Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 28 Aprili 2015 18:53

Uislamu na Mtindo wa Maisha (66)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (66)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni wasomaji na wafuatiliaji wa mtandao wa matangazo ya Idhaa ya Kiswahili redio Tehran na hii ikiwa ni sehemu nyingine ya kipindi cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kipindi chetu wiki hii kitatupia jicho mbinu za kuamrisha mema na kukataza maovu katika mtindo wa maisha wa Kiislamu.

>>>> >>>>>


Kama tulivyosema katika vipindi vilivyopita wakati tulipozungumzia adabu na taratibu za kuamiliana na watu katika jamii, hatima ya kila mwanadamu inafungamana na kushikamana na hatima ya wanadamu wenzake na jamii nzima. Kwa msingi huo si sahihi kwa mtu yeyote kupuuza na kufumbia macho yanayofanywa na wanadamu wengine kwa kisingizio kwamba yeye mwenyewe amefanya kuwa ni jukumu na wajibu wake. Viongozi wa dini yetu pia daima walikuwa wakiwahimiza wafuasi wao kutilia maanani yanayotendeka katika jamii na kutofumbia macho maasi yanayofanywa na watu wengine.
Imam Jaafar Swadiq (as) amenukuu kutoka kwa babu yake, Mtume Muhammad (saw) kwamba amesema: "Mtu anayefanya madhambi kwa siri madhara yake humpata yeye mwenyewe, lakini anapofanya madhambi waziwazi bila ya watu wengi kukabiliana naye na kumzuia, madhara yake yataipata jamii nzima." (Biharul Anwar: 97-78)
Kuamrisha mema na kukataza maovu ni miongoni mwa vigezo muhimu vya mtindo wa maisha wa Kiislamu na dini hiyo pamoja na viongozi wake wanapaswa kufanya jitihada kubwa za kuhakikisha faradhi hiyo muhimu inatekelezwa ipasavyo katika jamii. Wajibu wa kuamrisha mema na kukataza maovu si wa mtu au kundi makhsusi bali ni wadhifa wa watu wote. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, ni aina fulani ya usimamizi wa umma na wa Waislamu wote, mwanamke kwa mwanaume na mkubwa na mdogo. Umuhimu wa kuamrisha mema na kukataza maovu unatokana na kwamba, huwa sababu ya kuong'oka wanadamu na hudhamini uzima na usalama wa kiroho wa jamii nzima. Kazi ya kuamrisha mema na kukataza maovu ni kazi ya kuwasilisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa watenda maasi ambayo hufanywa na waja wema na wastahiki. Ujumbe huo huwa mithili ya matone ya maji safi ya mvua ambayo hunyesha katika ardhi ya nyoyo za watenda madhambi na kuzima moto wa maasia katika nyoyo hizo.
Jambo lenye umuhimu mkubwa katika kazi hii ya kuamrisha mema na kukataza maovu ni kujua vyema mbinu za kutekeleza wajibu huo. Hii ni kwa sababu yumkini mwanadamu anayefanya kazi hii akatumia mbinu ambazo hazitazaa matunda au hata zikawa na matokeo kinyume na makusudia na matarajio yake.
Moja kati ya misingi muhimu inayopaswa kutiliwa maanani katika faradhi hii ya kuamrisha mema na kukataza maovu ni kwamba mtu anayefanya kazi hiyo mwenyewe anapaswa kutekeleza mema anayowaamrisha wengine kuyafanya na kujiepusha na yale anayowakataza watu kuyafanya. Hii ni ka sababu, mtu asiyefanya mema na kujiepusha na maovu hawezi kuwaamuru wengine kufanya au kujiepusha na mambo hayo. Akili na mantiki pia vinahukumu kwamba, ili maneno yetu yaweze kuwa na taathira katika nyoyo za wenzetu, maneno yetu sisi wenyewe yanapaswa kuoana na kwenda sawa na matendo yetu. Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya za 2 na 3 za Suratu Saff kwamba: Enyi mlioamini! Kwa nini mnasema msiyoyatenda? Ni chukizo kubwa kwa Mwenyezi Mungu kusema msiyoyatenda". Qur'ani Tukufu pia inakemea watu wanaowaamuru wenzao kufanya mambo mema mbayo wao wenyewe hawayafanyi au kuwakataza maovu wanayoyafanya wao na kulitambua jambo hilo kuwa ni miongoni mwa dalili za kutokua na akili na busara. Aya ya 44 ya Suratul Baqara inasema: "Je, mnawaamrisha watu kutenda mema na mnajisahau, ilhali mnasoma Kitabu, Basi je, hamna akili?"
Kwa upande mwingine viongozi wa dini yetu daima walikuwa wakiwaamuru wafuasi wao kuwalingania watu mema na dini kwa matendo yao badala ya kutumia maneno na ndimi zao. Imam Jaafar Swadiq (sa) anasema: "Walinganieni watu mema bila ya kutumia ndimi zenu."
Mwanafikra wa Kiislamu Shahid Murtadha Mutahhari anasema: Kila mtu anayetaka kurekebisha umma anapaswa kujirekebisha yeye kwanza kabla ya watu wengine. Kama Mtume Muhammad (saw) asingekuwa mstari wa mbele katika yale aliyokuwa akiwaamrisha watu kuyafanya basi ingekuwa muhali watu wengine kumfuata na kukubali mafundisho yake. Aliwataka Waislamu kuswali na kutilia maanani swala za usiku huku yenye mwenyewe akiwa kinara na mstari wa mbele katika ibada na hakuwaamrisha watu kutoa walicho nacho katika njia ya Mwenyezi Mungu ila kutokana na kwamba yeye mwenyewe alikuwa mbele ya wanadamu wote katika kutenda mema, kujitolea na kusabilia kila alichokuwa nacho kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kwa maslahi ya umma wake.

>>>>>>> <


Mbinu nyingine ya kuamrisha mema na kukataza maovu ni kutumia maneno laini na mazuri katika kutekeleza faradhi hiyo ya Mwenyezi Mungu. Ili kuweza kuwa na taathira katika nyonyo za walengwa, mtu anayeamrisha mema na kukataza maovu anapaswa kutumia maneo mazuri yanayotoa harufu njema ya uturi na marashi. Hii ni kwa sababu, maneno mabaya si tu kwamba hayawezi kuwaongoza waliopotea, bali huwafanya kuwa watu wenye vinyongo, wabishi, wakaidi, wachoyo na wabinafsi. Ni wazi kuwa watu wa aina hii hawawezi kuongoka kirahisi baada ya kuchukua msimamo kama huo mbele ya haki na kweli. Katika sehemu moja ya wasia wake kwa mwanaye Hassan, Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema: Usichupe mipaka katika kuwalaumu na kuwakemea watu kwani jambo hilo huwatia vinyongo nyoyoni mwao."
Hivyo basi inafaa kutumia maneno laini, mazuri na matamu katika kuamrisha mema na kukataza maovu kwa sababu mtu anayefanya kazi hiyo kwa hakika huwa mbeba ujumbe wa Mwenyezi Mungu, na kwa msingi huo anapaswa kujipamba kwa maneno mazuri, ya kuvutia na yasiyokera ili kuweza kuwasilisha ujumbe huo kwa njia nzuri, sahihi na yenye taathira.
Mbinu nyingine yenye taathira katika kuamrisha mema na kukataza maovu ni kujaribu kuvutia imani ya watu. Msikilizaji asiyekuwa na imani kwa mtu anayemnasihi na kumlingania mema hawezi kuathiriwa na maneno yake; hivyo mtu anayeamrisha mema na kukataza maovu anapaswa kuwathibitishia watu anaowalingania kuwa anawatakia kheri, ufanisi na mambo mema. Tunapaswa kuelewa hapa kuwa miongoni mwa siri za mafanikio ya Mitume wa Mwenyezi Mungu hususan Mtume wetu Muhammad (saw) ni kwamba watu walikuwa na imani kwamba watukufu hao hawakufanya jambo lolote kwa ajili ya maslahi yao binafsi wala kwa ajili ya tamaa ya dunia na hawakuwa na nia yoyote isipokuwa kurekebisha na kuboresha hali ya wafuasi wao. Qur'ani Tukufu inasisitiza jambo hilo kuhusu Mtume Muhammad (saw) katika aya ya 128 ya Suratu Tauba na kusema: "Hakika amekujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe, yanamhuzunisha yanayowataabisha, anawahangaikia nyinyi sana na kwa waumini ni mpole na mwenye huruma."
Kwa msingi huo kuvutia imani ya wanaolinganiwa kuna nafasi muhimu katika taathira nzuri ya kuamrisha mema na kukataza maovu.
Suala jingine linalopaswa kupewa mazingatio wakati wa kuamrisha mema na kukataza maovu ni kuheshimu itikadi za watu wengine. Wakati mwingine watu hufanya makosa kutokana na kwamba wanaamini kuwa ni amali sahihi na yumkini wakayatukuza na hata kuyaabudu mambo hayo yasiyo sahihi. Katika kuamiliana na watu wa aina hii unalazimika kutovunjia heshima au kudharau itikadi na imani zao bali jambo muhimu hapa ni kutumia busara na mantiki na kujadiliana nao kwa maneno mazuri ili waweze kuelewa makosa yao ya kiitikadi. Aya ya 125 ya Suratu Nahl inasema: Waite watu katika njia ya Mola Wako kwa hekima na mawaidha mazuri, na jadiliana nao kwa namna iliyobora. Hakika Mola Wako ndiye anayemjua zaidi aliyepotea njia yake na Yeye ndiye anayewajua zaidi walioongoka."
Ni wazi kuwa itikadi za kila mtu huwa na heshima na taadhima maalumu kwa mwenyewe na kuyavunjia heshima mambo hayo ni sawa kabisa na kumvunjia heshima mtu mwenye itikadi na imani hizo, jambo ambalo bila shaka litakabiliwa na jibu kali. Kuvunjia heshima na kudharau itikadi hata za batili za watu wengine hakuwezi kuwa njia sahihi ya kuwaongoza bali yumkini kukazidisha inadi yao na kuwatumbukiza zaidi katika batili na upotofu. Aya ya 108 ya Suratul An'am inawatahadharisha waumini na jambo hilo na kusema: Na wala msiwatukane wale wanaoomba asiye Mwenyezi Mungu wasije wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua. Hivi ndivyo tumewapambia kila umma vitendo vyao kisha marejeo yao yatakuwa kwa Mola wao, naye atawaambia yale waliyokuwa wakiyatenda."
Kuheshimu shakhsia za watu wanaolinganiwa kwa kuamrisha mema na kukataza maovu ni msingi mwingine muhimu unapaswa kutiliwa maanani wakati wa kutekeleza faradhi hiyo muhimu, ili nasaha na mawaidha mema yasiwe sababu na uasi na ubishi na hata majibu makali na yasiyofaa.

>>

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)