Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 20 Mei 2015 21:05

Uislamu na Mtindo wa Maisha (68)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (68)

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Warakatuh. Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya kipindi cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kipindi chetu cha wiki hii kitaendelea kutupia jicho adabu za kuamiliana na watu na kuwajulia hali hususan wagonjwa. Karibuni....

>>>>


Sira ya Mtume na Ahlibaiti zake watoharifu na vilevile mafundisho ya dini ya Uislamu yanaonesha kuwa, kuwahudumia watu kwa njia mbalimbali ndiyo wasila na wenzo muhimu zaidi wa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu baada ya kutekeleza amali za wajibu na kujiepusha na haramu. Historia inaonesha kuwa, watu wa Mwenyezi Mungu na rijali adhimu na wateule daima walikuwa wakiwahudumia watu na walikuwa wakifanya kila wawezalo kukidhi haja na mahitaji yao. Imepokewa kuwa masahaba walimuuliza Mtume Muhammad (saw) kwamba: Ni mtu yupi anayependwa zaidi ya Mwenyezi Mungu? Alisema: Ni yule anayewanufaisha zaidi wanadamu. (Usul Kafi:2-126) Kushughulikia masuala ya waja wa Mwenyezi Mungu mbali na kwamba kunatatua matatizo yao, vilevile huwa na taathira nzuri za kimalezi kwa mtu anayetoa huduma na humwondolea tabia za kujiona, uchoyo na kadhalika na kumpamba kwa sifa nzuri za Mwenyezi Mungu. Mtume (saw) anasema kuhusu suala la kushughulikia na kukidhi matatizo ya waja kwamba: Waumini ni mithili ya mwili mmoja ambaao pale kiungo chake kimoja kinapopatwa na maumivu viungo vingine pia huumia na kuharakia kukisaidia." (Safinatul Bihar:1-13)
Kwa msingi huo Mwislamu hapaswi kupuuza na kufumbia macho mashaka na matatizo ya wanadamu wenzake. Bali anapaswa kuimarisha moyo wa kupenda kuwasaidia wanadamu wenzake ndani ya nafsi yake na kujali yanayowakuta na kuwazonga. Kila mara anapomuona ndugu yake katika dini katika mashaka na matatizo aharakie kumsaidia na kujaribu kukidhi matakwa yake na kumuondolea ghamu na mashaka kadiri ya uwezo wake. Si hayo tu bali inasisitizwa kwamba Mwislamu anapaswa kuharakia kukidhi haja za muumini mwenzake hata kabla ya kuombwa msaada na auni. Imam Swadiq (as) amesema: Kila Mwislamu anayekidhi haja ya Mwislamu mwenzake, Mwenyezi Mungu SW hunadi na kusema: Thawabu na malipo yako yako kwangu mimi, na sitaridhia kukupa jazaa na malipo yasiyokuwa pepo." (Biharul Anwar: 71-285) Miongoni mwa mambo yaliyosisitizwa sana katika Uislamu katika jinsi ya kuamiliana na watu ni kutembelea wagonjwa. Katika utamaduni wa Kiislamu, suala la kutembelea na kuwajulia hali wagonjwa limepewa umuhimu mkubwa sana kwa sababu mwenendo huo mzuri unamfurahisha Mwenyezi Mungu na huwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mahusiano ya kibinadamu na kuzidisha upendo baina ya watu.
Mtume (saw) amebainisha nafasi adhimu ya wale wanaotembea wagonjwa na kuwajulia hali mbele ya Mwenyezi Mungu akisema: Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atamlaumu mmoja kati ya waja wake akisema: Mja wangu! Kitu gali kilikuzuia kuja kunijulia hali wakati nilipokuwa mgonjwa? Mja atasema: Mola wangu Mlezi! Wewe ni muumba wa dunia na maumivu, mashaka na maradhi ni vitu visivyo na maana kwako wewe. Umetukuka kupatwa na maradhi na ugonjwa." Mwenyezi Mungu atasema: Ndugu yako muumini aliumwa na hukwenda kumjulia hali. Naapa kwa izza na jalali yangu kwamba, lau ungekwenda kumjulia hali ungenikuta mimi huko na ningekidhi haja zako zote. Hii ni kutokana na heshima na hadhi ya muumini kwangu mimi, na Mimi ni Rahman mwingi wa rehma na Rahiim mwenye kurehemu." (Aamali Sheikh Tusi: 629)


