Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 20 Aprili 2015 16:04

Uislamu na Mtindo wa Maisha (65)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (65)

Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya kipindi cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kipindi chetu cha wiki hii kitaendelea kujadili misingi ya mahusiano ya kijamii katika mtindo wa Maisha wa Kiislamu.
Kama mnavyojua, mwanadamu ni kiumbe wa kijamii, hivyo kuendelea kuwepo kwake kunafungamana na mahusiano yake na watu wengine katika jamii kupitia upendo, maelewano na kuheshimiana. Kwa msingi huo katika maisha ya kijamii, mwanadamu anapaswa kuwatendea na kuwatakia wanadamu wenzake yale anayopenda yeye atendewe na kufanyiwa. Kama anapenda ukweli, kutimiziwa ahadi na kutendewa wema basi yeye pia anapaswa kufungamana na kuheshimu vitu hivyo. Muktadhaa wa msingi huu ni kwamba, mwanadamu asiwe mchoyo na kujiangalie yeye mwenyewe katika kutenda amali njema. Kwa maana kwamba asijitakie yeye peke yake mema na mazuri ya kimaadili bali afanye jitihada za kueneza mema katika jamii na duniani kote na kukabiliana vivyo hivyo na mabaya na maovu.
Imesisitizwa katika mafundisho ya Uislamu kwamba, Waislamu wanapaswa kuguswa na kufuatilia yanayotokea katika jamii. Kila Mwislamu anawajibika kuwalingania mema jamaa, marafiki na wanadamu wenzake na kuwakataza maovu na mambo mabaya. Wadhifa huu umesisitizwa sana katika mafundisho ya Uislamu chini ya anwani ya "kuamrisha mema na kukataza maovu". Suala hili ni miongoni mwa mambo muhimu sana ya kijamii katika mtindo wa maisha wa Kiislamu. Neno "maaruf" lililotumiwa katika istahi ya Kiislamu kueleza msingi huo wa kuamrisha mema, lina maana ya kinachojulikana na kutambulika, na "munkar" lina maana ya kisichojulikana. Katika Uislamu, kazi nzuri na njema zinatajwa kuwa ni "maaruf" na zinazojulikana kutokana na kwamba zinatambuliwa na maumbile safi na ya kifitra ya mwanadamu, na vitendo na amali mbaya zinazokinzana na fitra na maumbile safi zimetajwa kuwa ni "munkar" na zisizojulikana na fitra na maumbile.
Menyezi Mungu SW ametaja msingi huu muhimu katika aya kadhaa za Qur'ani Tukufu na kusisitiza kuwa, kuamrisha mema na kukataza maovu ni miongoni wa sifa makhsusi za waumini. Aya ya 71 ya Suratu Tauba inasema: Na waumini wanaume na waumini wanawake ni marafiki wao kwa wao, huamrishana mema na kukatazana maovu, na husimamisha Swala na kutoa Zaka, na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Kwa mujibu wa aya hii ya Qur'ani, sharti la imani kamili ni kuwa na uhusiano wa kirafiki na mwema na waumini na kutilia maanani hali na maisha yao. Na sharti ya kupendana baina ya wanadamu ni kuongozana na kuelekezana katika mambo mema na kukosoana wakati mmoja wetu anapofanya mambo mabaya na yasiyofaa. Vilevile aya hiyo ya Qur'ani inasema kuwa, miongoni mwa masharti ya kuamrishana mema na kukatazana maovu ni kusimamisha Swala, kueneza masuala ya kiroho na kimaanawi, kutii amri za Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kuwasaidia wasiojiweza kupitia njia ya kutoa Zaka. Na matunda ya yote hayo ni kuteremshiwa rehma na baraka za Mwenyezi Mungu.
Watu wanaoamrisha mema na kukataza maovu ndio sharifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu SW na Mtume (saw). Swahaba mmoja alimuuliza Mtume (saw) kwamba: Ya Rasulallah! Ni yupi mtu bora kuliko wengine? Alisema: Ni yule anayeamrisha zaidi mema na kukataza maovu na yule mwenye taqwa na mchamungu zaidi, anayeridhia zaidi matakwa ya na makadirio ya Mwenyezi Mungu kuliko watu wengine."
Imam Ali bin Abi Twalib pia amesema kuhusu nafasi adhimu ya kuamrisha mema na kukataza maovu kwamba: Amali zote njema na kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu ni mithili ya tone la maji ya habari kubwa vikilinganishwa na kuamrisha mema na kukataza maovu, na bora zaidi ya yote ni neno la uadilifu na haki linalosemwa mbele ya mtawala dhalimu. (Nahjul Balagha, hikima:374) >>
