Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 20 Septemba 2015 13:22

Uislamu na Mtindo wa Maisha (81)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (81)

Kama bado mnakumbuka katika makala ya wiki iliyopita tulizungumzia umuhimu wa mali na utajiri na utumiaji wake katika shughuli za uzalishaji. Wiki hii tutajadili nafasi na umuhimu wa jinsi ya kutumia mali na utajiri katika mtindo wa maisha wa Kiislamu. Karibuni...
Kwa vile neno iqtisadi (yaani uchumi kwa Kiswahili) lina maana ya kuwa na mwendo wa wastani na wa kati na kati, hivyo basi uchumi pia unahusiana na masuala ya jinsi ya kutumia mali na kuendesha masuala ya nyumba na jamii. Kwa sababu hiyo pia sehemu kubwa ya mafundisho ya kiuchumi ya Uislamu inahusiana na utumiaji na jinsi ya kudhibiti na kuendesha suala hilo. Qur'ani Tukufu imewausia wanadamu kutumia vyema neema za Mwenyezi Mungu. Amri hiyo ya Qur'ani ni kwa ajili ya kutayarisha uwanja mzuri wa kumhimiza mwanadamu kutumia vyema na kwa njia sahihi neema za Allah kwa shabaha ya kupata ustawi wa kimaada na kiroho. Qur'ani inaitaja mali na utajiri kuwa ni neema ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake na uwanja mzuri unaoweza kutumiwa na waja kwa ajili ya kumshukuru muumba wao. Aya ya 172 ya Suratul Baqara inasema: "Enyi mlioamini! Kuleni vizuri tulivyokuruzukuni, na mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamuabudu Yeye tu."
Katika dini ya Uislamu misingi na thamani za kimaadili na kidini zinazotawala jinsi na njia za matumizi zina umuhimu mkubwa katika kuweka wazi na kuainisha mwenendo wa matumizi katika mtindo wa maisha wa Kiislamu. Japokuwa mwenendo wa matumizi ya vitu mbalimbali unatofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa kutilia maana zama, eneo, watu, mazingira makhsusi ya kiuchumi na utamaduni wao, lakini inawezekana kulindwa misingi mikuu katika hali na mazingira hayo yote. Hapa tutaashiria baadhi ya misingi hiyo
Moja kati ya misingi hiyo inayotawala matumizi ya mwanadamu kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu ni kujiepusha na israfu na ufujaji. Neno israfu lina maana ya kuchupa mpaka wa ulinganifu. Tunapoangalia mafundisho ya dini kuhusu israfu na ufujaji inatubainikia zaidi kwamba suala hilo ni haramu. Hata hivyo inatupasa kutambua kwamba, israfu na ufujaji vina maana pana zaidi na yenye vielelezo vingi lakini misdaki na kielelezo chake kikubwa zaidi ni israfu na kufuja mali. Sisitizo la Mwenyezi Mungu katika Qur'ani juu ya udharura wa kujiepusha na israfu linaonesha umuhimu mkubwa katika kuainisha mwenendo wa utumiaji sahihi katika mtindo wa maisha wa Kiislamu. Miongoni mwa athari mbaya za israfu na ufujaji ni kupoteza bure mali na utajiri na kuharibu maliasili na suhula za kimaada.
Suala la kujiepusha na israfu na ufujaji ni miongoni mwa masuala ambayo Mwenyezi Mungu ameyazungumzia sana katika aya nyingi za Qur'ani Tukufu. Kwa mfano tu sehemu ya aya ya 141 ya Suratul An'am inasema: "Kuleni matunda yake inapozaa, na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake. Wala msitumie kwa fujo. Hakika Yeye hawapendi watumiayo kwa fujo."
Utumiaji wa kila kitu una mipaka yake katika mtazamo wa mafundisho ya Mwenyezi Mungu ambayo iwapo italindwa na kuzingatiwa inaweza kumsaidia mwanadamu kufikia ustawi wa mtu binafsi na wa kijamii. Na iwapo mipaka hiyo itakiukwa kwa namna moja au nyingine basi mfumo wa maisha wa kiumbe huyo utavurugika na kukumbwa na matatizo. Kwa msingi huo dini ya Uislamu imesisitiza sana juu ya udharura wa kulindwa mlingano, uadilifu na njia ya kati na kati katika kila kitu.
Ufujaji na israfu pia una taathira mbaya sana katika jamii. Miongoni mwa taathira za moja kwa moja za israfu na ufujaji katika jamii hususan zile zenye suhula na utajiri kiasi ni umaskini na ufukara. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Mtume (saw) akasema: Mtu yeyote anayefanya israfu na ufujaji katika mali yake, Mwenyezi Mungu humfanya maskini.
