Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 05 Oktoba 2015 15:26

Uislamu na Mtindo wa Maisha-83

Uislamu na Mtindo wa Maisha-83

Kama tulivyosema katika makala zilizotangulia, mtindo wa maisha (Life style) ni mfumo wa maisha unaoumpa mtu, familia au jamii utambulisho makhsusi. Mtindo wa maisha unaweza kuwa jumla ya utendaji na mwenendo kamili na wenye uwiano wa mtu binafsi. Aina ya utumiaji wa bidhaa, maisha ya kila siku, aina ya mavazi, jinsi ya kuzungumza, burudani, jinsi ya kutumia wakati wa mapumziko, mapambo na dhahiri ya mtu, adabu na taratibu za kula na kunywa, usanifu majengo wa miji, masoko na nyumba na kadhalika vyote vinaakisi mtindo wa maisha wa mtu au jamii fulani. Mambo haya ya dhahiri, mienendo na kadhalika vinadhihirisha shakhsia zetu, itikadi zetu, imani zetu na vitu tunavyovitukuza katika maisha yetu ya kila siku. Kwa hakika mtindo wa maisha wa kila mtu au jamii hutokana na mtazamo wa mtu au jamii husika kwa mwanadamu na dunia. Kwa msingi huo haiwezekani kutenganisha baina ya mtindo wa maisha na itikadi na matukufu ya jamii au mtu husika. Kwa kawaida mtindo wa maisha ni jambo la khiari na linalochaguliwa na mtu au jamii kwa mujibu wa itikadi, imani na matukufu yake.
Mjadala wa mtindo wa maisha wa Kiislamu katika uwanja wa mtu binafsi na jamii ni miongoni mwa mijadala yenye umuhimu mkubwa, kwa sababu ni nguzo kuu ya utambulisho wa jamii, itikadi na mtindo wa maisha. inasikitisha kuona kwamba, jamii za Kiislamu hazijaweza kujenga uhusiano imara na unaokubalika baina ya itikadi na matukufu yao kwa upande mmoja na mtindo na mwenendo wao wa kimaisha katika masuala mbalimbali ya kijamii katika upande mwingine. Hii ni kwa sababu, mtindo wa maisha (life style) katika jamii nyingi za Waislamu umeathiriwa sana au hata kutekwa na utamaduni, ada na mielekeo isiyo ya Kiislamu na wakati mwingine inayopingana na Uislamu. Sababu za mpasuko na mmomonyoko huo zinaweza kuchunguzwa kwa kina katika makala au mfululizo mwingine wa vipindi, lakini inaonekana kuwa, miongoni mwa sababu muhimu za suala hilo ni uchache wa maarifa na elimu. Kwa maana kwamba, watu wengi katika jamii za Waislamu hawana utambuzi wa kutosha kuhusu utamaduni, desturi na mtindo wa maisha wa Kiislamu na thamani aali za dini hiyo na kwa msingi huo hawatumii vitu hivyo katika mienendo yao ya kila siku. Kwa sababu wakati watu wanaposhindwa kujenga uhusiano imara baina ya mtindo wao wa maisha na itikadi na imani zao kuna uwezekano baada ya muda watatupilia mbali kabisa itikadi na imani zao au kuzihoji na kuziona kuwa zimepitwa na wakati.
Hapana shaka kuwa kughafilika na kutojua mtindo wa maisha wa Kiislamu katika dunia ya leo kunazisukuma na kuzielekeza jamii za Waislamu katika upande wa utamaduni na mtindo wa maisha wa Kimagharibi. Hii leo ambapo nchi za Magharibi zinafanya kila liwezekanalo kufuta dini na imani za kidini katika maisha ya mwanadamu, kuna udharura wa kuarifisha ipasavyo mafundisho na mtazamo kamili wa Uislamu kuhusu maisha na mwanadamu. Uislamu ambayo ni dini kamili na inayohusu pande zote za maisha ya mwanadamu, umejumuisha na kukusanya mambo yote ya maisha kuanzia masuala ya familia, uchumi, jamii na siasa bali hata jinsi la kula, kutumia wakati wa mapumziko, safari na kwa ujumla jinsi mwanadamu anavyopaswa kuamiliana na nafsi yake mwenyewe, wanadamu wenzake, dunia na Mola Muumba wa vyote hivyo. Taratibu na mafunzo hayo ni majmui kubwa inayounda mtindo wa maisha wa Mwislamu. Mafunzo hayo yamesimama katika imani ya Tauhidi na utawala wa Mwenyezi Mungu Mola wa Ulimwengu na vilivyomo. >>>

