Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Septemba 2015 15:45

Duara la njama za kuuangusha mfumo wa Kiislamu wa Iran

Duara la njama za kuuangusha mfumo wa Kiislamu wa Iran

Nchini Iran wiki tuliyoko inajulikana kama ‘Wiki ya kujihami kutakatifu’ kwa mnasaba wa kukumbuka watati utawala wa Kibaath wa Iraq ulipoanzisha vita dhidi ya Iran mwaka 1980. Wananadharia na wataalamu wametoa tathmini mbali mbali kuhusu sababu za kuanza vita vya kulazimishwa vya Saddam dhidi ya Iran. Uchunguzi na utafiti uliofanyika umebaini nukta moja ya pamoja kuwa, lengo la vita hivyo vya kulazimishwa lilikuwa ni kuuangusha Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na  kwamba Marekani iliipatia Iraq jukumu hilo la kistratijia.

Suala la Marekani kumchochea na kumhimiza Saddam aishambulie Iran ni suala ambalo lina ushahidi wa nyaraka na kauli za watu mbali mbali. Zbigniew Brzezinski mshauri wa usalama wa taifa katika serikali ya Jimmy Carter rais wa wakati huo wa Marekani alikuwa kati ya walioratibu na kuandaa mazingira ya kuitayarisha Iraq kuanzisha vita. Brzezinski alishiriki katika vikao kadhaa vya siri na wakuu wa Iraq. Jarida la Wall Street Journal tarehe 8 Februari mwaka 1980 lilifichua kuhusu moja ya safari hizo za siri. Hali kadhalika gazeti la Times la London Juni 17 mwaka 1980 lilithibitisha habari hiyo kuhusu mkutano wa siri baina ya Brzezinski  na Saddam Hussein. Katika moja ya ripoti hiyo gazeti hilo liliandika hivi:"… Baada ya safari yake ya siri Baghdad mwanzoni mwa mwaka 1980, Brzezinski katika mahojiano ya televisheni alisema: 'Sisi hatuoni hitilafu za maana baina ya Marekani na Iraq. Sisi tunaamini kuwa Iraq ambayo inataka kuwa huru inatamani kuona usalama katika Ghuba ya Kiarabu (Uajemi) na hatuoni uwezekano wa kuzorota uhusiano wa Iraq na Marekani.'

Kenneth Timmerman mwandishi habari na mweledi wa masuala ya kisiasa mwaka 1991 katika kitabu chake chenye anwani ya: The Death Lobby: How the West Armed Iraq, aliandika hivi: "Brzezinski pia alifika Amman mji mkuu wa Jordan na kukutana kwa siri na kiongozi wa Iraq katika wiki ya kwanza ya mwezi Julai mwaka 1980. Mkutano huo ulifanyika kwa lengo la kufanya mazungumzo kuhusu njia za kuratibu harakati za Marekani nchini Iraq na kupinga sera za Iran."

Anaendelea kuandika: "Kwa vyo vyote vile, akiwa safarini nchini Jordan, Brzezinski alikutana na Mfalme Hussein ambapo huko Baghdad mkutano huo ulihesabiwa kuwa ni idhini ya Marekani kwa Iraq kuingia vitani na Iran."

Mwandishi huyo anaendelea kuandika kuwa: "Kwa mtazamo wa mwanastratijia aliyeboboea kama Brzezinski, hii ilikuwa hatari kubwa kubeba dhima yake hasa kwa kuzingatia kuwa uchaguzi wa rais Marekani ulikuwa ufanyike mwezi Novemba."

William Leman mchambuzi katika televisheni za Marekani tarehe 16 Februari mwaka 1993 alisema: "Mradi wa pamoja uliogharimu kiasi kikubwa zaidi cha fedha baina ya Marekani na Saudi Arabia ni ule wa jitihada za kusambaratisha mapinduzi ya Iran ambapo Saddam Hussein alitumika kuutekeleza."  Leman aliendelea kusema: "Agosti mwaka 1980, Saddam Hussein alifanya safari rasmi nchini Saudi Arabia na kuwafahamisha wakuu wa Saudia kuhusu mpango wake wa kuishambulia Iran. Wiki sita baadaye, askari wa Iraq walianzisha uvamizi."

Kenneth Timmerman katika mahojiano hayo alisema: "Msimu wa joto mwaka 1980 Wairaqi walikuwa wanataka kupata idhini ya Marekani ya kuishambulia Iran. Walituma waziri wao wa mambo ya nje Saudi Arabia na Jordan ili afanye mazungumzo na Wamarekani ili kupata yakini kuwa Marekani haingepinga uvamizi wa Iraq dhidi ya Iran. Kama ilivyotarajiwa Wamarekani hawakupinga."

Lakini swali linaloulizwa ni hili kuwa je, kwa nini pamoja na kuwepo nchi nyingi zinazopakana na Iran, Iraq ilichaguliwa kutekekeza uvamizi huo.?

Kwa mtazamo wa baadhi ya weledi wa mambo, Iraq ndio nchi pekee ambayo ingeweza kutekeleza mpango huo wa kishetani wa Marekani kutokana na sababu kadhaa. Awali ni nafasi ya kijiografia ya Iraq kama nchi yenye mpaka mrefu na Iran sambamba na kuwa na idadi kubwa ya watu na jeshi lililokuwa na mielekeo ya idiolojia ya ukaumu wa Kiarabu. Nukta muhimi zaidi ni kuwa nchi hiyo na jeshi lake iliongozwa na Saddam ambaye alitambuliwa kama mtu mwenye kutafuta kila fursa kujigamba na kujitanua. Nukta nyingine ni kuwa kulikuwepo uhasama wa kihistoria baina ya Iran na Iraq. Jimmy Carter rais wa wakati huo wa Marekani katika hotuba moja aliyotoa huko Los Angeles aliashiria kwa njia isiyo ya moja kwa moja matarajio yake  kuhusu  natija ya uvamizi wa Iraq nchini Iran kwa kusema: "Ni matumaini yangu kuwa katika vita vya Iraq na Iran kutapatikana kasi ya kuachiiliwa mateka wa Marekani na Iran ipate funzo kutokana na vita hivyo kuwa amani na utulivu ni muhimu kwa uchumi wenye nguvu katika kila nchi….Marekani inatarajia kuwa katika vita vya Iran na Iraq, nchi ya Iran itahitajia vipuri na ili kukidhi hitajio hilo itakubali masharti ya Marekani kuhusu kuachiliwa huru mateka."

Katika nyaraka za siri zilizokuwa na alama ya "Siri Kubwa' ambazo zilikuwa zimetayarishwa na ubalozi wa Marekani mjini Tehran wakati wa kukaribia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu zilikuwa zimeandikwa hivi: "…Kuna uwezekano mdogo sana kwa Iran kuvamiwa kijeshi na dola la kigeni. Kwa msingi huo Iraq ilikuwa chaguo pekee lililosalia la kuanzisha vita dhidi ya Iran. Hujuma ya Iraq ilipangwa kulenga maeneo yenye utajiri wa mafuta Iran kwa malengo maalumu. Kwa kuzingatia mazingira yaliyoandaliwa, utawala wa Iraq mnamo 17 Septemba mwaka 1980, ulichukua uamuzi wa upande mmoja na kubatilisha mkataba wake wa mpaka na Iran uliokuwa umetiwa saini mwaka 1975 huko Algiers. Baada ya hapo tarehe 21 Septemba utawala wa Kibaathi Iraq ulianzisha hujuma ya nchi kavu, angani na baharini dhidi ya Iran. Kwa msingi huo vikaanza vita vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran.

Samson Henderson mwandishi Mmarekani katika kitabu chake kuhusu malengo ya Iraq katika kuihujumu Iran aliandika: "Lengo la Saddam lilikuwa ni kuleta utawala mpya nchini Iran. Stratijia hii ilikuwa imejengeka kwa dhana kuwa watu wa Iran wakiona wana chaguo jingine wataiangusha serikali ya Ayatullah Khomeini."

Taha Yasin Ramadhan naibu waziri mkuu wa Iraq katika mahojiano na gazeti la At Thaura la chama tawala cha Baath mwanzoni mwa mwaka 1981 alisema: "Sisi tunasisitiza kuwa vita havitamalizika hadi pale utawala ulioko Iran uangamizwe kikamilifu. Hii ni kwa sababu hitilafu zilizopo hazitokani na hitilafu za mita chache za ardhi… Kwa hivyo vita na Iran si mzozo kuhusu mpaka na hivyo haviwezi kusimamishwa. Hivi ni vita vya kuainisha hatima."

Lengo la pili la hujuma dhidi ya Iran ilikuwa ni kuigawa vipande vipande nchi hii na kuibua nchi kubwa ya Kiarabu ikiongozwa na chama cha Baath cha Iraq.

Henderson anaandika hivi kuhusu suala hili: "Wakati vikosi vya Saddam vilipojipenyeza kusini magharibi mwa Iran, kwa matumaini kuwa eneo la Khuzestan lingekuwa ardhi ya Iraq lilipachikwa jina la 'Ardhi ya Kiarabu'.

Katika mahojiano ya Januari 19 mwaka 1981, Saddam Hussein alisema: "Nchini Iran kuna kaumu tano tafauti na kila moja yazo inapaswa kupewa mamlaka ya ndani. Sisi tutawaunga mkono ndugu zetu walio katika 'Ardhi ya Kiarabu' Iran." Kwa maelezo hayo utafiti kuhusu vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran umebaini kuwa, nukta tatu zilikuwa muhimu katika kuanza vita. Awali ni ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuangushwa utawala wa kiimla wa Shah ambaye alikuwa kibaraka muhimu wa Marekani Mashariki ya Kati. Kwa msingi huo mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulitizamwa kama tishio kubwa kwa mfumo wa kibeberu uliokuwa uliongozwa na Marekani.

Nukta ya pili katika kuanza vita ilikuwa ni kuanzisha mlingano mpya wa kijeshi katika eneo. Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Shah wa Iran, alikuwa akihesabiwa kama nyapara wa mabebeu katika eneo na mtetezi wa maslahi ya Marekani. Kwa hivyo Marekani ilitaka kuuangusha mfumo wa Kiislamu Iran ili kumuwezesha Saddam achukue nafasi ya unyapara katika eneo. Sababu ya tatu ya Saddam kuchochewa kuanzisha vita dhidi ya Iran ilikuwa ni kuzuia Mapinduzi ya Kiislamu kuwa kigezo kwa nchi zingine katika eneo. Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, wakati akiwa katika nafasi ya rais wa nchi katika hotuba aliyoitoa mwaka 1988 baada ya Iran kukubali azimio 598 la kusimamisha vita Julai 20 alisema: "Hujuma ya kijeshi ya Iraq dhidi ya Iran ilijiri katika kipindi nyeti sana. Ingawa weledi wa mambo duniani katika miaka yote hii wamekuwa wakijaribu kuonyesha kuwa uvamizi huu ulitokana na hitilafu za kimpaka baina ya Iran na Iraq au hitilafu za kimadhehebu na kikaumu na kadhalika, lakini ukweli ni kuwa hivi vita vilikuwa vimepangwa dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa lengo la kuuangusha mfumo wa kimapinduzi Iran na kusambaratisha Mapinduzi ya Kiislamu…" Aliongeza kuwa…."Katika mwanzo wa hujuma ya utawala wa Iraq nchini Iran, maudhui muhimu sana iliyobainika kwa njia ya wazi katika mahojiano ya rais wa Iraq na wapambe wake ni kuwa walikuwa wanalenga kuipindua Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wala hawakuficha hilo. Walitangaza wazi kuwa lengo lao ni kuiangusha serikali ya Jamhuri ya Kiislamu na kulitenga eneo lenye utajiri mkubwa la Kuzhuestan kutoka katika ardhi ya Iran. Sera hii ya utawala wa Iraq ilikuwa imeratibiwa tokea mwanzo na kadiri muda ulivyosonga mbele ilibainika kuwa hujuma hii ilitekelezwa kwa uchochezi wa madola makubwa kwa lengo la kusambaratisha Mapinduzi machanga katika eneo hili."   

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …