Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 08 Disemba 2015 13:06

Imam Hassan AS nembo ya subira, ushujaa na kutotetereka

Imam Hassan AS nembo ya subira, ushujaa na kutotetereka

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji. Mwezi 28 Mfunguo Tano Safar mwaka wa 50 Hijiria aliuawa shahidi mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW na mwana wa Bibi Fatimatuz Zahra SA, Imam Hassan al-Mujtaba AS ambaye pia ni Imam wa pili kutoka kizazi kitoharifu cha Bwana Mtume SAW. Mtukufu huyo aliuawa shahidi kwa kupewa sumu na mkewe aliyejulikana kwa jina la Ja'da bint al Ash'ath ibn Qays al Kindi. Ushahidi wa kihistoria unathibitisha kuwa Muawiyya bin Sufyan alimrubuni mke wa Imam Hassan AS, dirham 1000 na kumwahidi angeruhusu aolewe na mwanawe Yazid kama angemuua Imam Hassan AS. Ja'da alihadaika na njama hiyo na akamuua kidhulma kwa kumpa sumu Imam Hassan AS. Leo tumekuandalieni makala maalumu kwa ajili ya kuzungumzia kwa ufupi maudhui hiyo kama ambavyo pia tutajaribu kunukuu hadithi kadhaa zenye mafunzo mazuri kutoka kwa mtukufu huyo tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa yale yatakayokuwemo kwenye makala hii.

Kabla ya kuuawa shahidi Imam Hassan al Mujtaba AS alimuusia ndugu yake Imam Hussein AS kwamba mara atakapokata roho na kurejea kwa Mola wake, auoshe yeye mwili wake, auvishe sanda na akisha kuuweka kwenye jeneza aupeleke kwenye kaburi la babu yake, Bwana Mtume Muhammad SAW. Imam Husain AS alifanya kama alivyousiwa na kaka na Imam wake, Imam Hassan AS. Lakini wakati jeneza la mtukufu huyo lilipokuwa linapelekwa kwenye kaburi la babu yake Bwana Mtume Muhammad SAW. Bani Umayya walikusanyika na kufunga njia ya msafara huo wa maziko ya mjukuu huyo wa Bwana Mtume na kuonesha ukatili na unyama wa hali ya juu dhidi ya Ahlul Bait wa Mtume kiasi kwamba waliulenga msafara huo wa jeneza la Imam Hassan AS kwa mishale na mikuki. Hatimaye ghasia hizo zilizuia msafara huo kuelekea kwenye kaburi la Bwana Mtume Muhammad SAW na mwili wa Imam Hassan AS ulizikwa katika makaburi ya Baqee.
Chuki walizokuwa nazo Bani Umayya ziliwafanya wasahau maneno matukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW aliposema: "Hassan ni ua langu lenye harufu nzuri. Ewe Mwenyezi Mungu! Ninampenda Hassan basi na Wewe mpende, na mpende kila anayempenda."
Pia Bani Umayya walionesha chuki zao kubwa dhidi ya mjukuu huyo wa Bwana Mtume na kuzisahau aya ya tatu na ya nne ya sura ya 53 ya an Najm, Mwenyezi Mungu aliposema: Wala (huyu Muhammad) hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya (anayoyasema) ila ni ufunuo uliofunuliwa (na Mwenyezi Mungu).
Bani Umayya walimfanyia dhulma hiyo mjukuu huyo wa Mtume ambaye Bwana Mtume Muhammad SAW amenukuliwa akisema: Hassan na Husain ni mabwana wa vijana wa peponi. Hassan na Husain AS ni maua mawili yenye harufu nzuri ya Bwana Mtume Muhammad SAW. Hassan na Husain AS ni Maimamu wa Waislamu katika hali yoyote, wawe wamesimama au wawe wamekaa kitako. Ni wajukuu hao wa Bwana Mtume ndio waliomfanya mtukufu huyo arefusha sijda zake katika Sala mpaka washuke mgongoni mwake. Bani Umayya walionesha uadui wao dhidi ya wajukuu hao watukufu wa Bwana Mtume ambao kuwapenda wao ni ibada. Kuwapenda wao ni kumpenda Mtume na anayempenda Mtume anapendwa na Mwenyezi Mungu na anayemchukia Mtume, ajiandae kwa hasira na adhabu kubwa ya Mwenyezi Mungu.

