Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 24 Novemba 2014 17:06

Uislamu na Mtindo wa Maisha (44)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (44)

Assalamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki cha Uislamu na Mtindo wa Maisha. Karibuni katika sehemu nyingine ya mfululizo wa kipindi hiki kinachowajia mara moja kwa wiki. Kipindi chetu cha leo kinaendelea kuzungumzia sifa za familia yenye mlingano katika mtindo wa maisha wa Kiislamu.

>

Kama bado mnakumbuka katika kipindi cha wiki iliyopita tulizungumzia umuhimu wa kutunza siri za watu hususan wanafamilia hasa baina ya mke na mume. Tulisema moja ya majina matukufu ya Mwenyezi Mungu ni Sattarul Uyub kwa maana ya Mwenye kusitiri sana nakisi na aibu za waja wake na kwamba ni muhimu sana kwetu sisi kujipamba kwa sifa njema za Mola Muumba. Vilevile tulinukuu hadithi za Mtume (saw) na maimamu watoharifu katika kizazi chake ikiwemo ile ya Mtume inayosema: "Mtu anayesitiri aibu ya muumini huwa bora kuliko yule anayeokoa mtoto wa kike aliyezikwa akiwa hai." Mtume (saw) alikuwa akiashiria ada mbaya iliyokuwapo katika zama za ujahilia na kabla ya kudhihiri Uislamu ya kuwatambua watoto wa kike kuwa ni aibu na kuwazika wakiwa hai ili kuficha aibu hiyo. Uislamu ulikemea vikali na kupiga marufuku kitendo hicho kiovu na kumpa hadhi na heshima kubwa mwanamke. Imam Ali bin Abi Twalib (as) pia anasema: "Miongoni mwa maovu makubwa na aibu mbaya kuliko zote ni kufuatilia na kuanika aibu za watu wengine."
Kwa kutilia maanani hayo yote tulisema kuwa kufichua aibu za mwenzi wako katika ndoa huwaweka wanandoa hao mbali na jicho la rehma ya Mwenyezi Mungu na kushusha hadhi na heshima yao. Kitendo hicho huwafanya watu wawaone duni na hakiri. Vilevile kitendo hicho cha kufichua siri za mke au mume wako huvunja mipaka ya heshima ya familia na kuwapa watu wengine ruhusa ya kuingilia masuala ya ndani na maisha ya kibinafsi ya watu wa familia husika.
Katika upande mwingine hitilafu nyingi zinazotokea kati ya mke na mume hutulia na kutoweka haraka lakini taswira mbaya iliyoundika katika fikra za watu kuhusu mke au mume ambaye siri na aibu zake zimeanikwa hadharani na mwenzi wake, hubakia muda mrefu na huwa vigumu kutoweka kirahisi. Watu wote hupenda kujifakharisha kwa mafanikio ya wake au waume zao na kuona mke au mume huyo anaheshimika mbele ya wenzake. Kinyume chake, kutolinda siri na kuficha aibu za mwenzi wako katika ndoa hupunguza heshima yake na kuwafanya watu wengine wamwangalie kwa jicho la dharau, shaka na wasiwasi. Mbali na hayo pale mke au mume anapoelewa kwamba mwenzake katika ndoa amefichua siri na aibu zake, suala hilo huibua matatizo mengine ndani ya familia, na kutokana na kuhisi kwamba heshima yake imetoweka mbele ya familia na marafiki, yumkini akajitenga nao na kuwa na maingiano machache sana na watu.
Suala jingine la kuashiria hapa kuhusu athari mbaya za kufichua siri za wanandoa ni kuwa heshima na hadhi ya wanandoa wawili imefungamana na kushikamana. Ushahidi wa suala hilo ni kuwa wakati mke au mume anaposifiwa na kupongezwa, mwenzi wake pia huhisi fakhari na heshima. Hivyo basi hapana shaka kuwa pale mke au mume anapofanya jitihada za kumdhoofisha mwenzi wake kwa ajili ya kulipiza kisasi, kudhihirisha nafsi yake au sababu nyingine, kwa hakika huwa ameidunisha nafsi yake mwenyewe na kuporomosha chini heshima yake.

