Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 06 Agosti 2015 13:37

Uislamu na Mtindo wa Maisha-75

Uislamu na Mtindo wa Maisha-75

Katika makala ya wiki iliyopita tulisema kuwa mwanadamu ana majukumu ya kufanya mkabala wa mazingira na maumbile ya dunia na kwamba matumizi ya neema hiyo kubwa yana sheria na kanuni zake. Kama tunavyojua sisi sote, mazingira ya maisha ya mwanadamu na viumbe wengine hai kuanzia anga ya nyumbani, mitaani, mabustani ya umma, misitu, nyanda, maeneo ya kandokando ya mito na hata vituo vya elimu, utafiti, utamaduni, huduma za umma, ofisi na maeneo ya ibada yote hayo ni mazingira ya maisha ya mwanadamu. Usalama na uzima wa mazingira una mfungamano mkubwa sana na usalama na uzima wa jamii ya mwanadamu. Na kama ambavyo afya na kinga hutangulizwa na kuwekwa mbele zaidi kuliko kutibu kuhusiana na uzima wa mwili wa mwanadamu, vivyo hivyo uzima na usalama wa mazingira unatangulizwa na kupewa umuhimu zaidi kuliko juhudi za kufidia hasara zinazosababishwa na uharibifu wa mazingira. Kutunzwa mazingira na kuyalinda na uharibifu kuna maana na kulinda haki za ardhi, anga, maji, udongo, bahari, mito, majangwa, milima, nyanda, mimea, wanyama na viumbe wengine hai.
Mafundisho ya dini ya Uislamu yametukataza kuchafua mazingira na wakati huo huo yametuamuru kuyasafisha pale yanapochafuliwa. Mtume Muhammad (saw) amesema: Mwenyezi Mungu ni msafi na hupenda usafi. Hivyo basi safisheni mazingira yenu ya maisha".
Hadithi hii inatufunza mambo kadhaa: Kwanza ni kwamba kuchunga usafi na unadhifu wa mwili, maeneo ya kazi, mazingira ya elimu na vituo vya utamaduni na ibada ni kwa ajili ya kuwa mwanadamu ambaye ni khalifa wa Mwenyezi Mungu katika ardhi, analazimika kutekeleza maagizo hayo ya Mwenyezi Mungu na kuyafanya sira na mwenendo wake. Vilevile analazimika kupendelea usafi na unadhifu kwa sababu ni vitu vinavyopendwa na Mwenyezi Mungu.
Nukta nyingine ni kuwa amri hiyo ya usafi na kuwa nadhifu inawahusu wanadamu wote, nyakati zote na pande zote kwa kadiri kwamba wanadamu wote, wanawake kwa wanaume, katika vipindi vyote vya maisha na katika kila upande wanapaswa kusafisha miili, nyumba, na maeneo yao ya kazi na ibada na kuyalinda na uchafu au kuyasafisha pale yanapochafuliwa.
Maumbile ya dunia na mazingira vilipewa umuhimu sana katika maisha na sira ya viongozi wetu wa dini kiasi kwamba Imam Jaafar Swadiq ananukuu hadithi kuhusu maisha ya babu yake, Mtume Muhammad (saw) akisema: Mtume (saw) alipokuwa akipeleka jeshi vitani alikuwa akilikataza kukata mti isipokuwa kama hapana budi kufanya hivyo. (Usulul Kafi:J-5). Amri hiyo ya Mtume ya kukataza kukata miti ni kutokana na taathira kubwa ya miti katika usalama na uzima wa mazingira. Hivyo ni muhimu sana kwa Waislamu kulipa umuhimu suala la kupanda miti kutokana na taathira zake kubwa katika usafi na uzima wa mazingira na hewa. Uislamu umelipa umuhimu mkubwa suala la kupanda miti kiasi cha kulitambua kwamba ni miongoni mwa kazi tukufu za kheri. Imepokewa kwamba Mtume Muhammad (saw) amekuorodhesha kupanda miti katika kazi zenye faida kubwa kama kutoa elimu na mafunzo, kujenga misikiti, kurithisha vitabu na kadhalika. Umuhimu wa kuchunga miti katika Uislamu ni mkubwa sana kiasi kwamba imenukuliwa kwamba Mtume (saw) amesema: "Mtu anayeumwagilia maji mti unaohitaji maji ni sawa na mtu anayempa maji ya kunywa muumini mwenye kiu." Vilevile imepokewa kutokwa kwa mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib kwamba amesema: Matunda ya kujiepusha na ufuska na matunda ya kuwa nadhifu, kusafisha mazingira na kuosha vyombo ni utajiri na kujitosheleza." Hadithi hii ya mjukuu wa Mtume wetu amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Aali zake, inatujuza faida za usafi wa aina mbili, yaani usafi wa roho ya mwanadamu na usafi wa mazingira yake na kutukumbusha kwamba, amali na matendo ya waja yana taathira pia katika maisha yao ya kidunia. Mafundisho ya dini ya Kiislamu pia yanasisitiza kuwa iwapo jamii au taifa litaacha kwa makusudi kujali mazingira na kunyamazia kimya au kupuuza uchafuzi wa neema hiyo kubwa, basi jamii au taifa hilo litashukiwa na hasira ya Mwenyezi Mungu. Imepokewa pia kutokwa kwa Mtume Muhammad (saw) kwamba amesema: Makundi matatu ya watu yatakuwa mbali na rehma za Mwenyezi Mungu: Mtu anayechafua maeneo ya umma (kama barabara, mitaa na mabustani), mtu anayezuia hisa ya maji ya watu wengine, na mtu anayefunga njia ya watu kupita."
Ni wazi kuwa matukio mbalimbali ya dunia yanafuata amali na matendo yanayofanywa na wanadamu. Kwa maana kwamba, kama watamtii Mwenyezi Mungu na kuchagua njia ya kuwa waja wema, hapana shaka kwamba watafunguliwa milango ya baraka na rehma zake. Na kama watapotoka na kuipa mgongo njia ya haki na maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu, basi jamii itakumbwa na ufisadi na uharibifu na mataifa yatakumbwa na maangamizi kutokana na dhulma, vita na ukosefu wa amani na mabalaa mengine. Uhakika huu unaelezwa na Mwenyezi Mungu katika aya 30 ya Suratu Shuura inayosema: "Na misiba inayokusibuni ni kwa sababu ya vitendo vya mikono yenu. Naye anasamehe mengi."
Qur'ani Tukufu inayasanifu mabalaa yaliyozikuta kaumu za Thamud na Aad katika matukio kama haya. Taathira za amali na matendo maovu ya wanadamu katika matukio mengi mabaya hususan katika mazingira zimeashiriwa sana katika Qur'ani Tukufu na hadithi za Mtume (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu. Kwa mfano tu hadithi iliyopokewa kutoka kwa mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) Imam Muhammad al Baqir (as) inasema: Wakati jamii inapofanya madhambi, Mwenyezi Mungu huwa hawapeleki tena watu wa jamii hiyo mvua aliyokuwa amewatengea na badala yake mvua hiyo hunyesha majangwani, milimani na mabarini."
>>>>> <

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)