Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 08 Juni 2015 15:48

Uislamu na Mtindo wa Maisha (70)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (70)

Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya kipindi cha Uislamu na Mtindo wa Maisha ambacho leo kitaendelea kujadili umuhimu wa kufanya ihsani na wema katika mtindo wa maisha wa Kiislamu. Tafadhali endelea kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki.

>>>


Kama tuliyosema katika kipindi kilichopita, ihsani na kutenda wema ni amali na kitendo cha kifitra na kimaumbile kinachokubaliwa na kuungwa mkono na wanadamu wote kwa ujumla. Dini zote za mbinguni hususan Uislamu zimetilia mkazo na kuipa umuhimu mkubwa sifa hiyo njema na kibinadamu.
Watu wema katika vipindi na zama zote hufanya jitihada za kujipamba kwa sifa hiyo njema. Mwenyezi Mungu Mtukufu pia hutazama dunia na vilivyomo kwa jicho la ihsani na anawataka viumbe wake bora yaani wanadamu, kutenda ihsani na wema. Jamii huwa kama familia kubwa ambayo mfungamano baina ya wanachama wake hutengenezwa na hisia za upendo huruma na kutenda ihsani. Ni upendo, huruma na ihsani ndivyo vinavyowakutanisha pamoja wanadamu na kuwafanya wanachama wa familia moja.
Pamoja na hayo tunapaswa kusema kuwa, sifa hii ya ihsani na kutenda wema haipatikana isipokuwa katika wanadamu wenye imani na itikadi ya Mwenyezi Mungu na Siku ya Malipo au watu ambao wao wenyewe walishawahi kukumbana na mashaka na tabu na wanajua vyema uchungu na maumivu ya watu wenye haja na matatizo ya kimaisha. Hii ni kwa sababu watu ambao hawaelewi vyema uchungu na matatizo hawawezi kuumizwa na matatizo ya wanadamu wenzao wala kufanya jitihada za kuwafariji na kuwaondolea matatizo yao. Imam Mussa al Kadhim (as) anasema: Kufanya ihsani na kutenda wema hakuna thamani wala nasafi kwa mtu ambaye hajawahi kuonja shida na matatizo,." (Biharul Anwar, 78:33)
Uislamu kuliko dini, mifumo na kanuni zote za wanadamu, umetilia mkazo na kuhimiza mno suala la ihsani na kuwasaidia watu wasiojiweza katika jamii na kukidhi mahitaji yao ya kimaada na kiroho. Qur'ani Tukufu, Suna za Mtume na Ahlibaiti zake watoharifu na fiqhi na sheria za Uislamu zimejaa kanuni na miongozo ya jinsi ya kudhamini mahitaaji ya watu wenye haja katika jamii.
Katika jamii ya Kiislamu maslahi ya mtu mmoja yanafungamana kikamilifu na ya wanadamu wenzake na wote kwa pamoja huwa kama ngome imara na walinzi wa kila mmoja wao, na wana wajibu wa kushughulikia matatizo ya kila mmoja wao. Hii ni kwa sababu jamii ya Kiislamu imejengeka kwa msingi wa muawana, mfungamano na kusaidiana. Watu wote katika jamii ya Kiislamu huwa mithili ya viungo vya mwili mmoja na kila mmoja wao anawajibika mbele ya Mwislamu mwenzake sawa kabisa anavyowajibika kulinda uhai na hali bora ya kimaisha yake yeye mwenyewe.
Uislamu umelifanya suala la kuondoa matatizo na mashaka ya wanadamu wenye tabu kuwa sehemu ya ratiba zake za kimsingi na situ kwamba umewatengea thawabu na malipo maalumu ya dunia na Alkhera watu wanaotenda wema na ihsani, bali pia umeainisha majukumu ya kila Mwislamu katika uwanja huo na jinsi na kukidhi mahitaji na kuondoa mashaka ya watu. Mbali na haki za wajibu za kifedha zilizoainishwa na Uislamu kama Zaka na Khumusi (moja ya tano ya mali inayosalia baada ya matumizi ya mwaka), dini hiyo pia imeweka kanuni nyingine zinazowahusu matajiri na wenye uwezo wa kifedha na kuwausia kujiepusha na israfu, ufujaji na kadhalika na kutumia uwezo wao wa kifedha kwa ajili ya kuwasaidia wasiojiweka au watu wenye mashaka na haja.
Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya ya 7 ya Suratu Twalaq kwamba: "Mwenye wasaa (katika mali miongoni mwenu) atoe kadiri ya wasaa wake, na yule aliyepungukiwa katika rizki yake atoe katika kile alichopewa na Mwenyezi Mungu (kadiri ya uwezo wake), Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu yeyote ila kwa kadiri ya alichompa, na atajaalia Mwenyezi Mungu baada ya dhiki faraja."
