Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 09 Machi 2015 11:49

Uislamu na Mtindo wa Maisha (59)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (59)

Katika makala ya wiki iliyopita tulisema kuwa kipindi cha uzeeni kama vilivyo vipindi vya utotoni, ujana na utu uzima ni katika awamu mbalimbali za ukamilifu wa mwanadamu kwa tofauti kwamba, kipindi cha utotoni na ujana huandamana na nishati, utanashati na nguvu, wakati kile cha uzeeni hufuatana na kupungua nguvu za kimwili na hakati za kifiziolojia. Kupanda juu umri wa mwanadamu husababisha mabadiliko makubwa katika mwili wake na inawezekana kuzuia baadhi ya matatizo kwa kuchunga mambo kadhaa muhimu katika kipindi hicho. Maisha ya kipindi cha uzeeni yanapaswa kuandamana na kuchunga masuala ya afya, kufanya mazoezi na kupata mlo wenye mlingano.

Kipindi cha uzeeni kina umuhimu sana na kinapaswa kupewa mazingatio maalumu na mzee mwenyewe na watu wanaomzunguka. Katika kipindi hicho baba na mama huwa dhaifu na hupoteza nguvu za kufanya kazi; kwa msingi huo wanawahitajia zaidi watoto wao. Hata hivyo tunapaswa kuelewa kwamba katika kipindi cha maisha yao na hata katika kipindi cha uzeeni, wazazi wengi wanahitajia zaidi upendo wa watoto wao, kuwajali na kuwa karibu nao kuliko masuala ya kimaada. Kwa kawaida kipindi cha uzeeni huambatana na magonjwa na matatizo ya aina mbalimbali. Ni wazi kuwa wakati huo wazazi wawili wazee huhitajia msaada wa watoto wao. Ni jambo la kawaida kuwa katika kipindi hicho cha uzeeni mwanadamu hupoteza nguvu na uwezo wake wa kawaida wa kimwili na hata sehemu ya uwezo wake wa kifikra na kinafsi. Wakati mwingine mzee husahau hata yale aliyojifunza na kujua hapo awali. Suala hili husababisha matatizo mengi kwa wazee na familia zao. Kwa msingi huo kujua vyema na kwa njia sahihi kipindi hiki cha uzeeni na kutambua mahitaji yao halisi kunaweza kuwasaidia watoto kwa ajili ya kuwa na mwenendo sahihi na unaonasibiana na baba na mama wazee.
Wakati mwingine baadhi ya watoto vijana na wasio na uzoefu na tajiriba na kutokana na kukosa subira na uvumilivu au ghururi na majivuno au kutokana na vyeo na nafasi zao za kazi hushindwa kutekeleza haki za wazazi wao wazee kama inavyostahiki. Yumkini pia watoto wa aina hii wakataka kujionesha kuwa wakamilifu na wenye nafasi ya juu zaidi mbele ya wazazi wao. Hata hivyo hatupasi kusahau kuwa, kuamiliana na wazazi wawili kwa kiburi na majivuno ni kukufuru neema ya Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu Qur'ani Tukufu inatukataza kuwa na mwenendo mbaya na wazazi wawili na inatutaka kuwa wanyenyekevu mbele yao na kuzungumza nao maneno mazuri na yanayofaa. Aya za 23 na 24 za Suratul Israa zinasema: "Mmoja wao akifikia uzee naye yuko kwako au wote wawili, basi usiwaambie ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa heshima. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma na useme: Mola wangu! Warehemu kama walivyonilea utotoni."
Vilevile tumesema katika vipindi vilivyopita kwamba miongoni mwa haki za wazazi kwa watoto wao ni kwamba wasiwaite kwa kutumia majina yao, wasiwatangulie wakati wa kutembea, wasiketi chini kabla ya wazazi kuketi na wala wasifanye jambo litakalowafanya watu wawaseme vibaya wazazi wao.
Katika utamaduni wa Kiislamu wazee na watu wazima wamepewa nafasi maalumu na yenye thamani kubwa. Watu wa familia wanapaswa kuwaheshimu na kuwaenzi wazee, kushauriana nao katika kazi na majukumu mbalimbali na kujali maamuzi na maoni yao wakati kunapotokea hitilafu. Kwa kawaida watoto na watu wa familia hujua neema na faida za wazee na watu wazima baada ya wao kuondoka hapa duniani hususan pale zinapojitokeza hitilafu za kifamilia ambazo mara nyingi hutatuliwa kwa neno moja au maneno machache tu ya mzee na mkuu wa familia husika. Ni kwa sababu hii ndiyo maana Mtume (saw) anasema: "Mzee katika familia yake ni mithili ya Mtume katika umma wake." Hadithi hii inaashiria nafasi adhimu na mchango mkubwa wa wazee katika kuongoza na kuelekeza vyema watu wa familia na jamaa zake. Kwa msingi huo nafasi hiyo ya watu wazima inapasa kulindwa na kuimarishwa. Vilevile tunapaswa kuelewa kwamba, kutilia maanani nafasi ya wazazi wazee huwa na taathira katika kuboresha hali yao ya kiroho na kinafsi. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Uislamu umetilia mkazo na kuhimiza sana jambo hilo.


>


Kuwajali na kuwathamini wazee huwafanya wasijihisi kuwa ni watu waliotengwa na kutupiliwa mbali na wakati huo huo huwawezesha vijana kupata tajiriba na uzofu wao wa miaka mingi. Kwa kuwa wazee na watu wazima ni kama tochi na nguzo ya mshikamano ndani ya familia, ni vyema kuwakirimu na kuwapa nafasi ya juu watu hao sharifu. Kuwaheshimu watu wazima na kuwarehemu na kuwaonea huruma wadogo ni miongoni mwa maagizo ya kiakhlaki ya dini ya Uislamu. Imepokewa kwamba, Imam Ali bin Abi Twalib (as) amesema: "Siku moja Mtume (saw) alituhutubia kisha akasema: "Waheshimuni watu wazima miongoni mwenu na warehemuni wadogo zenu."
Vilevile imepokewa kutoka kwa mjukuu wake Imam Jaafar Swadiq (as) kwamba amesema: "Si katika sisi (Waislamu) mtu asiyewaheshimu watu wazima na asiyewaonea huruma wadogo."
Imam Ali bin Abi Twalib pia amesema: "Mwanazuoni anapaswa kuheshimiwa kutokana na elimu yake na mtu mzima anapaswa kuheshimiwa kutokana na umri wake."
Pale vijana wanapokosa kuwaenzi na kuwaheshimu wazee suala hilo hupelekea kukatika mahusiano ya karibu ya kibinadamu na kukosa upendo na tajiriba ya watu watu wazima.
Jambo jingine muhimu la kuashiriwa hapa kuhusu umuhimu wa kuwakirimu na kuwaheshimu wazee na watu wazima ni suala la kuhamisha utamaduni huo kwa kizazi kijacho. Miongoni mwa njia za kuhamisha utamaduni kutoka kizazi kimoja kwenda kingine ni mienendo ya baba, mama, walezi na walimu. Watoto hujifunza na kuiga yale wanayoyaona yakifanywa na wakubwa wao kiumri. Kwa msingi huo watoto hujifunza utamaduni wa kuwaheshimu na kuwakirimu watu wazima pale wanapoona kivitendo wakubwa wao wakiwaheshimu na kuwakirimu wazee na watu wazima. Hivyo basi mtu anayetaka kuona watoto wake wakimheshimu na kumkirimu anapaswa yeye mwenyewe aamiliane hivyo hivyo na baba na mama yake ili watoto wajifunze kutoka kwake. Imepokewa kwamba Imam Ali bin Abi Twalib (as) amesema: "Waheshimuni wakubwa wenu ili mupate kuheshimiwa na wadogo wenu." Vilevile Imam Swadiq (as) amesema: "Watendeeni mema baba zenu ili watoto wenu wakutendeeni mema." Suala hili lina maana ya kuchuma mazao yanayopandwa na mwanadamu katika roho na moyo wa watoto kwa mwenendo wake. Tunapaswa kuelewa kwamba, somo muhimu zaidi la malezi ni lile linalotolewa kwa matendo na mienendo yetu na kwamba watoto wetu huwa wanafunzi makini sana katika kujifunza masomo ya kivitendo kutokana na mienendo yetu. Hivyo basi kama hatutawaheshimu wazee na watu wazima tutatarajia vipi kuona watoto wetu wakituheshimu na kutuenzi?

>>>>


Nukta nyingine ya kutiliwa maanani kuhusu wazee na watu wazima ni suala la afya zao za kiroho na kinafsi. Dakta Ahmad Bepajuh ambaye ni mtaalamu wa elimu nafsi nchini Iran anasema: Wazee na watu wazima wanapaswa kufanya jitihada za kuyapa maana maisha yao kwa kutumia vyema wakati wao wa mapumziko na kushiriki vilivyo katika masuala ya kijamii. Anasema: Kuanzisha uhusiano na watu wengine na kuwa wanachama katika makundi ya kijamii kunaweza kuwasaidia sana wazee katika upande huo. Kwa mfano mzee anaweza kujishughulisha na mambo mbalimbali kama kufanya kazi za kujitolea katika jumuiya zisizo za serikali, taasisi za kielimu, makundi ya kidini na kadhalika. Vilevile kuchagua burudani maalumu, kujishughulisha na kazi za sanaa na kaligrafia, kusafiri na watu wa familia au marafiki na kadhalika vinaweza pia kumsaidia mzee kiroho na kinafsi.

>>>>>>

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)