Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 04 Oktoba 2015 22:10

Uislamu na Mtindo wa Maisha (82)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (82)

Ni wakati mwingine wa kuwaletea mfululizo wa vipindi hivi vya Uislamu na Mtindo wa Maisha na hii ikiwa ni sehemu ya 82. Kipindi chetu leo kitakamilisha mjadala kuhusu kazi na pato halali na haramu katika mtindo wa maisha wa Kiislamu.

>>>


Kama tulivyosema hapo awali, mafundisho ya Uislamu katika nyanja mbalimbali yametilia mkazo ustawi wa kiroho na kimaanawi wa mwanadamu. Kwa msingi huo kazi na shughuli za kutafuta chumo na pato havipaswi kuzuia ustawi na ukamilifu wa kiroho wa mwanadamu. Japkuwa wanadamu wana uhuru na khiyari ya kuchagua kazi na shughuli wanayopenda, lakini Uislamu pia umeharamisha na kukataza baadhi ya kazi zenye madhara ya kimaada u kiroho au zinazosababisha madhara kwa jamii. Katika utamaduni wa Kiislamu mwanadamu haruhusiwi kutumia njia yoyote ile kwa ajili ya kupata riziki na pato; kwa msingi huo kai na shughuli zinazofanywa na Mwislamu zimewekewa masharti na mipaka katika mtindo wa maisha wa Kiislamu. Kwa mfano tu Mwislamu haruhusiwi kufanya kazi au biashara ambayo inahesabiwa kuwa ni aina fulani ya kusaidia au kushiriki katika dhambi, dhulma, unyang'anyi au kudhoofisha Waislamu. Katika mfumo wa thamani wa Uislamu kazi yoyote ile inapaswa kuwa halali na isipingane na hadhi na thamani za kibinadamu.
Kazi zilizopigwa marufuku na kukatazwa katika Uislamu zinaitwa kazi na haramu. Falsafa ya kuharamishwa kazi na shughuli kama hizo ni kwamba mbali na madhara yake ya kijamii na kiutamaduni, kazi na shughuli hizo husababisha mtikisiko na mmomonyoko wa kimaanawi na kiroho katika nafsi ya mwanadamu. Mkabala wake, kazi ambazo imeruhusiwa kuzifanya zinatambuliwa kuwa ni kazi safi na halali na kufanya kazi hizo kwa nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu humfanya mja apewe thawabu na ujira mwema. Kwa msingi huo ni lazima kwa Mwislamu kujua kazi za halali na haramu kabla ya kuanza shughuli yoyote na kutambua vyema au kwa ujumla sheria na kanuni za Kiislamu kuhusu biashara au miamala yake ili asije akapotoka.
Kutafuta rizki kwa njia za halali kumepewa umuhimu mkubwa katika Uislamu kwa kadiri kwamba Mtume Muhammad(saw) alikutambua kuwa ni wenzo wa kusamehewa baadhi ya dhambi. Mtukufu huyo anasema: "Baadhi ya madhambi hayafutiki isipokuwa kwa kufanya jitihada za kutafuta rizki." Kuhusu taathira za kutafuta rizki ya halali katika kukubaliwa maombi na dua, Mtume (saw) anasema: Mtu anayetaka dua yake ikubaliwe anapaswa kuhakikisha kwamba kazi na rizki yake ni halali; kwani kama mja atakula mali ya haramu au kuwadhulumu waja wengine, dua yake haiwezi kukubaliwa.
Miongoni mwa kazi haramu katika Uislamu ni kutafuta rizki kwa njia ya riba. Katika muamala wa aina hii mtu humpa mwingine mkopo kwa sharti la kurejesha mkopo huo na ziada ya riba juu yake. Kwa maneno mengine ni kuwa, mwenye pesa hukusanya peza ziada kutokana na mkopo huo anaompa mwanadamu mwenzake bila ya kufanya kazi yoyote ya uzalishaji au biashara. Riba ina athari mbaya sana na zenye uharibifu wa kiuchumi ikiwa ni pamoja na kudhoofisha uwezo wa kipesa na hatimaye kudhoofisha uwezo wa kiuchumi wa watu na jamii. Miongoni mwa sababu za kuharamishwa riba ni kuzuia ufisadi na kutumika vibaya fedha. Kwa sababu riba huwa sababu ya kulimbikizwa mali na utajiri sehemu moja tu na kwa maslahi ya matajiri na wenye fedha na hivyo kuzidisha ufa wa kimatabaka. Vilevile katika mfumo wa Kiislamu mwanadamu anakatazwa kukusanya mali na utajiri kwa njia za wizi, ulaghai, kughushi, hiana na kadhalika. Kimsingi Uislamu na sheria zake zimekataza na kuharamisha muamala wowote wa kilaghai.
