Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 24 Disemba 2015 11:28

Isa Masih AS, hazina ya kipekee ya rehema na mapenzi ya Allah

Isa Masih AS, hazina ya kipekee ya rehema na mapenzi ya Allah

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika makala hii maalumu tuliyokuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Nabii Issa bin Maryam AS. Tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwa kila anayempwekesha Mwenyezi Mungu na kutomshirikisha na chochote, kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Nabii wa amani na mapenzi, ambaye ni msaidizi wa Imam Mahdi AS, mwokozi muahidiwa wa ulimwengu, yaani Nabii Isa Masih AS. Hivi sasa tumo katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa mtukufu huyo ambaye atarejea ardhini katika zama za mwisho wa dunia na kuwa msaidizi wa mwokozi wa ulimwengu, kwa ajili ya kuijaza dunia amani na uadilifu. Tunaianza makala hii kwa kunukuu maneno ya Nabii Isa AS aliponukuliwa akisema katika kitabu cha Mathayo mistari ya 43 hadi 44 kwamba: Mmesikia kwamba ilisemwa: Mpende jirani yako na kumchukia adui yako. Lakini mimi nawaambieni, wapendeni adui zenu na kuwaombea wale wanaowadhulumu ninyi.
Amma mafundisho yanayodhihirika kwa uwazi zaidi kati ya mafundisho ya Nabii Isa AS ni mapenzi, huruma, upole na kusamehe. Katika kitabu cha Yakobo, amenukuliwa Nabii Isa AS akisema: Mpende binadamu mwenzako kama unavyojipenda wewe mwenyewe, mtakuwa mnafanya vema kabisa. Lakini mkiwabagua watu, basi, mwatenda dhambi, nayo Sheria inawahukumu ninyi kuwa mna hatia.

Mpenzi msikilizaji, kuna nukulu nyingi zimenukuliwa kuhusiana na maisha ya Nabii Isa AS. Hata hivyo sisi tutategemea marejeo ya Kiislamu ya Qur'ani Tukufu, kitabu ambacho hakina shaka ndani yake na hadithi kwa ajili ya kuelezea machache kuhusiana na Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu. Sababu nyengine inayotufanya tutumie marejeo hayo ni kuwa, hakuna marejeo yoyote ya kihistoria na kidini yaliyomzungumzia vizuri Nabii Isa AS kama inavyofanya Qur'ani tukufu na marejeo ya Kiislamu. Marejeo hayo yanamtaja Nabii Isa AS kuwa anatokana na kizazi kitoharifu cha Nabii Ibrahim AS, na alipambika kwa sifa bora tangu kuzaliwa hadi kurejea kwake kwa Mola wake na hadi atakapokufa na kufufuliwa. Qur'ani Tukufu inachora kwa njia bora kabisa sira ya maisha ya Nabii Isa AS ambaye yeye mwenyewe alisema, ametumwa kutoa bishara njema ya kudhihiri Mtume wa Mwisho. Mtu yeyote hawezi kuwa Muislamu bila ya kumwamini Nabii huyo mtukufu ambaye Mwenyezi Mungu amempandisha daraja la kufikia kumwita kuwa ni roho Yake.
Nabii Isa AS anatajwa na Qur'ani Tukufu kwa majina ya Masih, Ruhullah yaani roho ya Allah, Abdullah yaani mja wa Allah, mwenye kubarikiwa na Kalimatullah yaani Neno la Allah. Nabii Isa AS ameitwa kwa jina la Neno la Allah kutokana na kuzaliwa kimiujiza kwa amri ya Mwenyezi Mungu ambaye anapotaka jambo huliambia kuwa na hapo hapo linakuwa. Katika hadithi za Bwana Mtume Muhammad SAW pia, moja ya lakabu za Isa bin Maryam AS imetajwa kuwa ni Ruhullah. Lakabu nyingine za mtukufu huyo tunaweza kusema kuwa ni Muallimul Khayri (Mwalimu wa Kheri) na Ruhul Amin.
Vyanzo vya Kiislamu vimetoa maelezo mazuri kuhusiana na shakhsia ya Nabii Isa AS. Masih Isa AS alizaliwa kimiujiza bila ya baba. Alizaliwa na mama mtoharifu, Maryam bint Imran AS, bila ya bibi huyo mtoharifu kuguswa na mwanamme yeyote. Qur'ani Tukufu inamzungumzia kwa njia bora kabisa bibi Maryam AS ambaye alikuwa mtoharifu tangu utotoni mwake na alipambika kwa maadili bora na uchaji Mungu wa hali ya juu kiasi kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa anamshushia chakula kutoka mbinguni. Katika sehemu moja ya aya ya 37 ya Sura ya tatu ya Aal Imran, Mwenyezi Mungu anasema: Kila mara Zakariya alipoingia chumbani kwake (Maryam) alimkuta na vyakula. Basi alimwambia: Ewe Maryamu! Unavipata wapi hivi? Naye akasema: Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.
Hata hivyo, baada ya kumzaa Nabii Isa AS, bibi huyo mtoharifu alianza kuvurumishiwa tuhuma za kila namna na Mayahudi. Hata hivyo kitoto hicho kichanga, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, kilianza kuzungumza kimiujiza kikiwa bado kisusuni na kumtetea mama yake mtoharifu. Qur'ani inahadithia kwa sura nzuri kabisa tukio hilo katika Surat Maryam.
Alipotimia miaka mitatu, Nabii Isa AS alikuwa huja ya Mwenyezi Mungu kwa waja Wake. Alipewa Utume akiwa na umri wa miaka saba na tangu wakati huo alianza kufanya miujiza. Hata hivyo ilikuwa ni katika umri wa miaka 30 ndipo alipopewa amri ya kutangaza hadharani Utume wake kwa Bani Israil. Kwa mara ya kwanza alipokea wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu akiwa katika mlima Sa'ir. Alipaishwa kwenda mbingu akiwa na umri wa miaka 33.

