Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 20 Januari 2016 20:48

Kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyofariki dunia bibi Maasuma AS

Kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyofariki dunia bibi Maasuma AS

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyofariki dunia Bibi Fatima al Maasuma, Alayha Salam, mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu SAW.


******

Mtume Mtukufu SAW, Maimamu Watoharifu AS pamoja na watoto wao watukufu wana daraja na utukufu mkubwa kati ya viumbe vyote. Mwenyezi Mungu SW amewafanya kuwa ruwaza za kweli kati kwa wanaadamu. Kadiri ufahamu na maarifa kuhusiana na watukufu hao unavyozidi kuwa mkubwa, ndivyo mtu anavyohisi kuwa na mapenzi na mahaba zaidi kwa watukufu hao moyoni mwake. Hapana shaka kuwa, mapenzi ya kweli hupatikana kutokana na kuwafahamu na kuwajua vyema watu wao watukufu. Moja ya njia za kuweza kuwafahamu mawalii wa Mwenyezi Mungu ni kutwalii na kutafakari sira na mwenendo wa maisha yao, na pia kukumbuka nafasi ya kimaanawi na ubora wao wa kiakhlaki na kimaadili. Njia hiyo ya ufahamu, mbali na kuwa kiasili huleta athari muhimu ya kujenga na kuzidisha mapenzi nyoyoni, lakini pia humfanya mtu awafanye ruwaza na kigezo bora watuhufu hao na afuate mafunzo yao na kuiga matendo yao. Hii ni kwa sababu, hakuna mtu anayeweza kupata malezi sahihi, ufanisi na kufikia ukamilifu, ila atakapokuwa tayari kufuata njia na kuiga mwenendo wa watu ambao wana daraja ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa watukufu hao ni Bibi Fatima al Maasuma AS, binti wa Imam Musa bin Jaafar AS, ambaye katika siku ya leo tunakumbuka kufariki kwake dunia. Tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani na haswa kwa wapenzi wa Mtume Mtufuku SAW na watu wa nyumba yake tukufu kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kufariki dunia mjukuu huyo wa Mtume mtukufu.


******

Kwa mtazamo wa dini tukufu ya Kiislamu, kuwa mwanamme au mwanamke si kigezo cha kuwa mbora au kuwa mtukufu zaidi, kwani mafunzo ya Uislamu yanamlenga mwanadamu na wala si jinsia ya mtu. Kama ambavyo wanaume kama Mitume na Maimamu watoharifu AS walikuwa mifano bora kwa wengine, wanawake watukufu pia kama vile Bibi Asya mke wa Firaun, Bibi Maryam, Bibi Khadija, Bibi Fatimatul Zahra, Bibi Zainabul Qubra na Fatima al Maasuma AS nao wanahesabiwa kuwa vigezo na mifano bora kwa wanawake wote duniani. Kwa msingi huo, kutwalii historia ya maisha, sira ya kivitendo na kila kinachohusu mienendo ya watukufu hao walioteuliwa na Mwenyezi Mungu, ni njia bora ya kujifunza maadili bora ya kumfikisha mwanadamu katika ufanisi, maisha bora na ukamilifu wa kibinadamu. Pia kuwafahamu vyema watu hao huwa ni mwanga wa uongofu katika maisha ya watu wote. Ni wazi kuwa mmea utakaomea katika bustani ya Uimamu na kupata nishati kwa kustafidi na nuru hiyo iliyojaa utukufu, hauchakai wala kupukutika majani kwa kupita muda, bali kadiri muda unavyopita ndivyo unavyozidi kustawi na matawi yake huchanua na kupendeza zaidi, kutokana na utukufu wa shajara njema ya familia ya Mtume Mtukufu SAW. Bibi Fatima al Maasuma AS ni binti katika familia hiyo, ambaye alizaliwa mjini Madina tarehe Mosi Mfunguo Pili mwaka 173 Hijria. Bibi huyo alilelewa na kuishi katika nyumba aliyokuwa pia akiishi baba yake Imam Musa Khadhim AS na kaka yake Imam Ridha AS. Bibi Fatima al Maasuma Alayhas Salaam alikulia katika malezi ya ucha Mungu na katika chemchemu ya maarifa, hekima, elimu na kujikabidhi kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu na kupata utakasifu mkubwa wa mwili na roho kutoka kwa Muumba wake. Akiwa bado mdogo, alikumbwa na msiba mkubwa wa kuuawa shahidi baba yake kipenzi kwenye jela ya Haroun al Rashid katika mji wa Baghdad. Hivyo kuanzia wakati huo akawa chini ya usimamizi na ulezi wa kaka yake Imam Ali bin Musa ar Ridha A.S.


******

Ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kwamba chimbuko na chemchemu ya ufanisi na ukamilifu wa mwanadamu na kuwa karibu na Allah, ni kuwa na imani thabiti juu ya dhati iliyotakasika ya Mwenyezi Mungu na kufuata vyema na ipasavyo maamrisho Yake. Mwenyezi Mungu aanasema, maisha mazuri ni matokeo ya imani na amali njema, na katika Suratul Nahl amemuahidi kila mwanamume au mwanamke atakayetenda amali njema, kuwa atapata maisha mazuri. Bibi Fatima al Maasuma AS ni miongoni mwa wanawake ambao imeelezwa kuwa aliwazidi wengine katika kufuata mwenendo huo. Mtaalamu mashuhuri wa hadithi, marhum Haji Sheikh Abbas Qumi anaandika kuhusiana na watoto wa kike wa Imam Musa al Kadhim AS kuwa: Kwa mujibu wa yale yaliyotufikia, wabora kati yao ni Bibi Jalilah Muadhama na Fatima binti wa Imam Musa al Kadhim AS maarufu kwa jina la Bibi Maasuma.
Bibi huyo mwenye fadhila alikuwa na utukufu mkubwa, na Maimamu watoharifu walikuwa wakimtaja kwa utukufu na heshima kubwa kiasi kwamba hata kabla ya kuzaliwa kwake, baba yake mtukufu alikuwa tayari amelisikia jina lake kutoka kwa baadhi ya Maimamu, na tayari utukufu na nafasi yake adhimu ilikuwa imeshazungumziwa. Imenukuliwa kutoka kwa Imam Jafar Sadiq AS akisema: Mwanamke kutoka katika watoto wangu atafariki dunia katika mji wa Qum, ambaye jina lake ni Fatima binti Musa. Wafuasi wangu wataingia peponi kwa kuombewa shifaa na yeye.
Sifa nyingine bora za Bibi Fatima al Maasum AS, ni uwezo wake wa kubainisha na kuchambua hadithi, na kutokana na kipaji hicho alijulikana kwa jina la 'Muhadditha.' Jina la Fatima binti Musa bin Jaafar pia linaonekana katika silsila ya sanadi za baadhi ya wapokezi wa hadithi, na maulamaa wa Kisuni na Kishia wanazielezea riwaya zake kuwa ni sahihi na zenye kukubalika. Miongoni mwa hadithi hizo ambazo mapokezi yake yanaenda hadi kwa Bibi Fatimatul Zahra AS na Mtume Mtukufu SAW ni Hadith ya Ghadir na Hadithi ya Manzila, ambazo zinaelezea utukufu wa Imam Ali AS. Aidha kuna riwaya nyingi zimepokewa kuhusu ubora wa kielimu aliokuwa nao bibi huyo mtukufu tangu udogoni mwake. Hapa ni vyema nikakunukulieni kisa kimoja. Imepokewa katika vitabu vya historia kwamba siku moja kundi moja la wafuasi wa Ahlul Bait AS walikwenda nyumbani kwa Imam Musa bin Jaafar al Kadhim AS wakiwa na maswali yao mjini Madina. Hata hivyo Imam Kadhim AS hakuwepo nyumbani, alikuwa safarini. Wafuasi hao wa Ahlul Bait AS walimkabidhi Bibi Maasuma AS maswali yao, ili atakaporejea baba yake Imam Kadhim AS ampe na watakuja siku ya pili kufuata majibu yao. Hata hivyo walipokuja siku ya pili, Imam Kadhim AS alikuwa bado hajarejea safarini. Sehemu waliyokuwa wametoka watu wale ilikuwa ni mbali na mji mtakatifu wa Madina, hivyo waliomba warejeshewe maswali yao kwa nia ya kuja siku nyingine. Wakati huo bibi Maasuma alikuwa msichana mdogo sana. Aliwarejeshea maswali yale yakiwa yameshajibiwa. Waliyaangalia majibu hayo, wakaridhishwa nayo, wakafunga safari ya kurejea walikotoka. Mwenyezi Mungu alikuwa amekadiria kuwa, wakutane na Imam Kadhim njiani, na walipokwisha kumhadithia kisa chao, walimuonesha majibu waliyopewa na Bibi Maasuma kuhusu maswali yao. Wapokezi wa hadithi wanasema, Imam Musa bin Jafar AS alipoyasoma majibu hayo, alisema mara tatu, baba yake awe fidia yake.
Bibi Fatima al Maasuma AS alikuwa akimpenda sana kaka yake Imam Ridha AS. Mapenzi hayo hayakutokana tu na uhusiano wa kinasaba kati ya kaka na dada, bali ufahamu wa bibi huyo mtukufu juu ya nafasi ya uongozi katika Uislamu. Mapenzi hayo yalimfanya bibi huyo afunge safari ambayo ilikuwa na nafasi muhimu mno katika maisha yake.

******

Safari ya Imam Ridha AS ya kubaidishwa kutoka mji wa Madina na kupelekwa Marwa nchini Iran mwaka 200 Hijiria, ilifanyika kutokana na sisitizo na vitisho vya Maamun mtawala wa Bani Abbas, na mtukufu huyo alielekea katika mji wa Khorasan nchini Iran bila ya kufuatana na mtu yoyote wa familia yake au watu wa nyumbani kwake. Mwaka mmoja baada ya kuhamishwa kwa nguvu kaka yake, Bibi Fatima al Maasuma aliamua kufunga safari ya kumfuata kaka yake Imam Ridha AS akifuatana na baadhi ya kaka zake na watoto wa kaka zake. Alianza safari ya kuelekea Khorasan kwa ajili ya kumuona kaka yake huyo na muhimu zaidi kutekeleza jukumu la kutetea nafasi ya "wilaya" na uongozi. Msafara wake ulipokelewa na kulakiwa na watu wengi katika kila mji waliopita. Bibi huyo mtukufu pia aliwafikishia Waislamu ujumbe wa kudhulumiwa na kuachwa pekee kaka yake, kama alivyofanya Bibi Zaynab AS, na kuonyesha upinzani wake na wa Watu wa Nyumba ya Mtume AS dhidi ya utawala uliokuwa umejaa hila wa Bani Abbas.
Msafara wa bibi huyo mtukufu ulishambuliwa ukiwa njia na baadhi ya watu waliokuwa wakiwapinga Ahlul Bait na ambao walikuwa wakiungwa mkono na vibaraka wa utawala wa wakati huo. Uvamizi dhidi ya msafara wa bibi huyo ulipelekea karibu wanaume wote wa msafara huo kuuwawa shahidi. Kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya hadithi, Bibi Fatima al Maasuma naye pia alipewa sumu na watu hao waovu. Alaakullihaal, Bibi Fatima al Maasuma aliugua, labda kutokana na majonzi na huzuni kubwa iliyotokana na tukio hilo au kutokana na athari ya sumu aliyopewa, na kwa kuwa hakuweza tena kuendelea na safari yake hadi Khorasan, aliamua kwenda katika mji wa Qum. Alisema: 'Nipelekeni katika mji wa Qum, kwani nilimsikia baba yangu akisema kwamba, mji wa Qum ni kituo cha wafuasi wetu.'


******

Wakuu wa mji wa Qum walipopata habari ya kuja kwake waliharakisha kwenda kumlaki. Musa bin Khazraj mmoja wa wazee wa mji huo aliwatangulia watu wote kwenda kumlaki bibi huyo mtukufu. Bibi Fatima al Maasuma aliwasili katika mji mtukufu wa Qum, mwezi 23 Mfunguo Saba mwaka 201 Hijiria. Aliishi katika mji huo kwa muda wa siku 17 na katika wakati huo alijishughulisha na ibada, dua na kujikurubisha kwa Mola Muumba. Eneo alilokuwa akifanyia ibada bibi huyo mtukufu hadi leo linajulikana kama 'Baitun Nur, na hadi leo hii linatembelewa na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad SAW.
Mwishowe ilipofika mwezi 10 Mfunguo Saba mwaka 201 Hijiria, Bibi Fatima al Maasuma alifariki dunia huku akiwa katika upweke na majonzi makubwa na hakuweza kuonana tena na kaka yake, yaani Imam Ali bin Musa ar Ridha AS. Watu wa Qum na wapenzi wa Ahlul Bait waliuzika mwili wa bibi huyo mtukufu katika eneo ambalo wakati huo lilikuwa nje ya mji. Baada ya kuzikwa mtukufu huyo, mmoja wa wazee wa Qum wakati huo, Musa bin Khazraj Saibani aliweka juu ya kaburi la mtukufu huyo mikeka mingi. Hali hiyo ilibaki hivyo hadi mwaka 256 Hijria wakati Bibi Zaynab binti wa Imam Jawad AS alijenga kuba la kwanza juu ya kaburi la bibi yake huyo mtukufu, na kuanzia wakati huo, alipozikwa mtukufu huyo, likawa kivutio cha nyoyo za wapenzi na maashiki wa Ahlul Bait AS. Kutokana na baraka ya eneo hilo, hadi hii leo mji wa Qum ni moja ya vituo vikubwa vya elimu ya Ahlul Bait AS na dini tukufu ya Uislamu. Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani na haswa wapenzi wa Mtume Mtufuku SAW na Watu wa Nyumba yake toharifu kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyofariki dunia mjukuu huyo wa Mtume SAW.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …