Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 12 Mei 2019 13:21

Khadija al-Kubra; johari inayong’ara katika nyumba ya Bwana Mtume SAW

 

 

 


Assalamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kukumbusha siku ya kufunga ndoa Bwana Mtume SAW na Bibi Khadija binti Khuwaylid AS.
Huku nikitoa mkono wa kheri na baraka kwa wanandoa wote na wanaofanya harakati kwa ajili ya kuhakikisha maadili bora yanatawala katika jamii, nataraji  mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibuni.

*********

Bibi Khadija binti Khuwaylid AS alikuwa akiishi akiwa huru kifikra, kivitendo na kujiamini na alikuwa akiendesha gurudumu la maisha yake, biashara na masuala ya kiuchumi kwa kutegemea akili na kipaji chake alichokuwa nacho. Ndoa yake na Bwana Mtume SAW haikufanana wala kushabihiana na ndoa nyingine na ndoa yake haikuwa na mithili. Hii ni kutokana na kuwa, ndoa yao hiyo tukufu ilikuwa imejengeka juu ya msingi wa malengo aali na harakati ya Bibi Khadija ya kutafuta fadhila na ukamilifu na katu haikuwa na msukumo au malengo ya kimaada au mapenzi na ladha za kupita.

Bibi Khadija alizaliwa katika familia ya heshima na iliyokuwa na asili ya Kikureishi. Watu wa familia yake wote walikuwa wakisifika kwa fadhila, kujitolea na kuitetea na kuihami nyumba ya Mwenyezi Mungu al-Kaaba. Bibi Khadija ni binti ya Khuwaylid bin Asad ibn Abd-Al-Uzza. Asad ibn Abd-Al-Uzza ni babu wa Bibi Khadija upande wa baba ambaye alikuwa shakhsia na mtu mahiri katika zama zake. Miaka 23 kabla ya kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad SAW baadhi ya shakhsia wakubwa wa Makka akiwemo Asad ibn Abd-Al-Uzza wakiwa na lengo la kuweka usalama wa Makka na viunga vyake, waliitisha kikao cha mashauriano na kuwekeana mkataba wa kushuhughulikia na kutetea haki za madhulumina na watu wasiojiweza na hivyo kuwaokoa na dhulma na uonevu.

Mtume SAW alijiunga na makubaliano hayo katika miaka hiyo hiyo ya awali ya kuasisiwa kwake, huku akiwa na umri wa miaka 20 tu. Mtume SAW alikuwa akiuheshima mno mkataba huo kiasi kwamba, alisema baada ya kubaathiwa na kupewa Utume kwamba: Endapo hivi sasa pia wataniita katika kuwa mwanachama katika mkataba huo, nitakubali na kuitikia mwito huo.


Amani na rehema za Allah zimwendee mke kipenzi wa Mtume Muhammad, Bibi Khadijatul Kubra SA


Bibi Khadija binti Khuwaylid AS alikulia na kulelewa katikak familia ya heshima na iliyokuwa na mizizi katika Bara Arabu na akachanua katika jamii hiyo. Hata hivyo, hadhi, heshima na utukufu wake haukutokana tu na asili ya familia yake, bali yeye mwenyewe bibi mwema huyo alijipamba kwa sifa njema na kuondokea kuwa mashuhuri kwa mwenendo mwema. Kila mhitaji ambaye alikuwa amekata tamaa ya kupata msaada kwa wengine, alikuwa akikata shauri na kuelekea katika nyumba ya Bibi Khadija na kukimbilia katika ngome hiyo ya huba, huruma na mapenzi ambayo ilikuwa ni dafina na hazina ya ukarimu, na kwa baraka za mapenzi ya ukarimu wa bibi mwema huyo, machungu ya maisha ya wahitaji hao yalikuwa yakipata pozo.

Bi Khadija bint Khuwaylid alikuwa akipenda mno kuwasaidia masikini na wenye shida. Kiasi kwamba, njia ya kuelekea nyumbani kwake daima ilikuwa na msongamano wa wahitaji. Bi Khadija alikuwa akiwasaidia wakati wowote ule wa mchana au usiku na kuwafanya warejee walikotoka wakiwa na tabasamu,  bashasha na matumaini mapya. Si hivyo tu, bali alikuwa akizungumza nao kwa lugha ya upole na huruma na kusikiliza kwa makini shida na matatizo yao. Alikuwa akifuta machozi ya mayatima na akina mama na kisha kuwaita wafanyakazi wake na kuwataka walete mifuko ya pesa na mchele na kugawa baina ya masikini na wenye kuhitaji.


Mwezi 10 Mfunguo Sita ni siku ya kukumbuka wakati Bwana Mtume Muhammad SAW alipofunga ndoa ni bibi Khadijatul Kubra AS


Pamoja na ukarimu, kujiheshimu pamoja na umashuhuri, Bi Khadija alifahamika pia mjini Makka kama mwanamke mzuri na mwenye ujamali wa aina yake. Imam Hassan bin Ali al-Mujtaba AS ambaye alikuwa akipigiwa mfano wa ujamali na uzuri wa kidhahiri baina ya Bani Hashim, alikuwa akihesabiwa kuwa mtu aliyefanana sana na Bibi Khadija.

Bibi Khadija aliheshimiwa sana na watu wa Makka kwa sababu ya tabia yake ya kuigwa na uwezo wake wa kupanga mambo. Kama ambavyo watu wa Makka walikuwa wakimuita Muhammad ‘Sadiqul- Amin’, yaani mkweli mwaminifu, walikuwa wakimuita Bibi Khadija ‘Tahira’, yenye maana ya “Aliye safi.” Alikuwa akijulikana pia miongoni mwa Waarabu kama ‘Malkia wa Wafanyabiashara.