Nabii Isa alikuwa na kimo cha kati na rangi nyeupe inayoelekea kwenye wekundu na nywele za mawimbi. Amma katika upande wa maadili bora, utawa na ucha Mungu, hakuwa na mfano wake hata mmoja katika zama zake. Muda mwingi alikuwa akifunga saumu, akivaa nguo chakavu na kula mkate mgumu wa shairi. Hakuwa na nyumba wala mwana na hadi mwisho wa umri wake hakuwahi kuwinda hata mara moja. Alikuwa akisimama kusali popote anapokuwa kila jua lilipozama na akiendelea na ibada hadi jua linapochomoza.
Imam Ali AS anasema hivi kuhusiana na Nabii Isa AS. "Na kama mnataka nikuelezeni kuhusu Isa bin Maryam AS jueni kwamba mto wake wa kulalia ulikuwa ni jiwe, akivaa kitambaa kigumu kilichochakaa na akila chakula msichoweza kukila na mchuzi wake ilikuwa ni njaa. Hakuwa na mke wa kumzonga, wala mwana wa kumtia huzuni, wala mali za kumshughulisha na dunia na wala tamaa ya dunia. Kipandio chake ilikuwa ni miguu yake miwili na mtumishi wake ilikuwa ni mikono yake miwili.
Nabii Isa AS ni miongoni mwa Mitume watano bora wanaotajwa na Qur'ani Tukufu kwa jina la Ulul 'Azm waliopambika mno kwa sira za taqwa, kumzingatia Mwenyezi Mungu, subira na kuwasamehe wanaowakosea. Ijapokuwa maadui walimfanyia istihzai Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu kama walivyofanyiwa Mitume wengine akiwemo Bwana Mtume Muhammad SAW, lakini kejeli na istihzai hizo hazikumfanya asite hata kwa sekunde moja kufikisha risala yake kwa Bani Israil. Nabii Isa AS alizingatia mno kukabiliana na madhalimu na kupinga ufisadi wa wakuu wa dini ya Kiyahudi. Kuna maneno mengi ya mfululizo yaliyonukuliwa kutoka kwa Nabii Isa AS akiwaita wakuu wa dini ya Kiyahudi kwa majina ya mafisadi, wala haramu na wasio na maadili mema. Nabii Isa AS alisafiri maeneo mengi kwa ajili ya kufikisha risala aliyotumwa na Mola wake Mlezi, na kumenukuliwa mawaidha mengi sana kutoka kwa mtukufu huyo. Miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakisisitizwa mno na Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu ni tawhidi na kumwamudu Mungu Mmoja asiye na mshirika, akisisitiza sana kujipamba kwa maadili bora, kulinda haki na uadilifu. Mara zote alikuwa akisisitiza kuwa, kuna Mtume atakuja baada yake, na jina lake ni Ahmad. Akisisitiza sana kwamba, hakutumwa kubadilisha hukumu za Taurati bali ametumwa kuzikamilisha.
Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, Nabii Isa AS ni hazina ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kueneza uadilifu duniani. Hivyo Mwenyezi Mungu amembakisha hai hadi atakapodhihiri Imam Mahdi AS ulimwenguni na atarejea ardhini kuwa msaidizi wa mwokozi huyo wa dunia.
Wakristo wanasubiri kurejea duniani Nabii Isa AS ili kusimamisha amri za Mwenyezi Mungu ardhini. Waislamu wanasubiri kudhihiri Imam Mahdi, kutoka kizazi kitoharifu cha Bwana Mtume Muhammad SAW ili kuijaza dunia haki na uadilifu na wanaamini kuwa, Nabii Isa AS atarejea ardhini baada ya kudhihiri Imam Mahdi AS na kusaidiana naye katika kusimamisha dola ya haki na uadilifu. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri mwokozi wa ulimwengu, Imam Mahdi AS na iwe sababu ya kurejea duniani Nabii Isa AS ili dhulma na batili iangamie na haki na uadilifu uijaze dunia.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …