Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Ijumaa, 02 Oktoba 2015 12:10

Ghadir, njia nyoofu ya saada ya ufanisi

Ghadir, njia nyoofu ya saada ya ufanisi

Assalamu Alaykum Warahmatullah Wabarakatuh. Baada ya Mtume Mtukufu (saw) kumaliza Hija yake ya mwisho, aliamua kurejea Madina. Akiwa njiani, kulitoa tukio kubwa ambalo lilibadili kabisa historia. Siku hiyo mtukufu huyo aliwataka Waislamu waliokuwa wamekamilisha ibada ya Hija na kuanza kutawanyika wakielekea makwao wakusanyike katika sehemu moja iliyojulikana kwa jina la Ghadir Khum ili apate kuwapa habari muhimu na ujumbe mkubwa kutoka kwa Mola wake. Je kulikuwa na jambo gani ambalo lilikuwa limetokea katika siku hiyo?
Kwa amri ya Mwenyezi Mungu, katika siku hiyo ya Ghadir Mtume (saw) ulimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib (as) kwamba ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa kiongozi na khalifa wa Mtume ambaye atachukua nafasi ya mtukufu huyo baada ya kuondoka dunia kuuongoza Umma wa Kiislamu. Tonatoa mkono wa pongezi na fanaka kwa Waislamu wote duniani na hasa wapenda haki na uadilifu, kwa mnasaba wa kuwadia siku hii adhimu. >>
Wasikilizaji wapenzi, Mtume Mtukufu ambaye alikuwa katika siku za mwisho za umri wake alikuwa na haja ua kuuacha mti mchanga wa Kiislamu katika mikono ya mtu aliyeaminika zaidi ambaye angeulea mti huo kwa njia inayofaa baada ya kuondoka yeye. Katika kipindi cha miaka yote aliyokuwa Mtume, mjumbe huyo wa Mwenyezi Mungu hakuwahi hata siku moja kuiacha jamii ya Kiislamu bila ya mlinzi na mchungaji. Kila mara alipoondoka katika mji wa Madina, ambayo ndiyo yaliyokuwa makao makuu ya serikali ya Kiislamu katika zama zake, Mtume alikuwa akimchagua mtu wa kusimamia mambo ya Waislamu. Kwa kuzingatia hali ya wasiwasi iliyokuwepo juu ya mustakbali wa Umma wa Kiislamu, jamii ilihitajia viongozi wanaofaa na wa kuaminika ili kufsiri na kutekeleza kwa njia sahihi aya za Qur'ani Tukufu na mafundisho ya Mtukufu Mtume. Ahlul Bait wa Mtume (saw) wakiongozwa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) ndio waliokuwa chaguo bora zaidi la kutegemewa katika kuwaongoza Waislamu kwa msingi wa Kitabu kitakatifu cha Qur'ani. Katika siku ya Ghadir Khum iliyosadifiana na tarehe 18 Mfunguo tatu Dhilhaji, Mtume alisisitiza ukweli huo na kutilia mkazo nukta hii kwamba, Ahlul Bait wake na Qur'ani Takatifu ni vitu viwili vyenye thamani kubwa ambavyo kamwe havitatengana, kwa sababu vitu viwili hivyo ni chimbuko la elimu na siri za hekima ya mbinguni. Hilo ni jambo ambalo lilisisitizwa bayana na Mtume katika siku ya Ghadir.
Tukio la Ghadir
Tarehe 18 Dhilhaji mwaka wa 10 Hijiria, msafara wa Mtume na Waislamu ambao walikuwa wamekamilisha ibada ya Hija ulikuwa njiani kurejea Madina na majira ya karibu na adhuhuri, msafara huo ulifika eneo liitwalo Ghadiri Khum. Mtume wa Mwenyezi Mungu aliawataka Waislamu kusimama katika eneo hilo na akaamuru Waislamu wote waliotawanyika wakusanyike tena ili apate kuwasilisha ujumbe muhimu kutoka mbinguni. Mtume aliwaamuru masabaha wake wanne wa karibu ambao ni Miqdad, Salman, Ammar na Abu Dhar kutengeneza mimbari chini ya mti mmoja mkubwa. Watu walikuwa wakijiuliza kuhusu umuhimu wa jambo alilokuwa nalo Mtume ambalo lilimlazimu awasimamishe katika jangwa hilo pana na lililokuwa na joto kali. Taratibu sauti zilianza kufifia na kimya kikaenea kila upande.
Rabia ambaye alikuwa na sauti kubwa alichaguliwa kukariri maneno ya Mtume kwa watu ambao kidogo walikuwa mbali na mtukufu huyo na ambao hawakuweza kusikia vizuri maneneo yake. Baada ya kuswalisha Swala ya Adhuhuri, Mtume alipanda mimbari ambayo alikuwa ametengenezewa kutokana na vifaa vya ngamia huku akiwa ni mwenye kutabasamu na aliyejaa furaha. Kisha alimwita Ali bin Abi Twalib na kumwambia asimame upande wake wa kulia. Mtume ambaye alikuwa ameuweka mkono wake wa kulia katika bega la Imam Ali (as) alishukuru na kumhimidi Mwenyezi Mungu, na kuwaambia Waislamu waliokuwa wamekusanyika sehemu hiyo kwamba alikuwa na ujumbe muhimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambao ameamriwa awafikishie. Aliwaambia kwamba, kama hangefikisha ujumbe huo hangekuwa ametekeleza jukumu lake alilopewa na Mwenyezi Mungu. Baada ya kuzungumzia mambo kadhaa, Mtume aliunyanyua juu mkono wa Imam Ali bin Abi Twalib (as) na kusema: "Kila mtu ambaye mimi ni kiongozi wake basi huyu Ali pia ni kiongozi wake. Mwenyezi Mungu ampende atakayempenda, na amfanyie uadui atakayemfanyia uadui." Mtume SAW pia aliwausia Waislamu kushikamana na Qur'ani na Ahlubaiti wake na akasema viwili hivyo havitatengana hadi vitakapomkuta yeye katika hodhi ya Kauthar, Siku ya Kiyama.
Baada ya maneno hayo ya Mtume, malaika wa wahyi aliteremka kwa Mtume na kumsomea aya ya 3 ya Suratul Maidah ambayo inasema: "Leo nimekukamilishieni dini yenu, na kukutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe dini yenu."
Hivyo ndivyo historia ya Ghadir ilivyoanza kusajiliwa na kuainisha mustakbali wa jamii ya mwanadamu. >>>
Maana ya hadithi ya Ghadir na umuhimu wa siku hiyo:
Ibn Talha Shafi' anasema katika kitabu cha Matalibu's- Suul kwamba: "Kila maana itakayotolewa kwa neno 'maula' ambalo lilitumiwa na Mtume katika kumuarifisha Imam Ali bin Abi Twalib katika eneo hilo la Ghadiri Khum, litakuwa bila shaka linamhusu Ali, jambo ambalo linatosha kubainisha nafasi ya juu aliyopewa na Mtume (saw). Kwa msingi huo, siku hiyo ni siku ya furaha," mwisho wa kunukuu.
Dakta Iswam al-Imad, mtafiti mashuhuri ambaye mwanzoni alikuwa Wahabi na kufundisha katika vyuo vikuu vya Saudi Arabia, miaka kadhaa iliyopita aliongoka na kuchagua madhehebu sahihi ya Watu wa Nyumba ya Mtume (as) baada ya kufanya utafiti na uchunguzi wa muda mrefu. Amesema, alichukua uamuzi wa kubadili madhehebu yake baada ya kufahamu sifa nyingi za Imam Ali (As) zilizoashiriwa na Mtume Mtukufu (saw). Anasema: "Katika hadithi za Mtume, baada ya kuashiria suala la Tauhidi, Utume na Siku ya Kiama, nimetambua kwamba mtukufu huyo amemsifu sana Imam Ali (as). Mtume alikuwa akisisitiza na kujaribu sana kutangaza jina na matukufu ya Ali katika nyakati na sehemu mbalimba katika. Sisitizo hilo la Mtume lililokuwa na lengo la kuweka wazi sifa za kipekee za Imam Ali, lilinishangaza na kunistaajabisha mno. Hatimaye baada ya kufanya uchunguzi na utafiti wa muda mrefu nilitambua chanzo na sababu ya mapenzi makubwa ya Mtume kwa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Katika uchunguzi wangu, kwanza nilitambua dhulma kubwa aliyofanyiwa Imam Ali na kuhisi katika nafsi yangu kwamba nilikuwa nimevutiwa sana na mtukufu huyo."
Ujumbe wa Ghadir
Tukio muhimu la Ghadiri Khum limechunguzwa na kuzungumziwa na wasomi wengi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu. Abul Faraj bin Jauzi Hambali, mmoja wa wanafikra na wasomi wa Kiislamu anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: "Wataalamu wa historia na sira ya Mtume, wote wanaafikiana kwamba, tukio la Ghadir lilitokea wakati Mtume (saw) alipokuwa njiani kurejea Madina katika Hija yake ya mwisho. Katika siku hiyo masahaba, Waarabu na wakazi wa viunga vya mji wa Makka wapatao laki moja na elfu 20 walikuwa na Mtume. Hiyo ndiyo idadi ya watu waliosikia hadithi inayohusiana na uongozi wa Ali (as) kutoka kwa Mtume katika siku ya Ghadir."
Tunapasa kuzingatia nukta hii hapa kwamba, tukio la Ghadir ni la kihistoria linalobeba ujumbe kwamba, ni watu wema na wasafi tu ndio wanaofaa kupewa fursa ya kushika hatamu za kuwaongoza wanadamu.
Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa pongezi na fanaka kwa Waislamu wote duniani na wakati huohuo kuomba dua na kumtumia salamu Mtume Muhammad (saw) pamoja na Aali zake watoharifu (as(.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …