Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Ijumaa, 12 Juni 2015 11:35

Uislamu na Mtindo wa Maisha (72)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (72)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya kipindi cha Uislamu na Mtindo wa Maisha ambacho leo kitajadili jinsi ya kuamiliana na watu wa aina mbalimbali katika mtindo wa maisha wa Kiislamu. >
Kama bado mnakumbuka katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia suala la jinsi ya kuamiliana na wasio Waislamu na kusisitiza kuwa Uislamu umewahimizia wafuasi wake kuwalinda na kuwajali kwa upendo na mahaba hata wasio Waislamu. Sheria za dini hiyo daima zinasisitiza kulindwa sheria, kuwa na mwenendo mzuri, kuishi kwa amani na wanadamu wote hususan wafuasi wa dini nyingine, sawa wawe wale wanaoishi katika jamii na utawala wa Kiislamu au katika jamii isiyo ya Kiislamu.
Leo tunatupia jicho vigezo muhimu vya namna na jinsi ya kuamiliana na watu wengine katika mtindo wa maisha wa Kiislamu na kutokana na umuhimu wake, jambo hilo linahesabiwa kuwa ni miongoni mwa matawi ya dini. Vigezo hivyo ni vile vinavyotajwa katika istilahi za Kiislamu kwa maneno ya "tawali" na "tabarri". Neno tawalli lina maana ya kufanya urafiki na usuhuba na marafiki wa Mwenyezi Mungu, na tabarri linamaanisha kujitenga na kuwa mbali na maadui wa Mwenyezi Mungu. Suala la urafiki na uadui lina historia ndefu. Makabiliano na mpambano wa urafiki na uadui vilianza baina ya wanadamu baada ya kumwagwa kidhulma damu ya mwana wa Nabii Adam, Habiil, bali kabla yake wakati Iblis aliyelaaniwa alipokataa kumsujudia Adam kutokana na kiburi na kujiona na akafukuzwa katika neema za Mwenyezi Mungu. Suala hilo limekuwa sababu ya mwanadamu daima kujiona njia panda, baina ya njia ya kheri na shari, haki na batili huku akiwa na uhuru wa kuchagua moja kati ya njia hizo mbili.
Kama mnavyojua, dunia hii inatawaliwa na kanuni ya nguvu ya mvutano. Kwa maana kwamba, viumbe vya dunia hii huvuta na kuvutwa na vitu vinavyooana navyo, na kusukumia mbali vile visivyowiana na kuoana navyo. Vivyo hivyo mwanadamu, ameumbwa kwa namna ambayo huvuta vitu anavyonasibiana na kuoana navyo na kusukumia mbali vile visivyonasibiana na yeye. Kila anapongalia na kuchungua vyema nafsi yake ataona kuwa, ana hamu ya kupenda na kuvutiwa na kitu au kuchukia na kukataa kitu fulani na matendo na kazi, mwenendo na hali zote za kiumbe huyo zinarejea kwenye hamu hiyo ya kupenda au kuchukia kitu au jambo fulani. Kwa hakika tunaweza kusema kuwa, hali hii ya kinafsi na ya ndani ya dhati ya mwanadamu huwa chanzo cha matendo na mwenendo wake. Mwenyezi Mungu SW ameweka hisi za aina mbalimbali kama za ghadhabu na hasira katika nafsi ya mwanadamu ili aweze kuzitumia kwa ajili ya kulinda ujudi na kuwepo kwake. Kwa mfano hisi za upendo na kupenda zimewekwa katika dhati ya mwanadamu ili azitumiwe kuvuta vitu vinavyonasibiana na kuwiana na ujudi na uwepo wa kiumbe huyo, na zile za ghadhabu na hasira zimewekwa katika nafsi yake ili zitumike kusukumia mbali na kujilinda na vitu visivyonasibiana na kuweza kujinda. Kama mwanadamu hatakuwa na hisi kama hizi katika dhati na nafsi yake basi hapana shaka kuwa hatavutiwa kimaumbile na mambo kama chakula, maji na kadhalika au hatakuwa na msukumo wa kidhati na kimaumbile wa kujilinda na hatari zinazomkabili; na matokeo ya hali kama hii ni kuangamia kiumbe mwanadamu.
Nukta nyingine muhimu ni kuwa, katika maisha yake mwanadamu huwa na neema kubwa na yenye thamani ambayo na uhuru wa kukhitari na kuchagua. Tunaweza kusema kuwa saada na ufanisi au maangamizi na hasara ya milele ya mwanadamu inafungamana kwa kiwango kikubwa na vitendo anavyofanya kwa kutumia neema hii ya kukhitari na uhuru wa kuchagua. Irada ya mwanadamu pia kwa upande wake inapatikana kutokana na hamu ya kupenda au kuchukia kitu. Ni wazi kuwa mwanadamu mzima kiroho na kinafsi hawezi kuwa na mtazamo sawa kuhusu kila kitu au watu wote katika maisha yake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mwanadamu katika maisha yake ya dunia kuna vitu anavyopenda na kuchukia vingine katika jitihada zake za kufikia malengo yake maishani. Kwa msingi huo huwapenda baadhi ya watu wanaooana na malengo yake na kuwachukia wengine. Ni kutokana na ukweli huu ndiyo maana hisi za ndani ya nafsi ya mwanadamu hususan hizi ya kupenda na kuchukia, vikapewa umuhimu mkubwa katika mtindo wa maisha wa Kiislamu.
Imepokewa kwamba siku moja Mtume (saw) aliwauliza maswahaba zake kwamba: Ni ipi sababu na nguzo imara zaidi ya imani? Walisema: Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanajua zaidi. Baadhi walisema ni Swala, wengine wakasema ni Zaka na wengine wakasema ni Hija na Umra. Masahaba wengine waliingilia kati na kusema ni kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Mtume (saw) alisema: Kila kimoja kati ya yaliyosemwa kila ubora wake lakini si sababu na nguzo imara zaidi ya imani, bali nguzo hiyo ni kupenda katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuwafuata vipenzi vyake, na vilevile kuchukia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu."
Umuhimu wa suala hilo unatokana na kwamba urafiki na uadui hufuatiwa na matendo, kuathiri au kuathiriwa na kuainisha mwenendo na njia ya kufuata katika maisha ya mtu binafsi na jamii. Kufaulu na kuangamia kwa mwanadamu pia hufungamana na suala kwamba anampenda na kumfuata nani maishani mwake. Imepokewa kutoka kwa Nabii Mussa (as) kwamba Mwenyezi Mungu alimteremshia wahyi na ufunuo akisema: Je, hadi sasa ulishawahi kufanya amali yoyote kwa ajili yangu mimi? Musa alisema: Ndiyo Mola wangu. Nimeswali kwa ajili yako, nikafunga swaumu kwa ajili yako wewe, nikatoa mali yangu kwa ajili yako na ninakutaja na kukumbuka wewe." Mwenyezi Mungu alisema: Swala kwako wewe ni alama ya haki, na swaumu ni ngao na kinga yako na moto, kutoa mali ni kivuli chako katika Siku ya Kiyama na kunitaja na kunikumbuka mimi ni nuru yako. Sasa hebu nambie ni amali ipi uliyoifanya kwa ajili yangu mimi tu?
Mussa alisema: Mola wangu! Nielekeza Wewe. Mwenyezi Mungu alisema: Je, ulishawahi kumpenda mtu yeyote kwa ajili yangu mimi na kumchukia mtu yeyote kwa ajili yangu? Hapa ndipo Nabii Mussa alipoelewa kwamba amali bora zaidi ni kupenda na kuchukia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.
Jambo tunalopaswa kusema hapa kuhusu kupenda na kuchukia katika mtindo wa maisha wa Kiislamu ni kwamba, kupenda ya kufanya uadui haviwekwi katika safu moja na amali nyingine njema za mwanadamu bali nguzo hizo mbili muhimu huzipa roho amali nyingine zote za mja.
Imepokewa kutoka kwa Imam Muhammad al Baqir (as) kwamba amesema: Kama unataka kujua kwamba wewe ni mwanadamu mzuri basi angalia moyo wako. Kama unawapenda watu wanaomtii Mwenyezi Mungu na kuwachukia wanaomuasi basi wewe ni mwanadamu mzuri na unapendwa pia na Mwenyezi Mungu. Lakini kama unawachukia watu wanaomtii na kumcha Mwenyezi Mungu na kuwapenda wanaomuasi basi elewa kuwa hakuna kheri katika roho na nafsi yako na Mwenyezi Mungu atakuwa adui yako, kwa sababu mwanadamu daima huambatanishwa na anachokipenda."
Maneno haya ya Imam Baqir (as) yanaonesha taathira ya kupenda na kuchukia katika mfumo wa mtindo wa maisha wa Kiislamu. Na kwa kuwa katika mtazamo wa Kiislamu, Mwenyezi Mungu SW ndiye mwenye ukamilifu na uzuri wote, waumini humtambua Yeye SW kuwa ndiye chimbuko la ukamilifu na kila jema na hivyo humpenda na kumuashiki Yeye kuliko kila kitu walichonacho. Kwa msingi huo kupenda na kuchukia au uadui katika mtindo wa maisha wa Kiislamu kunapaswa kufanyika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Hivyo basi kama kupenda na kuchukia kitu chochote kutafanyika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu mafungamano na uhamasa na uadui wote wa mwanadamu utafanyika katika mipaka yake Mola Muumba na kwa ajili ya kupata radhi Zake. >>>
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu leo umemalizikaa. Tukutane wiki ijayo katika kipindi kingine inshaallah. Kwaherini....

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)