Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Ijumaa, 18 Machi 2016 09:53

Tarehe 29 Esfand, Siku ya Kutaifishwa Sekta ya Mafuta Iran

Tarehe 29 Esfand, Siku ya Kutaifishwa Sekta ya Mafuta Iran

Tarehe 29 Isfand mwaka 1329 Hijria Shamsia sawia na Machi 20 1950 ni moja ya siku zenye kukumbukwa katika historia ya mapambano ya taifa la Iran na madola ya kibeberu.

Siku hii hukumbukwa katika kalenda ya Iran kama 'Siku ya Kutaifishwa Sekta ya Mafuta'. Tarehe 29 Isfand ni siku ya ushindi wa taifa la Iran katika mapambano na utawala wa kiimla ndani ya nchi na mabeberu wa kigeni.
Katika historia ya Iran ya kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kulijiri matukio machungu kama vile kudhalilishwa na kukiukwa haki za taifa la Iran sambamba na kuporwa utajiri wa nchi hii. Kusainiwa mikataba mikubwa na ya kiutumwa kama vile mkataba wa Golestan na Torkmancheh ni ishara ya namna nchi hii ilivyopata masaibu na kuwa mhanga katika medani ya mashindano ya serikali za Ulaya na Russia na baadaye Marekani. Katika mkondo wa historia ya Iran, madola ya kibeberu yaliilazimisha nchi hii kukubali sera zao za kujitakia makuu kwa kutumia hila, mabavu na udhaifu wa watawala ambao walikuwa tegemezi. Kwa njia hiyo madola hayo yaliweza kupata faida kubwa kupita kiasi chini ya kile kilichotajwa kuwa ni mikataba baina yao na watawala wa kiimla wasiostahiili kuingoza Iran.
Ni kwa msingi huo ndio tunaweza kubaini chanzo cha harakati ya kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran ambayo chimbuko lake ni mkataba wa mafuta ya petroli ya Iran ambao ulianza mwaka 1870.
Moja ya mikataba ya kushangaza zaidi ulikuwa mkataba baina ya serikali ya Iran na Baron Julius de Reuter. Kwa mujibu wa mkataba huo shirika moja la kigeni lilipata haki ya miaka 70 ya kumiliki na kutumia misitu, mito, madini ya mkaa wa mawe, chuma, shaba, madini ya risasi, mafuta ya petroli n.k. Haki ya Iran baada ya kuchimbwa madini au mafuta ilikuwa asilimia 15 tu.
Mkataba huu ulikuwa wa kushangaza sana kiasi kwamba hata Lord Curzon mmoja kati ya wanasiasa mashuhuri wa Uingereza na ambaye alikuwa kati ya waanzilishi wa sera za kibeberu za nchi hiyo alisema hivi kuhusu mkataba huo: "Kukabidhi vyanzo vyote vya kiviwanda vya nchi kwa dola la kigeni ni jambo la ajabu na urafiki wa karibu wa Uingereza na Iran haujawahi kufikia kiwango hiki." Katika Mkataba baina ya serikali ya Iran na Baron Julius de Reuter, kipengee cha 11 kilisema hivi: "Petroli ambayo ina umuhimu mkubwa itakuwa sawa na mkaa wa mawe, shaba na madini ya risasi." Miaka 30 baadaye yaani mwaka 1902, watawala wa wakati huo wa Iran walilipatia shirika lingine la Uingereza haki ya muda wa miaka sitini kutafuta, kuchimba, kuzalisha na kuuza mafuta ya petroli katika maeneo yote ndani ya Iran isipokuwa maeneo ya kaskazini. Mkataba huo ulitiwa saini kati ya Iran na Muingereza William Knox D'Arcy. Hisa ya Iran katika mkataba huu ilikuwa ni asilimia 16 tu. Cha kushangaza ni kuwa, pamoja na kuwa faida ya Iran ilikuwa ndogo sana lakini pia hawakuwa tayari kulipa kiasi hicho kidogo na hivyo shirika hilo la Uingereza lilipata faida kubwa sana katika shughuli zake za uchimbaji mafuata nchini.
Baada ya kukaliwa kwa mabavu Iran na Uingereza kisha Shirikisho la Sovieti na baadaye Marekani baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, mashindano ya madola ya kibeberu kuhusu maslahi yao nchini hasa mafuta yalishadidi. Serikali ya Uingereza ilikuwa ikitaka kulinda satwa yake katika sekta ya mafuta kusini mwa Iran na kwa msingi huo ikatia saini mkataba mwingine na Iran mwaka 1933. Mkataba huo ulilalamikiwa vikali na wananchi wa matabaka mbali mbali haswa Ayatullah Kashani ambaye alikuwa akihesabiwa kama mmoja kati ya wanazuoni wanamapambano katika bunge la Iran wakati huo. Ayatullah Kashani alitoa tamko kali sana dhidi ya Shirika la Mafuta la Uingereza na kufuatia malalamikio hayo baadhi ya wabunge walifikisha bungeni pendekezo la kubatilishwa mkataba huo. Hapo serikali ya Uingereza ilianzisha njama za kubadilisha hali ya mambo kwa maslahi yake na kwa msingi huo, Ayatullah Kashani, alikamatwa na vibaraka wa mtawala Shah na kisha akapelekewa huko Kerman Shah na baadaye akabaidishiwa nchini Lebanon. Katika kipindi hicho kuliundwa Bunge la Waasisi ambalo lilikuwa bunge kibaraka na la kimaonyesho tu kwa lengo la kubadilisha katiba. Katika mabadiliko hayo ya katiba mtawala Shah alipewa uwezo mkubwa kama vile wa kuvunja bunge. Shah alichukua hatua za kuupa msingi wa sheria mkataba wa mwaka 1933 na katika pendekezo lililojaa uhaini aliwasilisha mswada wa 'Mkataba Ziada' na kuufikisha bungeni lakini haukupitishwa na hapo muhula wa bunge la awamu ya 15 likafika ukingoni. Katika duru ya 16 ya Bunge, Ayatullah Kashani alichaguliwa na wananchi wa Tehran huku baadhi ya Maulamaa wakifanya jitihada za kuhakikisha anarejea nchini kutoka uhamishoni. Katika moja ya vikao vya bunge la awamu ya 16, Ayatullah Kashani alitoa ujumbe mkali akilaani kubaidishwa kwake kinyume cha sheria. Aidha alisema miswada ya Bunge la Waasisi (Bunge la zamani la Senate) ya kulazimisha mkataba wa mafuta ilikuwa batili. Ujumbe huo ulisomwa bungeni na Dakta Mossadeq. Sehemu ya ujumbe huo inasema hivi: "Mafuta ni ya taifa la Iran kwa hivyo haikubaliki kulazimisha mikataba iliyo kinyume cha sheria. Mikataba kama hiyo haina itibari ya kisheria na wala haiwezi kulinyima taifa la Iran haki zake za kimsingi." Hapo lilianza vuguvugu la kutaifisha sekta ya mafuta ya Iran. Ayatullah Kashani alitoa tamko refu ambapo alibainisha kuwa, utaifishwaji setka ya mafuta ni wajibu wa kidini na kitaifa wa wananchi Waislamu wa Iran. Kwa uongozi wa Ayatullah Kashani wananchi na wabunge walishiriki katika maandamano na mijumuiko ya kuunga mkono kutaifishwa sekta ya mafuta. Hatimaye tarehe 29 Isfand mwaka 1329 Hijria Shamsia sawa na Machi 20 1950, sekta ya mafuta Iran ilitaifishwa rasmi baada ya muswada kuidhinishwa katika Majlisi.
Kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran hakukumaanisha kumalizika njama za Uingereza dhidi ya taifa hili. Baada ya kupoteza satwa na ushawishi wao haramu katika sehemu kubwa ya mafuta ya Mashariki ya Kati mababeru walianzisha njama mpya dhidi ya Iran. Ni kwa msingi huo ndio maana mwaka 1953 madola ya kibeberu ya Uingereza na Marekani yakashirikiana katika njama ya kuipindua serikali ya wakati huo ya waziri mkuu wa Iran Mohammad Mosaddegh. Baada ya mapinduzi hayo mashirika mengi ya Marekani na Uingereza yaliingia Iran kupora mafuta ya nchi hii chini ya ubia mpya.
Ubia huo uliundwa na mashirika kama vile Shell Petroleum, Gulf Oil, Mobile Oil, Standard Oil, Oil Company of California, Texas Oil n.k. Kufuatia kuundwa ubia huo, Ayatullah Kashani alianzisha tena mapambano na kuandikia barua Umoja wa Mataifa akibainisha kutokuwa na itibari mkataba uliotiwa saini baina ya utawala na ubia huo. Pamoja na hayo, madola ya kibeberu ya Uingereza na Marekani kwa kutegemea uungaji mkono wa mtawala Shah, walilazimisha Iran kukubali ubia huo wa mashirika 16 ya mafuta ya Ulaya na Marekani na kwa msingi huo wakaendelea kupora mafuta ya Iran. Baada ya kutiwa saini mkataba huo baina ya utawala kibaraka wa Shah na mashirika hayo ya kimagharibi, ule mswada wa kutaifishwa sekta ya mafuta ulitupiliwa mbali. Mashirika hayo ya Magharibi yalihodhi kila kitu kuanzia kutafuta, kuchimba, kuzalisha na kuuza mafuta ya Iran. Uchumi wa Iran ulikuwa tegemezi sana kwa sekta ya mafuta jambo ambalo lilihatarisha mustakabali wa nchi. Hali hiyo ya kisikitisha iliendelea hadi ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini mwaka 1979. Punde baada ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu, Iraq ilivamia kijeshi Iran na hapo taathira mbaya za kutegemea sekta ya mafuta zikabainika wazi baada ya adui kuhujumu na kuharibu viwanda muhimu vya mafuta na kuyumbisha uchumi wa nchi. Ni kwa sababu hii ndio leo, kwa kuzingatia uzoefu mchungu wa huko nyuma, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikatekeleza sera za kuacha kutegemea sekta ya mafuta. Hakuna shaka kuwa kuwepo mafuta katika nchi ni nukta nzuri ambayo inaweza kuimarisha uchumi iwapo pato litatumika vyema katika kuimarisha miundo msingi na uwezo wa kielimu na kisayansi katika nchi. Katika sera mpya za uchumi wa kimapambano wa Iran, kuna mkakati mkubwa wa kuondoa utegemezi kwa pato la mafuta. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kubainisha vigezo vya uchumi wa kimapambano anasema: "Utegemezi huu wa mafuta ni turathi chungu ya miaka 100 iliyopita. Tunavitazama vikwazo kwa mtazamo huu. Tunapaswa kutumia fursa hii kuhakikisha kuwa pato la mafuta linaacha kutegemewa kwa kuanzisha harakati mbadala za kiuchumi...; Kiongozi Muadhamu pia anasisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa sayansi za msingi na uzalishaji wa elimu ili nchi iweze kustawi. Kwa msingi huo sera za uchumi wa kimapambano zilizowasilishwa nchini zimeashiria nukta muhimu kama vile kuibua ubunifu katika sekta mbali mbali, kuimarisha uwezo wa kuzalisha gesi na mafuta hasa katika medani za pamoja na nchi jirani, kuimarisha uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na mafuta na gesi n.k. Hivi sasa miongoni mwa nchi jirani na Iran, sekta ya mafuta ya Iran imepiga hatua kubwa zaidi ya kimaendeleo. Katika miongo miwili iliyopita, pamoja na kuweko vikwazo vya madola ya kibeberu, Iran imeweza kupata mafanikio makubwa sana. Nchi hii kwa kuwategemea wahandisi na wataalamu vijana Wairani wameweza kutekeleza miradi mikubwa ya viwanda vya kusafisha mafuta, viwanda vya petrokemikali na uzalishaji gesi sambamba na kuzalisha bidhaa mbali mbali za mafuta na gesi.
Waziri wa Mafuta wa Iran mwezi Desemba mwaka 2015 alizindua mbinu mpya ziltakazotumika katika mikataba ya sekta ya mafuta nchini. Kikao hicho kilihudhuriwa na mashirika makubwa ya mafuta duniani kama vile Shell ya Uingereza na Uholanzi, Total ya Ufaransa, Ani ya Italia, Petronas ya Malaysia, Lukoil ya Russia, na CNPC ya China.
Kuimarisha uchimbaji na kuongeza uwezo wa uzalishaji mafuta na gesi wa Iran, kuinua kiwango cha teknolojia nchini na kuwezesha sekta binafsi katika sekta ya mafuta ni kati ya misingi muhimu ya mikataba mpya ya mafuta nchini Iran.
Waziri wa Mafuta wa Iran, Bijan Namdar Zangeneh amesema Iran inalenga kuvutia uwekezaji wa dola bilioni 40 kila mwaka katika sekta ya mafuta katika fremu ya mpango wa sita wa ustawi. Amesema uwekezaji huo utapelekea kuongezeka kiwango cha gesi inayochimbwa na Iran katika visima vya pamoja na nchi jirani katika eneo la Pars Kusini, ilkilinganishwa na nchi jirani. Msingi mkuu katika ustawi wa sekta ya mafuta nchini ni kushirikishwa sekta binafsi.
Historia ya sekta ya mafuta Iran na mipango ya maendeleo ya sekta hii inaonyesha utegemezi wa mashirika ya kigeni jambo ambapo lilipelekea kudhoofika miundo msingi ya sekta hii. Lakini hivi sasa moja ya sifa mpya za sekta ya mafuta Iran ni kuimarishwa ushiriki wa mashirika ya ndani ya nchi. Sekta ya mafuta Iran imepita kipindi kigumu lna hivi sasa imepata muelekeo mzuri na endelevu katika fremu ya uchumi wa kimapambano. Ili kufanikisha sekta hii, kuna uwekezaji wa dola bilioni 134 katika kitengo asili cha sekta ya mafuta na gesi na vile vile uwekezaji wa dola bilioni 70 katika sekta zingine husika. Nukta muhimu ni kuwa ustawi wa sekta ya mafuta Iran ni kwa msingi wa kuunga mkono uwezo wa ndani ya nchi na wataalamu Wairani.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …