Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 12 Mei 2015 13:34

Uislamu na Mtindo wa Maisha (67)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (67)

Ni wakati mwingine wa kuwaletea mfululizo wa kipindi cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kipindi chetu wiki hii kitatupia jicho mafundisho ya Uislamu kuhusu adabu na taratibu za kuishi na jirani. Basi fuatilieni kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Kuongezeka hii leo kwa idadi ya watu kumeleta mfungamano na msongamano mkubwa baina ya wanadamu hususan katika maeneo ya mijini, suala ambalo limekuwa na taathira za aina mbalimbali nzuri na wakati mwingine hasi kutokana na ukosefu wa uendeshaji mzuri. Kwa msingi huo kuna udharura wa kutungwa sheria na kanuni maalumu za kupanga na kuratibu maisha ya jamii na ili wanadamu waweze kuishi kwa pamoja katika hali ya maelewano na amani.
Miongoni mwa matokeo ya kuongezeka idadi ya watu ni kuenea mtindo wa watu kuishi kwenye maghorofa na nyumba za watu katika maeneo ya mijini ambayo yanawalazimu watu kuwa na taratibu maalumu za maisha na maingiliano na majirani zao. Maisha kama hayo ya watu wengi katika ghorofa au nyumba moja kubwa huandamana na mashaka mengi na pengine ugomvi, mivutano na kadhalika.
Majirani na watu wanaoishi katika jengo moja kubwa lenye nyumba kadhaa huwa katika mawasiliano ya mara kwa mara, kwa msingi huo maisha kama hayo yanawalazimu wahusika kuchunga baadhi ya taratibu na kanuni za kimaadili na kisheria.
Dini ya Uislamu imelipa umuhimu mkubwa suala la jinsi ya kuamiliana na jirani na Qur'ani Tukufu imeliusia suala hilo sambamba na masuala kama kumwabudu Mwenyezi Mungu Mmoja, kuwafanyia ihsani na wema wazazi wawili na jamaa wa karibu. Aya ya 36 ya Suratu Nisaa inasema: Na mwabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote, na watendeeni wema wazazi wawili na akraba na yatima, na maskini na jirani wa karibu na jirani wa mbali...
Kama tunavyoona miongoni mwa mambo yaliyozungumziwa katika aya hii ni kuwatendea wema majirani wa karibu na wa mbali. Wafasiri wa Qur'ani wamesema mengi kuhusu maana ya jirani wa karibu na jirani wa mbali. Baadhi ya wafasiri hao wanasema umbali na ukaribu unaozungumziwa katika aya hii ni umbali wa eneo, kwa sababu majirani wa karibu zaidi wana haki na heshima zaidi. Kwa kawaida anapozungumziwa jirani humaanisha jirani wa karibu yako; hata hivyo Uislamu umepanua zaidi maana ya jirani wa mbali na jirani wa karibu yako kieneo. Umezungumzia pia jirani wa mbali ukikusudia jirani katika itikadi na imani, mwenzako katika dini na kadhalika. Pamoja na hayo tunapaswa kutambua kwamba kipaumbele katika kulinda haki za jirani ni kwa ajili ya jirani wa karibu.
Haki za ujirani katika Uislamu zimepewa umuhimu sana kwa kadiri kwamba zimesisitizwa sana katika wasia wa mwisho wa Mtume wetu Muhammad (saw). Imam Ali bin Abi Twalib (as) ambaye ndiye aliyekuwa karibu zaidi na mtukufu huyo kuliko watu wengine anasema: Mtume (saw) alituusia kuwafanyia wema majirani hadi tukadhani kwamba atawaamuru majirani kurithishana. (Nahjul Balagha: Barua 74)
Haki za jirani katika Uislamu zimepewa umuhimu mkubwa kiasi kwamba Waislamu wameamrishwa kuchunga zaidi na zaidi haki hizo kuliko hata jinsi ya kuchunga ndugu katika imani. Imam Zainul Abidin (as) ambaye ni mjukuu wa Mtume Muhamamd (saw) anasema: Hazi za jirani ni kulinda heshima yake wakati anapokuwa ghaibu na kumheshimu anapokua hadhira. Akidhulumiwa umsaidie, usichokonoe aibu na kasoro zake na umfichie mabaya yake. Kama unajua kwamba atakubali nasaha zako basi mnasihi katika faragha. Usmwache peke yake anapopatwa na mashaka, fumbia macho makosa na kuteleza kwake na samehe madhambi yake na ishi nae kwa wema. (Al Khisal: 965)
Mtume Muhammad (saw) anasema kuhusu haki za jirani kwamba: Akikuomba msaada msaidie, akiomba deni mkopeshe na akiwa mhitaji basi mkidhie haja zake. Akipatwa na msiba mliwaze na akipata kheri na jema mpongeze na akiumwa mtembelee kumjulia hali na akifariki dunia shiriki kusindikiza jeneza lake. Usijali nyumba yako kuwa ndefu zaidi ya yake ili usizue upepo kumfikia isipokuwa baada ya ruhusa yake." mwisho wa hadithi. (Maskanul Fuad: 501)