Ujamali na uzuri wa Bibi Khadija na ukarimu ulikuwa hauna mithili kiasi kwamba, jamii ya wakati huo ya Waarabu iliyokuwa imezama na kughiriki katika ufisadi na upotofu ilikuwa ikimuita kuwa ni 'Malkia wa Kiarabu'. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana, viongozi wa makabila mbalimbali ya Kiarabu, mashuujaa wa Kikureishi, shakhsia wakubwa wa Bani Hashim, wafalme wa Yemen na viongozi wa Taifa wote walijitokeza na kumposa Bibi Khadija. Hata hivyo wote hao hawakukubaliwa.


Amani ya Allah iwe juu yako bibi Khadijatul Kubra


Bibi Khadija AS alikuwa mfuasi wa mafundisho ya Nabii Ibrahim AS na alikuwa na ufahamu kuhusiana na Mtume wa Mwisho kupitia vitabu vya dini za kale na kupitia kwa mshauri mwenye hekima na msomi kama Waraqah bin Nawfal. Baada ya ushahidi na sifa mbalimbali kuonyesha kwamba, Mtume wa Mwisho anaweza kuwa ni Muhammad Amin, Bibi Khadija alikuwa na hamu ya kumuona Muhammad. Akiwa na lengo la kumtahini na kumtathmini, alimkabidhi mali zake na kisha kumtuma katika safari ya kibiashara. Aidha katika safari hiyo, alimtuma pamoja na Muhammad mmoja wa mtumishi wake aliyejulikana kwa jina la Maisarah ili atathmini utendaji wake katika safari hiyo.

Bi Khadija alifanya uchunguzi kuhusiana na maisha ya Mtume Muhammad akichunga heshima yake na kujiepusha kabisa na hisia za kike. Maisarah naye baada ya kurejea kutoka safarini alimbainisha Bi Khadija matukio yote yaliyotokea safarini pamoja na maneno ya kiongozi wa kidini wa Kiyahudi ambaye alimwambia: Nifikishie salamu zangu kwa Bibi Khadija na umpe khabari kwamba, atakuwa mke wa kiongozi wa duniani na akhera. Mwambie kwamba, muda si mrefu atakuwa na daraja ambayo ni ya juu kuliko wote. Ewe Maisarah! Muda si mrefu Mwenyezi Mungu atakifanya kizazi cha mama mheshimiwa wako kutoka katika kizazi cha huyu mwanaume na jina la bibi wako litabakia milele. Mwambie kauli hii kutoka kwangu kwamba, hakuna mtu atakayeingia peponi bila ya kumuuamini bwana huyu na kusadikisha risala na ujumbe wake….

Baada ya Bibi Khadija kusikia maneno hayo, alimuendea Waraqah bin Nawfal na kutaka ushauri kutoka kwake. Wakati huo uwepo wake wote ulikuwa umetawaliwa na mapenzi na huba kwa Mtume SAW. Baada ya hafla ya uchumba na ndoa, alimtumia  Muhammad SAW mali nyingi kama zawadi kwa Mtume na kuumwambia Waraqh bin Nawfal kwamba, watangazie watu wote kuwa, kuanzia sasa na kuendelea, utajiri na suhula zote za kibiashara na kiuchumi za Khadija ni za Muhammad ambazo amempatia kwa moyo mkunjufu, nia safi na fakhari kamili. Waraqah bin Nawfal alifanya kama alivyotakiwa ambapo akiwa amesisima baina ya Zamzam na maqam Ibrahim aliwaita watu wote kwa sauti ya juu na kusema: Enyi watu! Shuhudieni na mtambue kwamba, Khadija amempatia Muhammad utajiri wake wote kuanzia mashamba, bustani, mifugo mpaka watumwa na watumishi na hata huba na mapenzi yake na amempokea na kumkubali.


Kwa hakika Bibi Khadija AS si tu kwamba, aliamini mafundisho yaliyoletwa na Mtume SAW, bali alijitolea pia kwa moyo wake wote kusaidia kueneza mafundisho hayo. Bi Khadija alikuwa akituliza na kupunguza machungu ya Mtume SAW ya kukadhibishwa na kuudhiwa na munafikina. Mtume SAW alifunga ndoa na bibi Khadija akiwa na umri wa takribani miaka 25. Kwa muda wa miaka 24 Bi Khadija alikuwa mwenza na mke wa Mtume SAW. Mtume SAW hakuoa mke mwingine katika kipindi cha uhai wa Bibi Khadija. Baada ya kuaga dunia Bi Khadija, Mtume SAW alioa wanawake wengine kulingana na hekima na sababu mbalimbali na kutoka kwa makabila mbalimbali, hata hivyo hakuna mwanamke  yeyote kati ya wake zake hao aliyeweza kujaza pengo la Bibi Khadija. Aidha Mtume SAW hakujaaliwa kupata mtoto yeyote kutoka kwa wake zake hao wengine na hivyo kizazi cha Mtume SAW kuendelea na kubakia kupitia kwa Bibi Khadija.

Salama na salamu za Allah ziwe juu yako Ewe Bibi Khadija, mama wa waumini, mke mwema wa mbora wa viumbe Mtume Muhammad SAW, mama wa Bibi Fatima na bibi wa Imam Hassan na Hussein AS.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …