Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 06 Aprili 2015 17:41

Uislamu na Mtindo wa Maisha (63)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (63)

Ni wakati mwingine wa kuwaletea mfululizo wa makala za Uislamu na Mtindo wa Maisha na hiki kikiwa ni kipindi cha 63. Katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia umuhimu wa kukirimu mgeni na adabu za ugeni katika fremu ya suna nzuri ya Kiislamu ya kuunga udugu. Leo tutazungumzia mahusiano zaidi yaina ya wanadamu yaani namna ya kuamiliana na majirani, jamii na makundi ya watu wengine. Hata hivyo kabla ya kuingia moja kwa moja kwenye maudhui hiyo hebu kwanza tutupie jicho uchadhura na umuhimu wa mahusiano ya kijamii.
Maana ya mahusiano na maingiliano ya kijamii ni mwenendo, maingiliano na mahusiano yetu na watu wengine kama wanadamu wenzetu, bila ya kujali kuwa ni ndugu, jamaa, jirani, wenzetu katika mji mmoja au nchi moja. Kwa maana nyingine ni kuwa ni jinsi ya kuamiliana na kila mtu ambaye ni mwanachama wa familia kubwa ya wanadamu. Uislamu umesisitiza sana juu ya kuamiliana vyema na wanadamu wenzetu na kuainisha mipaka na kanuni za miamala na mahusiano hayo na hata mtindo wa maisha wa Waislamu katika uwanja huo. Leo tunataka kutazama mafundisho ya Uislamu kuhusu misingi inayotawala mahusiano ya kijamii.
Baina yetu na katika maeneo mbalimbali duniani kunashuhudiwa baadhi ya watu wasiopenda kuwa na mahusiano na mlahaka na wanadamu wenzao. Watu wa aina hii hupendelea kuishi katika upweke na faraghani na wana sababu zao wenyewe wanazotumia kutetea mwenendo huo. Kwa mfano tu utawasikia baadhi yao wakisema kuwa, miongoni mwa faida za mwenendo huo wa kuishi katika upweke ni kuwa mwanadamu anaishi katika utulivu wa kifikra na kujishughulisha kwa utulivu kamili na maombi na kumtaradhia Mola Muumba wao. Vilevile husema kuwa huepuka athari mbaya za tuhuma, husuda na dhana mbaya za watu wenye fikra mbaya. Hata hivyo tunapaswa kusema kuwa, kuamiliana na kuwa na mahusiano mema na mlahaka na wanadamu wengine ni miongoni mwa mahitaji muhimu ya kiroho na kifikra ya mwanadamu. Kimaumbile, mwanadamu hupendelea kuwa na maisha ya kijamii, kwani hakuna mwanadamu, hata katika mazingira ya kawaida, anayeweza kuendeleza maisha akiwa peke yake. Ni katika jamii ndipo mwanadamu anapoweza kudumisha maisha yake na kuyaboresha zaidi. Mwanadamu anahitaji wanadamu wenzake si wakati wa kuanza maisha pekee bali katika vipindi na awamu zote za maisha yake. Katika mahusiano yake na wanadamu wengine ndipo mwanadamu anapoweza kujitambua vyema, kutambua sifa na uwezo wake na kupata taswira sahihi kuhusu nafsi yake. Hivi ulishawahi kujiuliza ni kwa nini moja ya adhabu kali zinazotolewa kwa wahalifu ni kufungwa katika seri ya mtu mmoja? Ni kutaka kumuweka mbali na wanadamu wenzake, kumtenga, kukata mahusiano yake na watu wengine kumnyima haki na kuzungumza nao na mengine kama hayo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mashaka anayopata mtu anayefungwa katika jela na seli ya mtu mmoja na kuwekwa mbali na wanadamu wenzake ni makubwa zaidi kuliko mashaka na tabu anazopata kwa kunyimwa chakula, mavazi na kadhalika.
Nukta nyingine kuhusu umuhimu wa kuwa na mahusiano na wanadamu wenzetu ni kuwa, sifa njema za kimaadili na zile mbaya za kiakhlaki huweza kudhihiri na kuonekana waziwazi katika kalibu ya mahusiano na mlahaka wa mtu na wanadamu wenzake. Maisha ya kijamii na kuamiliana na wanadamu wenzetu huwa medani ya kudhihiri sifa na maadili mema kama uadilifu, insafu, ihsani, kujitolea, ukarimu, upole, uaminifu, ukweli, utakasifu na kadhalika. Vilevile tabia na sifa mbaya za kimaadili kama dhulma, kukanyaga haki za watu, uchoyo, kiburi, usaliti, kusema uongo, kusengenya, husuda, ria na kadhalika hudhihiri na kuonekana wakati mtu anapokuwa katika mahusiano ya kijamii na wanadamu wenzake, na hapana shaka kuwa anawajibika kukabiliana na maovu na tabia mbaya na kufanya jitihada za kueneza maadili na tabia nzuri na njema.
Tunapotazama mafundisho ya Uislamu tunaona kuwa dini hiyo haiamuru au kukataza kwa sura mutlaki suala la kuwa na mahusiano ya kijamii. Suala la kuwa na mahusiano na mlahaka na watu wengine halina thamani ya kidhati, bali uzuri na ubaya wake unategemea malengo na makusudio yake na vilevile taathita zake kwa wanadamu. Miongoni mwa malengo ya kuwa na uhusiano na mlahaka na watu wengine ni kueneza maadili aali, kufaidika na akhlaki njema na kujiendeleza katika malezi ya nafsi. Hivyo basi, iwapo kuwa na uhusiano na kulahikiana na mtu au kundi la watu kutamtumbukiza mwanadamu katika maasia, madhambi na upotofu wa kimaadili na kumuweka mbali na njia ya saada na ufanisi, ni wazi kuwa mahusiano kama hayo ni kinyume na muradi na malengo, na mwanadamu anapaswa kuepukana nayo. Kinyume chake, pale uhusiano na mlahaka na mtu au watu unapokuwa sababu ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kuimarisha imani na misingi ya dini na maadili mema, basi uhusiano kama huu unapaswa kulindwa, kuimarishwa na kupanuliwa zaidi.
Uislamu hauamuru aina zote za mahusiano, bali inatambua baadhi ya mahusiano hayo kuwa yana madhara na uharibifu, na kwa msingi huo unayakataza na kuyaharamisha. Imepokewa kwamba Mtume Muhammad (saw) alimwambia sahaba wake mwema Abu Dharr al Ghifari (ra) kwamba: Ewe Abu Dharr! Mwenza na sahiba mwema ni bora kuliko upweke, na upweke ni bora kuliko mwenza na sahiba muovu." (Bihar aal Anwar-74:84)
Miongoni mwa aina za mahusiano ya kijamii ni mahusiano na wenzako katika imani na dini. Mahusiano ya mtu na wenzake katika imani na itikadi hujulikana kwa jina mahusiano ya kidini. Kwa mfano tu Mwislamu ana majukumu na wajibu mbele ya Waislamu wenzake. Bila shaka umeshawahi kusikia hadithi ya Mtume (saw) inayosema: Mwislamu anayesikia kilio cha ndugu yake Mwislamu na hakumsaidia, basi huyo si Mwislamu."
Vilevile kila mmoja wetu ana uhusiano makhsusi na watu wa mji au eneo lake ambao hauonekana baina yetu na watu wa eneo jingine. Mara nyingi tunachagua baadhi ya watu wa eneo, mji au dini yetu na kuwafanya marafiki wa chanda na pete. Jambo hili huwa sababu ya kujitokeza majumu makhsusi ya kiakhlaki na kimaadili baina ya pande hizo mbili. Mahusiano kama haya yamepewa mazingatio maalumu na Uislamu, mawalii wa Mwenyezi Mungu na maulamaa na wasomi wa akhlaki kutokana na taathira zake kubwa. Baadhi ya hadithi zinasema, miongoni mwa njia za kutambua itikadi, tabia na maadili ya watu ni kuwatambua marafiki na masahiba zao. Malenga maarufu wa Kiirani, Saadi, anasema katika moja ya mashairi yake kwamba: "Niambie unaishi na nani, ntakwambia wewe ni nani." Kwa maana kwamba nitakapojua unasuhubiana na kina nani nitajua shakhsia yako na kujua wewe ni nani na hata fikra na itikadi zako.
Hapana shaka yoyote kwamba kusuhubiana na watu waovu na wabaya humwelekeza mwanadamu upande wa mambo mabaya na maovu. Kimsingi sifa za rafiki na sahiba wa mtu huhamia kwa mwenzi wake kwa njia zisizo za moja kwa moja. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema: Msisuhubiane na watu waovu ili msije mkaathirika na tabia zao."
Miongoni mwa misingi inayosisitizwa na Uislamu katika mahusiano ya kijamii ni kuwatakia na kuwatendea wanadamu wenzako unayopenda wao wakufanyie wewe. Siku moja Mwarabu wa jangwani alikwenda kwa Mtume (saw) na kumwambia: Yaa Rasulallah! Nifundishe amali mbayo nikiifanya nitaingia peponi. Kwa kutilia maanani hali ya Mwarabu huyo ambaye hakuwa na uwezo wa kuja Madina mara kwa mara ili kupata miongozo ya Mtukufu huyo, Mtume (saw) alipaswa kumfunza amali ambayo itakuwa msingi na chanzo cha thamani nyingi za kimaadili. Kwa maana ya amali ambayo itakuwa kigezo na kipimo ambacho iwapo atakifanyia kazi kitakuwa sababu ya kuingia peponi. Mtume (saw) alimwambia: Watendee watu unayopenda wewe wakutendee, na jiepushe kuwafanyia watu usiyopenda wewe kufanyiwa."
Katika sehemu moja ya barua yake iliyojaa hekima na busara kwa mwanaye Hassan (as), Imam Ali bin Abi Twalib ameandika kwamba: Mwanangu Hassan! Kuwa mizani baina yako na wanadamu wengine; hivyo basi wapendee wenzako unayoyapenda wewe, na usiwatakie usiyotaka na kuyapenda wewe mwenyewe. Usidhulumu kama ambavyo hupendi kudhulumiwa, na tenda wema kama unavyopenda kutendewa wema. Wapendee watu unayoyapenda wewe mwenyewe na usiwaambie usiyopenda kuyasikia wewe..." > ... ....

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)