Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 21 Septemba 2015 13:55

Kufa shahidi Imam Muhammad Baqir (AS)

Kufa shahidi Imam Muhammad Baqir (AS)

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Tarehe 7 Mfunguo Tatu Dhulhijjah inasadifiana na siku aliyokufa shahidi Imam Muhammad Baqir (AS). Imam mtukufu ambaye, alikuwa nuru iliyoangaza kwenye giza totoro la zama zilizotawaliwa na ujahili na dhulma, na akayapa uhai mpya mafundisho aali na matukufu ya Uislamu. Katika siku kama ya leo mnamo mwaka 114 hijria, Ulimwengu wa Kiislamu ulighariki kwenye lindi la huzuni na majonzi ya kuondokewa na Imam huyo mtukufu. Tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote, hususan wafuasi na wapenzi wa Ahlul Bayt wa Bwana Mtume SAW, na kukukaribisheni wapenzi wasikilizaji kusikiliza kipindi hiki maalumu nilichokuandalieni ili kuzungumzia machache kuhusu maisha ya Imam Baqir (AS).

Habari ya kufa shahidi Imam Muhammad Baqir (AS) ilikuwa nzito zaidi na ya majonzi makubwa zaidi kwa wanafunzi wake kama Jabir bin Yazid Ja'afi. Jabir alikuwa siku zote akiukumbuka usia wa kwanza aliowahi kuusikia kutoka kwa Imam Baqir, siku alipokutana kwa mara ya kwanza na mtukufu huyo kwenye msikiti wa Bwana Mtume (SAW) mjini Madina. Siku hiyo alimsikia Imam akisema:"Tafuteni elimu, kwa sababu kutafuta elimu ni jambo jema. Elimu ni dira yako katika kiza na msaidizi katika tabu na shida na rafiki mpenzi kwa mtu".

Usia huo ulimfanya Jabir ashiriki kwenye vikao vye elimu na majadiliano vya Imam Baqir (AS) na kunufaika na bahari ya elimu ya mtukufu huyo. Jabir bin Yazid Ja'afi alikuwa akibubujikwa na machozi kwa kuondokewa na Imam, pale alipokumbuka huruma zake na kuukumbuka usia mwengine aliopewa na mtukufu huyo. Yalimpitikia akilini mwake maneno ya Imam Muhammad Baqir alipomwambia:"Ewe Jabir, mtu anayeiona raha ya kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndani ya nafsi yake, hauwezi moyo wake kushughulishwa (na mapenzi) ya kitu kingine."

Wapenzi wasikilizaji, moja ya mambo yaliyomshughulisha zaidi Bwana Mtume (SAW) na Ahlu Bayt zake (AS) ilikuwa ni kufikiria jinsi ya kuwaongoza watu kwenye njia ya saada na uongofu. Kwa sababu hiyo kila mmoja kati ya watukufu hao, kwa kuzingatia hali na mazingira tofauti ya kijamii na kisiasa aliyoishi, alitumia mbinu mbalimbali ili lengo hilo muhimu liweze kufikiwa. Kipindi cha Uimamu wa Imam Muhammad Baqir (AS) kilichukua muda wa miaka 19, na mazingira ya wakati huo yalimfanya mtukufu huyo aelekeze zaidi harakati zake za kuuongoza na kuuelimisha umma katika kubainisha na kueneza mafundisho matukufu ya Uislamu. Imam Baqir alikuwa maarufu kwa lakabu ya Baaqirul-uluum", kwa maana ya mpasuaji wa elimu, lakabu ambayo alipewa na babu yake, Bwana Mtume (SAW). Sahaba Jabir bin Abdullah al-Ansari anasimulia kuwa siku moja Bwana Mtume (SAW) alimwambia:" Baada yangu utakuja kukutana na mmoja wa watu wa nyumba yangu mwenye jina langu na aliyeshabihiana nami. Yeye ataipasua elimu na kuwafungulia watu milango ya elimu".

Imam Baqir (AS) alilipa umuhimu mkubwa sana suala la ufundishaji na uenezaji wa elimu. Miongoni mwa kazi kubwa zilizofanywa na mtukufu huyo ilikuwa ni kubainisha masuala ya kiitikadi na mafundisho ya dini kwa njia ya majadiliano na wanazuoni wa zama zake. Njia ya mjadala ilikuwa moja ya njia bora kabisa ambayo iliwezesha kuchipua na kuenea elimu katika jamii ya Kiislamu. Majadiliano ni mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika baina ya maulamaa wawili wenye mitazamo miwili inayotafautiana kabisa. Mazungumzo hayo yalikuwa yakifanyika kwa msingi wa kujali na kuheshimu maoni ya upande wa pili kwa kumpa fursa ya kusema na kumsikiliza. Kuhusiana na jambo hilo, Imam Baqir (AS) alikuwa akisema: "Maulamaa wanapaswa wawe na pupa zaidi ya kusikiliza kuliko kuzungumza. Mbali na kuwa na uhodari wa kuzungumza vizuri, wanatakiwa wajijenge pia kuwa wasikilizaji wazuri".