Kuhusu udharura wa kumsaidia kifedha jirani na kujali hali yake ya kimaisha, Mtume (saw) anasema: Hajaniamini mimi mtu anayelala na shibe huku jirani yake akiwa na njaa." (Mustadrakul Wasaail: 8-924)
Imam Kadhim (as) ambaye ni mjukuu wa Mtume (saw) anafasiri maana ya ujirani mwema akisema: Ujirani mwema si kutomuudhi jirani bali ni kustahamili na kuvumilia maudhi ya jirani."
Hii ina maana kwamba tunapaswa kuamiliana na majirani kwa jicho la ihsani, upendo na urafiki na si kwa mujibu wa mipaka ya sheria na kanuni pekee. Kwa msingi huo jirani mwema ni yule asiyelipiza kisasi cha maudhi na adha za jirani yake bali hujitahidi kufumbia jicho maudhi na adha hizo na kuamiliana naye kwa ihsani, upendo na uvulivu. Na hata kama atalazimika kukabiliana na jirani yake basi afanye hivyo kwa kutumia maneno laini na uso wa tabasamu na bashasha kiasi kwamba jirani yake huyo hataudhika kwa maneno na mwenendo wake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba Mtume (saw) anasema kumuudhi na kumkera jirani humuweka mtu mbali na rehma za Mwenyezi Mungu na kumtumbukiza katika moto wa Jahannam. Mtukufu huyo amesema: Hataingia peponi mtu anayemuudhi jirani yake. (Nahlul Fasaha:2352)
Imepokewa pia kutoka kwa Mtume (saw) kwamba amesema: Naapa kwa jila la Mwenyezi Mungu kwamba mtu kama huyu hana imani.." Maswahaba waliuliza: Ni mtu gani huyo unayekusudia ya Rasullah? Alisema: "Ni yule anayemkera na kumuudhi jirani yake."
Ni wazi kuwa maisha ya sasa ya kijamii husababisha migongano ya hapa na pale na yumkini yakatayarisha uwanja na mazingira ya baadhi ya watu kutokubali na kuzingatia baadhi ya masuala ya kimaadili na hivyo kuwakera na kuwaudhi wenzao. Mambo kama haya huwa sababu ya kujitokeza mivutano na malumbamo baina ya watu hususan majirani.
Hadithi nyingi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu zimezungumzia baraka na taathira nzuri za kuamiliana vyema na kumtendea mema jirani ikiwa ni pamoja na ustawi wa miji, kunawiri uchumi na kuzidisha umri. Hii ni kutokana na ukweli kwamba majirani wazuri husaidiana na kushirikiana kwa upendo na mahaba na kusaidiana wakati wa mashaka na taabu. Wakati huo huo kukidhiwa matatizo ya kifedha na kiuchumi ya jirani huwa sababu ya kupatikana utulivu wa kiroho na kinafsi, suala ambalo kwa upande wake huzidisha umri wa watu katika jamii husika. Malumbano na ugomvi unaotokea baina ya majirani huathiti myoyo yao wote wawili na kusababisha matatizo na pengine maradhi ya kinafsi na kimwili ambayo huwa sababu ya kupungua umri wao. Pamoja na hayo tunapaswa kuelewa kwamba hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume na Ahlibaiti zake zinasisitiza kuwa Mwenyezi Mungu huwapenda na kuwazidishia baraka na umri majirani wenye mwenendo mzuri. Mtume Muhammad (saw) anasema: Kuunga udungu, tabia njema na kuamiliana vyema na jirani hustawisha nchi na huzidisha umri wa watu. (Nahjul Fasaha: 9381) Vilevile mjukuu wake, Imam Jaafar Swadiq anasema: Ujirani mwema huwa sababu ya kustawi maeneo mbalimbali na kuzidishiwa umri.
Miongoni mwa athari nzuri za kuamiliana vyema na jirani ni kupendwa na Mwenyezi Mungu Karima. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kutenda wema ni miongoni kwa sifa za Mwenyezi Mungu na hapana shaka kuwa Allah SW huwapenda watu wanaojipamba kwa sifa zake njema. Mtume anasisitiza jambo hilo katika hadithi tukufu akisema: Kama mnataka kupendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, semeni ukweli na amilianeni vyema na majirani zenu. (Nahjul Fasaha: 455)
Anasema katika hadithi nyingine kwamba: Boresheni tabia zenu, amilianeni vizuri na majirani zenu na waheshimuni wake zenu ili mupate kuingia peponi bila ya hisabu. (Al Tauhid: 721).

>>>>


Msikose kufuatilia mfululizo wa kipindi hiki wiki ijayo panapo majaaliwa. Wassalam Alaykum warahmatullah...

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)