Wapenzi wasikilizaji, licha ya kupita karne nyingi tokea lilipotokea tukio hilo chungu katika historia ya Uislamu, lakini bado nyoyo za Waislamu na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Mtukufu SAW zingali zinahuzunika kutokana na uonevu na dhulma kubwa aliyofanyiwa Imam Hassan al Mujtaba AS. Imam Hassan AS aliyezaliwa katika nyumba ya Wahyi, akalelewa katika nyumba hiyo, kwenye mikono mitukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW na Bibi Fatimatuz Zahra SA na Imam Ali AS, alipambika kwa sifa aali na bora kabisa za ukamilifu wa mwanadamu. Jambo linalowashangaza wengi kuhusiana na Imam Hassan AS ni subira kubwa aliyoionyesha katika kipindi cha mwishoni mwa maisha yake yaliyojaa baraka hapa duniani. Imam Hassan AS alionyesha subira na uvumilivu mkubwa hata kwa maadui waliomuua, kwa kumtaka ndugu yake Imam Hussein AS asilipize kisasi. Imehadithiwa katika vitabu vyenye itibari vya historia kwamba, wakati Imam Hassan al Mujtaba AS alipokaribia sekunde za mwisho za maisha yake, alimwambia ndugu yake Imam Hussein AS: "Ndugu yangu! Karibuni hivi nitaachana nawe na nitakwenda mbele ya Mwenyezi Mungu. Wamenipa sumu na ninajua ni nani aliyefanya haya na sababu ya kufanyiwa dhulma hii. Nitakabiliana naye mwenyewe mbele ya Mwenyezi Mungu. Ninaapa kwa haki niliyo nayo kwako, usilipize kisasi kwa jambo hili. Subiri uamuzi wa Mwenyezi Mungu. Yeye Ndiye atakayenilipia dhulma hii niliyofanyiwa."
Imam Hassan al-Mujitaba AS alikuwa na sifa nyingi bora za ukamilifu wa kibinadamu na sifa zake za maadili bora zilienea katika kila kona na zilikuwa zikizungumziwa na wengi katika zama zake. Tumetangulia kusema kuwa moja ya sifa zake bora ilikuwa ni subira na uvumilivu mkubwa. Vitabu vingi vya historia vimeizungumzia kwa upana sifa yake hiyo bora. Hata maadui wakubwa wa Ahlul Bait wa Bwana Mtume Muhammad SAW kama vile Marwan walishindwa kuficha sifa hiyo na walikiri waziwazi kwamba uvumilivu na subira ya Imam Hassan AS ilikuwa imara kama mlima.

Miongoni mwa matukio muhimu sana yaliyorekodiwa katika historia kuhusiana na maisha ya Imam Hassan al Mujtaba AS ni suluhu aliyoweka kati yake na Muawiya. Baada ya kuuawa shahidi Imam Ali AS, Waislamu walim-bai na kutangaza utiifu wao kwa Imam Hassan AS. Tokea wakati huo, Muawiya alianza kufanya njama za kuzitia shaka fikra za watu kwa kueneza mambo ya uongo, uzushi na uvumi na alifanikiwa kuwarubuni baadhi ya wafuasi mahsusi wa Imam kwa kuwapa hongo. Baada ya kuona kuwa baadhi ya wafuasi wake walikuwa wamefanya khiana na kutekwa na njama za Muawiya, Imam Hassan AS alilazimika kufanya suluhu na Muawiya ili kulinda roho na mali za Waislamu. Ni kutokana na ukweli huo mchungu ndipo uongozi wa Imam Hassan AS ulidumu kwa miezi sita na siku chache tu tangu Waislamu walipotangaza utiifu wao kwake. Suluhu ya Imam Hassan AS ni baadhi ya hatua nzuri zilizokuwa na faida kubwa kwa umma wa Kiislamu kwa sababu zilipelekea kulindwa Uislamu. Ni wazi kuwa vita vya Waislamu wenyewe kwa wenyewe havingekuwa na manufaa yoyote kwa ulimwengu wa Kiislamu bali vingekuwa na madhara makubwa. Hii ni kwa sababu ufalme wa Roma ambao katika kipindi hicho ulikuwa umeshindwa vibaya sana na Waislamu ulikuwa ukisubiri kwa hamu kubwa kuona ulimwengu wa Kiislamu unakumbwa na mizozo na kudhoofika nguvu zao ili uweze kutumia fursa hiyo kuuvamia na kulipiza kisasi cha kushindwa na Waislamu huko nyuma, na hiyo ni moja ya sababu zilizomfanya Imam Hassan AS akubali kufanya suluhu na Muawiya.
Katika upande wa pili, hali ya watu wa Iraq ilikuwa mbaya na wala hawakuwa tayari kuunda jeshi la kumsaidia Imam Hassan AS kupambana na maadui wake. Ni jambo lililo wazi kuwa kwenda kwenye medani ya vita na watu kama hao ambao hawakuwa na motisha ya kupigana vita kusingelikuwa na natija nyingine ghairi ya kushindwa tu. Imam Hassan AS alifanya subira kubwa mbele ya hiana na welewa mdogo wa watu wa zama zake ambao hawakuwa na mwamko wowote wa Kiislamu ili kulinda Uislamu usije ukapotea, na ndio maana alikubali kufanya suluhu na Muawiya.
Imam Hassan al Mujtaba AS alitumia muda mwingi kuwaelimisha watu hao, lakini ni wachache waliokuwa tayari kumsikiliza. Aliwaambia: "Watu hufanya suluhu kwa kuhofia dhulma ya watawala wao, lakini mimi ninafanya suluhu kwa kuhofia dhulma ya wafuasi wangu. Nilikuamrisheni mpigane jihadi na maadui lakini mlikataa. Nilikukumbusheni haki lakini hamkusikia na sasa hata kabla ya kumalizika hotuba yangu mnatawanyika kama walivyofanya watu wa Sabaa, na mmedanganyana kwa kujificha kwenye vazi la mawaidha na ushauri."
Sifa ya subira na uvumilivu aliyokuwa nayo Imam Hassan al Mujtaba AS ilikuwa kubwa kiasi kwamba, mtukufu huyo alipata umaarufu kwa sifa hiyo aali. Uvumilifu na subira ya aina yake aliyokuwa nayo Imam AS ilipelekea kulindwa Uislamu na kuzidi kupata nguvu dini hiyo tukufu hadi hadi leo licha ya kupita karne nyingi za zama alizoishi duniani mtukufu huyo. Uvumilivu wa mtukufu huyo ulifikia kilele cha kunawiri baada ya kuwekeana makubaliano ya suluhu na Muawiya. Kama si subira na uvumilivu mkubwa, Imam asingeliweza kukabiliana na kipindi hicho kigumu mno katika maisha yake matukufu. Kama tulivyosema, Imam Hassan AS alilazimika kukubali suluhu hiyo ya kulazimishwa, ili kuilinda dini aliyokuja nayo babu yake, Bwana Mtume Muhammad SAW. Ni jambo lililo wazi kuwa, nguzo na msingi mkuu wa Uislamu ungelikuwa hatarini kama asingelikubali suluhu hiyo. Mbali na kuvumilia vitimbi vya Muawiya, Imam alilazimika pia kuvumilia lawama kutoka kwa watu waliokosa kuwa na muono wa mbali. Aliwajibu watu waliokuwa wakimkosoa na kulalamika suluhu yake na Muawiya kwa kuwaambia: "Mimi nimefanya suluhu kwa ajili ya kulinda damu ya Waislamu. Kama nisingelifanya hivyo basi hakuna hata mmoja kati ya wafuasi wetu ambaye angebaki hai duniani... Ole wenu! Hamjui nimefanya hivyo kwa lengo gani? Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, kukubali suluhu kwa ajili ya wafuasi wangu ni bora zaidi kuliko kile kinachoangaziwa na jua wakati wa kuchomoza na kutua kwake..."

