Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 18 Januari 2016 14:07

Kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Hassan Askari AS

Kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Hassan Askari AS

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nami katika makala yetu ya leo ambayo inawajieni kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Hassan Askari AS. Ni matumaini yangu kuwa mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.
Tarehe 8 Mfunguo Saba Rabiuthani inasadifia na siku aliyozaliwa Imamu Hassan Askari AS ambaye ni mmoja kati ya wajukuu wa Nabi wetu Muhammad SAW. Imamu Askari alizaliwa mwaka 232 Hijria na japokuwa hakuishi zaidi ya umri wa miaka 28 lakini ametuachia hazina kubwa ya elimu na maarifa ya Kiislamu.
Vitabu vya historia na wasifu wa shakhsia za Kiislamu vimeandika kuwa, Imamu Hassan Askari AS alikuwa na sura yenye haiba na mvuto makhsusi, mpole, mwingi wa huruma na moyo mkunjufu. Historia inahadithia watu kadhaa ambao awali walijiweka mbali na mtukufu huyo kutokana na kutomjua vyema lakini baadaye wakabadilika na kuwa miongoni mwa masahaba zake wa karibu baada ya kukutana na kuzungumza naye. Kipindi cha Uimamu wake kilidumu kwa karibu miaka sita ambayo sehemu yake kubwa alikuwa uhamishoni au katika jela za watawala wa Kiabbasi. Mjukuu huyo wa Mtume Muhammad SAW aliishi katika vipindi vya makhalifa watatu wa kizazi cha Bani Abbas ambao ni Muutaz, Mahdi na Muutamid.
Akiwa bado mtoto mchanga, Imamu Hassan Askari AS alilazimishwa na watalawala wa Kiabbasi yeye na familia yake kuondoka mjini Madina huko Hijaz karibu na kaburi la babu yake, Mtume Muhammad SAW na kuhamia Samurra, Iraq, makao makuu ya wakati huo ya utawala wa Bani Abbas. Katika zama hizo ambapo udikteita na ukandamizaji vilishadidi zaidi, ilikuwa vigumu mno kwa Imamu kupata fursa ya kufanya vikao vya darsa na mijadala ya kielimu na alikuwa akikutana na mikusanyiko ya watu na watafutaji elimu na maarifa kwa taabu na mashaka makubwa. Kwa msingi huo mtukufu huyo aliwasiliana na watu na kubainisha maarifa ya Kiislamu kupitia njia mbalimbali hususan mawasiliano ya barua na maandiko.
Ali bin Muhammad Maliki mashuhuri kwa jina la Ibn Swabbagh ambaye ni miongoni mwa wasomi wakubwa wa Kiislamu, amesema yafuatayo kuhusu Imamu Hassan Askari AS: "Alikuwa wa kipekee na hakuwa na kifani katika zama zake. Hakuna mtu yeyote aliyekuwa kama yeye. Alikuwa kinara wa elimu na daima alikuwa akitatua mushkeli na matatizo yote ya watu. Alikuwa akifafanua na kuweka wazi uhakika wa mambo kwa kutumia fikra zake madhubuti."
Moja ya masuala muhimu kwa Ahlubaiti wa Mtume Muhammad SAW ilikuwa kubainisha umuhimu wa suala la Uimamu na uongozi wa jamii ya Kiislamu. Ahlubaiti wa Mtume walitumia fursa mbalimbali kuwaelimisha wananchi kuhusu sifa za kiongozi bora, mwaminifu na mwadilifu. Walikumbusha kwamba, wakati wowote watu madhalimu na fasiki wanaposhika hatamu za kuongoza Umma, jamii hupatwa na matatizo na hatimaye kuporomoka kama ilivyoshuhudiwa katika historia ya muda mrefu ya mwanadamu. Kuhusu umuhimu na nafasi ya Imamu na kiongozi katika jamii, Imamu Hassan Askari AS alimwandikia barua Ismail Naishaburi akisema: Mtu ambaye hajamtambua Imamu na kiongozi wake duniani huwa katika hali ya kutapatapa na mfadhaiko." Anasema katika sehemu nyingine ya barua hiyo kwamba:"Ni katika rehema za Mwenyezi Mungu kwamba amewajibisha baadhi ya mambo kwa waumini ambayo katika medani ya majaribio ya maisha, yanaweka wazi mema na maovu na kutahini yaliyoko nyoyoni mwenu. Kuweni wa kwanza kuelekea kwenye rehema za Mola Mlezi kwa kutekeleza wajibu na faradhi za kidini ili nafasi na hadhi za wenye takwa zidhihirike."
Kuwasaidia na kutoa auni kwa watu mbali ya kuwa kunapanda mbegu za furaha na bashasha katika nyoyo na kufumbua baadhi ya matatizo yao, hueneza moyo wa upendo, mahaba na ushirikiano katika jamii. Kwa sababu hiyo, Imamu Hassan Askari AS amevitaja vitu viwili yaani uchamungu na kuwasaidia watu, kuwa ni sifa mbili kubwa za ukamilifu wa mwanadamu. Anasema: "Kuwa na imani na Mwenyezi Mungu na kuwafaidisha watu ni sifa mbili ambazo hakuna sifa bora na iliyo juu zaidi ya hizo."
Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Muhammad bin Hassan anasema: Siku moja nilimwandikia barua Imamu Askari SA nikizungumzia umaskini na ukata wangu. Imamu alijibu barua hiyo kwa maneno ambayo yalinitia moyo na kuniliwaza. Aliandika kwamba: "Sisi Ahlubaiti wa Mtume Muhammad SAW ni makimbilio ya watu wanaoomba hifadhi kwetu, na nuru na mwanga kwa wanaotaka uongofu. Anayetupenda sisi Ahlul Baiti wa Mtume atakuwa pamoja nasi katika daraja za juu za peponi."
Abu Hashim Jaafari anasimulia kwamba: Siku moja nilibanwa na ukata na nikataka kuomba dinari kadhaa kutoka kwa Imamu Hassan Askari AS. Nilimwendea mtukufu huyo lakini nikashindwa kusema lolote kwa kuona soni, na baadaye nikarejea nyumbani. Hata hivyo Imamu alielewa matatizo yangu. Muda mfupi baadaye mjumbe wa Imamu Askari alibisha hodi na kunipa dinari mia moja kutoka kwa mtukufu huyo pamoja na ujumbe uliokuwa na maandishi yafuatayo: Uwapo na haja usiwe na haya na woga wa kusema. Omba unachotaka, utapewa."
Kuhusu umuhimu wa kutambua haki za ndugu katika dini na kuwa mpole mbele yao, Imamu Askari anasema: "Mtu anayetambua zaidi haki za ndugu zake hufanya juhudi kubwa zaidi za kutekeleza haki hizo na kuwa na nafasi ya juu kwa Mwenyezi Mungu SW. Mtu mpole kwa ndugu zake duniani atakuwa pamoja na siddiqin kwa Mola Mlezi.

>>>


Moja ya sifa makhsusi za maisha ya Imamu Hassan Askari AS ni kutosalimu amri mbele ya madhalimu na madikteita na kusimama kwake imara katika njia ya haki. Mbali na jukumu lake kubwa la kuwaongoza watu katika kipindi cha Uimamu wake, Imamu alikuwa na wadhifa mwingine ambao ni kutayarisha Umma kwa ajili ya kipindi cha ghaiba ya Imamu Mahdi AS. Kwani Imamu wa Zama na Mwokozi Aliyeahidiwa wa walimwengu ni mwana wa Imamu Hassan Askari na alianza kipindi cha ghaiba ndogo baada tu ya kipindi cha uongozi wa baba yake. Katika kipindi hicho kilichojaa ukandamizaji, maisha ya mwana huyo wa Imamu Askari yalitishiwa na watawala madhalimu wa Bani Abbas. Hata hivyo Imamu Mahdi AF alisalimika na njama za watawala hao kwa rehema zake Mola Muweza na tadbiri ya Imamu Hassan Askari AS. Imamu Mahdi alikwenda ghaiba baada ya kufariki dunia baba yake na hapana shaka atadhihiri tena na kubomoa misingi ya dhulma inayotawala dunia ya sasa na kuijaza usawa na uadilifu kwa idhini ya Mola Muumba kama ilivyoahidiwa na Mtume Muhammad SAW katika hadithi nyingi zilizopokelewa na wanahistoria na wapokezi wa hadithi wa madhehebu karibu zote za Kiislamu.
Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu wote hususan wapenzi na wafuasi wa Ahlubaiti wa Nyumba tukufu ya Bwana Mtume SAW kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuzalia mjukuu wake Imamu Hassan Askari amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na baba zake watoharifu.
Nawatakia kila la kheri na kwaherini.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …