Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 02 Machi 2015 13:46

Uislamu na Mtindo wa Maisha (58)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (58)

Wafuatiliaji wa kipindi hiki karibuni  katika sehemu nyingine ya mfululizo wa makala hii ya Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kipindi chetu leo kinaendelea kuzungumzia nafasi ya wazazi wawili katika familia. >

Tunafungua kipindi chetu leo kwa aya za 23 na 24 za suratu Israa zinazosema: Na Mola wako amepitisha kuwa msimwabudu yeyote ila Yeye tu na muwatendee wema wazazi wawili. Mmoja wao akifikia uzee naye yuko kwako au wote wawili, basi usiwaambie ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa heshima. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma na useme: Mola wangu! Warehemu kama walivyonilea utotoni.

Katika aya hizi Mwenyezi Mungu SW anabainisha baadhi ya adabu za jinsi ya watoto wanavyopaswa kuamilia kwa heshima na wazazi wawili. Qur'ani Tukufu inaashiria hali ya uzee ya wazazi wawili wakati wanapohitajia zaidi msaada, upendo na himaya ya watoto wao kuliko wakati wowote mwingine na kusisitia kuwa, haijuzu kwa mtoto kumwambia mzazi wake hata neno dogo tu la dharau na udhia. Yumkini wazazi wawili au mmoja wao akashindwa hata kutembea au kuinuka chini bila ya msaada kutokana na uzee. Wakati huu watoto wao hukabiliwa na mtihani mkubwa. Je, mtoto atakutambua kuwepo mzazi kama huyo asiyejiweza kuwa ni sababu ya kuwafanyia rehma na wema au ni adhabu, balaa na usumbufu kwake? Je watoto watakuwa na subira ya kutosha ya kukaa kwa heshima na upendo na wazazi wao waliozeeka na kufikia umri wa kutojiweza au watakuwa wakiwadhalilisha na kuwaambia maneno yasiyopendeza yanayokera roho na nafsi zao?

Katika upande mwingine Qur'ani Tukufu inasema: Wakati wazazi wanapokuwa wazee usiwaambia neno uf, kwa maana kwamba usiwaambie hata neno dogo zaidi la kuwaumiza roho na kuwakasirisha, bali zungumza nao kwa heshima na adabu kubwa. Kisha Mwenyezi Mungu Karimu anatuamuru kuwa wanyenyekevu katika kuamiliana na wazazi wetu wawili na kudhihirisha upendo na mahaba kwao. Vilevile anatuamuru kuwaombea dua na kuwatakia rehma na kwamba tusisahau jinsi wao walivyoturehemu sisi na kutulea kwa upendo na mahaba wakati tulipokuwa wadogo.

Imepokewa kutoka kwa mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Jaafar Swadiq (as) kwamba amesema kuhusu aya hii kwamba: Iwapo kungekuwapo jambo dogo zaidi linaloweza kumkera mzazi kuliko hata kumwambia ah! Basi Mwenyezi Mungu angelikataza. Kuwaheshimu na kuwatunza vyema wazazi wawili kumepewa umuhimu sana katika dini ya Uislamu kwa kadiri kwamba, kumetangulizwa hata mbele ya vita vya jihadi katika baadhi ya hali. Historia inasema kuwa bwana mmoja alikwenda kwa Mtume (saw) na kusema: Mimi ni kijana shupavu na mwenye nguvu na ninapenda kwenda kupigana jihadi na maadui wa Mwenyezi Mungu lakini mama yangu anakasirishwa sana na jambo hilo. Mtume (saw) alisema: Rudi nyumbani na ukae na mama yako. Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu aliyenituma kwa mjumbe wake kwamba kumfurahisha mama yako usiku mmoja ni bora zaidi kuliko kupigana jihadi mwaka mzima katika njia ya Mwenyezi Mungu."

Hapa tunapaswa kuelewa kuwa, wajibu wa kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na kulinda dini yake unaanguka kwa Mwislamu maadamu wako watu wengine wanaotosheleza kupigana jihadi na maadui na maadamu dola la Kislamu halijavamiwa na madui la sivyo Mwislamu anawajibika kutanguliza jihadi na kutetea dini la dola la Kiislamu.

Dini ya Uislamu inamuusia mtoto kujilinda asije akalaaniwa na kukasirikiwa na wazazi wake. Mtume (saw) amesema: Jiepusheni kuwaasi na kuwatendea baya baba na mama zenu, kwani harufu ya pepo huhisika kutoka umbali wa masafa ya miaka 1000 lakini haitamfikia mtu aliyewaasi na kuwatendea uovu na baba na mama yake." Maneno ya hadithi hii ya Mtume yana ishara na busara kubwa inayotaka kutueleza kwamba, mtu aliyewaasi na kuwatendea uovu baba na mama yake situ kwamba hataingia peponi, bali hata harufu yake hataihisi na kuisikia.

Imenukuliwa kwamba katika zama za Mtume (saw) bwana mmoja alionekana akitufu na kuzunguka al Kaaba huku akiwa amembeba mama yake mabegani na kumsaidia kutufu Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Baadaye kidogo alimuona Mtume kisha akamuuliza: Yaa Rasulallah! Je, Nimetekeleza haki mama yangu kwa kazi hii? Mtume (saw) alimwambia: Hapana. Hujafidia hata ukulele wake mmoja tu wakati alipokuwa akijifungua mimba yako."

Vilevile imepokewa kwamba bwana mmoja alikwenda kwa Mtume (saw) na kumuuliza haki ya baba kwa mtoto wake. Mtume alisema: Asimwite kwa kutumia jina lake, asimtangulie wakati wa kutembea, asiketi chini kabla ya yeye kuketi na wala asifanye jambo litakalowafanya watu wamseme vibaya baba yake."

Hapa inatupasha kukumbusha kwamba wakati mwinginme wazazi wawili huwataka watoto wao kufanya jambo lisilo la kimantiki au kinyume cha sheria na dini. Ni wazi kuwa wakati huu si wajibu kuwatii katika mambo kama haya. Hata hivyo mtoto anawajibika kuamiliana nao kwa wema na upole.    >

Maadamu tumezungumzia kipindi cha uzee cha wazazi wawili ni vyema tugusia wala kwa ufupi maudhui ya wazee na nafasi ya watu wazima katika mtindo wa maisha wa Kiislamu. Dini hiyo tukufu imejali na kutilia maanani suala la jinsi ya kuamiliana na watu wazima katika familia na jinsi ya kukidhi haka na mahitaji yao.

Katika maisha yetu ya kila siku tunakutana na watu wengi ambao nyuso zao zinaonekana kuchoka na kula chumvi nyingi. Watu hawa wanawakilisha kizazi chenye kumbukumbu nyingi za zama zilizopita na hapana shaka kwamba kizazi kipya kinahitaji uzoefu na tajiriba yao. Utu uzuma na uzee si wakfu kwa watu duna ya wengine, bali sisi sote ipo siku tutakuwa wazee. Baadhi ya watu huomba dua wasizeeke kiasi cha kuwa mzigo na tabu kwa watu wengine. Wapo wengine wanaomba dua ya kupewa umri mrefu na wanalitambua suala hilo kuwa ni baraka na neema ya Mola Muumba. Uzee, wapenzi wasikilizaji, ni sehemu muhimu ya maisha ya mwanadamu na tunaweza kusema kuwa ni sehemu moja ya awamu za ukamilifu wa kiumbe huyo. Uzee huja baada ya kipindi cha utoto, ujana na utu uzima. Katika nchi nyingi duniani watu hutambuliwa kuwa ni wazee wanapofikia umri wa miaka 65. Mwanadamu hupitia awamu mbalimbali hadi anapofikia kipindi cha uzee na katika kipindi hicho chote hupata tajiriba na uzoefu mkubwa. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, uzee na utu uzima ni kipindi cha kukusanyika tajiriba na uzoefu wa mwanadamu. Ni kipindi cha kufikia na kutimia matakwa yote ya kiroho iwapo mwanadamu atakuwa amepitia awamu nyingine zote za maisha yake kwa mafanikio kama wanavyosema wataalamu wa elimu nafsi. Wataalamu hao wa elimu nafsi pia wanasema kuwa iwapo mahitaji ya kimaisha ya mwanadamu hayakukidhiwa ipasavyo katika kipindi cha maisha yake basi ni vigumu kutarajia mwenendo wenye ulingano wa kijamii kutoka kwa mtu huyo anapokuwa katika kipindi cha uzee.

Inatupasa kutambua kuwa kujitokeza matatizo mengi na ya aina mbalimbali katika kipindi cha uzee ni jambo la kawaida na kimaumbile. Hii ni kwa sababu nguvu za mwili na kiakili za mwanadamu hulika na kupungua kadiri umri wake unavyokita katika uzee. Kwa msingi huo huwenda hakuna kipindi chenye kutia wasiwasi zaidi kwa mwanadamu na chenye mishkeli na matatizo zaidi kuliko kipindi cha uzeeni. Kwa sababu hiyo wazee huhitajia kuwa katika mazingira yanayokwenda sambamba na umri wao ili watu wa umri huo waweze kubakia salama.    

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)