Katika makala hii ya Mtindo wa Maisha wa Kiislamu tumefanya jitihada za kuarifisha mafundisho yenye mvuto ya Uislamu kuhusu mtindo na mwenendo wa maisha katika nyanja mbalimbali kwa kutilia maanani mafundisho ya Qur'ani na mwenendo na sira ya Mtume (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu. Tumezungumzia sifa za mtindo wa maisha na jinsi mtindo huo unavyotengenezwa na kuundika, mchango na nafasi za itikadi na imani za watu katika mtindo wa maisha yao, jinsi mwanadamu anavyopaswa kuamiliana na nafsi yake mwenyewe kuanzia jinsi ya kutafakari hadi namna ya mavazi na mazungumzo yake. Vilevile tumeeleza mafundisho ya Uislamu kuhusu jinsi mwanadamu anavyopasa kuamiliana na wanadamu wenzake, kuanzia uhusiano wa kifamilia, namna ya kuamiliana na jirani na jinsi ya kuamiliana na Waislamu na wasio Waislamu. Vilevile tumezungumzia mwenendo wa Mwislamu na jinsi ya kutumia wakati wa mapumziko na burudani, jinsi ya kuamiliana na mazingira, mtindo wa maisha wa Mwislamu kuhusu masuala ya kiuchumi na kadhalika.
Katika mfululizo wa vipindi hivi tulibainisha kuwa mtindo wa maisha wa Kiislamu unatayarisha uwanja mzuri wa kuwa mja halisi wa Mwenyezi Mungu. Kwa utaratibu huo ada na desturi za Kiislamu katika mtindo wa maisha wa Kiislamu na kitauhidi ni desturi za kuwa mja wa Mwenyezi Mungu.
Desturi na mafundisho ya dini kwa hakika ni ratiba inayotengeneza mwenendo makhsusi wa kimaisha wa Mwislamu. Ni wazi kuwa mtu anayekutambua kujikurubisha zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuwa ndilo lengo lake kuu na la mwisho hujitahidi kadiri ya uwezo kuhakikisha kwamba mambo yake yote maishani kama ibada, kazi elimu, burudani, mavazi, utumiaji wa bidhaa mbalimbali, namna ya kujipamba na kadhalika yanafanyika katika fremu na mipaka ya lengo hilo. Kwa maana kwamba, mambo yake yote yatafanyika kwa mujibu wa mafundisho, desturi na amri za Mwenyezi Mungu. Kwa maneno mengine ni kuwa, atahakikisha mambo yake yote kuanzia anapokuwa msikitini, sokoni, nyumbani, darasani, shuleni, ofisini, mtaani na kadhalika yanafanyika kwa ajili ya kupata radhi za Mola Muumba. Kwa msingi huo imani ya ghaibu, imani ya Tauhidi, kumwamini Mtume Muhammad (saw) na yote aliyokuja nayo, kuamini Siku ya Mwisho na mengine mengi vitakuwa na taathira katika maisha na mtindo wa maisha wa mwanadamu Mwislamu. Hapa ndipo tunapotambua tofauti iliyopo baina ya fikra za kidini na zile za kisekulari katika mtindo wa maisha. Mfumo wa fikra za kisekulari, tofauti na mafundisho ya Uislamu, unailinganisha dini na dhuku na matakwa ya mtu binafsi na hauitambui kuwa ni kigezo kinachoainisha thamani za mwanadamu katika pande zote za maisha yake.
Ala kulli hal, tunamshukuru Mwenyezi Mungu SW kwa kutuwezesha kukamilisha sehemu ya 83 ya mfululizo huu wa Mtindo wa Maisha wa Kiislamu. Ni matarajio kwamba mumefaidika na yote tuliyokuandalieni katika kipindi hiki. Hadi wakati mwingine na katika mfululizo mwingine tunakutakieni kila la kheri. Kwaherini...

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)