>>>>>

Mke na mume wanaoishi pamoja hujua siri na nakisi za kila mmoja wao kuliko watu wengine. Kwa msingi huo haki ya usuhuba na kuishi pamoja inawalazimu wawili hao kuwa waaminifu kwa kila mmoja na kusitiri aibu zake. Hata hivyo kuna baadhi ya watu ambao si wastahamilivu na huanika na kusema aibu na nakisi za mwenzi wake katika ndoa mara tu wanapoona nakisi hizo. Kuna wengine wanaoweza kustahamili suala hilo na kuliweka vifuani lakini hujikuta wakianika siri na aibu hizo pale wanapokabiliwa na matatizo ya kifamilia kwa ajili ya kuonekana ni wenye haki au kwa ajili ya kupata huruma ya watu wengine. Wakati mwingine pia kutokubali kukosolewa humfanya mmoja kati ya wanandoa hao kufichua na kuanika hadharani siri za mwenzake.
Ni vyema tutambue kuwa kumkosoa mwanandoa mwenzako iwapo kutafanyika kwa njia sahihi na kwa lengo la kurekebisha nakisi na dosari zilizopo huondoa kiwingu cheusi katika uhusiano wa kifamilia.
Dakta Muhamamd Ridha Sharafi ambaye ni mtaalamu wa elimu nafsi nchini Iran anasema kuhusu umuhimu wa kutunza siri ndani ya familia kwamba:
Wakati mwingine watu wanaosumbuliwa na udhaifu katika shakhsia na nafsi zao hulazimishwa na hali hiyo ya uhakiri na uduni wa ndani ya nafsi zao kuharibu shakhsia na heshima za watu wengine kwa shabaha ya kufidia udhaifu huo. Kwa msingi huo huwa tayari kutoa siri za watu wengine ili kutuliza maumivu yao ya kinafsi. Inasikitisha kwamba suala hili pia wakati mwingine huonekana ndani ya baadhi ya familia, kwani baadhi ya wanaume au wanawake hutumia njia ya kuharibu sifa na shakhsia za wenzi wao katika ndoa na kuanika nje aibu na nakisi zao kwa shabaha ya kudhihirisha nafsi na shakhsia zao au kupunguza na kufifiza dosari na matatizo yao ya kinafsi.
Dakta Sharafi anaendelea kusema: Inasikitisha kuona kwamba, baadhi ya wake au waume huwalazimisha watoto wao kujasisi na kuchunga mienendo ya wake au waume zao. Mwenendo huu hupandikiza mbegu za kutoaminiana ndani ya roho za watoto wao bila ya kujua. Wazazi wa aina hii si tu kwamba huondoa anga ya kuaminiana ndani ya familia, bali pia hulea watoto ambao baadaye huwa na tabia ya kufichua na kuweka wazi siri za maisha ya familia zao.
Pamoja na hayo yote tunapaswa kusema hapa kuwa, kusema na kuanika nje matatizo ya kimaisha na aibu za mke au mume ni kosa na pengine dhambi kubwa, lakini wakati mwingine huwa lazima kuwaeleza watu waaminifu au vyombo vyenye dhamana siri na matatizo yetu ya kifamilia kwa ajili ya kutatua matatizo yetu ya ndani ya ndoa au ya familia. Hata hivyo pale kunapokuwepo udharura wa kueleza matatizo ya kimaisha na aibu za mke au mume, basi tunapaswa kutosheka kwa kutaja mambo ya dharura tu bila ya kuwa na haja ya kueleza kila kitu. Ni wazi kuwa, kusema siri na aibu za mke au mume katika mazingira kama hayo kunaweza kuwa sababu ya kutatuliwa au kutayarisha njia ya utatuzi wa matatizo yaliyopo. Kwa msingi huo tunaona kuwa, kueleza matatizo ya kimaisha kwa watu waaminifu na wenye ujuzi na uzoefu ni miongoni mwa mambo yanayousiwa na Qur'ani Tukufu na hata wataalamu wa masuala ya malezi na familia.

>>>>

Kipindi chetu kinaishia hapa kwa leo nikiwa na matumaini ya kukutana nanyi tena katika kipindi cha wiki ijayo panapo majaaliwa ya Mola Muumba.

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)