Wasii wa Mtume, Imam Ali bin Abi Twalib (as) pia alikuwa akilipa umuhimu mkubwa suala la kuwatembelea na kuwajulia hali wagonjwa. Anasema: "Miongoni mwa amali bora zaidi ni kuwatembelea na kuwajulia hali wagonjwa."
Imepokewa katika sira na mwenendo wa Mtume kwamba mtukufu huyo daima alikuwa akiwatembelea wagonjwa na muhimu zaidi ni kuwa alikuwa akiwaamuru Waislamu kufanya hivyo. Alilipa umuhimu mkubwa suala hilo kwa kadiri kwamba, imepokuwa kuwa mtukufu huyo alikuwa na jirani Myahudi ambaye alikuwa akimuudhi na kumfanyia vitimbi vya aina mbalimbali. Kila siku Myahudi huyo alikuwa akipanda juu ya paa ya nyumba yake na kumwagia Mtume majivu yenye moto kichwani mara zote alipokuwa akipita kando ya nyumba hiyo. Myahudi huyo alifanya kitendo hicho kiovu kwa kisingizio cha kutupa taka na majivu lakini hakika yake ilikuwa ni kuonesha kinyongo na chuki yake kubwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Hata hivyo mtukufu huyo daima alifumbia macho uovu huo. Siku moja Mtume (saw) alipita kando ya nyumba ya Myahudi huyo na hakuona maudhi aliyokuwa akifanyiwa na jirani huyo Myahudi. Mtume aliuliza hali yake na masahaba walimwambia: Kwa bahati nzuri Myahudi huyo anaumwa na hakuweza kumuudhi mtukufu huyo kutokana na maradhi."
Mtume (saw) alisema: Tupaswa kwenda kumtembelea na kumjulia hali. Kisha mtukufu huyo aliondoka na kwenda nyumbani kwa Yahudi. Alipobisha mlango, mke wa Yahudi aliuliza: Nani anabisha hodi? Mtume (saw) alisema: "Ni Mtume wa Waislamu amekuja kumtembelea na kumjulia hali jirani yake mgonjwa."
Mwanamke huyo alimueleza mumewe habari hiyo. Bwana yule Myahudi alimwamuru mkewe afungue mlango. Mtume (saw) aliingia ndani na kuketi kando ya ngonjwa na kuanza kumuuliza hali yake. Aliamiliana naye kwa upendo na huruma kana kwamba si yule Myahudi aliyekuwa akimwagia jivu la moto kutoka kwenye paa la nyumba. Bwana Myahudi ambaye alikuwa amefunika uso wake kutokana na haya ya mwenendo wa upole na upendo wa Mtume alistaajabu sana na kuuliza: Tabia na mwenendo huu ni wako wewe binafsi au ni katika mafundisho ya dini ya Uislamu? Mtume (saw) alisema: Ni sehemu ya mafundisho ya dini na tunawaamuru Waislamu wote kufanya hivi. Bwana Myahudi alisilimu papo hapo kutokana na mwenendo huo mwema wa Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Kwa msingi huo kuwatembelea na kuwajulia hali wagonjwa ni miongoni mwa haki ambazo Waislamu wanapaswa kuzichunga na kuzitekeleza mkabala wa Waislamu wenzao. Imepokewa kutoka kwa Mtume (saw) kwamba amesema: "Miongoni mwa haki za Mwislamu kwa Mwislamu mwenzake ni kumsalimia anapokutana naye, kumtembelea anapoumwa na kushiriki katika kusindikiza jeneza lake anapofariki dunia." (Makarimul Akhlaak: 359)
Suala jingine la kuashiriwa hapa ni kuwa kumtembelea mgonjwa kuna adabu na taratibu zinazopaswa kulindwa. Miongoni mwa adabu na taratibu hizo ni kumpelekea zawadi na hadiya ambako husaidia kuboresha hali yake kwa njia moja au nyingine. Imepokewa kwamba, baadhi ya maswahaba wa Imam Swadiq (as) waliokuwa njiani kwenda kumtembelea mgonjwa walikutana na mtukufu huyo ambaye aliwauliza wanakwenda wapi? Walisema: Tunakwenda kumtembelea mgonjwa. Imam alisema: Hivi mnemchukulia mgonjwa zawadi kama tufahi, pea uturi au kipande cha udi? Walisema hapana. Mtukufu huyo aliwaambia: Hivi hamujui kwamba kumpelekea zawadi mgonjwa kunatuliza moyo na kuboresha hali yake? (Wasailu Shia: 2-643)
Imepokewa kutoka kwa Mtume (saw) kwamba amesema: Mtu anayempa mgonjwa chakula anachokipenda, Mwenyezi Mungu Azza Wajalla atampa katika matunda ya peponi." (Biharul Anwar: 78-224)
Miongoni mwa adabu za kumtembelea mgonjwa ni kumpa moyo wa matumaini na kutuliza fikra na nafsi yake. Hii ni kwa sababu baadhi ya wagonjwa hupoteza moyo wa matumaini na yumkini hata wakatamani kufa kutokaana na hali hiyo ya kukata tamaa. Hivyo basi ni vizuri kwa mtu anayemtembelea mgonjwa kumpa moyo wa matumaini.
Jambo jingine ni kwamba inapendekezwa kufupisha wakati wa kutembelea mgonjwa isipokuwa kama yeye mwenyewe atataka ubakie pamoja naye muda mrefu zaidi. Wakati mwingine watu wanaotembelea wagonjwa hujisahau na kubakia muda mrefu kiasi cha kumchosha na pengine kumzidishia maumivu. Hivyo ni vuzuri kufupisha wakati wa kuketi na mgonjwa. Vilevile inausiwa kwamba kwa kuzingatia kuwa lengo la kumtembelea mgonjwa ni kuonesha upendo, kutekeleza haki ya muumini na mwanadamu mwenzako na vilevile kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na thawabu zake, hivyo basi mtu anayemtembelea mgonjwa asiwe na matarajio ya kukaribishwa kwa maakuli na kadhalika kwani mgonjwa mwenyewe anazongwa na maradhi na familia yake inashughulishwa na kumuuguza. Hivyo mtu anayetembelea mgonjwa anapaswa yeye mwenyewe kumsaidia na kumpunguzia mashaka kwa njia moja au nyingine badala ya kumzidishia mzigo na zahma.
Kumuombea dua mgonjwa ni katika adabu zinazousiwa katika Uislamu. Sahaba Salman al Farisi anasimulia kwamba: Siku moja Mtume (saw) alikuja kunitembelea nikiwa kitandani mgonjwa, kisha akaniombea dua kwa kusema: Ewe Salman! Mwenyezi Mungu akuondolee mashaka na maumivu yako, akuzidishie ujira mwema na aulinde mwili na dini yake hadi mwishoni mwa umri wako.

>>


Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umemalizika. Tukutane tena wiki ijayo katika kipindi kingine cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kwaherini....

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)