Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 15 Disemba 2014 14:52

Uislamu na Mtindo wa Maisha (47)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (47)

Ni wasaa mwingine wa kuwa nami tena katika sehemu nyingine ya makala ya Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kipindi chetu cha leo kitazungumzia jinsi wazazi wanavyopaswa kuamiliana na watoto wao.

>>> <

Tunafungua kipindi chetu kwa kauli iliyonukuliwa kutoka kwa mwanafalsafa mashuhuri wa Kigiriki Socrates. Inasemekana kwamba kabla ya kuhukumiwa kifo Socrates aliulizwa: Ni ni ipi ndoto na matarajio yako makubwa zaidi duniani? Alisema: Matarajio yangu makubwa zaidi ni kwenda katika eneo lililoko juu zaidi la Athens na kuwaambia watu kwamba: Marafiki zangu! Kwa nini mnamaliza kipindi bora zaidi cha umri wenu katika kukusanya mali kwa pupa na usongo mkubwa, wakati hamufanyi jitihada zinazostahili kwa ajili ya kuwapa elimu na malezi watoto wenu ambao ndio watakaorithi hizo mali munazokusanya?
Wasomi, maulamaa na wataalamu wa masuala ya malezi wanasema kuwa kipindi bora zaidi cha kufunza na kumpa malezi bora mtoto ni kile cha miaka ya mwanzoni mwa maisha yake. Shakhsia ya mtoto inaweza kuchanua na kukwea ngazi za ukamilifu wa kibinadamu pale anapotayarishiwa mazingira mazuri na yanayofaa. Hapana shaka kuwa kila mtoto ana jumla ya vipawa vilivyofichikana ndani ya nafsi yake na uzoefu wa miaka ya mwanzoni mwa uhai wake unaweza kusaidia katika kukua, kuchanua na kukamilika vipawa hivyo.
Mjadala wa malezi ya watoto umekuwa ukishughulisha fikra za wanadamu kwa karne nyingi. Mwenyezi Mungu Mtukufu pia amezungumzia sana suala la malezi ya mwanadamu katika Qur'ani na kueleza njia na mbinu mbora za malezi hayo. Malezi ya watoto, wafuatiliaji wa kipindi hiki, ndiyo wadhifa mkubwa zaidi wa baba na mama, kisha walimu na watu wengine. Hapana shaka kuwa ujenzi na ustawi wowote katika jamii unaanzia katika malezi ya watoto. Kwani iwapo watoto watapewa malezi mabaya na kuwa waovu, tabia na mwenendo wao mbaya utakuwa na taathira mbaya katika jamii nzima. Uzoefu unaonesha kuwa mienendo mibaya ya wanadamu inatokana ama na malezi yasiyo sahihi au mghafala na uzembe wa wazazi yaani baba na mama. Familia ambayo ndiyo nguzo muhimu ya malezi katika jamii, ina nafasi muhimu sana katika malezi ya watoto. Na kwa kuwa kituo cha kwanza cha malezi na elimu ya mtoto ni familia, mtoto huanza kujifunga elimu na mbinu za mawasiliano na watu wengine katika miaka ya awali ya maisha yake kutoka kwa wazazi wake. Ni kwa msingi huu ndiyo maana inasemwa kuwa, familia huwa na mchango mkubwa katika ustawi wa kimaadili wa mtoto.
Mwenyezi Mungu SW anasema katika sehemu ya aya ya 6 ya Suratu Tahrim kwamba: "Enyi mlioamini! Zilindeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe." Katika aya hii Mwenyezi Mungu SW anawataka baba na mama kuchunga nafsi zao na za ahli na watoto wao. Amri hii inahusiana na malezi na inawahusu wanachama wote wa familia.
Hapa linajitokeza swali kwamba kimsingi malezi ni nini?
Wataalamu wa elimu ya mienendo ya wanadamu wanasema, malezi yana maana ya kutayarisha mazingira ya kuchanua vipawa na uwezo wa nafsi ya mwanadamu. Mama na baba ambao ndio walezi wa kwanza wa mtoto, wanapaswa kuweka ratiba na mipango mizuri ya malezi ya mtoto kwa mujibu wa matakwa ya kimaumbile ya mtoto wao.
Suala jingine muhimu katika malezi ya watoto ni kujua wakati na vipindi mwafaka vya malezi ya mtoto. Wataalamu wa elimu nafsi wanashauri kuwa, si sahihi kufanya haraka katika malezi ya watoto au kuzembea na kudorora. Hii ni kwa sababu matatizo mengi ya kimalezi husababishwa na maamuzi ya haraka au kuzembea na kudorora katika malezi ya watoto. Vipawa vya mwanadamu ni sawa na kito cha lulu ilichojificha kwenye gamba la chaza. Hivyo basi, iwapo gamba la kito hicho itavunjwa kabla ya chaza hajakomaa, kito kitakuwa na mapungufu mengi. Malezi ya watoto wadogo pia yana mfumo wake wa kimaumbile na hapana budi kufuata mkondo na taratibu za maumbile hayo. Haipaswi kuharakisha malezi ya watoto au kuchelewesha na kupuuza mwenendo na mchakato huo, na jitihada zote za kupita njia ya mkato zitakuwa na taathira mbaya katika malezi ya mtoto huyo.

>>>

Huwenda kutenga wakati kwa ajili ya malezi ya watoto likawa suala gumu sana kwa wazazi katika kipindi cha sasa chenye shughuli na mihangaiko mingi ya kimaisha. Hata hivyo jambo lenye umuhimu mkubwa katika malezi ya watoto ni aina ya wakati wenyewe na si kiasi chake. Wazazi wanaweza kutumia vizuri fursa mbalimbali hata zile za dakika moja na dakika mbili kwa ajili ya kuzungumza na watoto wao, kujibu maswali yao, kuwaliwaza, kucheza nao, kuwafundisha kuchora na kadhalika. Wazazi pia wanaweza kuzungumza na watoto wao walau kwa simu wanapokuwa kazini na kuweka utaratibu maalumu kama wa kucheza na watoto kila siku katika kupanda baisikeli, kwenda kwenye bustani ya umma iliyo karibu na nyumbani, sinema na mambo mengine yanayomvutia na kumfurahisha mtoto. Hata hivyo inabidi tuelewe kuwa mahitaji, matakwa na burudani zinazopendwa na watoto hutofautiana kutoka mtoto mmoja hadi mwingine. Kwa mfano mahitaji na burudani za mtoto mwenye umri wa miaka 5 hutofautiana na zile za barobaro mwenye umri wa miaka 17, au burudani na mahitaji ya mtoto wa kike zinatofautiana sana na zile za mtoto wa kiume. Kwa msingi huo wazazi wanapaswa kutenga wakati wao kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kila mmoja wao.
Tangu miaka ya mwanzoni mwa uhai wao, watoto huvutiwa na kila jambo. Huchekeshwa na jambo dogo na kuathiriwa na vitu vingi vya kawaida. Watoto hupenda kudadisi na kujua kila kitu na huathiriwa sana na hisia na fikra za wazazi wao. Kwa msingi huo mitazamo hasi au chanya ya wazazi, ndugu na jamaa wa karibu kuhusu watoto hao hubakia muda mrefu katika fikra zao. Hivyo kadiri mitazamo ya wazazi kuhusu watoto wao inavyokuwa chanya, ndivyo kadiri inavyotayarisha uwanja nzuri wa kudhihiri na kustawi vipawa vya watoto wetu.
Malezi na ustawi sahihi wa watoto wetu unategemea mawasiliano sahihi na wazazi wao. Kutambua vyema misingi ya elimu nafsi ya kuwasiliana na watoto kunaweza kutusaidia katika kulea watoto salama na wema. Miongoni mwa mambo yanayoweza kuwasaidia wazazi kuwa na taathira katika nafsi za watoto wao ni kuwa na mtazamo chanya kuhusu watoto hao. Kwa maana kwamba, mzazi anapaswa kumuona mtoto kama hadiya na amana ya Mwenyezi Mungu na kumtambua kuwa ni kiumbe mwenye vipawa vingi vinavyohitaji kustawishwa. Mtazamo kama huu unamwezesha mtoto kutambua uwezo wake mwenyewe na kudhihirisha hisia zake. Familia inapaswa kuwa kituo cha upendo, heshima na mazingatio ili mtoto apate kigezo na ruwaza njema kutokana na upendo na mahaba ya wazazi wake.
Miongoni mwa njia kuu za kuzuia uhalifu na jinai ni kumjenga mwanadamu kiroho na kijamii na kulea shakhsia yake kwa mafundisho ya kiroho na kidini. Malezi kama hayo huanzia ndani ya familia; hivyo wazazi wawili wanaweza kuwa nafasi kubwa katika kuzuia uhalifu katika jamii kwa kumhamasisha mtoto na kumuelimisha sifa nzuri na za kibinadamu za kijamii na kuimarisha vipawa vyake, kumtayarishia mazingira ya kuwa na uwezo wa kujiamini na kuwajibika. Vilevile mitazamo na mienendo ya wazazi wawili inaweza kuwa kihamasishi au kizuizi cha ustawi na ukamilifu wake. Wazazi wakali kupita kiasi huwazuia watoto wao kuwa na mahusiano salama na watoto wa rika lao, suala ambalo huwa na taathira mbaya katika kujitegemea na kujiamini watoto hao. Wakati huo huo wazazi wawili wenye misimamo ya wastani huwa kimbilio la amani kwa watoto na vijana. Wazazi kama hawa si tu kwamba huwasaidia watoto wao kutatua matatizo yao mengi, bali pia huwahamasisha watoto wao kuwa na hisi ya kujitegemea, kujiamini na kuwajibika.

>>>>>

Wafuatiliaji wa makala hii tukutane tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi cha Uislamu na Mtindo wa Maisha.

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)