Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 12 Agosti 2015 16:41

Mtindo wa Maisha wa Kiislamu-76

Mtindo wa Maisha wa Kiislamu-76

Kama bado mnakumbuka, katika nakala iliyopita tulizungumzia majukumu ya mwanadamu kuhusu suala la kulinda mazingira na tukasema kwamba, Mwislamu anayatambua mazingira kuwa ni amana ya Mwenyezi Mungu kwake ambayo anapaswa kuichunga na kuilinda ipasavyo.

Vilevile kwamba, matukio ya dunia hii yanafungamana kwa kiasi fulani na amali na matendo ya waja. Kwa maana kwamba iwapo mwanadamu atamtii na kumcha Mwenyezi Mungu sambamba na kuwa mja mwema basi atafunguliwa milango ya neema na baraka tele; na kama atakhitari njia isiyo hiyo na kupotoka njia nyoofu, jamii ya kiumbe huyo itakumbwa na ufisadi kwa maana ya uharibifu na mabalaa ya aina mbalimbali yatakayoenea pande zote za maisha yake katika bara na baharini. Hii ni kwa sababu kama anavyosema mwanafikra mkubwa wa zama hizi Ayatullah Jawadi Amouli, mwanadamu ni sehemu ya mnyororo wa matukio ya dunia hii na iwapo sehemu moja ya mnyororo huo mkubwa, yaani mwanadamu, haitatekeleza vyema na ipasavyo majukumu yake, basi mfumo mzima wa dunia utakumbwa na dosari na uharibifu.

Qur'ani Tukufu imebainisha waziwazi mfungamano na uhusiano wa moja kwa moja uliopo baina ya matendo ya mwanadamu na maumbile ya dunia katika aya zake nyingi. Aya za Qur'ani zinazozungumzia uhusiano huo zinaweza kugawanywa katika makundi kadhaa. Kundi linalozungumzia asili ya mfungamano wa matendo ya wanadamu na matukio ya dunia, aya zinazozungumzia mfungamano wa matendo mema ya mwanadamu na matokeo yake mazuri duniani na nyingine zinazobainisha uhusiano wa kazi na amali mbaya za wanadamu na mabalaa na matukio ya kusikitisha ya dunia hii. Kwa mfano tu, aya ya 16 ya Suratul Jinn inasema: "Na lau kama wangesimama sawasawa juu ya njia tungeliwanywesha maji kwa wingi."

Kwa mujibu wa aya hii ya Qur'ani, kusimama sawasawa katika njia ya Mwenyezi Mungu ndiyo sababu ya kupewa maji mengi yanayonywesheleza mashamba, misitu, wanyama na wanadamu. Wafasiri wa Qur'ani wanasema kuwa, maana ya 'maji' katika aya hii si maji ya mvua pekee bali maji hapa yana maana pana inayojumuisha maji ya mito, chemchemi, maji ya chini ya ardhi kama ya visima na kadhalika. Hivyo basi Mwenyezi Mungu Muweza hulipa taifa au jamii neema na baraka za kimaada kutokana na amali na matendo mema ya watu wa jamii na taifa hilo, kama ambavyo amali mbaya na madhambi ya watu yumkini yakawa sababu ya kupungua maji na neema hiyo. Kwa mujibu wa aya hii ya Qur'ani, imani na uchamungu ni sababu ya neema na baraka za kiroho na kimaanawi na wakati huo huo huzidisha rizki za kimaada na neema nyingine za kidunia na ustawi na maendeleo.

Vilevile tunasoma katika aya ya 96 ya Suratul Aaraf kwamba: Na lau watu wa mji wangeamini na kumcha Mwenyezi Mungu tungewafungulia baraka za mbingu na ardhi..."

Kwa mujibu wa aya hii imani na taqwa ya watu wa mijini na vijijini huwa sababu ya kufunguliwa milango ya baraka za mbinguni na ardhini. Aya hii ya Qur'ani inabainisha na kuweka wazi uhusiano uliopo baina ya amali na matendo ya wanadamu na matukio ya dunia hii. Baraka za mbingu na ardhi zinaweza kufasiriwa kwa maana nyingi. Mfano wa baraka za mbingu ni kama mvua, theluji, jua na kadhalika na baraka za ardhini ni kama ardhi safi ya kilimo, mito na chemchemi, maziwa, kuota kwa mimea na matunda ya aina mbalimbali ambavyo vyote vinapatikana kutokana na amali  na matendo mema ya waja.

Katika aya ya 41 ya Suratu Rum, Mwenyezi Mungu Mtukufu anazungumzia aina nyingine ya taathira ya amali na matendo ya wanadamu katika mazingira na maumbile ya dunia. Aya hiyo inasema: Uharibifu umedhihiri bara na baharini kwa sababu ya iliyoyafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonjeshe baadhi ya waliyoyatenda, huenda wakarejea."

Ufisadi na uharibifu katika bahari yumkini ukatokea katika sura ya kupungua neema za baharini au ukosefu wa usalama wa baharini, vita vya baharini na kadhalika. Hata hivyo katika aya hii kunakozungumziwa adhabu ya Mwenyezi Mungu, maana ya kwanza inayokusudiwa huwa ni kuondokewa na neema mbalimbali kutokana na madhambi ya waja kisha kuangamia na kuhiliki kutokana na shirki.

Imepokewa kwamba mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Jafar Swadiq (as) amesema: Maisha ya viumbe wa baharini yanatokana na mvua. Kwani wakati mvua inapokosa kunyesha ufisadi na uharibifu huvipata viumbe vyote vya nchi kavu na baharini. Huu ni wakati madhambi ya waja yanapokithiri", mwisho wa hadithi.

Tunapaswa kuelewa kwamba uharibifu unaozungumziwa katika hadithi hii ni moja ya vielelezo vya uharibifu na kuhusu kunyesha kwa mvua na uhai wa viumbe wa baharini. Suala hili pia linathibitishwa na uzoefu na tajiriba kwamba wakati mvua inapopungua, mavuno ya samaki wa baharini pia hupungua. Vilevile tunasikia kutoka kwa wakazi wa pwani wakisema kwamba: Faida za mvua kwa bahari ni kubwa zaidi kuliko faida zake kwa maeneo ya jangwani.

Kwa mujibu wa aya tulizosoma, kuna mfungamano baina ya amali na matendo maovu na matukio mabaya na ya kusikitisha ya dunia hii. Vilevile tunaelewa kwamba, iwapo wanadamu watamtii na kumcha Mwenyezi Mungu watafunguliwa milango ya rehma na baraka zake, na iwapo watakengeuka haki na kuipa mgongo njia nyoofu watanyang'anywa neema na baraka hizo.

Katika mfumo wa thamani wa Kiislamu kazi na amali zote njema huwa na thamani na malipo mema japokuwa baadhi ya amali na matendo hayo hubakia milele kama vile kuandika kitabu chenye elimu na maarifa kwa wanadamu. Miongoni mwa amali njema zinazobakia ziku zote ni kuhuisha mazingira kama kupanda miti, kuchimba mifereji ya maji, visima, kujenga mabwawa ya kuhifadhi maji na shughuli nyingine ambazo hutayarisha uwanja mzuri kwa aili ya maisha bora ya wanadamu. Mafundisho ya dini ya Kiislamu yanasema iwapo mwanadamu atapanda mti au kufanya jambo linalowafaidisha wanadamu wenzake basi atakuwa akipata thawabu na malipo mema wakati wote jambo hilo litakapoendelea kuwepo na kutumiwa na watu. Suala hili huwahamasisha wanadamu kufanya mambo yenye faida za kudumu au za muda mrefu kwa umma hususan suala la kulinda na kutunza mazingira.

Ni jambo la dharura kwa Mwislamu kujali na kutunza mazingira na kufanya jitihada za kuyasafisha pale yanapochafuliwa. Umuhimu wa kutunza mazingira unaonekana katika hadithi ya Mtume Muhammad (saw) pale aliposema: Kama utakuwa na mche wa mti mkononi na ukawa umebakiwa na muda wa kupanda mti tu hadi kuwadia Kiama, basi panda mche huo wa mti." (Mustadrakul Wasail, juzuu 13:460)

Suala jingine la kupewa umuhimu kuhusu mazingira katika mtindo wa maisha wa Kiislamu ni kujali sana neema ya maji na kutofanya israfu na ufujaji katika matumizi yake. Maji yamepewa umuhimu mkubwa katika mafundisho ya Uislamu na suala hilo limesisitizwa sana katika sira na hadithi za Mtume (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu.    >>

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)