Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 05 Januari 2015 14:51

Uislamu na Mtindo wa Maisha (50)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (50)

Kama bado mnakumbuka katika kipindi kilichopita cha Uislamu na Mtindo wa Maisha tuliendelea kuzungumzia jinsi wazazi wawili wanavyopaswa kuamiliana na watoto wao. Hata hivyo suala lenye umuhimu mkubwa katika uwanja huo ni malezi ya kidini ya watoto ambalo ndilo suala tutakalolijadili katika kipindi chetu cha leo. Basi msiache kufuatilia makala hii.

>>>

Baadhi ya familia huwa na misimamo mikali katika suala la malezi ya watoto. Wakati huo huo kuna familia ambazo huwa na misimamo laini na kuamiliana kwa upole na uvumilivu katika kulea watoto wao. Kuna kundi jingine la tatu la wazazi lenye mbinu tofauti ya malezi ambao hujali na kutilia maanani njia ya wastani na ya kati na kati katika kukidhi mahitaji ya kimalezi ya watoto wao.
Familia zenye misimamo mikali katika malezi ya watoto husisitiza zaidi uwezo wa nguvu kupita kiasi ya wazazi. Malezi katika familia za aina hii hufuata kanuni na sheria ngumu kali kama msumeno. Kwa kadiri kwamba mtu mmoja huwa ndiye mtawala wa familia anayeainisha na kupanga kanuni hizo. Kwa kawaida mtu huyo huwa baba na wakati mwingine mama wa familia. Ktika familia kama hizi watoto hukosa haki zao makhsusi na hutwishwa kanuni na kaida ngumu.
Mhakiki wa Kijerumani kwa jina la Huffman amesema baada ya uchunguzi kuhusu suala hilo kwamba: Kwa kawaida watoto wanaokulia katika familia zenye misimamo mikali huwa watiifu na wenye kutekeleza amri wanazopewa. Lakini mara nyingi mwenendo wao huandamana na ukorofi. Watoto wa aina hii huwa hawapendwi sana baina ya watoto wenzao kwa sababu huwa hawaheshimu haki za wenzi wao. Vilevile huwa hawajali ukosoaji wa watu wazima.
Watoto wa wazazi wenye misimamo mikali kwa kawaida huwa hawashiriki katika kazi za kimakundi na hawajitegemei vya kutosha. Aghlabu yao huwa watu tegemezi na wasiokuwa wabunifu. Watoto wa aina hii bila ya kujua hujifananisha na wazazi wao na kuwa na mwenendo wa kihasama katika miamala yao na watu wengine. Matokeo yake ni kuwa huwaudhi na kuwakera watoto wa rika lao na wa chini yao.
Mkabala wa wazazi hawa wenye misimamo mikali wako wazazi na familia zenye mismamo poa na laini katika malezi ya watoto wanaochukulia kila kitu kwa urahisi na sahali. Wazazi wa aina hii huwaruhusu watoto wao kutimiza matakwa yao yote. Katika familia za aina hii kila mtu hufanya kila alitakalo na wenzake hawana haki ya kuingilia katika kazi zake.
Waungaji mkono wa mbinu hii ya malezi wanaamini kuwa, matamanio ya watoto wao hutawala mienendo yao; kwani kuwanyima watoto uhuru huwa sababu ya kupatwa na matatizo ya kinafsi na kisaikilojia. Kundi hilo linasema kuwa kila takwa huakisi haja ya ndani ya nafsi na kwamba kuna udharura wa haja hiyo kukidhiwa haraka iwezekanavyo. Kwa hakika kwa mujibu wa mtazamo wa watetezi wa mbinu hii ya malezi, matamanio na matakwa ya watoto ndiyo dira bora kwa ajili ya kudhamini usalama wa kimwili na kinafsi wa watoto hao. Familia zenye misimamo laini na poa huwa hazijali mafunzo ya mienendo ya kijamii, uingiliaji wa baba na mama katika kazi za watoto wao huwa hauna maana yoyote na kila mmoja kati ya wanachama wa familia husika hufanya kila analotaka.
Hapana shaka kuwa mbinu hii ya malezi pia ina taathira ngingi mbaya. Wataalamu wa elimu ya mwenendo wanasema kuwa, matokeo ya kuwa na misimamo laini na kuwapa watoto uhuru kupindukia ni mparaganyiko na ukosefu wa nidhamu katika uhusiano wa wanachama wa familia. Vilevile aghlabu ya watu wanaofuata matamanio na matakwa yao ya kinafsi huishi katika ndoto tupu na kuwa mbali na uhakika na maisha halisi. Vilevile watoto wa familia kama hizi huwa watu wasiojali sheria na mipaka ya dini na maadili na wasiokuwa na malengo na vilevile watu wasiowajibika mkabala wa wengine. Kwa msingi huo hushindwa kuwa na uhusiano mzuri na watu wengine. Japokuwa watoto wa familia kama hizi zenye misimamo poa na laini huwa watu wenye kujitegemea kifikra na katika matendo yao lakini hukumbwa na aina fulani ya mtetereko wa kiroho kutokana na kutokuwa na nidhamu na kanuni katika malezi yao. Mtetereko huo wa kiroho huwa sababu ya kujitokeza matatizo katika jinsi ya kuamiliana na watu binafsi na jamii.

>>>>

Mkabala wa mbinu hizo zilizochupa mipaka katika malezi ya watoto, kuna mbinu ya wastani, mantiki na mlingano. Katika familia zenye mlingano malezi ya watoto hufanyika kwa mujibu wa misingi sahihi ambayo mbali na kuwaruhusu wazazi wawili kusimamia na kudhuibiti mienendo ya watoto wao kwa njia ya moja kwa moja au siyo ya moja kwa moja, huwa haidhuru hisi ya kujitegemea na uhuru wa kifikra wa watoto. Malezi ya kidini ni miongoni mwa mbinu hizo zenye mlingano na sahihi zaidi. Mafundisho ya Uislamu yanatuhimiza sana kuchunga uadilifu na mlingano katika uhusiano wa wanachama wa familia hususan uhusiano kati ya wazazi wawili na watoto. Katika utamaduni wa Uislamu, watoto ni amana ya Mwenyezi Mungu na wazazi wanawajibika kulinda usalama, uzima, ustawi, malezi na ufanisi wao. Wazazi hawana ruhusa ya kukwamisha ustawi na ukamilifu wa watoto au kuwa sababu ya kupotoka kwao kutokana na misimamo mikali isiyokuwa na maana wala mantiki. Wazazi pia hawapaswi kuwapa watoto uhuru mutlaki na usio na mpaka au kuwa wepesi na poa kiasi kwamba watoto wanaweza kufanya lolote wanalotaka.
Katika aya ya sita ya Suratu Tahrim, Mwenyezi Mungu SW anatahadharisha akisema: Enyi mlioamini! Zilindeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe..". Baadhi ya wafasiri wa Qur'ani wanasema kuwa, maana ya kulinda familia na moto wa Jahannam katika aya hiyo ni kuwapa elimu na malezi sahihi watu wa familia na kuwatayarishia mazingira safi yaliyombali na aina zote za machafu ya kimaada na kiroho. Suala hilo linapaswa kuchungwa na kutekelezwa katika awamu zote za maisha hususan awamu za awali za malezi ya watoto. Kwani iwapo watoto wataachwa hivihivi basi watatumbukia katika upotofu na kuwa mbali na thamani za kimaadili na misingi ya malezi sahihi. Wakati huo huo iwapo wazazi wataamiliana na watoto kwa misimamo na kanuni kali kama msumeno kwa kadiri ya kuwafanya wahisi mbinyo na kubanwa na wazazi, basi watatokea kuwa waasi na kukabiliana na wazazi wao. Hivyo wazazi wanaweza kuchunga vyema amana hiyo ya Mwenyezi Mungu kwa usimamizi mzuri unaooana na muundo wa kiroho na kinafsi wa watoto.
Suala linalopewa umuhimu zaidi katika malezi ya kidini ni fitra na mahitaji ya kimaumbile ya watoto. Hii ni kwa sababu fitra na maumbile asili ndiyo chemchemi ya ndani ya nafsi ya malezi na sifa zote aali za kibinadamu. Tunaweza kusema kuwa kanuni na misingi ya malezi imewekwa ndani ya nafsi ya mwanadamu. Kwa msingi huo iwapo hakutakuwapo vikwazo na kukatayarishwa mazingira mazuri basi kito hicho kitachanua na kustawi katika nyanja na pande zote. Hivyo kimaumbile watoto humtambua Mwenyezi Mungu na huvutiwa na mambo mema na tabia bora. Baba na mama wanapaswa kufanya jitihada za kuhakikisha thamani hizo za kimaumbile zinastawi ndani ya nafsi ya mtoto na wasitosheke na mila na desturi za kidhahiri tu za kidini.
Katika malezi ya Kiislamu kunasisitizwa sana suala la kuwa na maarifa na uoni wa kidini. Vilevile Mtume Muhammad (saw) na maimamu watoharifu katika kizazi chake walikuwa wamesisitiza sana juu ya suala hilo la kuwa na maarifa ya kidini.

>>>>

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)