Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 06 Septemba 2015 18:30

Uislamu na Mtindo wa Maisha-80

Uislamu na Mtindo wa Maisha-80

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Ni wakati mwingine wa kuwaletea sehemu nyingine ya makala ya Uislamu na Mtindo wa Maisha. Wiki hii tutazungumzia umuhimu wa mali, utajiri na shughuli za uzalishaji katika mtindo wa maisha wa Kiislamu.  Basi fuatilieni mfululizo huu kuanzia mwanzo hadi mwisho ili muweze kunufaika na yale tuliyoweza kuwaandalia.

Uislamu umeitambua mali, utajiri na aina zote za neema za kimaada kuwa ni msingi na nguzo ya jamii. Qur'ani Tukufu pia imeipa umuhimu mali na kuitambua kuwa ni miongoni mwa sababu za ustawi wa mwanadamu. Katika aya ya 5 ya Suratu Nisaa, Mwenyezi Mungu SW anasema: Wala msiwape wapumbavu mali zenu ambazo Mwenyezi Mungu amewajaalia kuwaendeshea maisha…" Aya hii inaashiria taathira ya mali katika maisha na kuimarika kwa mtu na jamii na kubainisha uhakika kwamba kuharibiwa uchumi huitumbukiza jamii katika hatari kubwa. Kwa maneno mengine ni kuwa mali ni sawa na damu katika mishipa ya jamii na si sahihi kuitumia vibaya au kuwapa watu wapumbavu na wasio na akili na busara.

Qur'ani Tukufu pia inaitaja mali ambayo huwa sababu ya ustawi na maendeleo kuwa ni kheri na baraka. Aya ya 180 ya Suratul Baqarah inasema: Mmefaradhishiwa mmoja wenu anapofikwa na mauti, kama ataacha mali, kuwausia kitu wazazi wawili na akraba kwa namna nzuri. Ni haki haya kwa wenye taqwa."

Aya hii wapenzi wasikilizaji inaitaja mali na utajiri kuwa ni kheri. Ni wazi kuwa kitu kinachotambuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni kheri kina thamani na umuhimu makhsusi. Vilevile tunaweza kusema kuwa kutafuta mali kwa njia halali ni kheri na sifa njema na kufanya israfu na ufujaji ni shari na kazi mbaya.

Kufanya kazi na jitihada za kutafuta rizki ya halali pia vilipewa umuhimu mkuba na Mtume Muhammad (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu. Kinyume chake watukufu hao walikemea sana kulimbikiza mali na utajiri bila ya kuutumia vyema na mahala pake. Imepokewa kutoka kwa wasii wa Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Ali bin Abi Twalib (as) kwamba amesema: Taifa lenye maji na ardhi ya kutosha lakini likaacha kudhibiti maji hayo na kutengeneza ardhi hiyo kwa ajili ya kilimo na likahitajia na kuomba watu wengine kutokana na uzembe au utendaji mbaya, huwa mbali na rehma ya Mwenyezi Mungu.

Maana ya uzalishaji katika mafundisho ya kiuchumi ya Uislamu ni kazi yoyoteya halali inayofanywa kwa ajili ya kudhamini mahitaji ya kimaisha na maendeleo ya kiuchumi ya mtu binafsi na jamii. Viongozi wa Uislamu daima walikuwa wakiwahimiza Waislamu kujihusisha na kazi za uhunzi, kilimo, biashara na kadhalika na walikuwa wakisema kuwa kazi na uzalishaji ndiyo msingi wa izza na heshima yao. Mmoja wa masahaba wa Imam Swadiq (as) anasimulia kwamba: Siku moja Imam Swadiq aliniona nikienda sokoni (yaani sehemu ya kazi zangu)  nikiwa nimechelewa kidogo. Alisema: "Elekea kwenye izza na heshima yako asubuhi na mapena." Hatua hii ya Imam Swadiq (as) ya kutaka sehemu ya kazi kuwa ni izza na heshima ina maana kwamba uzalishaji na kufanya kazi kwa ajili ya kupata mali ni izza, hadhi na heshima ya mtu.

Uzalishaji katika mtazamo wa Kiislamu una malengo yenye thamani kubwa. Tunapotalii na kuchunguza aya za Qur'ani tukufu na Hadithi za Mtume wetu Muhammad (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu tunaona kuwa miongoni mwa malengo ya uzalishaji na shughuli za kiuchumi katika mtindo wa maisha wa Uislamu ni kulinda heshima na hadhi ya mja asiombe na kuwahitajia watu wengine, kueneza hali bora na inayokubalika ya maisha, kutumia mali na utajiri katika njia ya Mwenyezi Mungu na kukidhi mahitaji ya mtu binafsi ya jamii. Mjukuu wa Mtume wetu muhamamd (saw) Imam Muhammad Baqir (as) anasema: Mtu anayetafuta rizki hapa duniani ili asiwahitajie watu wengine, kukidhi mahitaji ya familia yake na kwa ajili ya kuonesha upendo na mahaba kwa jirani yake atakutana na Mwenyezi mungu SW Siku ya Kiama huku uso wake uking'ara kama mbala mwezi usiku wa tarehe 14."

Imepokewa kwamba bwana mmoja alikwenda kwa Imam Swadiq (as) na kusema: Nimetekwa na dunia na ninapenda kupata mali na utajiri. Imam alimuuliza: Unataka kuifanyia kazi gani mali hiyo? Bwana yule alisema: Ninataka kukidhi mahitaji ya familia yangu, kuunga udugu, kutoa sadaka na kwenda hija na umra. Imam Swadiq (as) alimwambia: "Huku si kutafuta na kutekwa na dunia bali ni kutafuta Akhera."

Kwa kutilia maanani yote tuliyosema inabainika kuwa lengo la uzalishaji na shughuli za kiuchumi katika Uislamu lina tofautiana na malengo ya mifumo mingine ya kifikra na kiuchumi. Mifumo yote ya kiuchumi inalipa umuhimu mkubwa suala la uzalishaji na inautambua ustawi wa kiuchumi kuwa ni miongoni mwa mambo ya dharura. Hata hivyo mifumo hiyo inatofautiana katika mitazamo yao kuhusu uzalishaji na ustawi wa kiuchumi. Katika baadhi ya mifumo ya kiuchumi inayotawala dunia lengo la uzalishaji huwa ni faida za kimaada tu. Kwa mfano tu katika mfumo wa ubepari, lengo kuu la shughuli za kiuchumi ni kuzidisha mtaji na kupata faidi kubwa zaidi kwa sababu mambo yote ya maisha katika mfumo huu yanaishia katika  masuala ya kimaada. Kinyume chake, katika teolojia ya Kiislamu, mwanadamu ana maisha ya kimaada na kiroho au maisha ya dunia na Akhera ambayo yote yanaandamana na kwenda pamoja; na maisha ya Akhera ya mwanadamu yanafuata aina ya maisha yake hapa duniani. Kwa msingi huo lengo la uzalishaji katika mfumo huu si kupata maisha bora ya kimaada na kidunia tu kwa sababu kuna saada na ufanisi na ulimwengu wa Akhera.

Hivyo basi katika mfumo kama huu suala la kudhamini mahitaji ya kimsingi ya maisha ya dunia linapaswa kufanyika katika fremu ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Kwa maana kwamba katika mtindo wa maisha wa Kiislamu sambamba na kufanya bidii katika kazi, uzalishaji na shughuli za kiuchumi mwanadamu anapaswa kutosahau lengo lake la mwisho na kuu yaani saada na ufanisi wake katika dunia ya Akhera.

Kwa kutilia maanani mtazamo wa Uislamu kwa suala la uzalishaji, vyanzo vya uzalishaji pia vina nafasi tofauti katika mfumo wa kiuchumi wa dini hiyo. Uislamu unatambua vyanzo vya uzalishaji yaani kazi, mitaji na uwezekaji, maliasili na kadhalika kuwa ni neema ya Mwenyezi Mungu ambazo amewapa waja wake kama amana kwa ajili ya kutimiza malengo maalumu. Aya nyingi za Qur'ani Tukufu zinamkumbusha mwanadamu tunu na neema nyingi za Mwenyezi Mungu kwa kiumbe huyo na kumhamasisha kuijenga na kuistawisha ardhi. vilevile baadhi ya aya za Qur'ani Tukufu zinasema kuwa lengo la kumsakhirishia mwanadamu mbingu na ardhi, kuumbwa usiku na mchana, kutumwa upepo na mvua na harakati za merikebu baharini ni kwa ajili ya kutafuta. Aya hizo pia zainawahamasisha wanadamu kutafuta rizki na kujishughuliza na kazi za uzalishaji.

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa: Katika mfumo wa uchumi wa Kiislamu kumeainishwa malengo ambayo hayawezi kutimia bila ya kuwepo uzalishaji na ustawi wa kiuchumi. Sisitizo la kutafuta hali bora ya maisha, nguvu na uwezo na nguvu ya jamii ni malengo ambayo hayawezi  kutimia bila ya kuustawishwa zaidi uzalishaji katika nyanja za kiuchumi. Vilevile sisitizo la kupambana na umaskini, uwekezaji katika uzalishaji, marufuku na kuharamisha tabia ya kuhodhi na kujilimbikizia bidhaa na kutelekeza mali na utajiri ni miongoni mwa mambo yanayotilia mkazo uzalishaji na ustawi wa kiuchumi.  >

Kipindi chetu kinaishia hapa kwa leo. Msikose kufuatilia mfululizo wa kipindi hiki juma lijalo.

     

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)