Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 19 Novemba 2014 11:58

Uislamu na Mtindo wa Maisha (43)

Uislamu na Mtindo wa Maisha (43)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni kuwa nasi tena katika sehemu nyingine ya makala ya Uislamu na Mtindo wa Maisha. Bado tunazungumzia sifa za familia yenye mlingano katika mtindo wa maisha wa Kiislamu na leo tutatupia jicho sifa ya kutunza na kuchunga siri kwa ujumla hususan ndani ya familia.

>>

Hapana shaka kuwa kuna sababu nyingi zinazochangia katika kuwa na familia yenye mlingano na mafanikio. Miongoni mwa sifa hizo ni ile ya kulinda na kutunza siri. Kuna udharura kwa mke na mume kulinda siri za kila mmoja wao kwa ajili ya kujenga maelewano na hali ya kuaminiana ndani ya familia kwani kutoa na kuvujisha siri za mwenzi wako katika maisha ya ndoa kuna madhara na athari nyingi mbaya.
Siri, wapenzi wasikilizaji, ni kila jambo ambalo linapaswa kuwekwa na kubakia moyoni na kama kuna udharura, lisemwe kwa watu makhsusi na waaminifu. Mwanadamu anapaswa kujifunza kwa Mwenyezi Mungu jinsi ya kutunza siri za wanadamu wenzake. Sisi sote tunajua kwamba, Mwenyezi Mungu SW anajua vyema amali, matendo, hali, mienendo, aibu, nakisi na madhambi ya waja wake kuliko mtu yeyote, lakini huruma, rehma, uvumilivu wake mkubwa na kutunza kwake siri za waja ni kukubwa zaidi. Kwa sababu hiyo moja ya majina matukufu ya Mwenyezi Mungu ni "Sattarul Uyub" kwa maana ya mwenye kusitiri sana aibu na nakisi za waja.
Hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (saw) na Ahlibaiti zake watoharifu pia zinasisitiza sana juu ya udharura wa kulindwa heshima na siri za waumini. Kila mwanadamu katika maisha yake ya kibinafsi na kijamii ana siri zake ambazo zinapaswa kutunzwa na kulindwa. Baadhi ya siri hizo zinahusiana na mwanadamu mwenyewe na nyingine zinahusu familia au jamii yake. Hii leo kutokana na maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano na utumiaji wake mkubwa katika maisha ya kila siku, kunaonekana udharura mkubwa zaidi wa kutunza siri za watu ambako mbali na kuwa ni sifa nzuri ya kimaadili, huwa na taathira pia katika ufanisi wa mwanadamu. Amirul Muumunin Ali bin Abi Twalib (as) amesema: "Mafanikio hupatikana kwa kuwa na azma kubwa, na azma inapatikana kwa kutafakari vyema, na kutafakari hupatikana kwa kutunza siri." Vilevile anasema katika kauli nyingine kwamba: "Siri yako ni mateka wako, ukiifichua utakuwa mateka wake."
Wakati huo huo kufichua siri huwa sababu ya kukosa mafanikio, kufeli na pengine kuanguka na kuporomoka. Mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) Imam Jaafar Swadiq (as) anasema: "Kuanika siri huwa sababu ya kufeli na kunguka."

>>>

Kama tulivyosema, kila mtu, familia na jamii ina siri zake ambazo watu wengine hawapasi kuzijua na kufichuliwa kwake kunaweza kusababisha madhara kwa mtu binafsi, familia au jamii. Wataalamu wa elimu nafsi wanasema kwamba, kutunza siri za watu ni dalili ya mtu mwenye uzima na siha ya kinafsi anayeweza kudhibiti mwenendo na maneno yake. Katika mtazamo wa kidini pia mtu anayetunza siri za wanadamu wenzake amesanifiwa kati ya watu wenye imani. Hadithi za viongozi wa dini zinasisitiza sana udharura wa kutunza siri na heshima za watu. Mtume Muhammad (saw) anasema: Mtu anayejua mabaya ya ndugu yake akayasitiri, Mwenyezi Mungu atasitiri siri zake Siku ya Kiyama." Vilevile anasema katika hadithi nyingine kwamba: Mtu anayesitiri aibu ya muumini huwa bora kuliko yule anayeokoa mtoto wa kike aliyezikwa akiwa hai." Wasii wake Imam Ali bin Abi Twalib (as) pia anasema: "Miongoni mwa maovu makubwa na aibu mbaya kuliko zote ni kufuatilia na kuanika aibu za watu wengine." Imam Baqir (as) amesema: "Muumini anawajibika kuficha madhambi makubwa sabini ya muumini mwenzake." (Usulul Kafi:2-207, hadithi ya 8)
Uzoefu umeonesha kuwa kutunza siri za watu huwa sababu ya mtu huyo kuaminiwa na watu wengine na vilevile huwa sababu ya kuimarisha uhusiano ndani ya familia. Hapana shaka kuwa, kutunza siri za mke na mume kunaweza kuwa na taathira kubwa kwa wawili hao na watoto wao. Mafundisho ya dini ya Uislamu yanawahimiza mke na mume kulinda heshima za kila mmoja na kukumbusha kuwa matatizo yanayotokea baina ya wanandoa wawili hayapasi kusemwa kwa watu wa nje ya familia.
Wataalamu wa masuala ya familia wanaamini kuwa, kwa kawaida mke na mume ambao hawana uhusiano mzuri wa kiroho na kimapenzi huwa hawazungumzii na kujadili kwa pamoja mahitaji na matatizo yao, na mahusiano ya maneno baina yao huwa nadra sana. Natija na matokeo yake masuala ya kifamilia ya wawili hawa hupelekwa na kuvujishwa nje. Japokuwa suala hili si la kimantiki, lakini wakati mwingine mke au mume hujiona hana njia nyingine isipokuwa kufichua siri zake kwa watu wengine ili huwenda akapunguza mashinikizo ya kinafsi yanayomsumbua. Hata hivyo wanandoa hawa wawili husahau kwamba, jambo hili lina madhara makubwa ambayo hapa tutaashiria baadhi yao.
Kufichua aibu za mwenzi wako katika ndoa huwaweka wanandoa hao mbali na jicho la rehma ya Mwenyezi Mungu na kushusha hadhi na heshima yao. Kitendo hicho huwafanya watu wawaone duni na hakiri. Vilevile kitendo hicho cha kufichua siri za mke au mume wako huvunja mipaka ya heshima ya familia na kuwapa wengine ruhusa ya kuingilia masuala ya ndani na maisha ya kibinafsi ya watu wa familia husika. Katika upande mwingine hitilafu nyingi zinazotokea kati ya mke na mume hutulia na kutoweka haraka lakini taswira mbaya iliyoundika katika fikra za watu kuhusu mke au mume ambaye siri na aibu zake zimeanikwa hadharani na mwenzi wake, hubakia muda mrefu na huwa vigumu kutoweka kirahisi. Watu wote hupenda kujifakharisha kwa mafanikio ya wake au waume zao na kuona mke au mume huyo anaheshimika mbele ya wenzake. Kinyume chake, kutolinda siri na kuficha aibu za mwenzi wako katika ndoa hupunguza heshima yake na kuwafanya watu wengine wamwangalie kwa jicho la dharau, shaka na wasiwasi. Mbali na hayo pale mke au mume anapoelewa kwamba mwenzake katika ndoa amefichua siri na aibu zake, suala hilo huibua matatizo mengine ndani ya familia, na kutokana na kuhisi kwamba heshima yake imetoweka mbele ya familia na marafiki, yumkini akajitenga nao na kuwa na maingiano machache sana na watu.

(((((())))))

Suala jingine la kuashiria hapa kuhusu athari mbaya za kufichua siri za wanandoa ni kuwa heshima na hadhi ya wanandoa wawili imefungamana na kushikamana. Ushahidi ni suala hilo ni kuwa wakati mke au mume anaposifiwa na kupongezwa, mwenzi wake pia huhisi fakhari na heshima. Hivyo basi hapana shaka kuwa pale mke au mume anapofanya jitihada za kumdhoofisha mwenzi wake kwa ajili ya kulipiza kisasi, kudhihirisha nafsi yake au sababu nyingine, kwa hakika huwa ameidunisha nafsi yake mwenyewe na kuporomosha chini heshima yake.

>>

Wafuatiliaji wa kipindi hiki kuweni nasi juma lijalo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki panapo majaliwa ya Mola ili tupate kukamilisha maudhui tuliyoianza leo.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)