Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 12 Januari 2015 17:23

Uislamu na Mtindo wa Maisha (51)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (51)

Assalamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na hii ikiwa ni sehemu ya 51 ya mfululizo wa kipindi chetu wa Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kipindi chetu cha leo kitaendela kuzungumzia malezi ya kidini ya watoto.

>>>

Hapana shaka kwamba familia ndiyo sehemu mtoto anakopata na kujifunza thamani za kimaadili, itikadi za kidini na malezi ya kijamii ya wazazi wawili na kumtayarishia mtoto ustawi wa kimwili na kiroho. Kwa msingi huo tunaweza kudai kuwa, taasisi ya familia ina mchango mkubwa sana katika kutoa malezi ya kidini kwa watoto. Wataalamu wa elimu nafsi wanasema kuwa, familia inapaswa kuanza mchakato wa kumuelekeza mtoto kwenye matukufu ya kidini tangu kipindi cha awali cha utotoni. Wakati mwingine baba na mama na hata walezi ambao, huwapa watoto mafundsho ya dini kwa nia njema, hughafilika na suala muhimu ambalo ni kutokuwa na maarifa ya kutosha kuhusu masuala ya kinafsi ya kisaikolojia ya watoto wao. Kwa sababu hiyo hujikuta wakiukera moyo na roho ya mtoto kwa kufanya makosa mengi. Katika kipindi cha utotoni imani na hisi za kidini zinapaswa kuundika katika anga ya urafiki na upendo na kwa kutumia njia sahihi; na malezi ya aina hiyo yanapaswa kutolewa kwa njia itakayoathiri fikra, mwenendo na roho ya mtoto.
Lengo kuu la dini ni kulea wanadamu na kustawisha hisia na mwenendo mzuri wa kimaadili na kiroho. Katika mazingira ya familia baba na mama huwa vigezo vya kwanza kabisa ambavyo mtoto hujifunza kwao thamani za kimaadili na kidini na masomo mengine mema ya maisha. Kwa msingi huo wazazi wawili wanapaswa kuwa picha na kigezo bora cha maadili mema na kutayarisha anga ya ndani ya familia kwa ajili ya ustawi wa kiroho na kimaadili wa watoto. Kwani pale walezi wanapokuwa kigezo bora katika matendo na mwenendo, suala hilo huwasaidia watoto kutekeleza faradhi na wajibu wao wa kidini. Katika uwanja huo, wataalamu wa elimu nafsi wanasisitiza kuwa, kujifunza kwa kuona kwa macho ndiyo njia bora zaidi ya kuwapa watoto malezi bora. Imam Jafar Swadiq (as) anasema: Baba yangu, Muhammad Baqir (as), alikuwa akimkumbuka na kumtaja Mwenyezi Mungu wakati wote. Nilipokuwa nikitembea naye, daima nilikuwa nikimuona katika hali ya kumdhukuru na kumtaja Mwenyezi Mungu. Alikuwa akimtaja Mwenyezi Mungu hata wakati anapozungumza na watu. Kabla ya kuchomoza jua, baba alikuwa akitukusanya pamoja na kumuamuru kusoma Qur'ani kila mtu anayeweza kusoma, na yule asiyeweza kusoma Qur'ani alikuwa akimwamuru kumdhukuru na kumtaja Mwenyezi Mungu."
Hadithi hiyo wapenzi wasikilizaji ina masuala mawili muhimu: Kwanza ni kuwa Imam Baqir (as) kama baba wa familia, alikuwa ruwaza njema na kigezo bora katika matendo na katika kumdhukuru na kumtaja Mwenyezi Mungu na daima maneno yake yaliambatana na kuoana na matendo yake. Suala la pili ni kuwa, watoto hawapaswi kuachwa hivihivi, bali sambamba na kupewa uhuru wa kimantiki, wanapaswa pia kutayarishiwa uwanja mzuri wa kustawi kiroho na kimaanawi na kuamrisha moyo wa kuwasiliana na Mola Muumba kwa kutumia mbinu mbalimbali.

>>>

Lengo la malezi ya kidini ni kuhuisha shauku na hamu ya kumjua na kumwabudu Mwenyezi Mungu ndani ya nafsi ya mwanadamu. Wataalamu wa elimu nafsi wanasema kuwa, wakati shauku na hamu ya kupenda dini na Mwenyezi Mungu inapoimarika ndani ya nafsi ya mwanadamu hususan watoto wadogo, suala hilo huwa na taathira kubwa za kimalezi katika roho na mwenendo wao. Kazi kubwa ya mlezi katika kustawisha hisi ya dini ndani ya nafsi za watoto ni kuhuisha hisi ya kupenda kudadisi na hamu ya kutafuta ukweli na matukufu ya mafunzo ya kidini. Katika njia ya kufikia lengo hilo wazazi na walezi wanapaswa kujiepusha na njia zote za kutaka kumtwisha au kupachika mtoto mafundisho ya kidini bila ya kwanza kutayarisha uwanja mzuri wa kukubali suala hilo.
Miongoni mwa matatizo yanayojitokeza katika njia ya malezi ya kidini ndani ya familia ni kutosheka na mbinu za kijujuu juu tu na za kupita katika kuwapa mafunzo watoto. Ukweli ni kuwa ili kupata mafanikio katika malezi ya kidini ya watoto kuna udharura wa kudumishwa malezi hayo hadi yanapokita na kuweka mizizi katika akili na nafsi ya mtoto. Njia hii yenye taathira kubwa katika malezi ndio mbinu ya kuhuisha mafundisho ya kidini katika nafsi mbayo inapaswa kuanza katika kipindi cha utotoni na kusimamiwa kwa njia sahihi hadi mwisho. Pale mafundisho ya dini ya Uislamu na utekelezaji wa faradhi na wajibu wa kidini vinapofundishwa tangu kipindi cha utotoni na kudumishwa hukita mizizi ndani ya nafsi na kuwa na taathira ya kudumu; kinyume chake malezi na mafundisho hayo hupoteza taathira na kushindwa kufikia malengo yake. Kwa msingi huo mafundisho ya kidini kwa watoto yanapaswa kudumishwa hadi yanapokita mizizi ndani ya nafsi ya watoto.
Mtaalamu wa elimu nafsi wa Iran Dakta Abdul Adhiim Karimi anasema: Miongoni mwa matatizo ya na changamoto kubwa za malezi ya kidini ni ukali na kuwalazimisha watoto kufanya ibada na amali ngumu na zenye mashaka. Kwa hakika miongoni mwa sababu za dini kuusia mwenendo wa upole na misimamo laini na ya wastani katika kufundisha dini ni kuwafanya watoto wasihisi kwamba wazazi wao wanawateza nguvu na kuwatwisha mitazamo yao. Hata hivyo tunapaswa kutambua kuwa, kuwa na misimamo laini katika kuamiliana na watoto hakuna maana ya kuwaacha hivihivi, bali maana yake ni kuchunga uadilifu na msimamo wa kati na kati na kujiepusha na misimamo mikali katika malezi yao.
Kuwahamasisha watoto kutekeleza wajibu na faradhi za kidini kwa kutumia njia mbalimbali za kuvutia na lugha tamu na nyepesi huwafanya watoto wazoee na kuwa na hamu zaidi ya kutekeleza mambo hayo. Wazazi wenye ufanisi hutayarisha uwanja mzuri kwa watoto wao kwa ajili ya kutekeleza wajibu wao wa kidini tena katika anga ya kuvutia, na wakati huo huo hufanya jitihada za kuzidisha uelewa na maarifa ya kidini ya watoto wao hatua kwa hatua.

>>>>

 

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)