Vilevile anasema katika aya ya 273 ya Suratul Baqarah kwamba: (Toeni mali zenu) kwa ajili ya mafukara waliozuiliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu, wasioweza kwenda huko na kule katika ardhi (kufanya kazi na kutafuta riziki). Asiyejua hali zao anawadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia kwao kuomba. Utawajua (kuwa ni wahitaji) kwa alama zao, hawaombi wakang'ang'ania. Na mali yoyote mnayoitoa kwa hakika Mwenyezi Mungu anaijua."
Vilevile hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu kuhusu suala la kuwasaidia wasiojiweza kifedha na wenye haja na kuwaondolea matatizo yao zinasisitiza sana udharura wa kusaidiwa watu hawa. Mtume (saw) amesema: Waumini ni ndugu na hukidhi haja za wenye haja miongoni mwao wao kwa wao, na Mwenyezi Mungu huwatimizia haja na matakwa yao. Amali bora zaidi ya muumini mbele ya Mwenyezi Mungu ni kumfurahisha muumini mwenzake, au kushibisha njaa yake au kumuondolea mashaka yake au kumlipia deni lake au kumpa mavazi na nguo", mwisho wa hadithi.
Kama tunavyoona katika aya za Qur'ani na Hadithi za Mtume, suala la kukidhi mahitaji ya ndugu wenye haja na matatizo katika dini linapaswa kuwa utamaduni na ada ya umma katika mtindo wa maisha wa Kiislamu, kwa kadiri kwamba watu wote katika jamii wanafanya jitihada za kukidhi haja za wenzao. Imam Ali bin Abi Twalib (as) alimuusia sahaba wake mwema, Kumail bin Ziad akisema: Ewe Kumail! Iamuru familia yako kufanya jitihada kubwa za kujipamba kwa maadili bora na ijipinde kukidhi haja na matakwa ya watu hata katika usiku wa giza totoro. Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu anayemiliki nafsi yangu kwamba, hakuna mtu anayemfurahisha muumini ila Mwenyezi Mungu huifanya amali hiyo njema kuwa hazina ya rehma yake inayomuokoa na kumfikia haraka kuliko maji yanayotitirika wakati inapoteremka balaa au wakati wa mashaka na taabu...."
Miongoni mwa njia za kuwasaidia wenye hata na matatizo katika utamaduni wa Kiislamu ni misaada ya kijamii. Misaada hiyo huwa huduma zinazotolewa na waumini na watu wote katika jamii ya Kiislamu ambapo kila mmoja wao huchukua dhamana ya kukidhi mahitaji ya mwenzake asiyejiweza kadiri ya uwezo wake. Misaada hiyo ya kijamii imetajwa katika Qur'ani na Suna za Mtume (saw) na Ahlubaiti zake kwa kutumia majina na anwani mbalimbali kama kutenda wema na ihsani, kujitolewa na kadhalika. Mfano wake ni waumini na matajiri katika jamii kusabilia sehemu ya pato lao kwa ajili ya kuwasaidia masikini na mafukara au kwa ajili ya kutumiwa kwa maslahi ya umma na jamii. Suala hilo huzuia kurundikana mali na utajiri wa taifa katika mikono ya kundi dogo la watu na kuimarisha moyo wa udugu na upendo katika jamii.
Kwa ujumla ni kuwa Uislamu umetambua juhudi za kuondoa umaskini na matatizo ya kimaisha katika jamii kuwa ni wajibu wa umma mzima. Kwa mnasaba huo Qur'ani Tukufu inasema kuwa miongoni mwa sifa makhsusi za watu wanaokadhibisha dini ni kutojali hali za watu maskini, mafukara na wasiojiweza. Aya ya kwanza hadi tatu za Suraatul Maau'n zinasema: Je, umemuona anayekadhibisha dini? Huyo ni yule ambaye humsukumia (mbali) yatima. Wala hawahimiza watu kumlisha maskini."
Kwa msingi wa aya hizo za Qur'ani, ni muhali kwa mtu anayeamini dini ya Uislamu kupuuza na kutojali hali ya watu maskini na wasiojiweza katika jamii hususan waumini na Waislamu wenzake.

>>>>>


Wapenzi wasikilizaji muda wetu umemalizika. Tukutane tenaa wiki ijayo katika sehemu nyingine yaa Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kwaherini.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)