Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 01 Juni 2015 14:07

Uislamu na Mtindo wa Maisha (69)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (69)

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kipindi chetu leo kitazungumzia umuhimu wa kuwasaidia wanadamu wenzetu na udharura wa kufanya ihsani na wema kwa mujibu wa mtindo wa maisha wa Kiislamu.

... >>>>> <....


Ihsani na kufanya wema ni jambo la kimaumbile na kifitra na la ndani ya dhati ya wanadamu. Bali tunaweza kusema kuwa, Mwneyezi Mungu Mtukufu ameweka hamu na hisi ya kupenda kufanya wema na kuwasadia wanadamu wenzetu katika dhati na nafsi zetu. Kimaumbile, wanadamu huvutiwa na mambo mazuri na ya kupendeza na ni kwa msingi huo ndiyo maana wanadamu husifu na kupongeza mambo mema na mazuri.
Kuetenda wema na ihsani kunatambuliwa kuwa ni miongoni mwa kazi nzuri na za kupendeza kutokana na kumpa mtu hisi nzuri na ladha za kiroho na kimaanawi, na jambo kama hilo hupongezwa na kupendwa na wanadamu wote isipokuwa wale wenye maradhi ya kinafsi. Katika aya nyingi z Qur'ani Tukurfu, Mwenyezi Mungu SW amesifu kufanya ihsani na vilevile watu wanaofanya ihsani. Aya ya 122 ya Suratul Baqara inasema: Sivyo hivyo, Yoyeto anayeusilimisha uso wake kwa Mwenyezi Mungu hali anatenda mema basi ana malipo yake kwa Mola wake, wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika."
Katika aya hii Mwenyezi Mungu SW anazungumzia suala la kufanya wema na kuwasaidia watu wengine baada ya kuzungumzia suala la mwanadamu kuelekea kwake Yeye. Hii inamaanisha kwamba, athari nzuri za kumwamini Mwenyezi Mungu zinadhihiri katika matendo ya mja kwa kuwatendea ihsani na mema waja wake. Dini zote za mbinguni hususan Uislamu zimelipa umuhimu mkubwa suala la ihsani na kutenda wema na waumini wa kweli na watu wenye fikra sahihi daima wamekuwa wakifanya jitihada za kujipamba kwa sifa hii njema.
Katika mafundisho na utamaduni wa Kiislamu, kufanya wema na ihsani ni bora zaidi kuliko hata kufanya uadilifu kwa sababu maana ya uadilifu ni mwanadamu kutenda wajibu wake na kuchukua haki yake; lakini ihsani ina maana ya mwanadamu kutenda zaidi ya wajibu na majukumu yake na kuchukua kidogo kuliko haki yake. Japokuwa Mwenyezi Mungu Sw ameiumba dunia kwa misngi wa uadilifu, na kanuni zake Mola Muumba zimewekwa kwa mujibu wa uadilifu, lakini inatupasa kuelewa kwamba, mahusiano baina ya wanadamu ni zaidi ya duara la uadilifu huu unaozungumziwa bali kwa hakika tunaweza kusema kuwa, uadilifu ni daraja ya chini kabisa ya mahusiano hayo na daraja yake ya juu kabisa ni ihsani na kutenda wema.
Kama tunataka kuzungumzia mahusiano ya kibinadamu kama inavyostahiki basi hatuna budi kuzungumzia suala hilo katika mitazamo miwili ya kisheria na kimaadili. Mahusiano baina ya wanadamu yamejengeka juu ya sheria ambazo zinadhamini kiwango cha chini kabisa cha mahuhusiano na miamala baina ya wandamu. Hata hivyo mfumo wa uhusiano baina ya wanadamu hauishii katika sheria na kanuni hizo. Mwanadamu ana akili na hisia na yote hayo mawili yana masharti na viambatanisho vyake. Uislamu umesisitiza sana suala la kufanya uadilifu na vilevile kutenda ihsani, na kufanya ihsani hakupingani na uadilifu. Kwa sababu ihsani ambayo katika mahusiano ya kibinadamu inafungamana na hisia za kiroho na moyo, inafanya jitihada za kwenda juu zaidi ya uadilifu na sheria na kuboresha zaidi jamii ya wanadamu kwa kutumia wenzo na wasila wa upendo, mahaba na kurehemeana.
Ihsani, kutoa na kutenda wema kuna taathira nyingi katika nafsi ya mwanadamu. Miongoni mwa taathira hizo ni kuimarisha moyo wa kujitolea na kutayarisha mazingira ya mtu kusabilia kila ulichonacho. Kufanya ihsani pia kunaleta anga ya mfungamana na utengamano baina ya wanadamu, suala ambalo lina thamani kubwa katika mahusiano ya kibinadamu. Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, kufanya ihsani na wema hakuhusu kundi, kaumu, tabaka au kizazi makhsusi cha watu na kazi hiyo inaweza kufanyika katika mazingira yote ya kifedha na wakati wowote na kwa uwezo wowote wa mtu. Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya ya 134 ya Suratu Aal Imran kwamba: Ambao hutoa katika raha na shida, na wazuiao ghadhabu na wenye kusamehe watu, na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao ihsani."
Hapa yumkini likajitokeza swali kwamba, watu maskini na wasio nacho wanaweza vipi kufanya ihsani na kutoa kwa watu wengine? Jibu ni kwamba, watu kama hawa wanaweza kuwasaidia wenzao kadiri ya uwezo wao. Wakati huo huo tunapaswa kutambua kuwa, kutoa ulichonacho na kufanya ihsani hakuishii katika kutoa mali na utajiri tu, bali kunajumuisha pia kipawa chochote alichopewa mwanadamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu sawa kipawa hicho kiwe mali na utajiri, elimu na maarifa au kitu kinginekinachoweza kuwafaidisha wanadamu. Kwa utaratibu huo Mwenyezi Mungu anataka moyo wa kujitolea na kusabilia tuliyonayo uenee hata baina ya watu maskini. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Uislamu mbali na kulipa umuhimu suala la kukomesha umaskini katika jamii, vilevile dini hiyo inalitazama suala hilo la ihsani katika mtazamo wa kimalezi, na hapana shaka kuwa maadili mema yanahusu wanadamu wote, tajiri na maskini.

....>>....


Ihsani inadhiriki katika sura mbili, katika medani ya maadili na mwenendo wa mtu binafsi na katika akhlaki na mwenendo wa kijamii. Pamoja na hayo inatupaswa kusema kuwa, maadili bora na mwenendo mzuri wa mtu hudhihiri katika miamala na mwenendso wake na wanadamu wenzake. Katika aya za Qur'ani Tukufu, Mwenyezi Mungu SW anayataja masuala kama Swala, subira, Swala za usiku, dua na istighfari nyakati za kabla ya alfajiri - ambazo ni kati ya amali za mtu binafsi- kuwa ni vielelezo vya ihsani. Hii ni kwa sababu kila moja kati ya amali hizo za mtu binafsi ina taathira kubwa katika maisha yake ya kijamii na inaweza kubadilisha kabisa mtindo wake wa maisha.
Kwa mfano kuwa na imani kumearifishwa kuwa ni miongoni mwa vielelezo vya kufanya ihsani. Hapana shaka kuwa kumwamini Mwenyezi Mungu, Siku ya Kiyama na Qur'ani Tukufu huwa na taathira katika mwenendo wa mwanadamu na kimsingi mtindo wa maisha na mwenendo wa mtu mwenye imani kama hiyo hubadilika kabisa na tunaweza kusema kuwa pande zote za maisha ya mwanadamu kama huyu huathiriwa na itikadi zake.
Katika medani ya mwenendo wa kijamii pia tunaweza kuashiria vielelezo vya aina mbili vya ihsani na kutenda wema na baadhi yao vina maana ya kuacha na kutofanya mambo yasiyofaa na vingine kwa maana ya kufanya mema na yanayofaa. Kwa maana kwamba, katika mtazamo wa Qur'ani ihsani si kufanya amali na jambo fulani tu bali wakati mwingine kuacha kufanya jambo baya na lisilofaa hutambuliwa kuwa ni ihsani. Miongoni mwa maeneo ambako Mwenyezi Mungu amekutambua kuacha kufanya jambo kuwa ni katika vielelezo vya ihsani ni katika kuzuia ghadhabu na hasira.
Vilevile Mwenyezi Mungu amekutaja kuwa na takwa na ucha-Mungu kuwa ni katika ihsani na kufanya wema. Hii ni kwa sababu Wachamungu hujiepusha na kila jambo ovu na chafu linalokatazwa na dini na akili. Hivyo basi mtu mwenye takwa na mchamungu kamili huwa na mwenendo mzuri sana wa mtu binafsi na wa kijamii. Vilevile kujiepusha na madhambi makubwa, ufuska na ufisadi vimetajwa katika Qur'ani tukufu kuwa ni vielelezo vya ishani na kutend wema.
Mwenyezi Mungu Mtukufu pia ametaka vitendo vinavyokubaliwa na akili na sheria kuwa amali nzuri. Miongoni mwa amali hizo ni kuchinja mnama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kutekeleza majukumu, kusamehe makosa ya watu, kusuluhisha baina ya watu katika masuala ya kifamilia, kujali hali za watu wazima na wazee, kulingania Uislamu, jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na mashaka yake, kuwasaidia wenye haja, kutoa Zaka na khumsi na kadhalika.
Vielelezo hivi vya ihsani vinaonesha kuwa, kufanya wema na ihsani ni daraja ya juu ya mwanadamu ambaye licha ya kwamba anaweza kufikia makamu aali na nafasi za juu ya kutekeleza uadilifu, lakini tunapaswa kutambua kuwa ubinadamu wa mwanadamu hufika kileleni kwa kufanya ihsani baada ya kuwa mwadilifu. Hivyo basi katika mtindo wa maisha wa Kiislamu, mbali na kuwa mwadilifu, mwenendo wa mwanadamu pia anapaswa kujipamba kwa ihsani na utendawema.

....>>>....


Wapenzi wasikilazi muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki ukemalizika. Tukutane tena juma lijalo panapo majaaliwa na Mwenyezi Mungu. Kwaherini..

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)