Kama tulivyosema mwanzoni, mafundisho ya Uislamu yanasisitiza kuwa, mwanadamu anapaswa kufuatilia na kujali maswala ya wanadamu wenzake na yanayojiri kandokando yake. Suala hili pia linasisitizwa katika adabu na kanuni za mahusiano ya Kiislamu kwa maana kuwa, kila Mwislamu anawajibika kutumia vyema fursa anazopata katika mahusiano yake ya wanadamu wenzake kwa ajili ya kuamrisha mema na kukataza maovu. Na kwa kuwa mahusiano hayo huanzia katika familia na kupanuka zaidi hadi katika jamii, basi suala la kuamrisha mema na kukataza maovu linapaswa kuanzia ndani ya familia. Kila mmoja wetu anatambua umuhimu wa kuamrisha mema na kukataza maovu ndani ya familia. Kila mmoja kati ya watu wa familia moja anapaswa kusimamia kazi na matendo ya mwenzake na wote wanapaswa kusaidiana katika maisha ya kimaada na kiroho. Japokuwa medani ya familia ni ndogo na finyu ikilinganishwa na medani nyinginezo za kijamii lakini mazingira ya kuamrisha mema na kukataza maovu ndani ya familia ni mapana zaidi na majukumu ya kila mmoja kati ya watu wa familia ni makubwa na mazito zaidi. Hii ni kwa sababu, kutokana na mfungamano wa daima wa wanachama wa familia moja, kila mmoja hujua na kutambua vyema zaidi mema na maovu ya wenzake. Maarifa na utambuzi huo humfanya mtu ajihisi kuwa na majukumu makubwa. Kwa sababu hiyo aya za Qur'ani Tukufu na Hadithi za Mtume na Ahlibaiti zake watoharifu, mbali na kutilia mkazo suala la kuamrisha mema na kukataza maovu kwa ujumla, zimesisitiza pia kwa njia makhsusi suala la kuamrisha mema na kukataza maovu ndani ya familia.
Sehemu ya aya ya 6 ya Suratu Tahrim inasema: Enyi mlioamini! Zilindeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe.."
Histora inasema kuwa, wakati aya hii ilipoteremshwa Mwislamu mmoja aliketi chini na kuanza kulia. Hadhirina walitaka kujua sababu ya kilio chake. Alisema: Mimi siwezi kujirekebisha nafsi yangu mimi mwenyewe na ninahofia kuingia katika moto wa Jahannam; sasa Mwenyezi Mungu SW amenitaka kuilinda familia yangu na moto wa Jahannam."
Maneno ya bwana huyo yalifika kwa Mtume (saw) ambaye alimwita na kumwambia: Usihuzunike, kwani inakutosha wewe kuwaamrisha unayoyafanya wewe mwenyewe, na kuwatakataza unayojizuia wewe kuyafanya."
Kuamrisha mema na kukataza maovu ni faradhi waliyoamrishwa Waislamu kuifanya pia katika jamii. Katika Uislamu hatima ya kila mtu na jamii inashikamana na ya mwenzake, na kuboreka au kuharibika kwa mtu mmoja au jamii moja huwa na taathira katika mtu au jamii nyingine. Hivyo basi mtu yeyote haruhusiwi kupuuza na kufumbia macho hatima na masuala ya watu wengine kwa kisingizio kwamba yeye mwenyewe anatekeleza wajibu na majukumu yake. Kupuuza na kufumbia macho madhambi na kukanyagwa thamani za dini ya Mwenyezi Mungu japo kunafanywa na watu wachache tu, huwa na taathira mbaya kwa jamii nzima baada ya kupita muda. Mfano wa taathira za dhambi na maasi ya mtu mmoja katika jamii ni mithili ya kundi la watu lililopanda meli na ilipofika katikati ya bahari mtu mmoja aliamua kutoboa mahala alipokuwa ameketi yeye. Iwapo wasafiri wengine wa meli hiyo watatazama tu kwa macho na kunyamazia kimya kitendo hicho kwa kisingizo kwamba mtu huyo anatoboa mahala anapokaa yeye mwenyewe, hapana shaka meli hiyo itazama na kuua wasafiri wote hata wale ambao wahakuitoboa. Vivyo hivyo kutenda madhambi na maovu katika jamii, ambavyo iwapo vitaenea kote, madhara yake yatawapata wana jamii wote. >
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha leo umemalizika. Msikose kuwa nasi katika kipindi cha wiki ijayo kitakachozungumzia mbinu sahihi za kiamrisha mema na kukataza maovu. Wassalamu alakum......

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)