Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 28 Disemba 2015 11:21

Sira ya Imam Sadiq (AS) ya Waislamu kuridhiana na kuwa wamoja

Sira ya Imam Sadiq (AS) ya Waislamu kuridhiana na kuwa wamoja

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Siku ya Ijumaa ya mwezi 17 Mfunguo Sita (Rabiul-Awwal) mwaka 83 Hijria, sawa na mwaka 702 Miladia, alizaliwa mja mbarikiwa, Imam Jaafar As-Sadiq (AS); shakhsia mkubwa katika Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW, ambaye jina lake limezipamba duru za kielimu na kidini katika zama zote za historia. Katika siku hii ya leo yenye baraka, inayosadifiana pia na maadhimisho ya maulidi ya Mtume wa mwisho wa Allah, Nabii Muhammad SAW, tunamswalia na kumtakia rehma na amani mtukufu huyo na mbora huyo wa viumbe pamoja na Ahlul Bayt zake sambamba na kukupeni nyinyi wapenzi wasikilizaji mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba huo.
Karibuni basi kusikiliza kipindi hiki maalumu kitakachodondoa machache katika sira ya Imam Sadiq (AS) kuhusu umoja baina ya Waislamu.

Imam Jaafar As-Sadiq (AS) alitumia kipindi cha miaka 34 ya umri wake wa miaka 65 kubeba mas-ulia mazito na hasasi ya Uimamu na uongozi wa umma wa Kiislamu. Kati ya Ahlu Bayt wa Bwana Mtume SAW, hakuna yeyote miongoni mwao aliyepata fursa kubwa zaidi kama aliyopata yeye ya kueneza mafundisho ya Uislamu na kuandaa shakhsia wateule na watajika. Zama za Imam Sadiq (AS) zinaweza kutajwa kuwa ni zama za migongano ya fikra na kuibuka madhehebu na matapo mbalimbali. Jambo hili lingeweza kuikosesha jamii ya Kiislamu mafundisho halisi ya dini hiyo na kuwaelekeza watu kwenye upotofu; lakini kuwepo kwa nuru ya shakhsia ya Imam Jaafar As- Sadiq (AS) kuling'arisha anga ya fikra za wenye kiu ya haki na kuwaacha vinywa wazi watu waliokuwa wakijigamba kuwa wajuzi wa elimu na maarifa.
Imam Sadiq (AS) alikuwa akisistiza kila mara juu ya kuwepo uhusiano wa kiutu na wa upendo mkubwa baina ya watu. Alikuwa akisema: "Shikamaneni, pendaneni, tendeaneni wema na ihsani na oneaneni huruma". Mtukufu huyo alikuwa akiusia mtu kuwa na upendo na urafiki na Waislamu wote; na hata akamuusia mmoja wa masahaba zake kwa kumwambia:" Wafikishie salamu wafuasi wetu na waambie Mwenyezi Mungu anamrehemu mja anayejijengea urafiki kwa watu".
Imam Jaafar As-Sadiq (AS) alikuwa akiamini kwamba watu wa jamii tofauti za kidini ni sehemu ya Jamii ya Kiislamu na wanapaswa kuheshimiwa. Yeye mwenyewe alikuwa katika zama ambazo waliishi ndani yake watu wa dini na madhehebu mbalimbali. Tunapoutalii mwamala na mlahaka wa Imam Sadiq kwa wafuasi wa dini na madhehebu nyengine tutabaini kwamba mtukufu huyo alikuwa akiwapokea katika darsa zake Waislamu wa madhehebu mbalimbali bali hata na wasiokuwa Waislamu. Abu Hanifa, Imam wa madhehebu ya Hanafi ni miongoni mwa watu hao, ambapo yeye mwenyewe aliwahi kusema, lau isingelikuwa miaka miwili aliyosoma kwenye darsa ya Imam Sadiq (AS), basi angeangamia.

