Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 01 Disemba 2014 15:02

Uislamu na Mtindo wa Maisha (45)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (45)

Hamjambo wafuatiliaji wa makala hii na karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya mfululizo wa kipindi hiki cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Kipindi chetu cha leo kitazungumzia udharura wa kuwa mkweli katika mahusiano ya mke na mume kwa mujibu wa mtindo wa maisha wa Kiislamu.

>

Ukweli ni miongoni mwa sifa anazopaswa kuwa nazo mwanadamu katika kipindi chote cha maisha yake. Ukweli umearifishwa kwa maneno mafupi kwa maana ya kudhihirisha kila kitu kilichoko katika ujudi na uwepo wetu. Ukweli hauna maana ya kusema ukweli katika maneno tu bali pia kuoana na kufanana maneno na matendo yetu ni miongoni mwa alama za kuwa mkweli. Katika mtazamo wa elimu nafsi ukweli una maana ya maneno na mwenendo ambavyo nia na malengo ya msemaji na mtendaji wake havitofautiani na maneno au matendo yeke. Wakati mwanadamu anapokosa kuwa mkweli katika mahusiano yake ya kimaneno au kimatendo, upande wa pili hupatwa na madhara na mahusiano ya wawili hao hutetereka na kuyumba. Kutokuwa mkweli kwa mke au mume huelekeza uhusiano wa wawili hao katika upande wa kutoaminiana na kudhaniana vibaya na kutayarisha mazingira ya kuzuka hitilafu baina yao. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana mafundisho ya Uislamu yanasisitiza sana juu ya udharura wa kuwa mkweli na kujiepusha na unafiki na kuwa na sura mbili.
Aya za Qur'ani Tukufu zimewahimiza sana wanadamu kuwa wakweli na kuwaahidi pepo wakweli na wenye kuwa na subira. Ukweli ulipewa umuhimu sana katika historia ya Uislamu kwa kadiri kwamba Bibi Khadija aliamua kuoana na Mtume Muhammad (saw) kutoka na ukweli na uaminifu wake.
Ukweli na uaminifu ni miongoni mwa sababu za kupendwa kwa mtu. Aghlabu ya wanadamu hupenda kuwa pamoja na mtu mkweli na mwaminifu na humwamini na kumtegemea katika kazi na mambo yao ya kimaisha. Sifa hii ya kuwa mkweli ina nafasi muhimu sana katika maisha ya ndoa. Mara nyingi sifa hii hutoweka au kuwa dhaifu sana katika familia zenye migogoro, mivutano ya mara kwa mara na malumbano ya kudumu. Kama tunataka kuelewa umuhimu wa sifa ya kuwa mkweli, hatuna budi kutilia maanani usemi wa Imam wa Waumini Ali bin Abi Twalib ambaye amesema: "Wokovu umo katika kuwa mkweli." Kuamini haswa maneno haya matukufu kunaimarisha zaidi sifa hiyo ya kuwa mwaminifu na mkweli katika ujudi na nafsi zetu. Kwani mtu yeyote anayeamini maneno hayo hutafuta njia ya wokovu na kujiondoa katika mashaka na hali ngumu kwa kuwa mkweli kwa nafsi yake na wenzake katika maneno na matendo yake na wala hatakuwa na hofu ya kusema au kutenda jema na lililo kweli.
Kutoweka ukweli katika uhusiano wa mke na mume hudhoofisha hali ya kuaminiana baina ya wawili hao. Ukweli na uaminifu unapaswa kutawala maisha ya wanadamu wote na kuonekana katika maneno na matendo yao hususan mke na mume ambao ndio nguzo ya kwanza ya familia na jamii. Familia zinapaswa kuwafunza watoto ukweli na uaminifu kama msingi wa maisha yao ya baadaye na hapana shaka kuwa mbinu bora zaidi ya kueneza tabia hii ya ukweli na uaminifu ni kwa baba na mama kuwa wakweli katika maneno na matendo yao.
Uchunguzi uliofanywa umeonesha kuwa sababu kuu ya watu kutokuwa wakweli na kusema urongo katika familia ni woga na hofu. Mke husema uongo kutokana na kumuogopa mumewe, hivyo hivyo mume husema uongo kwa kumuogopa mke wake, na watoto wanasema uongo kwa kuwaogopa wazazi wao. Kwa msingi huo mwenendo wetu sisi wenyewe ndio unaowafunza kusema urongo watu walioko karibu au kando yetu. Hebu tuweke wazi zaidi maneno haya kwa kutoa mfano.
Wakati tunapomuuliza mtoto: Nani aleyeharibu mwanasesere huyu, na mtoto akasema kuwa yeye ndiye aliyemharibu, jibu letu kwa msimamo huo wa mtoto huwa la aina mbili. Ama tunamuadhibu na kumtia adabu, au tunaeleza kusikitishwa na kitendo hicho cha mtoto kwa kumwambia kuwa tumekasirishwa na kitendo chake. Kwa msingi huo mtoto hujifunza kwamba, kusema ukweli ama huwa na madhara kwake kwa sababu ya kupigwa na kutiwa adabu au huwa na madhara kwa wazazi wake ambao hukasirika na kuumizwa na ukweli huo. Hali huwa hivyohivyo pia baina ya mke na mume, kwani pale mume au mke anaposema uongo kwa mkewe ni kwa sababu ama hataki kumuudhi au hataki kuwa mashakani yeye mwenyewe. Kwa msingi huo tunapasa kuondoa au kwa uchache kupunguza hali ya hofu na woga ndani ya familia na tusiwe na mwenendo ambao utawalazimisha wake, waume au watoto wetu kusema uongo. Sambamba na hayo mwanadamu mwenyewe pia anapaswa kuelewa kwamba, kusema urongo ni jambo baya ambalo haliwezi kumuokoa, kwani hatimaye urongo wake utafichuka na kupunguza uaminifu wake mbele ya watu.
Mazingira ya familia yanapaswa kutawaliwa na anga inayowafanya wanachama wa familia husika wajihisi kuwa, wokovu wao umo katika kuwa wakweli katika maneno na matendo yao.
Hata hivyo tunapaswa pia kuelewa kuwa, pale tunapong'amua urongo wa mmoja kati ya wanafamilia, haijuzu kuweka wazi suala hilo na kumtuhumu kuwa amesema uongo. Hatupaswi kung'ang'ania kuwa mke au mume au mtoto amesema uongo kuhusu suala au kadhia fulani ili msimamo huo usije ukamfungia mtuhumiwa katika kisima cha kusema urongo daima. Kinyume chake, tunapaswa kusitiri kosa lake.
Nukta muhimu ya kuzingatiwa ni kuwa ni haramu kusema urongo lakini pia tunapaswa kusema kuwa, si kila ukweli unapaswa kusemwa. Hii ni kwa sababu, kuna ukweli mwingi ambao iwapo utasemwa utasababisha anga isiyokuwa nzuri na hata uhasama baina ya watu. Kuhusu suala hili Imam Ali bin Abi Twalib (as) ametufunza vigezo kadhaa vinavyoweza kutusaidia katika mazingira kama haya. Anasema akieleza sifa za wachamungu kwamba: "Daima mantiki na maneno yao husibu haki". Maneno ya kweli yana sifa mbili kuu: Kwanza ni kwamba ni ya haki, na pili ni kuwa yanasemwa wakati mwafaka. Kwa msingi huo iwapo maneno yatakuwa ya kweli na haki lakini yakasemwa mahala pasipo na wakati usio mwafaka, basi hayatakuwa yamesibu na yumkini yakazusha uhasama, hitilafu na dhana mbaya na ukosefu wa maelewano.
Hata hivyo inapasa kuelewa kwamba, wakati mwingine ni makosa kuficha baadhi ya mambo au kutoonesha hisia kuhusu mambo hayo. Imetokea mara kwa mara kwamba tumekasirishwa na kujisikia vibaya kutokana na jambo fulani, lakini pale tunapoulizwa na wake, waume au jamaa zetu huwajibu kwa kusema: Hapana baya lolote. Jibu sahihi wakati kama huu ni kusema kwamba: Kwa sasa siwezi kuzungumza lolote kuhusu kadhia hii. Kutoonesha hisia zako kunaweza kuwa na madhara kwa mke au mume na wakati huo huo kusababisha matatizo ya kimwili na kinafsi.

>>>

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)