Imam Muhammad Baqir (AS) hakuwa mwasisi wa mbinu mpya ya ubainishaji fikra mpya tu katika Ulimwengu wa Kiislamu, lakini alifungua ukurasa mpya pia katika taarikh na historia ya Uislamu. Miongoni mwa mambo aliyoyafanya katika zama zake, ilikuwa ni pamoja na kubuni njia za kueneza elimu mbalimbali, pamoja na kuweka utaratibu maalumu na wa kimantiki kwa ajili ya kufafanua na kubainisha elimu na maarifa ya dini. Miongoni mwa jihadi za elimu zilizofanywa na mtukufu huyo ilikuwa ni kuanzisha chuo kikuu cha elimu za Kiislamu na kuandaa wanafunzi wengi katika taaluma mbalimbali. Idadi ya wanafunzi wa mtukufu huyo ilifikia 465, na kila mmoja kati ya wanafunzi na wafuasi hao hodari wa mtukufu huyo alihifadhi kupitia kwake maelfu ya hadithi, na kila alipopata fursa alifanya kazi ya kuzipanga na kuziandika hadithi hizo. Katika kuwashajiisha watu juu ya umuhimu wa kujifunza elimu, Imam Baqir alikuwa akisema: “Elimu ni hazina, ambazo ufunguo wake ni kuuliza. Basi ulizeni ili Mwenyezi Mungu akurehemuni; kwa sababu kuuliza kunawapatisha thawabu watu wanne: Muulizaji, mwalimu, msikilizaji na mtu anayetoa jawabu”.

Hatua nyengine aliyochukua Imam Baqir katika jihadi ya elimu ilikuwa ni kuiondoa elimu kwenye udhibiti na ukiritimba wa makhalifa wa Bani Umayyah na utegemezi wake kwa utawala huo. Tusisahau kwamba makhalifa wa Bani Umayyah walijaribu kuihodhi na kuiweka chini ya udhibiti na mamlaka yao harakati ya uendelezaji elimu. Lakini kinyume na muelekeo huo, mbinu ya uenezaji elimu iliyotumiwa na Imam Muhammad Baqir (AS) ilikuwa ni kuimarisha na kustawisha misingi ya elimu katika umma wote wa Kiislamu. Baada ya kuondolewa udhibiti huo na kuimarishwa misingi ya elimu yakapatikana mazingira ya kuchipua harakati ya kufasiri na kutarjumu athari za kielimu pia katika Ulimwengu wa Kiislamu. Miongoni mwa mambo yaliyopewa uzito na Imam Baqir katika jihadi ya elimu ilikuwa ni uenezaji na ufikishaji wake. Mtukufu huyo alikuwa akiwaambia watu:”Zaka ya elimu ni kuifundisha kwa waja wa Mwenyezi Mungu”.

Mbali na harakati za kielimu, Imam Muhammad Baqir alifanya kazi kubwa sana ya kushughulika kuirekebisha jamii na kupinga dhulma na madhalimu. Kwa sababu hiyo daima aliandamwa na chuki, uadui na njama za watawala wa Bani Umayyah. Miongoni mwao ni Hisham bin Abdulmalik ambaye alimtaabisha sana Imam kufikia hadi ya kumhamishia kwa nguvu kwenye makao ya utawala wake huko Sham na kumweka chini ya ulinzi mkali. Lakini pia alimweka kizuizini mtukufu huyo kwa muda kadhaa. Lakini kwa kuwa hatua zote hizo hazikumwezesha Hisham kufikia lengo lake bali zilikuwa na taathira mbaya kwake, aliamua kumrejesha tena Imam mjini Madina. Lakini kama ilivyo nuru ing’arayo, Imam Baqir (AS) aliendelea kuziangazia nyoyo na kuzielimisha fikra na akili za watu. Kwa sababu hiyo, kama walivyokuwa madhalimu wengine katika historia walioamini kwamba kubakia watu kwenye kiza cha ujinga na ujahili ndiko kutakakodhamini uhai wa tawala zao, kuendelea kuwepo Imam kulimtia kihoro na wasiwasi Hisham. Na hatimaye akatekeleza njama ya kumpa sumu na kumuua shahidi mtukufu huyo.

Wapenzi wasikilizaji tunahatimisha kipindi hiki maalumu kwa kunakili maneno ya usia yaliyotolewa na Imam Baqir (AS). Mtukufu huyo anasema:”Wafuasi wetu hawajulikani ila kwa khushuu, unyenyekevu na upole. Wao ni watu waaminifu na humdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi. Wanasali na kufunga na huwatendea wema wazazi. Hujitahidi kuwashughulikia jirani zao mafakiri na wasio na kitu na wanafikiria hali za mayatima, wenye madeni na wenye matatizo. (Wafuasi wetu) ni wasema kweli… na wanalinda ndimi zao na kuwasema watu kwa ubaya”. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/    

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …