitabu chake kiitwacho "Maisha ya Muhammad" Boodli ameandika hivi:" Katika maajabu ya zama zetu ni kuwashuhudia watu duniani wanaojenga taswira ya kumtazama Muhammad kwa jicho baya. Mimi nimekisoma kitabu kilichoandikwa dhidi yake kuhusu maisha yake. Mwandishi wa kitabu hicho amezichafua kurasa za kitabu chake kwa maneno machafu na yasiyo na mantiki pasina kutueleza ni vipi mtu kama huyu ameweza kuleta kanuni na sheria za ustawi na ufanisi kwa ajili ya maendeleo ya wanadamu? Boodli anaendelea kueleza hivi katika kitabu chake:" Kuwafanya waarabu wa majangwani wawe watu watiifu ni moja ya kazi kubwa alizofanya Muhammad. Unaweza kusema kuwa kazi hii inalingana na muujiza mkubwa kabisa. Yeye alileta umoja na muungano wa kustaajabisha baina ya makabila yote ya Waarabu. Kwa kuyatafakari maisha ya Muhammad mtu atashangazwa na hikma na tadbiri aliyokuwa nayo, na atamhisi Muhammad yuko hai, na hafi katika zama zozote zile".

Wapenzi wasikilizaji Thomas Carlyle, mwanafalsafa na mwandishi wa Kikristo raia wa Uingereza naye pia anasema, matusi ya baadhi ya watu wenye taasubu na chuki dhidi ya shakhsia ya Mtume wa Uislamu yanatokana na udhaifu wa mantiki yao. Anasema: "Hii ni aibu kubwa mno kwa watu wa leo waliostaarabika wanaosikiliza maneno ya mtu anayedai Muhammad alikuwa mdanganyifu. Wakati umewadia wa kupambana na maneno ya aina hii ambayo ni pepe na ya kuaibisha. Kwa sababu ni karne kadhaa sasa ujumbe na dini aliyoleta Mtume huyu inaendelea kuangaza mithili ya taa inayowaka. Ndugu zanguni, je mumewahi kumwona mtu mwongo anayeweza kujenga dini kama hii iliyokamilika na kuieneza duniani? Naapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa tuhuma hizi ni za kustaajabisha mno. Kwa sababu mtu asiye na elimu, ambaye hana uwezo hata wa kujenga nyumba moja vipi anaweza kuipa jamii ya wanadamu dini mfano wa Uislamu?" Thomas Carlyle anaendelea kusema hivi:" Haya ni mazonge na masaibu makubwa kwa mataifa ya ulimwengu kukubali kirahisi tuhuma kama hizi pasina kuwa na nguvu ya hoja na busara. Mimi ninasema, ni muhali kwa mtu huyu mkubwa (Mtume Muhammad) awe amesema maneno yasiyo ya kweli. Historia ya maisha yake inaonyesha kuwa tangu zama za ujana wake alikuwa mtu mjuzi na mwenye tafakuri. Asili ya maisha ya Muhammad, mambo yake yote na sifa zake zote njema zimesimama juu ya msingi wa usafi na ukweli. Nyinyi angalieni maneno yake, hamwoni ndani yake hali fulani ya wahyi na miujiza? Mtu huyu ni mleta ujumbe kutoka kwa chemchemi isiyo na kikomo ya asili ya ulimwengu kwa ajili ya sisi wanadamu. Mwenyezi Mungu amemfunza mtu huyu adhimu elimu na hikma."

Wapenzi wasikilizaji, maneno hayo yaliyosemwa na Thomas Carlyle, mwanafalsafa na mwandishi aliyeishi kati ya mwaka 1795 na 1881 miladia kuhusu Nabii wa rehma Muhammad SAW ndiyo yanayotuhitimishia sehemu hii ya pili ya kipindi chetu hiki kwa juma hili. Nakuageni kutoka hapa studio hadi siku na saa nyengine kama ya leo panapo majaaliwa ya Mola.

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …