Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 15 Agosti 2015 13:02

Uislamu na Mtindo wa Maisha-77

Uislamu na Mtindo wa Maisha-77

Katika makala kadhaa zilivyopita tulizungumzia jinsi Mwislamu anavyopaswa kuamiliana na mazingira katika mtindo wa maisha wa dini hiyo. Leo tutatupia jicho mwenendo wa mwanadamu na wanyama katika mtindo wa maisha wa Kiislamu.          >>

Wanyama ni sehemu ya mapambo ya mazingira na maumbile ya dunia hii na hapana shaka kuwa kulindwa mlingano katika mazingira ya dunia kunafungamana na kuwepo kwa viumbe hao. Wanyama wana taathira na faida nyingi na za aina mbalimbali kwa wanadamu. Mwenyezi Mungu Karimu aliwaumba wanyama na kujaalia faida nyingi kwa ajili ya wanadamu katika wanyama hao. Kwa karne nyingi wanadamu wamekuwa wakitumia wanyama kwa ajili ya safari na kusafirisha mizigo yao, katika kilimo na kazi nyingine nzito. Utumiaji wa nyama, ngozi, maziwa na viungo vya wanyama unatambuliwa kuwa ni rasilimali kubwa sana kwa jamii za kijadi na hata za kisasa.

Miongoni mwa kazi halali zinazojulikana kwa ajili ya kudhamini kipato cha mwanadamu ni pamoja na ufugaji wanyama wa kawaida na ndege na vilevile ufugaji wa nyuki. Kwa kutilia maanani umuhimu na mchango wa wanyama katika maisha ya mwanadamu, dini ya Uislamu imelipa umuhimu mkubwa suala la haki za viumbe hao kwa kadiri kwamba, Waislamu wanawajibika na wana majukumu ya kutenda kuhusu wanyama. Mas'ulia na majukumu hayo ya kidini humfanya Mwislamu achunge na kuheshimu haki za wanyama kutokana na itikadi yake.

Uislamu umesisitiza sana juu ya udharura wa kuwa na mwenendo mzuri, wa upole na huruma kwa wanyama na vilevile kuwatumia vyema viumbe hao. Kwa msingi huo dini hiyo ya Mwenyezi Mungu haimruhusu Mwislamu kupuuza haki za wanyama kwa kutumia kisingizio cha ubora na utukufu wake kama kiumbe mwanadamu. Katika mtindo wa maisha wa Kiislamu inakatazwa kuamiliana vibaya na wanyama, kuwaudhi na kuacha kukidhi matakwa na mahitaji yao. Hivyo basi hata kutumia wanyama katika Uislamu kuna mipaka na sheria zake.

Aya za Qur'ani na hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu zinaonesha kuwa, wanyama pia wanadiriki na kuelewa kulingana na ujudi wao kama wanyama na vilevile wana hisia. Imam Swadiq (as) amesema: "Mwenyezi Mungu SW amewapa wanyama mambo manne: Kumjua Mwenyezi Muumba wao, kujua jinsi ya kutafuta rizki zao, kujua jike na dume miongoni mwao, na kuogopa kifo na mauti." (usulul Kafi, juzuu ya 6:539)

Miongoni mwa haki za wanyama kwa mwanadamu ni kukidhi mahitaji yao ya kimsingi kama kuwapa chakula na maji, kwa sababu wanyama hawawezi kueleza matakwa na mahitaji yao. Hivyo basi kumfungia mnyama nyumbani na kumnyima neema hizo za Allah ni jambo lisilokubalika. Imam Ali bin Abi Twalib (as) amesema: Siku moja Mtume (saw) alipokuwa akitawadha, paka alimsogelea mtukufu huyo. Mtume (saw) alitambua kwamba mnyama huyo ana kiu. Mtukufu huyo alimsogezea chombo kilichokuwa na maji na paka akanywa maji hayo. Kisha Mtume (saw) akatawadha."

Kwa msingi huo haki ya kimsingi kabisa ya wanyama inayotokana na haki ya kuishi ni kumtayarishia chakula, maji ya kunywa, makazi yanayofaa na usalama. Sheria za Kiislamu pia zinawahimiza wafuasi wa dini hiyo kumlinda mnyama na maudhi na kutodhuru mwili wake. Imam Mussa al Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa maimamu watukufu katika kizazi cha Mtume wetu Muhammad (saw) anasema: Mcheni Mwenyezi Mungu kuhusu viumbe wasiosema." Mtukufu huyo aliulizwa kwamba: Ni wepi hao wasiosema? Alijibu: Mbuzi, paka, njiwa na mithili yao."

Kwa kuzingatia kwamba katika zama za Mtume (saw) na Maimamu maasumu wanyama ndio waliokuwa chombo muhimu zaidi cha usafirishaji, watukufu hao walikuwa wakilinda na kuchunga haki za wanyama na kuwahamasisha Waislamu kuchunga haki hizo katika minasaba na matukio mbalimbali. Mwenendo mwema wa Mtume (saw) na Ahlubaiti zake kwa wanyama viliwahamasisha na kuwafunza Waislamu jinsi ya kuamiliana na viumbe hao.

Kama tunavyojua, miongoni mwa vitu vyenye faida kubwa ni kutumia wanyama katika usafirishaji. Hadithi za Mtume (saw) na maimamu watoharifu katika kizazi chake zinaeleza jinsi ya kuamiliana na wanyama hao. kwa mfano tu imepokewa kwamba Mtume (saw) amesema: "Usimlazimishe mnyama kubeba mzigo zaidi ya uwezo wake". Vilevile sheria za Uislamu zinakataza kumbebesha mnyama mzigo mzito kupita kiasi, kumfanya atembee masafa marefu bila ya kupumzika na watu watatu kumpanda mnyama mmoja.

Haki za wanyama na suala la kuwatendea uadilifu limetiliwa mkazo sana katika Uislamu kwa kadiri kwamba, Imam Ali bin Abi Twalib (as) hakuwa tayari hata kumnyang'anya na kumdhulumu chungu bua la shayiri mkabala wa kupewa dunia na vilivyomo.

Wanyama wanaokidhi mahitaji ya wanadamu yumkini wakawa wanapata rizki zao katika mazingira yao wenyewe kama nyikani na porini. Hivyo mmiliki wa wanyama kama hao analazimika kuwaachia huru kwa ajili ya malisho na kukidhi mahitaji yao mwenyewe. Wakati mwingine wanyama hao hufugwa na kufungiwa mazizini hivyo mmiliki analazimika kumtayarishia maji na chakula.

Sheria na fiqhi ya Kiislamu inamlazimisha kila mmiliki wa mnyama kukidhi mahitaji yake bila ya kutofautisha mnyama halali anayeliwa na yule asiyeliwa au ndege na kadhalika. Vilevile Uislamu umewahimiza wafuasi wake kumjali mnyama anayenyonyesha kwa sababu kuchunga haki za mnyama huyo ni kuchunga haki za wanyama wawili. Sahaba mmoja wa Mtume (saw) anasimulia kwamba: Siku moja Mtume alitunukiwa mnyama anayenyonyesha. Mtukufu huyo aliniamuru kumkama maziwa na nikakama maziwa mengi sana. Mtume (saw) alipoona hali hiyo aliniambia: Usikame maziwa kiasi hicho bali bakisha sehemu ya mtoto anayenyonya. Wakati mwingine kukama maziwa yote ya mnyama humdhuru pia mnyama mwenyewe."

Kulinda haki za mnyama anayenyonyesha hakuhusu wanyama halali na wanaoliwa pekee bali hata wale wasiokuwa halali kuliwa. Imepokewa kwamba wakati jeshi la Uislamu lilipokuwa njiani kwenda kukomboa mji wa Makka Mtume (saw) aliona mbwa aliyekuwa akibweka huku akinyonyesha watoto wake. Mtume alimuamuru mmoja kati ya masahaba zake asimame mahala hapo na kuchunga jeshi lisije likamdhuru mnyama huyo na watoto wake.

Tunakamilisha makala hii kwa hadithi ifuatayo. Imepokewa kwamba Mtume (saw) alipita sehemu fulani ambako alimuona ngamia mbele ya nyumba huku mguu wake ukiwa umefungwa kamba bila ya kupewa maji na chakula. Mtume aliuliza: Ngamia huyu ni wa nani? Kijana mmoja Muansari alisema ni ngamia wangu. Mtume alimwambia kijana huyo ambaye hakuwa akimpa mnyama huyo chakula kwa wakati wake kwamba: "Hivi humuogopi Mwenyezi Mungu kuhusu Mnyama huyu aliyemilikisha? Ama mpe maji na nyasi au mwachie huru ili yeye mwenyewe ajitafutie chakula."

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)