Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 15 Juni 2015 10:50

Uislamu na Mtindo wa Maisha (73)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (73)

Assalamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya kipindi cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Karibuni kuwa nasi tena katika kipindi cha wiki hii cha Uislamu na Mtindo wa Masha. Tulisema katika kilichopita kwamba mwanadamu anapongalia na kuchungua vyema nafsi yake ataona kuwa, ana hamu ya kupenda na kuvutiwa na kitu au kuchukia na kukataa kitu fulani na matendo na kazi, mwenendo na hali zote za kiumbe huyo zinarejea kwenye hamu hiyo ya kupenda au kuchukia kitu au jambo fulani. Tulisema hali hii ya kinafsi na ya ndani ya dhati ya mwanadamu huwa chanzo cha matendo na mwenendo wake. Kipindi chetu cha leo kinakamilisha mjadala huo. Karibuni......
Katika dini ya Kiislamu Mwenyezi Mungu SW ndiye chanzo na chimbuko la ukamilifu wote na yeye ndiye anayepaswa kupendwa zaidi kuliko jambo lolote lingine. Vilevile katika dini hiyo urafiki na uadui vinapaswa kufanywa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na Mola Muumba ndiye anayepaswa kuwa kigezo cha kupenda au kuchukia na kufanyia uadui kitu kingine chochote. Hivyo, iwapo Mwenyezi Mungu atakuwa kigezo na mizani katika mapenzi na uadui, mahusiano, biashara na mambo mengine yote ya kimaisha mwanadamu atakuwa katika ibada wakati wote na suala hilo litamtayarishia uwanja wa kupata radhi zake Mola Muumba.
Mtume (saw) anasema: Mpendeni Mwenyezi Mungu kwa dhati." Hii inaonesha kuwa, mapenzi ya mtu yeyote yule kwa Mwenyezi Mungu hayakamiliki bila kumpenda Yeye Mola Muumba kuliko kitu kingine chochote. Watu wanaompenda kwa dhati Mwenyezi Mungu Yeye pia huwapenda wa kuwanyooshea mambo yao. Imepokewa katika Hadithi Qudsi kwamba Mwenyezi Mungu amesema: Mimi ni rafiki wa mtu anayenipenda, mwenza wa anayeniweka mimi karibu yake na wa karibu zaidi kwa mtu anayekuwa pamoja na Mimi kwa kunitaja na kunikumbuka."
Kwa msingi huo katika mtindo wa maisha wa Kiislamu kigezo kikubwa zaidi cha urafiki na uadui ni Yeye Mwenyezi Mungu SW. Kumpenda Mwenyezi Mungu huupa mwelekeo mtindo wa maisha ya Mwislamu na wakati huo, yaani Mwenyezi Mungu anapofanywa kigezo cha kupenda au kuchukia kitu, muumini huwa na pande mbili muhimu katika maisha yake: Upande wa mwelekeo chanya kwa maana ya imani na kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, na upande wa mwelekeo hasi kwa maana ya kukana na kupinga matwaghuti, madhalimu, masanamu na kila kisichokuwa na uhusiano na Mola Muumba. Uhakika huu ndio unaoelezwa katika neno la Tauhidi la "Laa ilaha illallah", kwa maana kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu Mmoja. Muumini wa kweli awali hukana na kujiweka mbali na matwaghui na masanamu ya mawe na wanadamu, na kisha humwamini na kushikamana barabara na Mwenyezi Mungu.
Kwa msingi huo kila muumini anapawa kumwamini vilivyo Mwenyezi Mungu na haki na kupambana na dhulma na batili. Hivyo kuweka sawa na kuitazama kwa jicho moja haki na batili na kutotofautisha kati ya viwili hivyo kunakinzana na mafundisho ya Tauhidi na Uislamu. Kwani haiwezekani kwa mtu kumpenda Mwenyezi Mungu, Mtume na kizazi chake kitoharifu na wakati huo huo akaipenda batili, wafuasi wa batili na wale wanaopiga vita haki na kweli au wanaowapiga vita, kuwachukia na kuwaua Watu wa Nyumba ya Mtume (saw). Katika mafundisho ya Uislamu na Tauhidi mipaka ya mienendo ya kijamii, kisiasa na kadhalika ya mwanadamu inaainishwa na kuwapenda Waislamu na waumini wenzake na Mwenyezi Mungu na kujitenga na maadui zao. Aya ya 10 ya Suratul Hashr inaeleza umuhimu wa kuwapenda ndugu katika imani kwa kusema: Na waliokuja baada yao wanasema: Mola wetu! Tughufirie sisi na ndugu zetu waliotutangulia katika imani, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu kinyongo dhidi ya walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mpole, Mwingi wa rehema."
Kwa mujibu wa aya hii, moyo wa muumini haupaswi kuwa na kinyongo, chuki na uadui dhidi ya muumini na Mwislamu mwenzake. Qur'ani tukufu inawataka waumini kujiepusha na kitu chochote kinachosababisha chuki, kinyongo na uadui kwa muumini mwenzake na inawaamuru Waislamu kumwomba Mwenyezi Mungu asijaalie uadui na vinyongo baina yao na ndugu zao katika imani. >>>
Sheria na mafundisho ya Uislamu daima yanawahimiza wafuasi wa dini hiyo kujiepusha na hitilafu na badala yake waeneze moyo wa upendo, mahaba na kusaidiana katika jamii. Hata hivyo yumkini kukajitokeza ogomvi wa hapa na pale au hitilafu na ukosefu wa maelewano baina ya Waislamu kutokana na vishawishi vya shetani. Katika mazingira kama haya mafundisho ya Uislamu- kama ilivyonukuliwa kutoka kwa Mtume (saw)- yanasisitiza kuwa, hairuhusiwi kwa Waislamu kukasirikiana na kuendelea kuhasimiana kwa siku tatu bali wanalazimika kukomesha uhasama na ogomvi huo na kutatua hitilafu na ugomvi wao.
Katika upande mwingine Qur'ani tukufu imewawajisha Waislamu kujibari na kujitenga na maadui wa Mwenyezi Mungu na haki. Kwa mfano tu aya ya 22 ya Suratul Mujadila inasema: Huwapati watu wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho wakiwapenda wale wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao au watoto wao, au ndugu zao au jamaa zao. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amethibitisha imani katika nyoyo zao na akawatia nguvu kwa Roho itokayo kwake. Na atawaingiza katika mabustani ipitayo mito mbele yake, humo watakaa daima. Mwenyezi Mungu amekuwa radhi nao na wao wamekuwa radhi naye. Hao ndiyo kundi la Mwenyezi Mungu. Sikilizeni! Hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndilo linalofaulu."
Aya hii ya Qur'ani inatafunza kwamba, katika mtindo wa maisha wa Kiislamu haiwezekani kukusanya pamoja mapenzi ya Mwenyezi Mungu na kuwapenda maadui zake katika moyo mmoja na kwamba hapana budi kwa muumini kuchagua moja kati ya mawili hayo. Ama kumpenda Mwenyezi Mungu, Mitume wake na mawalii wake au kuwapenda maadui wa Mwenyezi Mungu, Mitume na mawalii wake. Hivyo basi wale wanaokusanya yote mawili ama wana imani dhaifu au ni wanafiki. Hivyo waumini wa kweli hawawezi kumpenda yoyote yule kuliko Mwenyezi Mungu. Si hayo tu bali kigezo cha kuwapenda watu azizi kwake kama baba, mama, ndugu na jamaa wa karibu ni watu hao kutofanya uadui na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kwa utaratibu huo inaeleweka kuwa, hata hisia za kiroho hazikuachwa hivi hivi bila ya kidhibiti wala mipaka ya mantiki na kanuni za dini.
Hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume na Ahlibaiti zake watoharifu pia zimetilia mkazo suala la kupenda na kuchukia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Imepokewa kwamba Mtume (saw) amesema: Msingi imara wa imani ni kupenda na kufanya uadui kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kushikamana na mawalii wake na kujitenga na maadui zake."
Tunakamilisha kipindi hiki kwa kusisitiza kuwa aya za Qur'ani Tukufu na Hadithi za Mtume na Ahlul Bait (as) zinatufunza kwamba kuwapenda watu wengine kunapaswa kutokana na kumpenda Mwenyezi Mungu na Mitume wake, mawalii wake na haki na kweli. Na huu ndio upande mmoja wa maana ya kalima ya Tauhidi ambayo upande wake mwingine una maana ya kujitenga na kujiepusha na matwaghuti, masanamu, madhalimu, maadui wa haki na kweli, na maadui wa dini ya Mwenyezi Mungu, mitume wake na maawalii wake.
Wapenzi wasikiliza muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi chetu umemalizika. Tukutane tena wiki ijayo panapo majaaliwa ya Allah. Kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)