Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 23 Agosti 2015 15:03

Uislamu na Mtindo wa Maisha-78

Uislamu na Mtindo wa Maisha-78

Makala yetu leo itafungua ukurasa mpya wa mtindo wa Maisha wa Kiislamu katika masuala ya uchumi. Karibuni....

Katika fikra na mafundisho ya Uislamu, itikadi na imani za watu huwa mwongozo wa mienendo yao ya kiuchumi na shughuli zao nyingine za kimaisha. Kwa msingi huo mjadala wa uchumi katika mtindo wa maisha wa Kiislamu, kama yalivyo masuala mengine, unafungamana barabara na mjadala na masuala ya kimaadili na kiitikadi.

Mfungamano uliopo baina ya uchumi na masuala ya kiikadi katika Uislamu ni mkubwa na wenye nguvu kiasi kwamba ni vigumu bali muhali wakati mwingine kuweza kutenganisha baina ya viwili hivyo. Kwa mfano tu baadhi ya wajibu wa kifedha kama kutoa humusi, kwa maana ya moja ya tano na kipato cha mtu kinachosalia baada ya matumizi ya mwaka mzima, kutoa zaka na kadhalika kidhahiri vinasanifiwa katika masuala ya kiuchumi, lakini kwa hakika vinahesabiwa kuwa ni sehemu ya masuala ya kiibada, na sharti la kukubaliwa mambo hayo mbele ya Mwenyezi Mungu ni mwanadamu kutia nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu.

Katika mfumo wa kifikra wa Kiislamu kazi na bidii vimefungamanishwa na masuala ya kiroho na kimaanawi kwa sababu dini hiyo inatambua kazi na bidii inayofanywa na mja kwa ajili ya kuboresha maisha na kukidhi mahitaji yake yeye na familia yake kuwa ni ibada. Kazi na harakati za kutafuta kipato mbali na kuwa sababu ya ustawi na maendeleo ya maisha ya kidunia iwapo itafanyika kwa nia ya kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu na kufanywa kwa ajili ya malengo aali zaidi, huwa sababu ya kupewa ujira na thawabu huko Akhera. Kwa sababu hiyo Mtume Muhammad (saw) amesema: "Dunia ni shamba la Akhera" kwa maana kwamba, dunia na vilivyomo vinaweza kutayarisha uwanja mzuri wa ustawi wa kiroho wa mwanadamu na kumdhaminia saada na ufanisi huko Akhera kwa sharti kwamba vitu hivyo vitumiwe kwa njia sahihi.

Kwa kutilia maanani malengo aali yaliyoainishwa kwa ajili ya mwanadamu katika mafundisho ya Uislamu, tunaweza kusema kuwa, mfumo wa uchumi wa Kiislamu unafanya bidii za kuimarisha zaidi thamani za kidini na kimaadili katika nafsi ya mwanadamu. Kwa hakika suala hilo ni msingi muhimu na hivyo basi malengo makuu katika mfumo wa uchumi wa Uislamu ikiwa ni pamoja na kujitegemea kiuchumi, uadilifu, hali bora ya maisha ya jamii, ustawi wa kiuchumi na kadhalika vinaarifishwa kwa mujibu wa malengo hayo. Katika mafundisho ya Uislamu akhlaki na maadili mema na thamani za kiroho hutawala mienendo ya kiuchumi ya mwanadamu ili kuzuia dhulma, kuchupa mipaka au kukanyaga haki za watu wengine. Harakati zote za kiuchumi za Mwislamu katika mtazamo huo hufanyika kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kutekeleza maamrisho na makatazo yake. Mwanadamu kama huyo hufuatilia faida na maslahi ya kiuchumi yanayooana tu na imani na itikadi zake. Mwanadamu kama huyu hufanya jitihada kadiri ya uwezo wake kuhakikisha kuwa wanadamu wenzake wanafaidika pia na neema za Mwenyezi Mungu. Mwanadamu anayefaa katika mfumo wa kiuchumi wa Kiislamu hutambua mali na utajiri kuwa ni amana aliyopewa na Mwenyezi Mungu ambayo analazimika kuitumia vyema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kimaada na kiroho ya jamii. Kwa msingi huo Mwislamu wa kweli hujitambua kuwa anawajibika kufanya kazi na bidii kwa ajili ya kuboresha na kuijenga dunia. Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya ya 61 ya Suratu Hud kwamba: Ni Yeye ndiye aliyekuumbeni kutokana na ardhi na akakupeni jukumu la kuijenga..".

Katika sehemu ya kwanza ya mjadala wa mtindo wa maisha wa Kiislamu katika masuala ya uchumi tutazungumzia umuhimu wa kazi na kufanya bidii japokuwa huko nyuma tuliwahi kuzungumzia suala hili lakini katika mtazamo wa taathira zake za kinafsi na za mtu binafsi.     >>>

Maana ya kazi hapa ni mkusanyiko wa shughuli na harakati za kimwili na kifikra za mwanadamu ambazo humletea manufaa ya kimaada. Katika mtazamo wa Uislamu, chimbuko la kuchapa kazi na kufanya bidii ni fitra na maumbile asili ya mwanadamu na hamu yake kubwa ya kutafuta ukamilifu. Kwa maana nyingine ni kuwa, sehemu moja ya juhudi za kupata ukamilifu mwanadamu hudhihirika katika kazi na juhudi zake. Hamu ya kufanya kazi na harakati kwa ajili ya kuwa na maisha bora, kama zilivyo hisi nyingine za mwanadamu, imewekwa katika ujudi na nafsi yake ili aweze kufanya bidii za kukidhi mahitaji yake na kufaidika na neema tele za maumbile ya dunia.

Hamu ya kutaka kufanya kazi huwa na taathira kubwa sana katika ustawi na maendeleo ya jamii na harakati za kiuchumi. Kama hakutatayarishwa uwanja mzuri na unaofaa wa kazi basi watu wenye vipawa na wavumbuzi hawataweza kudhihirisha matunda na uvumbuzi wao katika nyanja mbalimbali za sayansi na teknolojia. Hivyo basi kutokuwapo uwanja unaofaa wa kufanya kazi huwa sababu ya kupotea bure vipawa na uwezo huo wa ndani ya nafsi za watu hodari. Suala hilo katika upande mwingine linaweza kuwa sababu ya kuwaelekeza wanadamu katika kazi zisizofaa japokuwa zina pato la kimaada kama vile kuuza na kununua bidhaa na huduma zisizo za dharura au hata zenye madhara kwa mtu binafsi na jamii.

Kazi ni haja ya kimaumbile ya mwanadamu. Vilevile dini na mafundisho yake vinamhimiza na kumhamasisha mwanadamu kuchapakazi na kufanya bidii. Hii ndiyo maana ya msemo kwamba dini ni suala la kifitra na kimaumbile, kwa maana kwamba sheria na kanuni za dini zinaoana na kwenda sambamba na kanuni za kimaumbile, kwa sababu chanzo na chimbuko la kanuni zote hizo ni kimoja, yaani Mwenyezi Mungu Muumba wa mwanadamu na dunia.

Ili mwanadamu aweze kuishi kwa utulivu wa kinafsi na kumwabudu Mwenyezi Mungu bila ya dukuduku anahitajia kuwa na chakula, maji, makazi na mahitaji mengine ya kimaisha, na haya yote hayawezi kupatikana bila ya kujishughulisha na kazi na kufanya bidii. Hivyo basi ni haki ya wazi ya mwanadamu kukidhi mahitaji yake lakini kwa sharti kwamba si tu kudhamini na kukidhi mahitaji hayo kusizibe na kufunga njia yake ya ukamilifu bali pia kusawazishe na kumtengenezea zaidi mwanadamu njia ya ukamilifu wa kiroho.

Hadithi nyingi zilizopokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saw) Ahlubaiti zake watoharifu zinaonesha jinsi watukufu hao walivyolipa umuhimu mkubwa suala la kufanya kazi. Imepokewa katika sira ya Mtume (saw) kwamba alikuwa akifanya kazi tangu akiwa mtoto. Utotoni na katika kipindi cha ubarobaro, Mtume (saw) alifanya kazi ya kuchunga mbuzi, na ujanani mwake alijishughulisha na kazi ya biashara. Baada ya kupewa utume, Muhammad amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake hakuacha kuchapakazi na wala hakuishi maisha ya anasa kama wafanyavyo wafalme na watawala wengi. Alitingwa sana na kazi za utume na kuwasilisha ujumbu wa Allah kwa walimwengu. Mtukufu huyo alitumia wakati wake mwingi mjini Madina kushughulikia masuala ya kulingania dini na kulinda dola la Kiislamu lakini pamoja na hayo alitumia fursa yoyote iliyopatikana kwa ajili ya kufanya akzi na bidii katika masuala ya kimaisha.

Mtume (saw) amesema: Mwenyezi Mungu anapenda kumuona mja wake akiwa amechoka katika njia ya kutafuta rizki ya halali." Vilevile amesema katika hadithi nyingine kwamba: "Mtu mwenye maji na ardhi lakini akapatwa na umaskini kutokana na kujishughulisha na kazi huwa mbali na rehma za Mwenyezi Mungu."

Imenukuliwa kwamba siku moja Mtume (saw) alimuona kijana mwenye nguvu na misuli akifanya kazi tangu asubuhi na mapema. Baadhi ya maswahaba wa Mtume walisema: Kama kijana huyu angetumia nguvu ya ujana wake katika njia ya Mwenyezi Mungu angestahiki sifa na pongezi. Mtume (saw) alisema: Msiseme hivyo. Kama kijana huyu anafanya kazi ili akidhi mahitaji yake na asitegemee na kuwaombe watu wengine basi kwa hakika anafanya kazi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Vilevile kama anafanya kazi ili akidhi mahitaji ya baba na mama yake wasiojiweza au kwa ajili ya watoto wake wachanga anafanya kazi katika njia ya Mwenyezi Mungu."

Historia ya sira ya Mtume inasema, wakati wowote mtukufu huyo alipokuwa akivutiwa na mtu alikuwa akiuliza kuhusu shughuli na kazi yake; kama ataambiwa kuwa hana kazi Mtume alikuwa akisema kwamba: Haiba yake imeporoka mbele yangu, kwani muumini asiye na kazi hutumia dini yake kama wenzo wa kupata chumo la maisha yake.

Makusudi ya Mtume (saw) katika maneno haya ni kwamba, mtu anayepatwa na umaskini na ufukara suala hilo huathiri dini na itikadi zake na yumkini akafanya jambo lolote linalopingana na dini na itikadi zake kwa ajili ya kukidhi mahitaji yake ya kifedha na mahitaji mengine ya kimaisha.  

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)