Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 16 Machi 2015 14:28

Uislamu na Mtindo wa Maisha (60)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (60)

Ni wasaa mwingine wa kuwa nanyi wafuatiliaji wazuri wa vpindi hivi vya  Uislamu na Mtindo wa Maisha. Baada ya kuzungumzia uhusiano wa mke na mume, haki za kila mmoja kati yao katika familia, haki za watoto na jinsi ya kuwalea na kuamiliana nao nafasi na baba na mama katika familia na nafasi ya wazee na watu wazima, Makala lyetu leo itatupia jicho jinsi ya mtu kuamiliana na jamaa, marafiki na jamii kwa ujumla.  >>

Kuunga udugu ni miongoni mwa statijia muhimu za malezi ya Uislamu katika mtindo wa maisha wa Kiislamu. Statijia hiyo ina mchango na nafasi muhimu katika kujenga mshikamano wa kifamilia na kurekebisha jamii. Kuunga udugu kuna maana ya kuwafanyia wema jamaa na ndugu wa karibu na mbali na waumini. Wema na msaada huo unaweza kuwa wa kimaada, kimaanawi, kijamii na kadhalika. Suna na ada hiyo njema ina asili katika fitra na maumbile safi ya mwanadamu.

Miongoni mwa misingi muhimu ya fitra na maumbile safi ya mwanadamu ni kujali utukufu wa kiumbe mwanadamu. Kimaumbile mwanadamu ana utukufu, heshima na hadhi kubwa zaidi ya viumbe vingine. Utukufu wa mwanadamu una maana ya adhama na utukufu wa kiroho na kuwa mbali na uovu na uchafu. Katika mafundisho ya dini kuna sheria na kanuni nyingi zinazomwamuru mwanadamu kujithamini yeye na wanadamu wenzake. Utamaduni wa dini ya Uislamu umesisitiza sana juu ya kuthamini nafsi ya mwanadamu na kumkirimu kiumbe huyo katika mienendo na matendo yetu. Miongoni mwa vielelezo vya kumkirimu wanadamu ni kuwahudumia na kuwafanyia wema na ihsani chini ya kivuli cha suna na ada njema ya kuunga udugu. Hapana shaka kuwa mtu anayewaheshimu na kuwakirimu wenzake huwa amedhihirisha shakhsia yake na kitendo hicho huwavutia wanadamu upande wake.

Hisi ya kutaka kupendwa na kupenda pia ni katika vielelezo vya maumbile safi na ya asili ya mwanadamu ambayo kiumbe huyo anaihitajia katika vipindi vyote vya maisha yake. Haja hii hushibishwa kupitia kwa baba, mama, dada, kaka, mke na jamaa wengine wa mwanadamu. Kuunga udugu katika vielelezo vyake vipana zaidi ni dhihirisho na kuchanua kwa hisi hiyo ya kifitra na kimaumbile. Kwa msingi huo msingi wa vielelezo vyote vya kuunga udugu unapaswa kuwa mahaba na upendo. Hivyo basi katika kivuli cha uhusiano wa kidugu kila mwanadamu hushibisha na kukidhi haja ya upendo na mahaba ya ndugu zake na pia hukidhi na kushibisha haja yake ya kimaumbile ya kutaka kupendwa na wengine. Mtume wetu Muhammad (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu pia wametilia sana mkazo suala la kuwa na mwenendo wa mahaba na upendo na ndugu, jamaa na marafiki. Imepokewa kwamba Mtume (saw) amesema: Kupenda na upendo ndiyo msingi wa dini yangu.

Kuwapenda wanadamu pia ni miongoni kwa hisi za kimaumbile na misingi muhimu ya kujenga udugu. Kuwapenda wanadamu humuondoa mtu katika duara finyu la kujiona yeye mwenyewe peke yake na kuwapuuza watu wengine. Mwenendo wa kuwapenda wanadamu ni tabia na mwenendo wa kijamii unaosifiwa na wanadamu wote na unapokuwa baina ya ndugu na jamaa huwa kielelezo cha kujenga udugu. Imepokewa kwamba Mtume (saw) amesema: Mtu asiyejali na kufuatilia masuala na matatizo ya Waislamu basi huyo si Mwislamu.    >>>>>

Miongoni mwa hisi za kifitra ni ile ya kupenda kusaidia wanadamu wenzetu na suala hili linatambuliwa kuwa miongoni mwa misingi na nguzo muhimu za kuunga udugu. Hisi hii kawaida humwelekeza mwanadamu katika kuwapenda watu.

Hisi nyingine ya kifitra na kimaumbile ni ile ya kupenda kusamehe. Tabia hii njema imesisitizwa sana katika mafundisho ya Uislamu na vilevile katika mwenendo wa Mtume na Ahlubaiti zake. Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Mtume (saw) inasema: Sameheni kwa sababu kufanya hivyo huzidisha izza na utukufu.

Kusamehe kumepewa umuhimu sana katika dini ya Uislamu kwa kadiri kwamba, Mwenyezi Mungu SW anamwamuru Mtume (saw) kushikamana barabara na jambo hilo katika aya ya 199 ya Suratul Aaraf inayosema: Shikamana na usamehevu na amrisha mema na achana na wajinga.

Pale waumini wanapojipamba kwa sifa hii wanaweza kupiga hatua muhimu katika kustawisha ada nzuri ya kuunga udugu.

Hisi ya kuwa na saada na furaha ya kudumu pia ni miongoni mwa hisi zenye nguvu katika nafsi ya mwanadamu ambazo zina mchango mkubwa katika kujenga udugu. Watu ambao hisi yao ya kupenda kuwa na saada na furaha maishani bado haijafubaa na kunyauka, hupenda kuona wanadamu wote wakiwemo ndugu na jamaa zao, wakiwa na furaha na saada maishani mwao na kila wanapomuona mtu mwenye mashaka na matatizo hufanya kila wanaoweza kuhakikisha kwamba anapata saada na maisha yenye furaha. Hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu pia zimewasifu sana watu wanaofanya hima katika kuhakikisha kwamba wanadamu wenzao wanakuwa na saada na furaha maishani mwao. Imepokewa kwamba Mtume (saw) amesema: Anayemfurahisha muumini huwa amenifurahisha mimi, na anayenifurahisha mimi huwa amemfurahisha Mwenyezi Mungu. Vilevile imepokewa kutoka kwa mjukuu wake Imam Mussa al Kadhim (as) kwamba amesema: Chini ya ardhi ya Mwenyezi Mungu kuna kivuli ambacho hatakaa hapo isipokuwa yule aliyemfanyia wema na jambo la kheri ndugu yake katika dini au kumuondolea matatizo yake na kumfurahisha.

Wafuatiliaji wa kipindi hiki hayo yote ni katika fremu ya mafundisho ya kuunga udugu katika Uislamu ambako huleta mabadiliko makubwa katika uhusiano wa ndugu na jamaa.

Hayo tuliyosema ni baadhi ya hisi za kimaumbile ambazo ndio msingi wa ada na suna nzuri ya kuunga udugu kunakosisitizwa sana katika dini ya Kiislamu. Mambo haya yanapaswa kuimarishwa katika watu wa jamii ili athari zake nzuri zienee na kufaidisha watu wote wa jamii husika.   >>

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)