Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 09 Februari 2015 12:32

Uislamu na Mtindo wa Maisha (55)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (55)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya kipindi chetu cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Wiki hii tutazungumzia nafasi ya vijana na jinsi ya kuamiliana nao katika familia. Karibuni..

>>>


Familia ambayo ndiyo kituo muhimu zaidi cha maisha ya mwanadamu ina taathira kubwa katika mwenendo wa kiumbe huyo na katika kiwango cha mafanikio yake. Vilevile muamala wa wanachama wa familia huwa na taathira katika kuundika shakhsia ya kila mmoja kati ya wanachama hao. Miongoni mwa masuala yenye umuhimu mkubwa katika familia ni jinsi ya kuamiliana na vijana. Mtindo wa maisha wa Kiislamu umelipa umuhimu sana tabaka hilo la vijana.
Vijana ni mithili ya moyo wa jamii na kadiri moyo huo unavyofanya kazi yake vyema ndivyo mishipa ya mwili wa jamii unavyopata damu ya kutosha na mpya. Ujana ni msimu wa machipuo wa umri wa mwanadamu na alfajiri ya maisha ya kiumbe huyo. Katika kipindi hicho cha ujana, mwanadamu huwa na uoni mpana zaidi, na viongozi wa dini ya Uislamu wanautaja ujana kuwa ni miongoni mwa neema zenye thamani kubwa za Mwenyezi Mungu. Mtume Muhammad (saw) amesema: "Siku ya Kiyama mwanadamu hataweza kupiga hatua yoyote ile ila baada ya kujibu maswali kadhaa. Ataulizwa kuhusu umri wake aliutumia vipi na pili ujana wake ameutumia vipi na katika njia gani?
Katika mtazamo wa Uislamu ujana ni kipindi cha uwezo na ustawi na ni fursa nzuri ya kutumia neema ya maisha. Mtume wetu Muhammad (saw) aliwapa umuhimu mkubwa vijana na alikuwa akiwapa majukumu muhimu vijana wenye sifa na wastahiki. Vilevile alikuwa akiwasifu vijana na kuwausia wazazi kuwafanyia kheri. Imenukuliwa kwamba mtukufu huyo amesema:


انّ الله بعثنی بشیراً و نذیراً فحالفنی الشُّبّانُ و خالفن الشیوخُ


Mwenyezi Mungu SW alinituma kuwabashiria rehma zake na kuwaonya na adhabu yake. Vijana walinikubali na kufunga mkataba wa upendo na mimi na wazee wakanipinga..."


Roho ya kijana imejaa nishati na usafi na daima huwa mdadisi na mwenye kutaka kuchungua na kujua kila kitu. Kijana hutaka kujua yeye ni nani na ana mchango gani maishani? Hutaka kujua uhusiano wake na dunia inayomzunguka. Kijana kama huyu hufanya jitihada za kufikia ukamilifu zaidi wa kifikra na kiroho. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kujua nafsi humsaidia na kumuwezesha mwanadamu kumjua na kumtambua Mola wake Muumba. Pale kijana anapoijua vyema nafsi yake na uwezo wa ndani ya nafsi yake hupata hali ya kujiamini zaidi. Hivyo basi tunaweza kusema kuwa kuijua nafsi ni miongoni mwa mambo ya dharura ya kipindi cha ujana.
Wazazi wana nafasi kubwa na muhimu katika kuumbika utambulisho ya vijana. Muamala mwema na wa upendo wa wazazi na vijana huwasaidia kuwa na taswira chanya kuhusu nafsi zao. Kwa msingi huo miongoni mwa makosa ya wazazi wawili ni kwamba huhisi kuwa watoto huhitaji upendo na mahaba yao wakati wanapokuwa makinda na wadogo na si katika kipindi cha ujana na ubarubaru. Hii ni katika hali ambayo, mwanadamu huhitajia upendo na mahaba ya wazazi na watu wengine katika awamu zote za maisha. Mahaba na upendo wa familia kwa kijana humfanya ajihisi kuwa na amani, kuthaminiwa na kuwa na moyo wa kujiamini. Mahaba na upendo kama huo pia humuimarisha kiroho na kumpa mtazamo chana kijana. Suala hilo humuandalia kijana mazingira mazuri ya kuchanua vipawa na uwezo wake wa ndani ya nafsi.

>>>


Suala jingine lenye umuhimu mkubwa katika maisha ya kijana ni kuwa na lengo. Wazazi wanapaswa kumsaidia kijana katika kuchagua lengo la kimantiki na linalokubalika na kuwa na imani na lengo au malengo hayo. Vijana wenye malengo maalumu maishani huelekeza nguvu zao zote katika njia hiyo, suala ambalo humkurubisha zaidi katika muradi na malengo yake. Malengo aali na ya juu zaidi katika maisha ya kijana huwa kielelezo cha idara imara na hima yake kubwa. Kijana mwenye lengo huwa hapotezi muda na wakati wake katika mambo ya kipuuzi na suala hilo humfanya kijana kuwa mtu mwenye utambulisho na mwelekeo maalumu.
Vijana pia huhitaji kuthaminiwa na kuheshimiwa ndani ya familia. Vijana wanapaswa kuhisi kuwa wana nafasi na mchango katika familia zao na miongoni mwa njia za kujenga hisia hiyo ndani ya nafsi za vijana ni kushauriana nao na kuwapa majukumu ya kufanya. Kama tulivyotangulia kusema, Mtume Muhammad (saw) aliwapa umuhimu mkubwa vijana na katika vipindi na nyakati mbalimbali aliwapa majukumu ya kiutekelezaji au kuwashirikisha katika kuchukua maamuzi muhimu. Kushauriana na vijana huwaimarisha kiakili na kuwafanya wahisi kwamba wanakubaliwa na kuthaminiwa. Suala hilo pia hufungua mlango wa maelewano baina ya vijana na watu wazima. Mtaalamu wa saikolijia wa Iran Dakta Muhammad Ridha Sharafi anasema: Kijana huwa katika nafasi ya kupokea anachopewa na huupa umuhimu mwenendo wa watu wengine, hukumu na tathmini yao juu yake. Kwa msingi huo kuna udharura kwa watu wanaomzunguka kijana kuwa waangalifu sana katika kuamiliana naye kwa maana kwamba, wamulike zaidi upande chanya na mzuri wa kijana katika miamala na mwenendo wao.
Tumesema kuwa suala la kupata utambulsho na kujua nafsi lina umuhimu mkubwa sana kwa vijana na kwamba suala hilo linapaswa kupewa mazingatio maalumu na wazazi. Na tunasisitiza kuwa kijana ambaye anayeshindwa kupata utambulisho wake halisi na kuijua vyema nafsi na uwezo wake hukabiliwa na mgogo au kukumbwa na hali ya kutangatanga kinafsi na kiroho. Vijana wengi wanaokumbwa na tatizo la kukosa utambulisho na kutoijua vyema nafsi na uwezo wao hujihisi bure bilashi, mtu asiye na faida, mgeni wa nafsi yake mwenyewe na mpeke. Vilevile wataalamu wanasema matatizo mengi ya kijamii ya vijana ni matokeo ya kukosa utambulisho na kutoijua nafsi. Kijana asiye na lengo na asiyejiona kuwa na mchango na taathira yoyote hujiona kuwa bure, duni na asiye na thamani na kwa msingi huo huanza kujishughulisha na masuala mengine au hata kutumbukia katika uhalifu. Kwa mfano tu kijana kama huyo hujishughulisha na mambo kama ya kuvaa aina vulani ya mavazi, viatu au kuseti nywele zake kwa mtindo fulani ili kujaza uwazi uliosababishwa na kukosa utambulisho na malengo aali na muhimu maisha mwake.
Kwa msingi huo wazazi wawali wanawajibika kumsaidia kijana na katika kuchagua malengo sahihi, kujua nafsi na uwezo wake, kumfanya ajihisi anathaminiwa na kupendwa.

>>

Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi chetu umefikia ukingoni. Msikose kuwa nasi tena juma lijalo katika sehemu nyingine ya kipindi chqa Uislamu na Mtindo wa Maisha.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)