Israfu pia huwa sababu ya kupotea haki za watu wengine. Kwa mujibu wa misingi ya uchumi wa Kiislamu, utajiri na maliasili za ardhi ni mali ya wanadamu wote na kila mtu ana haki na kustafidi na kutumia utajiri na maliasili hizo katika mipaka ya mahitaji yake. Kwa msingi huo mtu anayefanya israfu kwa hakika huwa anatumia sehemu ya wanadamu wengine na kuharibu mali ya watu wengine. Mtume Muhammad (saw) anasema: Kuleni, kunyweni, vaeni na toeni sadaka lakini msifanye israfu. Watu wabaya zaidi katika umma wangu ni wale wenye anasa na utajiri ambao miili yao hustawi na kuota kutokana na israfu na ufujaji.
Mjukuu wake, yaani Imam Ali bin Mussa Ridha (as) anasema: Msifanye israfu katika matumizi ya familia kwani Mwenyezi Mungu hawapendi wafujaji na anasema waumini ni wale ambao wanapotoa na kutumia hawafanyi israfu.
Msingi mwingine unaotawala mwenendo wa matumizi ya mja katika mtindo wa maisha wa Kiislamu ni kufanya uadilifu. Msingi huu umesisitizwa sana katika mafundisho ya Uislamu na unaungwa mkono na kutiliwa mkazo na akili na maumbile safi ya mwanadamu. Kwa kutilia maana kwamba wanadamu wana mahitaji mbalimbali na tofauti, na katika upande wa pili suhula nyingi na maliasili za duniani hii zina mipaka na mwisho, hivyo basi hapana shaka kuwa iwapo kundi moja la watu litachupa mipaka katika utumiaji wake suala hili litasababisha madhara kwa wanadamu wengine. Kwa sababu hiyo kulinda haki za watu wengine kunatulazimisha kuwa waadilifu na kufuata njia ya kati na kati katika matumizi yetu. Kulindwa msingi huu wa kufuata njia ya kati na kati na uadilifu katika matumizi kuna taathira kubwa katika kuratibu vyema masuala ya kiuchumi, kupunguza gharama za maisha na hatimaye kuzuia umaskini wa mtu binafsi na jamii. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema: Kufuata njia ya wastani na ya kati na kati katika matumizi hustawisha na kuzidisha mali." Vilevile Mtume wetu Muhammad (saw) anasema: Mtu yeyote anayefuata njia ya wastani na uadilifu maishani mwake , Mwenyezi Mungu humzidishia rizki, na mtu anayefanya israfu na ufujaji Mwenyezi Mungu humpunguzia rizki.
Aya na hadithi nyingi zinaoesha kuwa, utulivu wa kweli na hali bora ya mwanadamu si kutumia bila mipaka wala kidhibiti bali umo katika kutohitaji na kutokuwa tegemezi kwa watu wengine. Kwa msingi huo mafundisho ya Uislamu yanasisitiza sana juu ya udharura wa kujiepusha na tamaa na tabia ya kupenda kujilimbikizia kila kitu.
Kutosheka na kuridhika ni miongoni mwa misingu ya mwenendo wa matumizi katika mtindo wa maisha wa Kiislamu. Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) anasema kuwa, maisha bora zaidi ya kiuchumi yanayomdhamini mwanadamu utulivu ni yake yanayoambatana na kuridhika na kutosheka. Kuridhika kuna maana na kutosheka na machache na suala hilo humwepusha mwanadamu na athari mbaya za pupa na tamaa na matatizo mengi ya kiuchumi. Mtume (saw) anasema: Watu bora zaidi katika umma wangu ni wale wenye kuridhika, na wabaya zaidi miongoni mwao ni watu wenye tamaa. Wasii na khalifa wake, Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema: Mtu ambaye Mwenyezi Mungu amemtunuku hali ya kuridhika ndiye mwenye maisha bora zaidi ya wote.
Miongoni mwa masuala muhimu yenye taathira katika mwenendo wa matumizi ni kuzunguka mali na utajiri kwa njia sahihi katika jamii na kujiepusha kurundika utajiri sehemu moja. Katika aya za 34 na 35 za Suratu Tauba, Mwenyezi Mungu SW anakemea vikali tabia ya kulimbikiza mali na utajiri na kuahidi kutoa adhabu kali kwa watu wenye tabia hiyo.
Mafundisho ya kiuchumi ya Kiislamu sambamba na kukataza ufujaji na israfu yanakemea sana tabia ya ubahili na kuwa na mkono wa birika ambayo husababisha mali na utajiri kuganda sehemu moja na kutokuwa na mzungumzo sahihi katika jamii. >

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)