Njia nyingine ya kazi na shughuli za haramu ni kununua au kuuza vileo. Imam Swadiq (as) anasema: Mwenyezi Mungu aliyeharamisha pombe ameharamisha pia thamani ya pombe", kwa maana ya fedha za kununua au kuuza pombe. Utumiaji wa vileo una madhara makubwa na yasiyoweza kufidika kwa mwili na roho ya mwanadamu na vilevile kwa jamii nzima. Ni kwa sababu hiyo kutayarisha, kuuza, kununua na kunywa vileo na pombe vimeharamishwa na kukatazwa. Vilevile Aya za Qur'ani tukufu zimeharamisha na kukataza kamari na mali inayopatikana kwa njia hiyo. Aya ya 90 ya Suratul Maida inasema: Enyi mlio amini! Bila ya Shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shet'ani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa.
Imepokewa kutoka kwa mjukuu wa Mtume wetu Muhammad(saw) yaani Imam Swadiq(as) kwamba amesema kuhusu aya hii kwamba: Maquraishi walikuwa wakicheza kamari mali, ahli na familia zao hivyo Mwenyezi Mungu akawakataza amali ya kamari.
Njia nyingine ya kukusanya pato na rizki kwa njia haramu ni ile ya kula na kutoa rushwa. Wanazuoni wa fiqhi ya Kiislamu wanasema rushwa ni wenzo wa kubatilisha haki au kuthibitisha batili na kwamba pesa inayopatikana kwa njia hiyo ni haramu. Wakati mwingine rushwa hutolewa au kupokewa na watu kwa kutumia majina mazuri na ya kuvutia kama zawadi, takrima na kadhalika. Hata hivyo tunapaswa kutambua kuwa kubadilishwa jina la rushwa na mlungula hakubadilishi hakika yake na pesa au mali inayopatikana kwa njia ya rushwa ni haramu. Tunasoma katika historia ya Uislamu kwamba siku moja mtu aliyejulikana kwa jina la Ash'ath bin Qais alikwenda nyumbani kwa Imam Ali bin Abi Twalib nyakati za usiku akiwa na chombo chenye halwa tamu kwa jina la zawadi na hadiya kwa ajili ya kupewa upendeleo. Imam alishtusha na kitendo hicho na kusema: Umefanya hivi kunirubuni? Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba lau ningepewa nchi saba na vilivyomo ili nimuasi Mwenyezi Mungu walau kwa kumnyang'anya mdudu chungu bua la shayiri kwa njia ya dhulma kamwe nisingefanya hivyo."(Nahjul Balagha,hotuba ya 125).
Njia nyingine ya kupata mali na pato kwa njia haramu ni kulimbikiza na kuhodhi bidhaa adimu na zinazohitajiwa na watu kwa matumaini ya bei ya bidhaa hiyo kupanda juu. Sheria za Uislamu zinasisitiza kuwa mali inayopatikana kutokana na bidhaa zilizohodhiwa na kulimbikizwa kwa ajili ya kupanda juu bei yake ni haramu kwa sababu maana ya kitendo hicho ni kutumia vibaya haja za watu kwa ajili ya kujifaidisha kwa njia isiyo halali.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa Uislamu umehimiza na kuungamkono kazi zote kama utabibu,kilimo, ufugaji, uhandisi na shughuli nyingine nyingi zinazokidhi mahitaji ya jamii. Na wakati huo huo dini hiyo ya Mwenyezi Mungu imekataza na kupiga marufuku kazi na shughuli zote zenye madhara ya kimaada na kiroho kwa watu na jamii kamam riba, rushwa, kuhodhi na kulimbikiza bidhaa, kughushi na kadhalika. Msikose kufuatilia wiki ijayo sehemu ya mwisho ya mfululizo huu wa Uislamu na Mtindo wa Maisha.

 

 

 

 

Zaidi katika kategoria hii: « Uislamu na Mtindo wa Maisha-83

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)