Mlahaka huo wa Imam Jaafar As-Sadiq (AS) ulileta faida nyingi sana kwa jamii ya Waislamu wa zama hizo. Miongoni mwa hizo ilikuwa ni ya watu kukutanika pamoja na kujdiliana, ambapo hata kama majadiliano yao hayakuishia kwa mmoja kukubali fikra na rai ya mwenzake, lakini yalijenga upendo na kuwafanya wamoja. Kwa sababu wakati watu wanapokaliana mbali hufikiriana dhana mbaya, na hilo ni jambo linalochangia sana kuwepo suutafahamu baina yao. Kuonana uso kwa uso kuna taathira kubwa ya kumfanya mtu awe na ufahamu sahihi na wa pande zote wa itikadi na mitazamo ya wenzake. Kuhudhuria darsa za Imam Sadiq (AS) kuliwafanya watu wenye fikra nyenginezo wamfahamu vizuri na kwa karibu zaidi Imam na kutambua adhama yake ya kielimu na utukufu wake wa kiroho. Kwa hakika sira hiyo ya tadbiri na hekima ya Imam Jaafar As-Sadiq (AS) inapasa kuwa dira na mwongozo wa kufuatwa na madhehebu mbalimbali; kwani sababu kubwa inayozifanya madhehebu leo hii ziwe mbalimbali ni suutafahamu juu ya itikadi na matendo baina ya madhehebu moja na nyengine. Na ni suutafahamu hiyo, ndiyo inayotumiwa na maadui kusababisha na kuchochea chuki na uadui baina ya Waislamu wenyewe.
Japokuwa watu waliokuwa wakishiriki kwenye darsa za Imam Jaafar As-Sadiq (AS) hawakuwa na mtazamo sawa kifikra na mtukufu huyo lakini walikuwa wakiitukuza daraja yake ya elimu na kukiri kwamba hawakuwahi kuona faqihi mkubwa zaidi ya Imam. Tab'an kuna idadi kubwa ya wanafunzi na wahudhuriaji wa darsa za Imam Jaafar As-Sadiq waliofuata njia yake. Mfano mmoja maarufu wa wanafunzi hao ni Hisham Ibn Hakam. Vitabu vya hadithi na historia vya Shia na Suni vimesimulia mengi kuhusu midahalo na mijadala aliyofanya Imam Jaafar As-Sadiq (AS) na viongozi wa madhehebu, wa kidini na hata wasio wa kidini wa zama zake. Lakini nukta muhimu ni kwamba mijadala hiyo haikuishia kwenye utengano wala uhasama. Kwani moja ya usuli ya kiakhlaqi ya Imam ilikuwa ni kushikamana na wasia wa Qur'ani usemao "jaadilhum billatii hiya ahsan", yaani kujadiliana na watu kwa upole na kwa wema. Kwa hivyo hata wapinzani wenyewe walikuwa wanakiri kwamba Imam Jaafar Sadiq alikuwa akichunga heshima ya mtu anayejadiliana naye na kusikiliza maneno yake hadi mwisho kwa hamu, utulivu na umakini. Kisha kwa kutumia maneno sahihi na yaliyokamilika, lakini machache na yenye kufikisha ujumbe, ndipo na yeye akawa anabainisha rai na maoni yake.
Kuhusu ulazima wa kudumisha umoja na kuwa kitu kimoja, Imam Sadiq (AS) alimueleza mmoja wa masahaba zake alitwaye Zaid Ibn Hisham kuhusu jinsi ya kulahikiana na kuamiliana na wafuasi wa madhehebu nyengine za Kiislamu kwa kusema:
"Ingieni na salini misikitini mwao; watembeleeni wagonjwa wao; shirikini kwenye maziko yao; na kuweni na tabia ya namna itakayowafanya wakujieni na kusali nyuma yenu....Mwenendo wenu utakapokuwa huo watasema, hawa wana madhehebu ya Jaafarii; Mwenyezi Mungu amrehemu Imam Sadiq, amelea wafuasi wazuri walioje.... Lakini kama akhlaqi zenu zitakuwa mbaya;... watasema hawa ni wafuasi wa Jaafari, na Imam Sadiq amelea wafuasi wabaya walioje."
Katika mahala pengine Imam Jaafar Sadiq (AS) amesema: "Muislamu ni ndugu wa Muislamu, na ni sawa na jicho, kioo na muongozo kwake; katu hamsaliti; hamhadai; hamdhulumu; hamwambii uongo na wala hamsengenyi."
Kwa hivyo kwa mtazamo wa Imam Jaafar Sadiq (AS) misingi ya kuimarisha na kuiunganisha jamii ya Waislamu ni kuwa na nia njema, kutakiana kheri, kushirikiana na kusaidiana. Ni matarajio hewa kudhani kwamba tutaweza kuwa na umma imara na ulioshikamana pasina kuandaa misingi hiyo ya kimwenendo na kitabia. Tuelewe kwamba mifarakano na kudhoofika kwa jamii ya Waislamu chimbuko lake ni utengano uliopo baina ya nyoyo za Waislamu wenyewe na kushamiri umimi na ubinafsi kati yao.
Wapenzi wasikilizaji, kwa mara nyengine tena ninachukua fursa hii kukupeni mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa siku hii ya kuadhimisha kuzaliwa Imam Jaafar As-Sadiq (AS). Ni matumaini yangu kuwa sira na miongozo ya mtukufu huyo itakuwa taa ya kumurikia na kuongozea njia kwa Umma wa Kiislamu kwa ajili ya kuleta umoja na mshikamano baina ya Waislamu duniani. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …