Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 08 Disemba 2014 15:11

Uislamu na Mtindo wa Maisha (46)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (46)

Hamjambo wafuatiliaji wa makala hii ya Uislamu na Mtindo wa Maisha. Wiki hii kipindi chetu kitazungumzia umuhimu wa kuheshimu ahadi na mapatano katika uhusiano wa kifamilia.

>>

Kutekeleza ahadi kuna maana ya kutimiza ahadi na makubaliano, na vilevile kuwa mwaminifu na kudumu katika urafiki.
Miongoni mwa matarajio ya mke kwa mume wake au mume kwa mke wake ni mwenzake kutekeleza na kutimiza ahadi zake zikiwemo zile zilizotolewa kabla ya kuoana. Mtume wa Uislamu Muhammad SAW anawahimiza sana Waislamu kutimiza ahadi zao na kusema: Mtu yeyote anayemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya Kiyama anapasa kutimiza ahadi zake. (Biharul Anwar 77-149) maneno haya ya Mtume wetu Muhammad SAW yanaonesha umuhimu mkubwa wa kutekeleza na kutimiza ahadi katika Uislamu, kiasi kwamba kumetajwa kuwa ni miongoni mwa alama za kuwa na imani na Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama.
Suala la kutimiza ahadi na makubaliano pia linaonekana sana katika sira na maisha ya viongozi wetu wa dini. Imenukuliwa kwamba Imam Ali bin Abi Twalib AS na bi Fatimatu-Zahra SA walikwenda kwa Mtume SAW baada ya kufunga ndoa kwa ajili ya kugawana majukumu. Mtume Mtukufu alisema: Kazi za ndani ya nyumba azifanye Fatima na zile za nje ya nyumba zifanywe na Ali. Kuanzia hapo, bi Fatimatu Zahra SA akawa akifanya kazi za nyumbani na mumewe Ali akabeba jukumu la kushughulikia kazi za nje ya nyumba na tangu wakati huo watukufu hawa wawili walishikamana na ahasdi na makubaliano hayo katika kipindi chote cha maisha yao.
Quran Tukufu inakutaja kutimiza ahadi na mapatano kuwa ni miongoni mwa sifa za watendao mema na aya nyingi za kitabu hicho zimewataka waumini kutekeleza na kutimiza ahadi na makubaliano yao. Mwenyezi Mungu SWT anawataka Waislamu katika aya nyingi za Quran Tukufu watimize ahadi na makubaliano baina yao na ndugu zao katika imani. Aya ya kwanza ya Suratul Maida inaeleza suala la kutimiza ahadi na mapatano kwa kusema: "Enyi mlioamini tekelezeni mapatano." Kuheshimu mapatano na ulazima wa kuyatekeleza kuna asili ya kifitra katika nafsi ya wanadamu. Kwa kadiri kwamba tunashuhudia hata watoto wadogo wenye fitra na maumbile safi wakitambua ulazima wa kutimizwa ahadi; na wanakemea na kuchukizwa na kutotimizwa ahadi na mapatano. Daima tunawaona watoto wakikasirishwa na hatua ya baadhi ya wazazi ya kutotekeleza ahadi zao kwao. Kwa msingi huo kukiuka ahadi na mapatano ni miongoni mwa maovu ya kiakhlaqi katika jamii na vilevile katika mazingira ya familia.
Tunaweza kusema kuwa mtaji muhimu zaidi wa waanandoa wawili ni ile hali ya kuaminiana iliyopo baina ya wawili hao. Vilevile kutimiza ahadi kwa wanachama wa familia kuna umuhimu kiasi kwamba iwapo baba na mama hawatatimiza ahadi na mapatano yao; suala hilo huwa na taathira mbaya za kinafsi kwa watoto na huwenda likawatumbukiza watoto hao katika tabia ya kusema urongo. Viongozi wa Kiislamu wamezungumzia sana umuhimu wa kutoa malezi sahihi kwa watoto na mafunzo ya kiakhlalaqi na mienendo mizuri ya kijamii. Mtume Mtukufu SAW amesema: Kila mtu anayetoa ahadi kwa mtoto mdogo, anawajibika kutimiza ahadi yake."
Kutekeleza na kuheshimu ahadi kuna taathira kubwa katika kuyafanya mazingira kuwa salama na kuimarisha uhusiano wa kifamilia na pia kuleta anga ya kuaminiana kati ya wanachama wa familia, hususan wanandoa wawili. Utimizaji wa ahadi na makubaliano katika familia unapokuwa mkubwa, wanandoa wawili na vilevile watoto huzidi kuamianiana na hatimaye huhisi amani na utulivu zaidi na hivyo kutekeleza majukumu yao kwa wepesi zaidi. Pale utimizaji wa ahadi katika familia unapokuwa wa kiwango cha chini, basi jambo hilo pia litakuwa na taathira hasi katika malezi ya watoto.
Wazazi hawalazimiki kutoa ahadi, lakini pale wanapotoa ahadi kwa watoto wao, wanapasa kuzitekeleza. Mtoto anayewatambua wazazi wake, hususan baba, kuwa si mtimizaji wa ahadi, humuona mzazi wake huyo kuwa muongo na taratibu hujitenga na hujiweka mbali naye. Kwa utaratibu huo, mtoto hupoteza imani na wazazi wake na imani yake kuhusu misingi ya matukufu ya kibinaamu na Kiislamu pia huanza kudhoofika. Watoto huwaona wazazi wao kuwa ndio tegemeo lao katika maisha na pale wanapoawaona wakivunja ahadi na mapatano yao hupatwa na hisi ya kukosa makimbilio na tegemo lao. Kwa maneno mengine ni kuwa pale mtoto amapoona maneno na vitendo vya wazazi wake kuwa ni vya kindamakuwili, huhisi kutokuwa na kimbilio na huchanganyikiwa. Kuna hadithi nyingi za viongozi wetu wa kidini kuhusu suala hilo na imepokewa kwamba Mtume SAW amesema: Wapendeni watoto wenu na amilianeni nao kwa upendo na huruma na iwapo mtawaahidi, basi timizeni ahadi zenu."

>>>

Kuna masuala mengi yanayohitajika ili kuweza kuwa na familia yenye mlingano na mafanikio, na baadhi ya mambo hayo tumeyazungumzia katika vipindi kadhaa vilivyopita na kuashiria vigezo muhimu zaidi katika uhusiano wa mume na mke. Vilevile tulizungumzia baadhi ya misingi ya kimaadili yenye taathira katika kuimarisha taasisi ya familia. Katika kuhitimisha mjadala huu tunapasa kusema kuwa, wanandoa katika familia zenye mafanikio ni wale wanaokidhiana mahitaji ya kawaida. Wanandoa hao hufahamiana kwa undani, kuthaminiana, kufarijiana na kuoneshana upendo na mahaba wakati wote. Mke na mume wa aina hii, huandaa mazingira ya ustawi na maendeleo ya kila mmoja wao na mbali na mahaba na mapenzi waliyonayo kwa kila mmoja wao, hufanya juhudi za kulinda taasisi ya familia. Iwapo katika uhusiano wa wanandoa kutakosekana kitu kimoja au masuala hayo yote tuliyotaja, basi kuanza kushuhudiwa ishara za kutoridhika kama vile mwanadoa mmoja kumkosoa mwenzake, kutokuwa na uvumilivu, kupuuziana, kukwaruzana, kupatwa na msongo wa mawazo, kusalitiana katika ndoa, kujiingiza katika mihadarati na mwishowe kutalikiana.
Wapenzi wafuatiliaji wa makala hii, kabla ya kuhitimisha kipindi hiki tunawanukulia matamsmhi ya Dakta Ghulamali Afruz mtaalamu wa elimu nafsi wa Kiirani ambaye ameashiria masuala muhimu zaidi kati ya wanandoa kwa ajili ya kuwa na uhusiano mzuri. Anasema: Wanandoa wenye mafanikio ni wale wanaolinda taasisi yao ya familia na aina zote za madhara yanayotokana na maneno na mienendo isiyofaa na kujitahidi kadiri ya uwezo kufarijiana, kuridhishana kiroho na kimwili na kuepusha uhusiano wao na hali ya kunyauka na kunyong'onyea. Wanandoa wenye mafanikio ni wale wanaohisi amani na utulivu wanapokuwa pamoja na kadiri muda wa ndoa yao unavyosonga mbele ndivyo uhusiano wao unavyoimarika zaidi, kuwa wa kirafiki zaidi na wenye vuguvugu na nishati kubwa zaidi.

>>

Tukutane tena wiki ijayo panapo majaaliwa ya Mola Karima.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)