Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 14 Aprili 2015 15:48

Uislamu na Mtindo wa Maisha (64)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (64)

Assalaam Alaykum wafuatiliaji wa makala hii ya Uislamu na Mtindo wa Maisha na hiki kikiwa ni kipindi cha 64. Kama bado mnakumbuka katika kipindi cha wiki iliyopita tulisema kuwa kimaumbile mwanadamu ni kiumbe wa kijamii na maisha yake yanafungamana na jamii. Vilevile tuliashiria misingi kadhaa ya maisha ya kijamii katika mtindo wa Kiislamu wa maisha. Leo tutaendelea kuzungumzia misingi na kanuni za Kiislamu za maingiliano baina ya wanadamu katika jamii. Karibuni..

>>


Miongoni mwa misingi ya maingiliano na watu iliyosisitizwa katika mafundisho ya Uislamu ni kuwa na mwenendo laini na tabia njema katika kuamiliana na wanadamu wenzetu. Mafundisho ya Uislamu yanawahimiza wafuasi wa dini hiyo kuwa na mienedo laini na tabia nzuri na kuwakataza tabia mbaya na kavu. Qur'ani Tukufu pia inaashiria akhlaki na tabia njema za Mtume wa Mwenyezi Mungu pale inapozungumzia na kusifia mwenendo wa mtukufu huyo. Moyo mkunjufu na uso wa bashasha na tabasamu wakati wa kuamiliana na watu wengine ni miomgoni mwa sifa nzuri na aali ambazo huzidisha upendo katika mahusiano ya kijamii na huwa na taathira kubwa katika maneno ya mtu mwenye sifa hizo. Kwa sababu hiyo Mwenyezi Mungu Rahmani aliwachagua Mitume wa wajumbe wake kati ya watu wenye tabia njema, wapole na wenye upendo ili waweze kuwa na taathira kubwa katika nyoyo na roho za watu na kuwaongoza katika njia iliyonyooka. Watu hawa adhimu waliamiliana kwa wema, upole na upendo na watu kiasi kwamba waliwaathiri na kuwavutia hata maadui zao. Kielelezo kamili cha ukweli huo ni Mtume wetu Muhammad (saw). Historia inasema kwamba baadhi ya watu waliokuwa wakienda kwa mtukufu huo kwa nia ya kumvunjia heshima, kumuudhi na kumtukana walikuwa wakijikuta wametekwa na tabia zake nzuri na hatimaye kukubali dini ya Uislamu na kumpenda kupindukia mtukufu huyo.
Ni wazi kuwa kimaumbile kila mwanadamu hupenda kuwa na tabia njema, moyo mkunjufu na mwenendo mzuri na kwa sababu hiyo moyo unaowafanyia uhasama na uadui waja wa Mwenyezi Mungu ni moyo uliojitenga na maumbile asili na ya kifitra ya awali kutokana na kuchafuliwa na maovu ya dunia, kujiona na fikra potofu. Tunapaswa kujua pia kwamba sharti la mtu kumpenda Mwenyezi Mungu ni kuwapenda waja wake na sharti la kuwapenda waja wa Allah ni kuwa na tabia na mwenendo mzuri.
Kuwa na misimamo laini, moyo mkunjufu, upendo na tabia njema ni miongoni mwa misingi ya maisha ya kijamii. Kuamiliana na watu kwa ukali na ukatili yumkini kukawasukuma baadhi ya watu katika upotofu na kuwaweka mbali na ukweli. Kwa msingi huo mafundisho ya Uislamu yanasisitiza sana udharura wa kuwa na mwenendo mzuri, laini na mwororo hata na watu waliopotea na madhalimu wakati wa kuwalingania haki na ukweli. Tunaona kuwa wakati Mwenyezi Mungu SW alipomtuma Mussa na Haruna kwa dhalimu na katili mkubwa kama Firauni aliwausia kuamiliana naye kwa upole na kumsemesha kwa maneno laini. Hii ni kwa sababu maneno laini na mwenendo mwema ndio unaoweza kulainisha nyoyo na roho za watu waliokubuhu katika maasi kama Firauni. Aya za 43 na 44 za Suratu Twaha zinasema: "Nendeni kwa Firauni, hakika yeye amepituka mipaka. Mwambieni maneno laini huwenda akazingatia au akaogopa (adhabu ya Mwenyezi Mungu)."
Imepokewa kwamba Imam Ali bin Abi Twalib (as) amemuusia mwanaye Muhammad bin Hanafiyya akisema: Elewa kwamba alama kubwa zaidi ya mwenye akili timamu baada ya ile ya kumwamini Mwenyezi Mungu ni kuamiliana kwa upole na watu.... Vitu vyote watu wanavyoishi navyo na kuvitumia katika kuamiliana na watu ni sawa na chombo ambacho thuluthi yake mbili ni kutenda wema na thuluthi (yake moja iliyobakia) ni kufumbia macho baadhi ya mambo.
Hata hivyo tunapaswa kusema hapa kuwa maana ya mwenendo laini na kufumbia jicho baadhi ya makosa ya watu katika mtazamo wa Uislamu si kunyamazia kimya maovu na dhulma na kutabasamu kwa wale wanaodhulumu na kutenda maovu. Tunapaswa kujua kuwa ni wajibu kwa Muislamu kukabiliana na maovu ambayo yanakanyaga thamani za kimaadili na kidini na kutishia uzima wa kiroho wa mtu na jamii.
Kwa ujumla tunasema kuwa mwenendo mzuri, laini na tabia njema katika mahusiano ya kijamii huimarisha upendo baina ya watu na kuwa sababu ya ustawi na maendeleo, umri mrefu, kupata rizki zaidi na kadhalika. Imam Jaafar Swadiq (as) anasema: Mtu mwenye akhlaki na tabia njema hufungukiwa na njia nyingi za maisha".
Miongoni mwa misingi na kanuni muhimu za mahusiano ya kijamii ni kuheshimu nafsi, mali na hadhi za watu wengine. Katika dini ya Uislamu kuna sheria ambazo mtu atazikengeuka na kuzikanyaga hufuatiliwa kisheria na kukatiwa hukumu ya Mwenyezi Mungu. Uislamu umeithamini na kuweka sheria za kulinda roho ya mwanadamu tangu akiwa katika tumbo la mama na kuwakemea sana wale wanaohatarisha roho za wanadamu wenzao. Qur'ani tukufu inasema katika aya ya 32 ya Suratul Maida kwamba: Anayeua nafsi ambayo haijaua nafsi (ya mtu mwingine) au kufanya ufisadi na maovu katika ardhi, basi ni kama ameua watu wote. Na mwenye kuokoa nafsi ni kama ameokoa watu wote.."
Mali za watu pia zina heshima kama zilivyo roho na nafsi zao. Kwa msingi huo mafundisho ya Uislamu sambamba na kuwataka watu kulinda nafsi za wenzao vilevile yametilia mkazo ulazima wa kulindwa na kuheshimiwa mali zao. Kuheshimu mali za watu kunajumuisha kuwa mwaminifu katika amana za watu, kujiepusha kutumia mali zao bila ya ruhusa ya wenyewe, kulipa haki na madeni ya watu na kulinda mali na milki zao. Hii yote ni kwa ajili ya kulinda haki za watu wote, kuepusha mauaji, vinyongo na uhasama katika jamii.
Kulinda hadhi na heshima za watu ni katika vitu vilivyosisitizwa sana katika mahusiano ya kijamii. Njia muhimu zaidi ya kulinda heshima na hadhi ya muumini na ndugu yako katika dini ni kusitiri nakisi na mapungufu yake na kutoyaanika kadamnasi. Sisi sote tunajua kwamba Mwenyezi Mungu Raufu huwa haaniki na kuonesha wazi nakisi na dosari za watu japo kuwa anajua na kuona yote wanayoyatenda. Hivyo basi inakuwa kwa mwanadamu ambaye yeye mwenyewe ana nakisi na aibu nyingi kaanika na kuweka wazi nakisi na dosari za mwanadamu mwenzake? Inakuwaje kwa mwanadamu mwenye mapungufu mengine akachapukia kusengenya, kutafuta aibu na dosari za mwanadamu mwenzake na kumsema mwenzake mbele ya watu ilhali yeye mwenye anazo kasoro na nakisi kama hizo?

>>>>


Usikose kufuatilia mfululizo wa makala hii wiki ijayo.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)