Mwanzoni mwa makala hii tumekunulieni aya ya tatu na ya nne ya sura ya 53 ya an Najm Mwenyezi Mungu aliposema: Wala (huyu Muhammad) hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya (anayoyasema) ila ni ufunuo uliofunuliwa (na Mwenyezi Mungu). Ni wazi kuwa Mtume SAW ambaye alikuwa na mtazamo mpana kuhusiana na ulimwengu, Mwenyezi Mungu alimfunulia mambo mengi yaliyofichikana na yaliyokadiriwa kutokea baadaye duniani. Bwana Mtume alimsifu mjukuu wake huyo kwa kusema: "Kama akili ingelidhihiri kwa sura ya mtu, basi mtu huyo angelikuwa ni Hassan AS."
Hata kama Imam Hassan AS alipambika kwa sifa nzuri ya uvumilivu na subira lakini kila ilipolazimu, alikuwa akikabiliana na mambo tofauti kwa msimamo thabiti na imara. Ni kwa sababu hiyo ndio maana historia imerekodi kwamba, katika maisha yake yaliyojaa baraka na licha ya kusifika kwa uvumilivu na subira, lakini Imam alisifika pia kwa ushujaa na kutotetereka mbele ya maadui. Pamoja na kuwa maadui walimuweka Imam Hassan AS katika mazingira magumu ambayo yangemlazimisha aachie mwenyewe madaraka bila ya kupenda, lakini hilo halikumfanya akubali dhulma kutoka kwa watawala madhalimu wa zama zake. Akiwa mjini Madina, Imam alitumia fursa tofauti zilizojitokeza kukemea na kukosoa vikali utawala usio wa Kiislamu wa Muawiya. Kwa mfano siku moja tu baada ya kufanyika suluhu, Muawiya alikwenda mjini Kufa na kumsema vibaya Imam Ali AS mbele ya umati mkubwa wa watu. Imam Hassan AS hakustahamili maneno hayo ya dharau na ghafla alipanda juu ya mimbar alipokuwa amesimama Muawiya na kumwambia: "Je, unamtukana Amirul Mu'minina Ali AS katika hali ambayo Mtume SAW amesema: 'Anayemtukana Ali AS, huwa amenitukana mimi na anayenitukana mimi huwa amemtukana Mwenyezi Mungu, anayemtukana Mwenyezi Mungu basi Mwenyezi Mungu atamuingiza kwenye moto mkali wa Jahannam na humo atapata adhabu kali itakayodumu milele." Kisha Imam Hassan AS aliteremka kutoka kwenye mimbar na kutoka nje ya msikiti huo kama alama ya kulalamikia kitendo hicho cha Muawiya. Kuna hatua nyingine nyingi imara na madhubuti kama hiyo zilizochukuliwa na Imam Hassan AS dhidi ya Muawiya na vibaraka wake.
Kwa uono wake mpana na wa mbali usio na kifani, na licha ya kushinikizwa na wafuasi wake, Imam Hassan AS alijikubalisha kustahmili istihzai na matusi ya maadui pamoja na malalamiko ya wafuasi wake wasio na mwamko kwa ajili tu ya kulinda Uislamu usiharibiwe na kupotoshwa na maadui. Imam alivumilia matatizo mengi ili kuwapa fursa watu watambue na kung'amua mienendo mibovu ya Muawiya na Bani Umayya. Muawiya alivunja ahadi za mkataba huo wa suluhu siku ileile ya kwanza alipoingia madarakani. Taratibu hali ikaanza kuwa mbaya kiasi kwamba siku moja Muawiya aliwaambia watu: "...Enyi watu wa Iraq! Mimi nilipigana na nyinyi ili nipate kukutawaleni tu!" Kisha alirarua mkataba huo wa suluhu na kuukanyaga kwa miguu yake.
Taratibu jambo hilo liliwafanya watu waanze kuamka kutoka kwenye mghafala wao mzito na kuanza kutambua uovu na ukhabithi wa Muawiya. Busara ya Imam Hassan AS ilikuwa ni kuwapa fursa watu waweze kutambua wenyewe ufisadi na dhulma ya Bani Umayya ili jambo hilo liweke msingi wa mapambano ya Bwana wa Mashahidi, Imam Husain AS. Kama watu wasingelijua vyema dhulma na ufisadi wa Bani Umayya ni wazi kuwa wangelitilia shaka lengo la mapambano ya Imam Husain AS dhidi ya watawala hao na hivyo kutoshirikiana naye katika mapambano hayo. Kwa hivyo ni wazi kuwa msingi wa kuendelea kuwepo Uislamu halisi wa Mtume Muhammad SAW uliwekwa na Imam Hassan AS, na kama alivyosema marhum Sheikh Radhi Aal Yassin kwamba, kisa cha Karbala kabla ya kuwa ni cha Imam Husain SA, ni cha Imam Hassan AS.
Tunamalizia makala hii kwa kukunukulieni baadhi ya hadithi zenye mafundisho mazuri za Imam Hassan al Mujtaba AS ambapo katika moja ya hadhithi zake, mtukufu huyo amenukuliwa akijibu swali aliloulizwa kwa nini sisi wanadamu tunaogopa kifo. Imam alijibu kwa kusema: "Ni kwa sababu mumefanya makosa kwa kuijenga imara dunia kana kwamba itabakia milele na kuiharibu Akhera kana kwamba hamtokufa! Mnaogopa mtaacha mlipopaimarisha kwenda kule mlikokuharibu."
Amma kuhusiana na umuhimu wa Qur'ani Tukufu na faida za aya za Kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu, Imam Hassan al Mujtaba AS amenukuliwa akisema: "Hakika katika Qur'ani hii kuna nuru ing'arayo na tiba ya vifua. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …