Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 10 Juni 2015 10:32

Uislamu na Mtindo wa Maisha (71)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (71)

Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi katika sehemu ya 71 ya Uislamu na Mtindo wa Maisha. Katika vipindi kadhaa vilivyopita tulizungumzia namna ya kuamiliana na makundi mbalimbali ya watu kama wagonjwa, jirani na watu wenye haja na matatizo kwa mujibu wa mtindo wa maisha wa Kiislamu. Kipindi chetu leo kitazungumzia jinsi ya kuamiliana na wasio Waislamu. .
Uislamu ni dini ambayo mafundisho yake yamesimama juu ya msingi wa upendo na mahaba na inasisitiza sana juu ya mahusiano mema ya kijamii. Dini hiyo imesisitiza sana suala hilo kiasi kwamba imewahimzia wafuasi wake kuwalinda na kuwajali kwa upendo na mahaba hata wasio Waislamu. Sheria za dini hiyo dima zinasisitiza kulindwa kanuni, kuwa na mwenendo mzuri, kuishi kwa amani na wanadamu wote hususan wafuasi wa dini nyingine sawa wawe wale wanaishi katika jamii na utawala wa Kiislamu au katika jamii isiyo ya Kiislamu. Tangu kudhihiri kwake, Uislamu ulitanguliza wito wa kuishi pamoja kwa amani na wafusi wa dini zote za mbinguni. Aya ya 64 ya Suratu Aal Imran inasema: Sema: Enyi watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno la usawa baina yetu na baina yenu kwamba, tusimwabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu wala tusimshirikishe na chochote. Wala baadhi yetu wasiwafanye baadhi kuwa waungu zaidi ya Mwenyezi Mungu. Wakikataa semeni: Shuhudieni ya kuwa sisi ni Waislamu."
Maagizo mengi ya Mtume (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu kuhusu suala la kuishi kwa amani na wafuasi wa dini nyingine yanaonesha kuwa, Uislamu hauna nia mbaya wala hautaki kuingia katika vita na wasio Waislamu bali mafundisho ya dini hiyo yanawahimiza wafuasi wake kuchunga uadilifu, insafu, haki na kujiepusha kuwakera na kuwaudhi wafuasi wa dini nyingine isipokuwa pale wanapovunja ahadi na makubaliano au kufanya uhaini, au kuwashambulia na kuwapiga vita Waislamu; na katika hali kama hii ndipo Uislamu unapowaamuru wafuasi wake kupambana na wahalifu kwa ajili ya kuzima fitina. Aya ya 8 ya Suratul Mumtahina inasema: Mwenyezi Mungu hakukatazeni kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu."
Katika sehemu ya barua yake kwa Malik al Ash'tar aliyemteua kuwa gavana wake nchini Misri, Imam Ali bin Abi Twalib anasema: Kama utafunga mkataba na adui au ukamwahidi kumpa hifadhi basi tekeleza ahadi zako na uziheshimu na uwe tayari kutoa nafsi yako katika kutekeleza ahadi hizo.. kamwe usivunje ahadi na makubaliano na usifanye hiana katika ahadi.
Katika sehemu nyingine ya barua yake kwa Malik al Ash'tar, Imam Ali (as) anasema: Ewe Malik! Kuwa mwema na mpole na watazame raia wako kwa jicho la upendo na kifua kilichojaa mahaba. Usipore mali na kuua nafsi za watu mithili ya mnyama. Ewe Malik! Elewa kuwa, raia wako ni watu wa aina mbili: Ama ndugu zako katika dini au wanadamu baki na wenzako wewe katika maumbile." Hivyo haifai kumfanyia uhamasa na uovu mtu ambaye ni sawa na wewe katika ubinadamu na maumbile.
Uislamu pia umewahimiza wafuasi wake kujiepusha na inadi, ukaidi na maneno machafu wakati wanapowalingania na kuwaita wafusi wengine katika neno la haki na ibada ya Mungu Mmoja na kuwataka wajadiliane nao kwa wema. Aya ya 46 ya Suratul Ankabut inasema: Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri kabisa, isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini yaliyoteremshwa kwetu na yaliyoteremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja. Na sisi ni wenye kusilimu kwake."
Katika aya hii Mwenyezi Mungu SW anaashiria jinsi ya kujadiliana na Ahlul Kitabu ambao ni pamoja na Wakristo na Wayahudi na kumwamuru Mtume wake ajadiliane nao kwa njia iliyobora kabisa. Wafasiri wa Qur'ani wanasema miongoni mwa vielelezo vya kujadiliana kwa wema na kwa njia bora ni kujiepusha na maneno machafu, ukaidi, uhasama na kudunisha na kudharau itikadi na matukufu ya upande wa pili.
Sira na mwenendo wa Mtume wetu Muhammad (saw) katika kuamiliana na wasio Waislamu pia ni kigezo na ruwaza njema ya mtindo wa maisha wa Kiislamu akwa wafusi wote wa mtukufu huyo. Mtume (saw) alikuwa akiamiliana na watu ambao hawakumwamini kwa upole, busara na mantiki. Aliamiliana na Mayahudi na Manaswara kwa upole, subra na kifua kipana na aliheshimu haki zao za kibinadamu na kuwadhaminia uhuru wao wa kidini licha ya ufidhuli na maovu yaliyokuwa yakifanywa na baadhi yao dhidi ya mtukufu huyo na Waislamu kwa ujumla. Alikuwa akivumilia matusi na maudhi ya baadhi ya makundi ya wasio Waislamu na daima alikuwa akimwomba Mwenyezi Mungu awaongoze njia iliyonyooka. Hakukata tamaa au kujibu baya kwa baya jingine, bali alijitahidi kadiri ya uwezo kuwaonesha mwanga na njia ya saada na ufanisi wa kudumu. Alikuwa tabibu anayezungukazunguka akiwatafuta wagonjwa na kujaribu kutibu maradhi yao ya kiroho na kiitikadi. Imam Ali bin Abi Twalib anasema: Mtume (saw) alikuwa tabibu aliyekuwa akiwafuata wagonjwa wake, na kuzunguka na dawa mkononi kuwatafuta wagonjwa waliosahaulika..."
Huyu ndiye yule tabibu aliyekuwa akiwafuata washirikina waliokuwa na maradhi ya nyoyo wa Makka huku baadhi yao wakimpiga kwa mawe na kumwita majnuni na mwendawazimu hadi walifikia kumfukuza katika mji huo na akalazimika kwenda milimani. Wakati huo Bibi Khadija na Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) walikuwa wakimfuata mtukufu huyo na kujaribu kufunga na kutia dawa kwenye majeraha yake. Hata hivyo Muhammad Mwaminifu badala ya kuwalaani washirikina hao daima alikuwa akiwaombea dua na kusema: "Mola wangu Mlezi! Wasamehe watu wa kaumu yangu, kwa sababu wao ni watu wasiojua."
Kwa hakika lengo la Mtume Muhammad (sawa) lilikuwa kuwaongoza washirikina na maadui wake na hata alipolazimika kukabiliana na maadui wake kwanza aliwalingania Uislamu na amani; na kama watakubali basi mambo yote yaliisha kwa amani na suluhu, kama ilivyokuwa katika vita vya Taif. Wakati huo Waislamu waliwazingira watu wa kabila la Thaqiif waliokiuka ahadi zao lakini watu hao waliamua kutuma ujumbe kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu na kukubali wito na mafundisho yake. Mtume (saw) alikubali kufanya suluhu na makubaliano na watu wa kabila hilo. Mtukufu huyo pia alifunga mikataba ya suluhu na amani hata na maadui zake wakubwa kabisa yaani Mayahudi. Aliwambia kuwa kama wataacha vitimbi na uadui wao wataishi kwa amani na usalama pamoja na Waislamu na hali iliendelea kuwa hivyo Mayahudi wakiishi kwa amani na usalama pamoja na Waislamu hadi Mayahudi wa banii Qainuqai walipowaua Waislamu kidhulma na kuvunja makubaliano ya suluhu na amani. Wakati huo Mtume (saw) alisimama kukabiliana nao. Hata hivyo hata baada ya yote hayo na kabla ya kuanza vita, Mtume aliwahutubia akisema: Enyi Mayahudi! Mwogopeni Mwenyezi Mungu ili musije kukumbwa na naliyowapata Makuraish. Silimuni ili mpate amani. Mnajua vyema kuwa mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mumeyaona hayo katika vitabu vyenu.."
Msimamo huo wa Mtume (saw) mbele ya Mayahudi waliokuwa wamevunja makubaliano na kukiuka ahadi unaonesha ni kwa kiwango gani mtukufu huyo alifanya jitihada za kuzuia umwagaji wa damu na vita hata na mahasimu wake wakubwa kama Mayahudi waliokuwa wakifanya vitimbi vya aina mbalimbali na kuua Waislamu wasio na hatia yoyote.
>> Wapenzi wasikiliza muda wa kipindi chetu umemalizika. Tukutane katika kipindi kijacho panapo majaaliwa ya Mola. Kwaherini.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)