Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 29 Julai 2015 13:44

Uislamu na Mtindo wa Maisha-74

Uislamu na Mtindo wa Maisha-74

Moja kati ya malengo ya dini tukufu ya Uislamu ni kumlea mwanadamu na kuimarisha itikadi yake ya kumwamini Mungu Mmoja. Suala hilo limepewa umuhimu mkubwa sana katika Uislamu na lilichukua sehemu kubwa zaidi ya ujumbe wa Mtume Muhammad (saw). Mwanadamu aliyelelewa na Uislamu kama kiumbe bora zaidi, analazimika kuratibu uhusiana na mwenendo wake na viumbe vingine vya dunia kwa njia ambayo haitakanyaga haki za kiumbe mwenzake. Kulinda haki za viumbe katika Uislamu hakuhusiani na haki za mwanadamu pekee bali hata mazingira yana haki ambazo Waislamu wanapaswa kuzilinda na kuziheshimu. Kwa maneno mengine ni kuwa, katika mtindo wa maisha wa Kiislamu maagizo ya dini yanamlingania Mwislamu jinsi ya kujenga uhusiano wake na Mwenyezi Mungu, uhusiano wa mja na mazingira anamoishi na uhusiano wake na jamii ya wanadamu wenzake. Uhusiano wa Mwenyezi Mungu na jamii ya wanadamu na mazingira ni uhusiano wa muumbaji na viumbe wake. Aya nyingi za Qur'ani Tukufu zinaonesha kuwa, mazingira na maumbile ya dunia yamesakhirishwa na kuwekwa chini ya udhibiti wa mwanadamu. Kwa maana kwamba Mwenyezi Mungu Muumba ameviumba kwa ajili ya kumhudumia mwanadamu. Hata hivyo uhusiano huo ni wa pande mbili kwa maana kwamba, mazingira na maumbile ya dunia ni amana ya Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu na jamii ya kiumbe huyo ina majukumu ya kufanya mkabala wa neema na amana hiyo. Hivyo basi wakati mwanadamu anapoitambua dunia na maumbile yake kuwa ni amana ya Mwenyezi Mungu kwa kiumbe huyo hapana shaka kwamba atajiepusha kuharibu mazingira na maumbile ya dunia na kulazimika kutumia vyema tunu na neema hiyo.
Mweyezi Mungu Mtukufu ameumba dunia na vilivyomo, ardhi na mazingira na akaviweka chini ya udhibiti wa mwanadamu ili amjaribu na kuona atatumia na kuchunga vipi amana na tunu hiyo katika kumtii na kumcha Yeye. Katika aya ya 7 ya Suratul Kahf, Mwenyezi Mungu SW anasema: "Kwa hakika tumevifanya vilivyoko juu ya ardhi kuwa ni pambo lake ili tuwafanyie mtihani, ni nani kati yao wenye vitendo vizuri zaidi."
Neema na suhula mbalimbali zinaweza kudhamini malengo ya maumbile pale zinapotumiwa vizuri bila ya kuchupa mipaka.
Mafundisho ya Uislamu yamelipa umuhimu mkubwa suala la kulinda mazingira na kutenga thawabu na malipo mema kwa watu wanaohuisha na kufanya juhudi za kulinda tunu hiyo ya Mwenyezi Mungu. Kwa mfano tu Mtume Muhammad (saw) amesema: Mtu yeyote anayepanda mti Mwenyezi Mungu SW humwandikia thawabu na malipo kadiri ya matunda yanayotolewa na mti huo."
Mkabala wake pia iwapo mazingira na maumbile ya dunia hayatatumiwa vizuri na ipasavyo basi jambo hilo litakuwa na athari mbaya na zenye uharibifu kwa mwanadamu. Vilevile Siku ya Kiama mwanadamu ataulizwa kuhusu jinsi alivyotumia neema zote alizopewa yakiwemo mazingira na maumbile ya dunia. Hivyo inatupasa kujua kuwa, mazingira ni neema ya wanadamu wote na kwamba tunawajibika kuilinda na kufanya jitihada za kuistawisha na kutumia vyema matunda yake. Imam Ja'far Swadiq (as) anasema: Maisha hayawezi kuwa matamu bila ya kuwa na hewa safi, maji mengi na ardhi yenye kutoa mazao." (Tuhaful Uqul:325)
Miongoni mwa matatizo makubwa ya dunia ya leo ni kuharibiwa maliasili na uchafuzi wa mazingira ambavyo vyote vinatishia maisha ya mwanadamu. Wataalamu wanasema kuwa, matatizo mengi ya kimaumbile kama mafuriko, uchafuzi wa hewa, kupungua kwa maji ya chini ya ardhi na kuharibiwa kwa Tabaka la Ozone vinasababishwa na uharibifu na uchafuzi wa mazingira. Kwa msingi huo mafundisho ya dini yanaliona suala la kulinda maliasili na mazingira kuwa miongoni mwa masuala muhimu ya kiakhlaki na kiuchumi.
Mtazamo wa Uislamu ambayo ndiyo dini kamili zaidi ya Mwenyezi Mungu kwa maumbile ya dunia na mazingira unatofautiana kikamilifu na mtazamo wa kimaslahi unaowahimiza wanadamu kutumia vibaya maumbile hayo bila ya kujali lolote. Uislamu unatazama mazingira kwa jicho la taadhima na mafundisho ya dini hiyo yanayatambua mazingira kuwa ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Mazingira na vilivyomo ni viumbe vya Allah Mtukufu na Mwenye hikima. Katika aya ya 29 ya Suratul Baqara, Qur'ani Tukufu inasema: Yeye (Mwenyezi Mungu) ndiye aliyewaumbia vyote vilivyomo katika ardhi tena akakusudia kuumba mbingu, na akazifanya mbingu saba. Naye ni mjuzi wa kila kitu."
Wakati huo huo Mwenyezi Mungu SW amejaalia maumbile ya dunia na mazingira kuwa neema kubwa kwa mwanadamu ili avitumia katika maisha yake. Aya ya 13 ya Suratul Jaathiya inasema: "Na (Yeye Mwenyezi Mungu) amevifanya viwatumikie vyote vilivyomo mbinguni na vilivyo katika ardhi, kutoka kwake. Hakika katika hayo zimo ishara kwa watu wanaotafakari."
Kwa utaratibu huo mwanadamu ambaye ni khalifa wa Mwenyezi Mungu duniani amepewa uwezo na elimu ya kutumia si vilivyomo ardhini pekee, bali hata vile vya mbinguni. Kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani pia kinamkataza mwanadamu kufanya ufisadi na uharibifu wa aina yoyote katika ardhi. Aya ya 85 ya Suratul Aaraf inasema: "Wala msifanye uharibifu katika ardhi baada ya kutengenea kwake.." Ni wazi kuwa kuharibu maliasili na kuchafua mazingira ni miongoni mwa vielelezo vya ufisadi na uharibifu wa ardhi unaokatazwa katika aya hiyo.
Hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume na Ahlibaiti zake watoharifu pia zinaitambua ardhi kuwa ni chanzo cha kheri na baraka nyingi na zimeitambua kuwa ni sawa na mama mwenye huruma na upendo kwa mtoto wake. Mtume Muhammad (saw) anasema: "Ilindeni ardhi kwa sababu ndiyo asili na chanzo chenu." Anasema katika hadithi nyingine kwamba: "Msikate mti isipokuwa wakati wa dharura." Katika hadithi nyingine Mtume (saw) anakufananisha kuumwagilia maji mti kuwa ni sawa na kumpa maji ya kunywa muumini mwenye kiu.
Kwa utaratibu huo, katika mtindo wa maisha wa Kiislamu mwanadamu anawajibika katika suala la kudumisha uhai wa maumbile ya dunia na mazingira yake na amewekewa mipaka na kanuni za jinsi ya kutumia neema za dunia. Kama tunavyojua, neema za Mwenyezi Mungu zinazojumuisha misitu, nyanda, milima, majangwa, mito, bahari, hewa na kadhalika ni miongoni mwa sababu za utulivu na salama wa kiumbe mwanadamu na viumbe wengine na kuharibiwa kwa neema hizo au utumiaji wake mbaya husababisha kuondoka usalama na utulivu wa viumbe hao. Pamoja hayo hii leo tunashuhudia jinsi mwanadamu wa leo anavyoharibu mazingira na kuyatumia vibaya, suala linaloifanya dunia ikabiliwe na mgogoro mkubwa. Mwanadamu wa leo amekuwa akitumia maumbile ya dunia, maliasili zake na mazingira kwa mujibu wa maslahi ya muda tu bila ya kujali mustakbali wa dunia na viumbe wenzake na hivyo kuvuruga uhusiano wa kiumbe huyo na mazingira na maumbile ya dunia anamoishi.
Mazingira ni miongoni mwa nguzo kuu za ustawi na maendeleo endelevu yenye taathira na nafasi kubwa katika maisha ya mwanadamu. Ustawi na maendeleo endelevu una maana ya maendeleo ambayo yanakwenda sambamba na kulindwa mazingira na maumbile ya dunia au uharibifu huo kupunguzwa sana na kufikia kiwango cha chini kabisa. Hata hivyo mwenendo wa sasa wa uharibifu wa mazingira unaonesha kuwa iwapo hali itaendelea kama ilivyo si tu kwamba mwanadamu hatapata ustawi na maendeleo endelevu bali pia uhai wa kiumbe huyo na viumbe wenzake utakabiliwa na hatari kubwa ya kuangamia. >>

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)